Home → simulizi
→ SIMULIZI YA LEO
NIPO SONGEA
By
B professional love
DALADALA imekolea mwendo. Kondakta wa daladala ametingwa kukusanya nauli. Pamoja na kutingwa kwake, bado hasahau kuwakumbusha abiria vituo. “Manzese Darajaniiiii!”
“Shushaaa!” Abiria mmoja wa kike anapaza sauti.
Omi, dereva wa daladala hilo lililoanza kuchoka anakanyaga breki. Konda anafungua mlango, mama huyo anashuka. Kijana mmoja wa makamo anaingia ndani ya daladala hilo. Nyuma yake anapanda binti mwingine. Anakwenda moja kwa moja kuketi kwenye siti iliyo wazi, ambayo awali ilikaliwa na mama huyo aliyeshuka.
Mtu huyo anapoketi tu, analegeza tai yake shingoni. Joto la Dar es Salaam si mchezo. Mchana huu jua linawaka kweli kweli, na kuwatoa jasho wakazi wake. Mabruki anailegeza vizuri tai yake na kuacha nafasi ya kutosha kuingiza hewa.
Kisha anachukua nakala yake ya gazeti lililosheheni habari za kisiasa na kuanza kusoma kwa utulivu. Hana habari na yeyote ndani ya gari hilo. Akili yote ipo kwenye gazeti lake.
Pembeni yake anaketi kimwana mmoja. Tangu Mabruki aingie ndani ya gari hilo, binti huyo katingwa na simu yake ya kiganjani. Anaandika na kusoma ujumbe. Soga mtandaoni kwa mtindo mmoja. Mabruki wala hana hata habari.
Mara simu yake inaita. Anatulia kidogo kuusikilizia mlio wake. Mlio pekee unamtosha kumfahamu mpigaji ni nani. Huku mapigo ya moyo yakienda kasi, anaitoa simu hiyo iliyokuwa ndani ya mfuko wa shati lake na kuipokea. Anaongea kwa sauti ya chini ili kutowabughudhi abiria wengine.
“Helo my dear.”
“Baba Zahra za leo?”
“Salama tu mama. Kwema huko?”
“Kwema kabisa. Hofu juu yako mpenzi. Habari za Songea?”
“Njema mama. Bado tunaendelea na semina. Kesho tunategemea kumaliza kama nilivyokueleza. By Friday ntakuwa njiani honey.”
“Jamani baba Zahra usisahau basi kuninunulia viazi vya Songea. Shogaangu mama Hamdani kaniambia huu ndo msimu wake. Si unajua dear vilivyo bomba sana viazi vya Wangoni?”
“Yah!” Anaitikia.
Mkewe anapata uwanja wa kumwaga sera. “Niambie basi honey, utaniletea? Halafu jamani huko ukibahatisha hata kakipande ka nyamapori dear. Si unajua sijala siku nyingi, tangu kipindi kile tulipoenda kwa mama Mngazi?”
“Tatizo upatilkanaji wake. Nitaulizia ulizia.”
“Halafu tena.”
Huyu naye! Mabruki anatamani kukata simu kabla konda hajaita kituo. Lakini mke wake anazidi kuzungumza pasi kuonesha dalili ya kukata simu haraka. Mambo ya Xtreme hayo.
“Halafu tena honey, yule fundi uliyesema atufungie dishi wala hajaja kufunga. Mpigie basi umwambie afanye fasta. Si unajua tena nakosa kuangalia ze komedi?”
“Ok! Nitampigia. Basi ngoja nimpigie, kisha nitakupigia baadaye kidogo.” Mabruki anaona hiyo ndiyo njia pekee ya kumaliza maongezi kwenye simu.
“Utampigia hata baadaye kidogo. Halafu nilitaka kusahau kukwambia.”
Huyu naye, nini tena? Kwa hasira anajikuta anauliza, “nini tena?”
“Hivi yule shogaangu wa Mwanyamala yule alikuja nyumbani majuzi jioni si unamkumbuka?”
Mambo ya shoga zake na mimi wapi na wapi? “Ndiyo namkumbuka.”
Anajibu haraka haraka kumaliza maongezi.
“Basi mwenzangu kumbe shida yake yote iliyomleta nyumbani ilikuwa ni kukopa pesa. Hakutegemea kukukuta. Alipokukuta tu, akaishiwa sera. Basi leo kaja tena.”
Sijui nimkatie simu? Mabruki akashindwa kujijibu. Akabaki kimya.
“Basi mi namshangaa sana. Anapenda sana kuchonga juu ya maisha ya wenzake, kumbe naye anategemea vya kukopa.”
“Mh!” Mabruki akaishia kuguna.
“Wala hata sijampa.”
Kabla hata hajajibu, anamsikia konda, “Shekilangooo?”
“Shushaaaa!”
Mabruki aliikata simu kama aliyewehuka ghafla. Mapigo ya moyo yakaruka mapigo. Jasho lilimtoka mithili ya mtu aliye jirani na tanuri la moto.
