USIKATE TAMAA. SIMULIZI FUPI : Kila nikikaa na kuyatafakari mapito magumu niliyokuwa nikiyapitia katika hii dunia huwa nabaki kuilaumu ardhi ni kwa nini iliachama na kuwaweza wazazi wangu na kuniachia majonzi makubwa na mazito yaliyoyatawala maisha yangu kwa muda mrefu. 👉 Ilikuwa ni mwaka 1994 wazazi wangu walipofanikiwa kunizaa na kunileta duniani,,kipindi wananizaa na kufanikiwa kunilea hadi nikafikisha umri wa kuanza darasa la kwanza kiukweli maisha ya familia yetu hayakuwa mabaya sana yalikuwa ni maisha mazuri tu ambayo kwa kiasi kikubwa yalitawaliwa na furaha kubwa ya ajabu isiyokuwa na mfano ambayo kwa matarajio yangu niliamini ingeendelea hadi kuufikia ule mwisho wa dahari.Mama yangu pamoja na baba yangu waliokuwa wakinipenda na kunipa faraja na matumaini katika maisha yangu walinilea vizuri wakanivisha vizuri pamoja na kunilinda hadi nikafanikiwa kuingia darasa la saba tayari kwa kuikamilisha safari yangu ya mwisho ya masomo ya elimu ya msingi.Sikujua kama furaha yangu ingekuja kuyeyuka na kupotezwa kabisa mithili ya blanketi zito liteketezwalo na moto mkali usiokuwa na chanzo maalumu.Maskini Mimi sijui nilikuwa nimemkosea nini tu Mungu wangu,sikujua nilikuwa nimeikosea nini dunia au Mungu wangu aliyeniruhusu nizaliwe na mama yangu tena kwa uchungu usiokuwa na kipimo maalumu.Sitokaa niisahau siku ya jumanne tarehe ya 23/7/2009 majira ya saa saba na nusu za mchana nilipoletewa habari ya kutisha na baba yangu mdogo kwamba wazazi wangu wawili yaani baba na mama wote wamefariki kwa ajali mbaya ya gari kipindi wanaelekea kijijini kumsalimia bibi yangu aliyekuwa amedhoofika kwa maradhi...taarifa hiyo niliipokea kwa majonzi sana kiasi kwamba ikafikia kipindi nikajikuta nikiichukia dunia pamoja na kuirushia matusi mazito ambayo hayakuwa na msaada wowote...nililia sana nikaziona kabisa ndoto zangu za kukanyaga chuo kikuu zimepotea mithili ya ukungu wa asubuhi upotezwapo na miali mikali ya jua.Siku ya mazishi ya wazazi wangu sikuchoka kuisalimia ardhi kila baada ya dakika mbili kupita ,nilikuwa nikizimia Mara kwa Mara na nikizinduka tu najikuta nikiipaza sauti yangu kulia kwa uchungu. Kwa kuwa wazazi wangu walinizaa Mimi pekee katika uzao wao wa kwanza sikuwa na ndugu wa kike wala wa kiume tofauti na baba yangu mdogo ambaye niliamini angekuja kunifariji pamoja na kuyatetea maisha yangu kwa ujumla.Baba huyo baada tu ya hayo mazishi ya wazazi wangu alinishuhudia kwa kinywa chake kwamba atanilea na kunisomesha mpaka pale nitakapo choka mwenyewe. Baada ya miezi mitano kupita huku baba yangu mdogo akiwa amenichukua nyumbani kwake alianza kunibadirikia,ahadi zote alizokuwa ameniahidi zilianza kufifia ikafikia kipindi akaanza kunichukia waziwazi kabisa.Siku nikinyimwa chakula na mama mdogo ,baba huyo hakunitetea hata kidogo badala yake akawa ananigeuzia vibao kwamba nitakoma kwa upumbavu wangu. Uvumilivu nilimshikilia kwa nguvu zangu zote lakini yeye hakunihurumia kabisa,,mpaka kufa sitakuja kuyasahau maneno haya ya kusingiziwa,aliyoyazungumza mama mdogo mbele ya baba mdogo na kunifanya Leo niiandike posti hii huku nikilia na kuomboleza kwa uchungu .Mama huyo alisema; "Baba Beatrice!! Huyu dubwana uliyeniletea hapa nyumbani ni zaidi ya mwendawazimu tena jambazi.Ukiendelea kumuatamia kama yai ipo siku utanikumbuka kwa haya ninayokuambia.Samwel ni jambazi tena amejifunza na uvutaji wa bangi..sasa kama una macho basi litazame hili kwa umakini ,kwa upande wangu huyu mtoto sitaki kumuona akiwa hapa nyumbani kwangu maana atawaharibu hata mabinti zangu Zulpha pamoja na Beatrice,, kwa hiyo chukua hatua maana muda ndio huu na ukumbuke usipoziba ufa basi jiandae kuujenga ukuta". Maneno hayo