MAPENZI YA FACEBOOK-02 Hakika mapenzi yalikuwa yakiniendesha sana wala siwezi kulipinga hilo. Kabla sijamfahamu huyu Cleopatra au Precious Girl katika mtandao wa facebook kipindi cha nyuma niliwahi kuwa katika mahusiano na msichana mmoja ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la Ester. Alikuwa ni msichana mrembo sana, alitokea kuuteka moyo wangu. Niliamua kufunga pingu za maisha na yeye ni kwasababu nilikuwa nikimpenda sana, alikuwa akinipenda na kunionyesha mapenzi ya dhati yaliyozidi kunifanya nimuone yeye tu katika sayari ya mapenzi. Uwepo wake katika maisha yangu ulikuwa ni wa thamani sana. Mapenzi yetu yalikuwa yametawaliwa na furaha sana, nilikuwa nikimpenda sana lakini naweza kusema ndoa yetu ilikuja kuingiliwa na mdudu. Mdudu ambaye amefanya mpaka leo hii nimeamua walau kuwasimulia kile kilichowahi kutokea katika maisha yangu hasahasa maisha ya kimahusiano. Facebook! Ndiyo mdudu aliyekuwa akiitafuna ndoa yangu na Ester. Licha ya mapenzi niliyokuwa nayo kwa mke wangu lakini bado Facebook ilizidi kuidhulumu nafsi yangu ya upendo. Nakumbuka siku ya kwanza Ester kujiunga na Facebook ilikuwa ni pale ambapo niliamua kumnunulia simu. Hii ilikuwa ni moja kati ya ahadi ambayo nilimuahidi kwa muda mrefu. Nilimuambia mambo mengi sana ambayo yanaweza kutokea katika mtandao huu. Nilimuambia juu ya maisha feki wanayoishi watu facebook. Sikutaka kumficha kitu ni kwasababu na mimi nilikuwa ni mtumiaji wa mtandao huu. “Jamani mume wangu inamaana huniamini au?” aliniuliza Ester kwa sauti ya kudeka. “Hapana sio kama sikuamini ila najaribu kukuambia tu,” nilimjibu huku nikimsogelea, wakati huo tulikuwa tupo chumbani. “Mimi sipendi jinsi unavyonihisi vibaya.” “Najua hupendi mke wangu ila nayasema haya ili kulilinda penzi langu.” “Hata kama mume wangu lakini unajua fika kuwa nakupenda wewe na siwezi kuwa na mwanaume mwingine zaidi yako.” aliniambia huku akiwa amejilaza kifuani mwagu, maneno yake yalipenya vyema masikioni mwangu na kunifanya nijihisi mwenye bahati hasa kwa kumpata mwanamke ambaye alikuwa akinipenda sana na hakuwa tayari kunipoteza katika maisha yake. “Chunga Facebook isije ikavuruga ndoa yetu,” nilimuambia huku nikimpapasa taratibu mgongoni. “Usijali Mume wangu nakupenda sana,” aliniambia kwa sauti ya kitoto. “Nakupenda pia,” nilimjibu katika namna ya utulivu sana. Niliwahi kushuhudia jinsi Facebook ilivyovuruga mahusiano ya watu. Facebook ndiyo ilikuwa chanzo cha migongano na mikanganyiko ya ndoa nyingi ambazo ziliwahi kuvunjika. Mimi ni shahidi katika hilo, nakumbuka Facebook ndiyo ilikuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa ya kaka yangu ambaye alikuwa akimpenda sana mkewe ambaye nilikuwa nikimuita shemeji. Kwa kweli sikutaka yale yaliyowahi kutokea katika maisha ya kaka yangu yaweze kunitokea. Nilijifunza mambo mengi sana hivyo nilikuwa makini sana hasa kwa kulilinda penzi langu, kuilinda ndoa yangu, roho yangu. Baada ya kupita wiki moja tangu mke wangu Ester ajiunge na Facebook nilianza kupatwa na wasiwasi mkubwa sana. Sikujua wasiwasi ule ulikuwa ukitokea wapi hasa kwani tayari Ester alikuwa ameshakuwa mke wangu, mke halali kidini. Simu yake ilikuwa ikipigwa kila wakati na namba ngeni. Niliamua kumuuliza kuwa namba zile zilikuwa ni za watu gani ila mara zote alikuwa akinijibu kuwa walikuwa ni watu wa Facebook ambao walikuwa wakimsumbua. Wivu ulianza kunisumbua Phidelis mimi ambaye nilizama katika dimbwi la mapenzi, ulianza kunitafuna taratibu na kuniacha na maumivu ambayo sikuyatarajia kwa kipindi kile. Kuna kipindi nilikuwa nikijilaumu ni kwanini niliamua kumnunulia simu ambayo iliweza kumuunganisha na mtandao huu wa Facebook. Je, nini kitaendelea? Usikose sehemu ijayo...

at 7:25 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top