MAPENZI YA FACEBOOK-03 Nilizidi kuwa katika wasiwasi mkubwa sana hasa baada ya kuona mke wangu Ester akianza kusumbuliwa na watu aliyodai kuwa walikuwa ni wa Facebook. “Huyu anayekupigia simu usiku huu ni nani?” nilimuuliza usiku mmoja, yalikuwa ni majira ya saa tano za usiku. “Simfahamu mume wangu halafu si unaona ni namba ngeni?” alinijibu huku akionekana kuipuuzia simu iliyokuwa ikipigwa. Mpigaji wa simu ile hakuchoka, alizidi kupiga kila wakati jambo lililozidi kunichukiza sana. Nilijiuliza maswali mengi sana, kila nililokuwa najiuliza lilikosa jibu kwa wakati ule. “Pokea simu,” nilimuambia baada ya kuona mpigaji wa simu hakuonekana kukata tamaa, alizidi kupiga tu!. “Hapana mume wangu huu ni usiku halafu sio vizuri kupokea simu za watu tusiowafahamu,” aliniambia. “Tusipokee au usipokee mbona unanihusisha.” “Mume wangu tusigombane kisa simu tuachane nayo,” aliniambia kisha akakata simu. Kitendo hicho kiliniumiza sana, sikutaka kuamini kama mke wangu Ester alikuwa na kiburi kiasi hicho. Ni hapa ambapo tuliingia katika mzozo na sababu kubwa ikiwa ni simu. “Kwanini umekata simu?” nilimuuliza. “Amna.” “Amna?” “Mume wangu embu tuyaache hayo.” “Kwanini unapenda kucheza na akili yangu?” “Kivipi?” “Nimekuuliza huyu aliyekuwa akikupigia simu ni nani?” “Simjui.” “Ester!” “Kweli mume wangu,” alinijibu katika namna ya kuielegeza sauti yake huku akinisogelea halafu akanikumbatia. “Mume wangu niamini, nimekuambia mara ngapi kuwa simfahamu huyu mtu halafu naomba mitandao isiharibu ndoa yangu nakupenda sana baba wa wanangu,” aliniambia huku akinipapasapapasa mgongoni. Nilizidi kuwa katika hali ya sintofahamu. Maneno ya Ester yalinifanya nimuone kama alikuwa akizungumza ukweli mtupu wala hakuwa akiniongopea lakini katika upande mwingine nilimuona kuwa alikuwa akitafuta njia za kutaka kunizunguka kiakili ili nisiweze kufahamu kile kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Hilo lilizidi kuniweka katika wakati mgumu sana. Nilianza kuiona ndoa yangu ikiingia dosari. Nilimpenda sana mke wangu, alikuwa ndiyo sababu ya furaha yangu, wakati mwingine nilikuwa nikijaribu kukumbuka yale yaliyowahi kutokea katika maisha yetu kipindi cha mahusiano yetu. Yale yote yaliyotokea sikutaka yaendelee kubaki moyoni mwangu, niliamua kuyasamehe na kufungua ukurasa mpya. Siku iliyofuata asubuhi na mapema niliamua kumueleza ukweli mke wangu juu ya jambo lile pamoja na maamuzi yangu niliyokuwa nimeyaamua. Hakika alionekana kufurahishwa sana. Pengine niseme ni katika siku ambayo ilikuwa ni ya aina yake kwani sikuwahi kumuona mke wangu akiwa katika furaha hiyo hapo kabla tangu ilipopita harusi yetu. “Asante mume wangu yani sikutegemea kama ungeamua hivyo,” aliniambia huku akinikumbatia kwa furaha. “Kwanini unasema hivyo?” nilimuuliza. “Unajua binafsi sikupendezewa na kile kilichotokea usiku ule, nakupenda eti mume wangu halafu Facebook inataka kuaribu ndoa yangu hivihivi,” aliniambia katika mtindo wa sauti ya kitoto. “Usijali ila kuna kitu nataka nikuambie,” nilimwambia. “Kitu gani hicho tena hubby?” aliniuliza kisha akajitoa katika lile kumbato. “Ni kuhusu Facebook.” “Imefanyaje?” “Nisingependa kuona tena usumbufu katika simu yako.” “Usijali Phidelis wangu, mwanaume wa maisha yangu,” aliniambia kisha akanibusu shavuni, busu ambalo lilizidi kuamsha hisia za dhati za kimapenzi. Niliamini Ester ndiye alikuwa kila kitu katika maisha yangu, nilimpenda kwa dhati ya moyo wangu. Niliamua kusahau yale yote yaliyopita na kuamua kuendelea na maisha yetu kama kawaida lakini ilikuwa ni kama vile najaribu kuigiza upofu wakati macho yangu yalikuwa ni mazima. Ester alizidi kunifanyia visa na chanzo kilikuwa ni mtandao wa facebook. Je, nini kitaendelea? Usikose sehemu ijayo….

at 7:26 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top