sikutaka kuyaamini kabisa maana hata siku moja sikuwa mtu wa tabia mbaya,nilijiheshimu Mimi pamoja na kuwaheshimu wao,sikujua hayo maneno ameyatolea wapi tu...nafsi ilinituma nikajitutumua na kuwahoji,niliwauliza swali dogo tu lakini swali hilo halikujibiwa kivingine zaidi ya kuambulia kipigo cha mbwa ambacho kiliniumiza sana.Baba mdogo hakuwa na muda tena wa kuniuliza chochote kile zaidi ya kuchukua maamuzi tu ya kunifukuza nyumbani kwake,aliingia ndani akachukua begi langu la nguo akalitupa mbele yangu huku akiniambia." Ondoka hapa nyumbani kwangu sitaki nikuone !! Kumbe wewe mtoto ni mpumbavu kiasi hiki ? Ondoka kabisa na milele daima sitaki nikuone umekanyaga hapa kwangu ukifanya hivyo nitakuua ".Baba mdogo hakuwa na chembe ya huruma hata kidogo ,alinisahau kabisa akawa ananiona Mimi kama hayawani tu asiyekuwa na thamani yoyote...nilijitahidi kuyapiga magoti yangu chini kumuomba msamaha lakini wala hakutaka kunielewa kabisa,,Nililia sana nikajiinamia kwa uchungu na kulitwaa begi langu chakavu lililokuwa likigaa gaa chini,,nilisimama kiunyonge nikawatizama Mara moja tu na kuwaachia neno hili " Baba nashukuru kwa yote uliyonifanyia,najua umeamua kunifanyia hivi kisa Mimi ni yatima sina baba wala mama ila tambua tu Mtetezi wangu yu hai ipo siku atayafuta machozi yangu maana ndiye aliyebakia kuwa baba yangu katika hii dunia,yote uliyonifanyia nimekusamehe...umezipokonya Mali zote nilizoachiwa na wazazi wangu pamoja na nyumba lakini tambua kwamba malipo ni hapa hapa duniani, nyie tembeleeni magari Mimi nitatembelea miguu maana ndio maisha!! Nitafanyaje kama sina baba wala mama? Kwaherini Nawatakia maisha marefu na Mungu awabariki". Niliongea kwa uchungu kisha nikaanza kujikongoja kuondoka mbele yao huku mkono wangu mmoja nikiwa nimeuweka shavuni..sikujua nielekee wapi lakini moyo wangu uliniambia nisonge tu mbele popote nitakapofika basi ndo huko.Kula kulala pamoja na mambo mengine hayo yote yaligeuka yakawa kitendawili na fumbo gumu sana kulitatua,,sikuwa na pakwenda lakini nikawa radhi tu kuishi popote pale hata majalalani sawa tu.Elimu yangu ya darasa la saba niliamini ingenisaidia tu hata kupata kibarua cha kuuza kalanga maana sikuwa na tumaini jingine zaidi ya kubakiza lile tu la kulisindikiza jua pamoja na kuishi kwa matumaini yasiyotimia.Nilitembea njia nzima nikitikisa kichwa changu pamoja na kujiongelesha maneno mengi ambayo hayakuweza kunisaidia kwa chochote kile .Sikutegemea na Mimi kama ningekuja kuingia katika ulimwengu huo wa kudharauliwa kwa kuita mtoto yatima,,sikujua nimlaumu nani lakini nikaishia kukishukuru tu kifo kwa yote kiliyonitendea.Nilitembea kwa mwendo wa kujikokota kokota mpaka nikaipata barabara moja iliyokuwa imepakana na miti tofauti tofauti nikainyoosha na kuzidi kuchanja mbuga.Kwa vile muda huo ulikuwa ni wa jioni ,Giza lilianza kutanda mbele yangu na kuzidi kuyapoteza kabisa matumaini yangu...haraka haraka wingu la mvua lilianza kutanda na hazikupita hata dakika tano mvua ikaanza kunyesha .Mvua hiyo yote iliyotawaliwa na mawe pamoja na upepo wa fujo ilifanikiwa kuninyeshea yote na kunilowanisha vibaya sana...nguo zote nilizokuwa nimezivaa zililowana pamoja na lile begi langu la nguo... Nilitetemeka sana,nikajikongoja hadi nikaufikia mti mmoja nikakaa juu ya matope na kuyanyanyua macho yangu juu kuitizama mbingu. "Ee mwenyezi Mungu wewe ni muweza wa yote, baba wa yatima,,mlezi wa wasiokuwa na wazazi nisaidie baba !! Mimi ni yatima baba,sina pa kukimbilia nimebaki peke yangu mithili ya kifaranga cha ndege kilichofiwa na mama yake katikati ya msitu mnene wa kutisha,,nisaidie baba,wote wanaonidharau wanione nikiinuliwa maishani ,ee baba!!".Niliyaongea hayo maneno kwa sauti ya kutetemeka huku machozi yakianza kuyalowanisha mashavu yangu.Sikuwa na la ziada baada ya hapo zaidi ya kulala chini pale pale kuutafuta usingizi.Bila kutarajia kwa mbali niliona taa mbili za gari ikija mbele yangu,sasa iliponifikia ikasita kuendelea na safari yake hivyo ikasimama ,baada ya muda kidogo alishuka baba mmoja wa makamu akawa kama anaelekea upande wa kulia ,alipoyageuza tu macho yake alishangaa sana kuniona nikiwa nimejikunyata chini tena kwenye matope huku nikiwa nimelowana muda huo huo nikitetemeka maradufu .Alinisogelea kwa kunyata nyata akanifikia na kunihoji maswali mawili matatu ambayo niliyajibu kwa ufasaha sana,aliniuliza Nina wazazi nikajibu sina na Mimi ni mtoto yatima tena nimefukuzwa kama mbwa nyumbani kwa baba yangu mdogo.Kiukweli baba yule alinihurumia sana akanishika mkono huku nikitetemeka nikaongozana nae hadi kwenye gari yake."Usiogope ingia twende nyumbani kwangu". Aliyaongea hayo na kunipa moyo nikaingia ndani ya gari hiyo na nilipoingia humo nikamkuta na mkewe amekaa pembeni ya kiti cha kulia cha ile gari ambapo nae alinihurumia Sana na kujikuta akiapa kunisaidia.Basi tulipoondoka hapo tukaelekea hadi nyumbani kwao,na tulipofika baba yule alinikaribisha vizuri na kuniambia nijisikie kama nipo nyumbani. Kiukweli mazingira ya pale yalivyokuwa iliashiria dhahiri familia hiyo ilikuwa ya matajiri.Sasa kwa vile nguo zangu nilizokuwa nimezivaa zililowana,mama wa nyumba aliingia ndani ya chumba kimoja akatoka na nguo kadha wa kadha akanipa nivae...moyo wangu ulifarijika sana furaha ikaanza kurejea tena.Baada ya hayo yote baba wa familia hiyo iliyokuwa na watoto watatu na Mimi wa nne alianza kufunguka mazito mbele yangu,,aliniambia kuanzia siku hiyo nitakuwa mwanae na atanisomesha hadi chuo kikuu.Ahadi yake hiyo aliitimiza vizuri sana maana alinipeleka sekondari katika shule ya kulipia almaarufu kwa jina la Loyola iliyopo jijini Dar es salaam ambapo nilisoma hadi nikahitimu kidato cha nne na kufanikiwa kufaulu vizuri kwa kupata daraja la kwanza.Nilichaguliwa kujiunga na shule ya wavulana ya Tosa Maganga kwa masomo ya kidato cha tano na sita kwa mchepuo wa masomo ya Economics, Geography pamoja na Mathematics. Baada ya hiyo miaka miwili kupita nilifaulu vizuri na kuchanguliwa kujiunga na masomo ya chuo kikuu, katika chuo cha Dar es salaam kwa kozi ya kompyuta na uhasibu.Nilihitimu vizuri kozi yangu hiyo na Mungu akanisaidia nikapata ajira kwenye banki moja ya NMB iliyoko mkoani Simiyu wilayani Itilima.Sijawasahau wazazi wangu hao walezi waliojitolea kulichukua jukumu zima la kunilea baada ya wazazi wangu halisi kufariki dunia,, niliwashukuru sana kwa matendo mazuri waliyonifanyia na kuniweka hapa nilipo.Kila siku sichoki kuwatendea mema na kila mwezi huwa nawarudishia fadhiri. Kwa sasa maisha yangu yanaendelea vizuri, machungu yote niliyokuwa nikiyapitia nimesha yasahau...nilinunua kiwanja cha maana sehemu moja ya Kariakoo jijini Dar es salaam nikajenga nyumba yangu nzuri tu na ya kutosha .Nilifanikiwa kumpata mke mwema ambaye hadi sasa ananipenda kwa dhati na tumefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume.Baba mdogo nimeshamsamehe na sina kinyongo nae,kwa sasa nimesikia ameshafirisika hana chochote na maisha yake ni magumu sana kwenye familia yake...Mali zake zote ziliyeyuka na mabinti zake hawakusoma na kufika popote zaidi ya kidato cha pili na kuambulia kubeba ujauzito. FUNZO: Usimdharau yeyote aliyepewa pumzi na mwenyezi Mungu kisa yeye ni masikini au yatima maana huwezi jua ni ridhiki ipi kapangiwa na Mungu wake kabla hajarudi mavumbini.

at 9:26 AM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top