Simu yake ikaanza kuita tena. Binti aliyeketi pembeni akishughulika na simu yake alikuwa akitabasamu kwa mbali. Dalili zote zilionesha alifanya jitihada za makusudi kuzuia kicheko chake kisitoke nje. Mabruki hakujisumbua naye. Akaonelea amwache ahangaike yake.
Akaitazama simu yake iliyokuwa ikiita kwa macho ya hofu tele. Mke wake hata hakuonesha dalili za kuchoka. Ilipokatika ikaita tena.
“Leggooo?”
“Shusha.” Mabruki akainuka haraka haraka na kushuka garini. Binti yule naye akashuka. Aliposhuka tu, akaenda haraka katika kibanda cha simu na kuzuga ananunua muda wa hewani.
Mabruki akaitazama simu iliyokuwa ikizidi kuita kwa mashaka tele. Kama atakuwa amesikia, itakuwaje? Ndilo swali lililomtawala. Akapiga moyo konde na kuipokea.
“Mbona ulikata jamani honey?” Mkewe alianza kwa lawama moja kwa moja.
“Mh eeh! Haina chaji ikazima.”
Upande mwingine jijini Dar es Salaam, mke wa Mabruki alitamani kuangua kicheko. Akaamua kuwa mstaarabu. Muda wote akizungumza kwenye simu, alikuwa ndani ya teksi. Alikuwa na haraka ya kufika mahali.
“Basi ukishaiweka chaji usisahau kunipigia mume wangu. Si unajua ninavyokumiss acha kabisa. Nakupenda sana.”
“Ok. Nami pia. Baadaye basi.”
Simu ikakatwa.
Mabruki akaenda moja kwa moja hadi ndani ya Leggo hoteli.
Yule binti aliyezuga akinunua muda wa maongezi, akainyanyua simu yake na kuzungumza huku akicheka.
“Mbona umechelewa sweetie?” Kidawa alianza kumwambia Mabruki baada ya salamu.
“Foleni mpenzi.”
“Pole sana mpenzi wangu.”
“Ahsante. Si ushakula, twen’zetu ndani.”
“Ok. Tena nina hamu nawe. Maana umekwenda Manzese umechelewa.”
“Si wale mafundi wamenichelewesha. Ila fremu yako watu wanaisifia sana. Sipati picha utakapoanza kupanga vipodozi kwenye shelfu zake patapendezaje? Hadi nina wasiwasi vijana wa siku hizi watanipora.”
Mkono wake kiunoni kwa Kidawa. Binti yule aliyekuwa akizuga kununua muda wa maongezi, akawa kesha maliza kuzungumza kwenye simu. Akaingia pale hotelini na kuagiza soda ya Mountain Dew.
“Wala hani wangu. Akupore nani wewe mwenyewe upo juu kama ndege ya Obama.”
Wote wakaangua kicheko.
Wakati wanachukua ufunguo wao mapokezi, binti yule aliwapita akiwa na chupa yake ya soda mkononi huku akizungumza na simu.
Wakaingia. Mabruki alikuwa ametoka hotelini hapo takribani masaa mawili nyuma.
Hivyo akapitiliza maliwatoni. Akakoga.
Kisha akaungana na Kidawa, mtoto wa mjini. Wakaanza kupeana mahaba.
“Ngo! Ngo! Ngo!” Mlango uligongwa wakati wao wakiwa wamezama katika bahari ya mahabadati.
“Nani?” Mabruki aliuliza kwa hasira na uchovu.
“Front office please. A minute please.”
Mabruki akamwashiria Kidawa akafungue.
Bibie Kidawa akavuta kipande cha kanga na kujisitiri japo kidogo. Akaenda mlangoni.
Akaufungua.
Wanawake wawili walikuwa wamesimama nyuma ya wanaume wawili, ambao nao walikuwa nyuma ya mhudumu wa hoteli.
Kidawa akapigwa na mshangao. Akababaika. Mmoja wa wanawake wale alimfahamu fika. Wale wanawake wawili wakapiga jicho moja kwa moja hadi ndani ili kuona kilichomo. Wakati Kidawa akiwa angali na butaa, akasukumiwa ndani mzima mzima. Kundi la watu wanne likaingia hadi ndani huku mhudumu akibaki koridoni pasipo kufahamu cha kufanya.
“Ndiyo Songea hapa?” Hilo ndilo swali pekee mama Zahra alilomudu kuliuliza.
Mabruki akabaki akiwatumbulia tu macho wageni wale mithili ya mbwa aliyekabwa na mfupa.
Mama Zahara alipojaribu kuuinua mdomo wake kuzungumza, mdomo pekee ndio uliofunguka lakini sauti haikutoka.
Mara akaanguka chini akiwa amezidiwa na mapigo ya moyo.
Kila mtu mle ndani akachanganyikiwa.
Mabruki akavaa suruali yake kwa kasi ya ajabu. Jambo lililowashangaza wote, Mabruki ndiye aliyekuwa wa kwanza kwenda kumnyanyua mke wake. Akambeba mzimamzima mithili ya kuli na gunia la nafaka.
Alipofika chini, akaita teksi haraka na kumkimbiza hospitali.
MWISHO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: