Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 6
Wakati anataka kutoka akasikia sauti,
“Moza lala”
Akashtuka sana na kugeuka ili aone sauti inatokea wapi, ila hakumuona mtu yoyote akataka akafungue malango tena, kasikia
“Moza lala”
Safari hii ile sauti ilimwambia kwa ukali kidogo. Moza alizidi kupatwa na uoga hadi akawaza kutoroka kwenye ile nyumba ila atatorokaje usiku huo na kuna mlinzi getini, yani akawa na mawazo mbali mbali mpaka akajihisi kuchanganyikiwa. Ila bado alikuwa na wazo la kwenda sebleni kukaa lakini sauti ile ilizidi kumwambia moza alale, alipoona ile sauti inazidi maana ilianza kuongea kama mwangwi,
“Moza lala, Moza lala, Moza lala”
Uoga ulimjaa Moza hadi akataka kutoka kwa nguvu ila alipofungua mlango ulikuwa mgumu na ile sauti ilizidi kumsihi alale, Moza alitetemeka zaidi akataka kupiga kelele ili afunguliwe mlango ila moyo mwingine ukamwambia ukipiga kelele ndio utamshtua mwenye nyumba kuja kukuadhibu, akaamua kwenda kukaa kitandani huku akiombea asilale ila sauti ya kumsihi kulala ilizidi na kumtia hofu zaidi. Alipotaka kuinuka tena muda huu alishtukia akipigwa kibao kilichomuangusha hadi chini halafu taa ya chumbani ilizimwa yani hapo ndio uoga zaidi ukamshika na kujikuta akishindwa kuinuka pale chini ila cha kumshangaza wakati anaogopa sana, usingizi ukampata pale pale.
Wakati amelala akajiona yupo mahali chini ya mti halafu kaja Yule dada anayeongeaga kati ya wale wadada watano, akaanza kuongea nae ila leo Moza hakuweza kujibu wala kuuliza swali.
“Moza, ni mbishi sana wewe ndiomana nimekufanyia hivi. Yani hujui kutofautisha kati ya mtego na kitu cha kweli. Yule mama angetaka ulale ili akufanyie mambo mabaya unafikiri angeongea kwa sauti kubwa vile? Kaongea kwa sauti kubwa sababu amejua wewe ni mbea na utasikiliza tu kwahiyo alikuwekea mtego, na usingelala ndio angejua kama ni mbea kweli maana kwanini unasikiliza maongezi yao? Halafu kwa sheria za huyu mama amfanyiagi kitu mbaya mtu akiwa amelala, ndiomana hata jana hakukufanya lolote sababu ulilala ila ungekuwa macho ungepatwa na makubwa. Usifikirie siku zote nitaweza kukusaidia, nimeweza leo sababu ile juzi uliunguza mboga kwahiyo nimepata nguvu. Jifunze kuelewa mitego Moza, tutakupoteza na wewe. Usifikirie ni rahisi hivyo kutoroka kwenye hii nyumba. Kitabu nilichokwambia kipekue kesho uanze kukisoma ndio kitakusaidia sana kwenye mambo yote ya kufanya. Halafu unatakiwa kuwa makini sana kwenye kila kitu unachofanya, yani fikiria kabla ya kutenda jambo lolote. Kwasasa lala tu”
Huyu mdada aliondoka, ila ni usingizi mzito sana ulimshika Moza wakati huo.
Kuja kushtuka ilikuwa ni kumeshakucha, akaamka pale chini na kujishangaa shangaa kuwa imekuwaje mpaka akalala hapo chini, akaanza kukumbuka matukio na kukumbuka kuwa mara ya mwisho alinaswa kibao na kuanguka hapo chini kisha kukawa na giza kubwa lililompa uoga na kupitiwa na usingizi kwa uoga, pia akakumbuka alivyoota. Akainuka pale chini haraka haraka baada ya kukumbuka kuwa alitakiwa kuadhibiwa, akatoka sebleni ila nyumba ilikuwa kimya kabisa yani ilionyesha hapakuwa na mtu yeyote mule ndani.
Akasogea mezani ambapo alikuta ujumbe, ‘UPIKE WALI, MAHARAGE NA SAMAKI’ akaelewa kuwa ujumbe huo umeachwa na mama mwenye nyumba, hivyo akahisi kuwa huenda nyumba nzima wameondoka na hivyo kwenda kuoga na kuanza kufanya kazi za hapa na pale mule ndani hadi alipoanza kupika kile chakula alichoagizwa.
Alipomaliza kupika alikiandaa kabisa mezani ila alikuta ujumbe mwingine ‘TENGENEZA NA JUISI YA MATUNDA YAPO KWENYE FRIJI’ akaangalia kulia na kushoto, mbele na nyuma na kujiuliza,
“Mbona ujumbe huu sikuukuta mwanzoni? Humu ndani si nimebaki mwenyewe? Au sikuangalia vizuri!”
Akajiuliza bila ya jibu kama kawaida kisha akaanza kuiandaa hiyo juisi na kuiweka kwenye friji, ila aliporudi mezani alikuta ujumbe mwingine ‘CHEMSHA MAJI YA KUOGA YA ANA UMUWEKEE KWENYE CHUPA’ hapo uoga ukamshika na kuanza kuhisi tofauti, kisha akajiuliza,
“Mbona huyo Ana hajawahi kusema nimchemshie maji ya kuoga? Huu ujumbe ananiwekea nani? Siwezi kwakweli, naogopa. Inamaana sikuuona pia?”
Alikuwa na mashaka sana ila akaenda kuchemsha hayo maji na kuyaweka kwenye chupa, alipomaliza alirudi tena mezani na kukuta ujumbe mwingine ‘DEKI TENA NYUMBA’
Aliogopa sana sasa hivi na kuamua kukimbilia nje hadi kwa mlinzi huku akihema juu juu, Yule mlinzi alimuuliza,
“Humo ndani sielewi”
“Huelewi nini?”
“Nimebaki peke yangu ila nakutana na ujumbe mezani, kila nikifanya nakuta ujumbe mwingine. Naogopa kwakweli”
Yule mlinzi alianza kucheka sana kisha akamuuliza,
“Kwahiyo wewe unahisi ni nini?”
“Nahisi labda ni jinni”
“Usinichekeshe wewe, hivi jini unalijua wewe? Ushawahi kuona jini?”
“Sijawahi”
“Sasa unaogopa nini?”
“Naona mambo ya ajabu, ukizingatia ndani nipo mwenyewe”
“Upo mwenyewe wapi wewe, fanya tu ujinga wako uone. Mama yupo ndani leo hajatoka”
Moza akapumua kidogo na kujiona kama mjinga, kwani alihisi mitego ya Yule mama iliendelea kwahiyo ikabidi ajipange na majibu kama mwenye nyumba akimuuliza.
Moza alirudi ndani sasa na kuanza kudeki, na alipomaliza Rose alitoka ndani na kwenda sebleni ila Moza hakuonyesha kushtushwa sababu ameshaambiwa na mlinzi kuwa Rose yupo ndani, huyu mama alimuangalia Moza na kumuuliza
“Mbona hujashtuka?”
“Nishtuke nini sasa mama?”
“Ushtuke kuniona”
“Sijashtuka sababu nilijua tu kuwa upo ndani”
“Umejuaje”
“Nilipoona ujumbe mara ya kwanza, na nilipoona mara ya pili nikajua tu kuwa upo ndani”
Rose akacheka kisha akamwambia Moza,
“Unajifanya mjanja eeh wakati ushafanya umbea kwanza, nilitaka leo kukufundisha kazi za kufanya maana ni uhakika hujui kazi za kufanya ndiomana unapata na muda wa kufanya umbea. Laiti kama ungekuwa na kazi za kufanya basi umbea usingefanya. Haya nenda kamwagilizie maua maji, na nikitoka nikute yamelowana haswaaa”
Moza alitoka nje na kwenda kufunga mpira na kuanza kumwagilia maua, wakati anamwagilia kuna sauti ikamtuma kupekua ua moja wapo, akahisi kama kuchimba mzizi wa lile ua. Ikabidi amwagilie kwanza ili pakilowana achimbe mzizi huo aone ni nini na kwanini hisia zake zinamtuma afanye hivyo.
Palivyolowana, akaitwa na Rose kwani Ana alikuwa tayari amesharudi. Moza alivyofika pale, akashangaa kumuona Ana akiwa amebeba mwenyewe begi lake halafu Yule mama alimwambia kwa ukali,
“Hivi Moza huoni mtoto anahangaika na begi, si umpokee”
Moza akataka kumpokea lile begi Ana, ila Ana akawa mkali sana na kumkatalia kisha akamwambia mama yake
“Hili lidada limbea sana, lisije likafungua begi langu bure. Siwezi kumruhusu tena abebe begi langu”
Ana akaondoka zake, Rose akamuangalia Moza na kumfokea pale,
“Unaona sasa faida ya umbea wako, hadi mwanangu hakutaki yani wewe sijui kama mwezi huu utamaliza humu ndani. Umbea wako utakuwa umekuponza, haya kaendelee na umwagiliaji huko, sasa ole wako nisikie unafanya umbea hadi kwenye maua yangu”
Moza akataka kutoka, wale mapacha nao walirudi na walikuwa wakilalamika njaa sana,
“Ila chakula nimeshaandaa mezani”
“Hivi wewe Moza si nishakwambia kaendelee na umwagiliaji, mtu gani wewe hujielewi. Kwani hawa wakilalamika njaa ni wanakulalamikia wewe? Wewe ndio unaetafuta chakula humu ndani au? Hebu nenda zako huko”
Moza akondoka kwa aibu maana hakutegemea kama muda huu huyu mama angesema hivi.
Alienda tena kwenye ile bustani ya maua na kuendelea kumwagilia,ila bado mawazo yake yalimtuma kwenye lile ua ili afukue mzizi ajue kuna nini ila akakumbuka ile sauti ya mwenye nyumba kuwa ole wako nisikie unafanya umbea kwenye maua yangu,ile kauli ikawa inamrudia ila akajisemea.
“Kwani mimi natafuta umbea au nataka kuangalia mizizi ya lile ua? Kwani kuangalia mizizi ni umbea nao? Hapana bhana si umbea, nataka tu kuridhisha roho yangu maana inanituma niangalie mizizi ya ua lile, mbona haujanionyesha ua lingine zaidi ya lile! Huu si umbea bhana”
Yani alikuwa anajihoji mwenyewe na kujijibu mwenyewe basi aliacha kumwagilia na kwenda kufukua, alipokuwa anafukua hakuona mizizi kama alivyodhani ila alichokiona alistaajabu sana kwani alikuta mfuko na kitu kimefungwa kama mpira akataka kukifungua ila akajua akifungua hapo atabambwa kwahiyo akakificha kwenye nguo zake ili akakifungue ndani akiingia chumbani kwake kulala.
Tangu amkificha kile kimfuko nguvu ya kumwagilia ilimuisha kabisa na akajisikia hamu ya kuangalia kuna nini ila akajikaza kuwa ataenda kuangalia ndani. Roho yake ikamtuma kuwa akipeleke chumbani kwake kabisa, basi akaacha tena kumwagilia na kuanza kutembea ili apelike ule mfuko ndani ila kadri alivyokuwa anatembea nguvu zilikuwa zinamuisha, yani mpaka anaingia chumbani kwake alianguka kabisa ndipo alipotoa ule mfuko haraka haraka, ila alipoutoa tu na kuutupia pembeni nguvu zake zilirejea tena na kumfanya awe na mashaka zaidi kuhusu ule mfuko,
“Kilichomo humu kwenye mfuko si kimpira kama ninavyodhani ila nadhani kuna kitu kingine haiwezekani nguvu ziniishe kiasi hiki, lazima niangalie kuwa ni nini”
Ila muda huo akaitwa na Sara na kumfanya ainuke na kwenda alipo Sara ambapo alienda moja kwa moja chumbani kwa Sara, alifikiwa na swali,
“Jana ulikuja na nani hapa nyumbani?”
“Jana?”
“Ndio jana, usijipumbaze”
“Aaah nilikuja na mtoto mmoja hivi anaitwa Salome”
“Ni nani huyo mtoto?”
“Kwani wewe kakwambia nani kama nilikuja nae?”
“Moza, unafikiri umbea unauweza peke yako tu? Usitake kujua kaniambia nani, ila nijibu huyo mtoto ni nani na anamahusiano gani na familia yetu?”
“Ila kwanini umeniuliza hivyo Sara?”
“Moza, usiniulize maswali ila nijibu nilichokuuliza”
“Kwakweli sijui nikujibu vipi hilo swali lako, ila Yule mtoto ni wa bosi wangu wa zamani yani mwanzoni nilikuwa nafanya kazi kwao. Nimekutana nae buchani sasa nikamlete ili apafahamu ninapoishi kwasasa”
“Mama anajua kama uliwahi kufanya kazi kwa mama wa huyo mtoto?”
“Hajui, kwani kuna uhusiano gani kati yenu na huyo mtoto?”
“Sitaki maswali Moza, ila hili swala lazima mama nimfikishie maana umemleta mtu bila ruhusa ya mama. Vipi baba alimuona?”
“Alimuona ndio wakati namsindikiza”
“Yani wewe Moza wewe unatafuta mabalaa ambayo huwezi kuyatatua. Sikia nikwambie ujue kama ulikuwa hujui, Yule mtoto aliwahi kusingiziwa baba kuwa mtoto wake yani ilitokea mtafaruku mkubwa sana hapa nyumbani. Kipindi hicho hadi mama akaanza kutafuta mtoto kwa haja zote ndio baada ya miaka kadhaa akampata Ana. Sasa mama ana hasira sana na familia ya Yule mtoto halafu wewe unaenda kumchukua na kumleta nyumbani”
“Lakini mimi nilikuwa siyajui yote hayo, na kama ndio hivyo mbona Salome hakuonyesha kama anapafahamu hapa?”
“Sikia Moza, kwanza Yule haitwi Salome nadhani hilo jina wamempa ukubwani. Alikuwa anaitwa Maria, mamake anapajua hapa vilivyo na hawezi kusogelea hapa. Yule mtoto hapajui hapa, usijaribu tena kumleta Yule mtoto kwenye nyumba hii”
“Lakini ningependa unieleweshe zaidi, mbona kafanana sana na baba”
“Moza Moza, naenda kukusemea kwa mama maana naona unazidi kuchokonoa mambo”
“Tafadhali, naomba unisamehe”
“Unamuogopa eeh”
“Ndio namuogopa”
“haya, kaendelee na shughuli zako”
Moza alitoka mule chumbani kwa Sara na kwenda jikoni kuosha vyombo ambavyo tayari walikuwa wamelia chakula, hapo akawaza tena kuhusu Salome kuwa Yule baba inasemekana kasingiziwa lakini inaonyesha wazi Salome ni mtoto wa Patrick, ila kwanini Patrick mwenyewe anauwalakini kuhusu mtoto wake huyo na kwanini Salome alibadilishwa jina kama ni kweli alibadilishwa jina, alitamani kujua kwa undani zaidi ambapo alijua wa kumjibu mwingine ni mama yake Salome ambaye ni Neema.
Alitamani apate muda wa kwenda kuzungumza na Neema ili ajue kwa undani zaidi,
“Lakini umbea huu loh hata kuacha sitamani, najikuta tu natamani kujua sijui nifanyeje masikini Moza mimi”
Kumbe maneno hayo aliongea kwa sauti ya kusikika, akasikia sauti ikimwambia, ilikuwa ni sauti ya Rose,
“Haya ni nini unachotamani kujua?”
Moza akashtuka na kumjibu kwa uoga uoga,
“Hakuna kitu mama”
“Usinichekeshe Moza, wakati nimekusikia kila kitu. Niambie unachotamani kukijua ili nikusaidie ukijue”
“Hakuna kitu mama”
“Hakuna kitu eeeh!”
“Ndio mama hakuna kitu”
“Mimi nakiona kipo”
Rose alimshika mkono Moza na kuanza kumkokota, kwakweli Moza alishikwa na uoga kwani moja kwa moja Rose alimpeleka Moza kwenye kile chumba chenye chumba kidogo ndani kisha akamwambia,
“Unataka kujua kilichopo mule eeeh!”
Moza alikuwa kimya tu,
“Najua unajiuliza kuwa ukubali au ukatae, huku moyo wako mwingine ukitamani kujua siri iliyomo kwenye chumba kile. Haya chukua funguo hapo juu”
Rose alimwambia Moza kwa kumkaripia ambapo Moza alichukua funguo huku akitetemeka,
“Haya fungua sasa”
Moza alianza kufungua huku akitetemeka kwani alihisi kama hapelekwi nay eye kwenye chumba hiko basi ataona vitu vya ajabu, ila leo tofauti na siku ile aliyotaka kuchungulia kwani alipigwa na shoti ila leo hakupigwa na cheche yoyote. Na alipofungua tu alijiona yupo nje,
“Umeona sasa, huu ni mlango wa kutoka nje. Sasa wewe ulikuwa unafikiria ni nini?”
“Hapana mama, sijafikiria chochote”
“Haya tuzunguke tukaingie ndani”
Wakazunguka na kuingia ndani tena, kisha Rose akamuuliza moza,
“Sasa una amani eeh”
Moza aliitikia kwa kichwa tu kuwa ameridhika, Rose alicheka na kumuacha moza anaenda jikoni ambapo alienda kumalizia vile vyombo vyake ila alikuwa na mawazo mengi sana.
Moza aliingia chumbani kwake ila bado alikuwa na maswali mengi sana, kwanza kabisa alijiuliza kuhusu chumba alichopelekwa ambacho mlango wa ndani ulimtoa nje,
“Mmmh huyu mama hajanifanyia mtego kweli, mbona kama chumba sio kile? Nahisi kanifanyia mchezo Yule mama lakini kwanini anifanyie mchezo wakati mimi si chochote wala lolote kwenye hii familia”
Wazo lingine likamjia ni kuhusu Ana maana siku hizi Ana hakutaka kitu chochote afanyiwe na Moza jambo ambalo lilimchanganya pia. Wakati anawaza hayo, mlango wake uligongwa alipoenda kufungua alimkuta mama mwenye nyumba ambaye alimwambia
“Dawa yako inachemka”
Huyu mama akaondoka, Moza akatoka na kwenda jikoni huku akiangalia hiyo dawa aliyoambiwa inachemka iko wapi maana hakubandika dawa yoyote kwahiyo ule usemi wa dawa yako inachemka kwa muda huo hakuelewa alijua ni dawa kweli.
Moza alivyoona hakuna dawa inayochemka alirudi tena chumbani,muda huu akili ikamtuma achunguze ule mfuko alioutoa kwenye maua. Akuchukua ule mfuko na kuanza kuuchunguza kwa kuufunua ambapo kweli alikuta kama mpira wa makaratasi umefungwa fungwa. Moza akaanza kufungua ila kadri alivyofungua ndivyo nguvu zilivyomuisha, hadi mwishoni akaanguka kabisa na kuwa kimya hapo hapo.
Itaendelea kesho usiku kama kawaida…..!!!!!!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: