Home → simulizi
→ NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 45
Nilielekea kuoga haraka na kuvaa nguo zangu kimyakimya nikamuacha Rabia akiwa kitandani akiota njozi njema. Nikatoka nje kwa kunyata na kuelekea kanisani.
Kijua kilikuwa kimeshaanza kuchomoza na njiani nilipishana na watu wengi mtaani kila mmoja akienda kwenye mihangaiko yake. Ulimwengu kwangu ulikuwa tofauti sana na kila mmoja wenu anavyouona na hii ilikuwa ni baada ya kutoka kuzimu.
Nikiwa muoga wa nafsi kiasi hicho nilishangaa wanadamu wenzangu wakiwa hawana wasiwasi wowote na zaidi wakionekana kuwa na haraka kulitumikia tumbo na mambo ya kidunia kuliko kufika peponi.
Sasa nilikaribia kanisani pale kanisa Katoliki la Mbezi Beach, nikaingia ndani kwa kuwa mlango daima hapo huachwa wazi. Niliingia moja kwa moja hadi kwenye sehemu ya kuungamia na kumkuta padre akiwa anaandaa mambo muhimu kwa ajili ya misa ya asubuhi. Aliponiona nikielekea upande wake akaja na kuketi kwenye kizimba cha kitubio ambapo alikaa bila kuniona usoni.
Akaniambia ungama mwanangu, nikasali ile sala ya toba huku machozi yakinitoka, nikaapa kamwe sitarudia kufanya dhambi na nilijutia kwa kuwa ni mchezo wa shetani kwenye akili za watu.
Yule Padre alionekana kushangaa kwa jinsi nilivyojutia akaniambia nimueleze nini kilichonikuta mpaka nimejutia kwa moyo kiasi hicho; hapo ndiyo nikaanza kumueleza kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari yangu hasa baada ya kukutana na Lusifa.
Padre alinitazama kwa kupigwa na butwaa akanipa pole lakini alionekana hakuamini chochote na kuniona pengine nimechanganyikiwa, akaniambia; "mwanangu pole kwa yaliyokukuta, tafadhali ukitoka hapa pitia hospitali kuna kitu wanaweza kukusaidia."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: