Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 3
Hapo akazimia, na lilipita lisaa limoja akazinduka akiwa amechoka sana, akajaribu kuinuka akaweza, kisha akatoka na kufunga mlango halafu funguo akazirudishia pale pale juu. Akaelekea sebleni sasa, Mara akakutana na mama mwenye nyumba nae anaingia sebleni kutoka nje akiwa na hasira sana. Alikuwa anahema juu juu, akamsogelea Moza na kumuuliza kwa ukali
“Umefanya nini?”
“Sijafanya chochote mama”
Rose alimuacha Moza pale sebleni na kuelekea mitaa ya chumbani ambapo moja kwa moja alielekea kwenye kile chumba, Moza alienda jikoni huku uoga ukiwa umemshika na kuomba kuwa huyu mama asijue kama aliingia mule chumbani. Ingawa moza alikuwa kamaliza kupika ila alikaa tu jikoni akiwaza, muda kidogo Rose alirudi sebleni na kumuita Moza kwa ukali, kitendo ambacho kilimuogopesha Moza na kuhisi kuwa pengine Rose amegundua. Alienda sebleni kwa uoga kiasi, kisha huyu mama akamuuliza,
“Baba aliamka toka ameenda kulala?”
“Hapana mama, toka muda ule sijamuona tena sebleni?”
“Sikia Moza, naomba vitu vya nyumba hii uviache kama vilivyo”
“Ila sijafanya kitu mama”
“Nilikuwa mbali sana, ila kuna kitu kimefanyika ndani nimepata taarifa ndiomana nikaja haraka sana. Ila kwavile umesema hujafanya kitu, basi. Hata hivyo hicho kitu ambacho nilikuwa nakihisi kuwa umekifanya basi muda huu ningekukuta na hali mbaya sana. Tafadhali Moza, vitu vya nyumba hii viache kama vilivyo. Unaweza ukanishangaa kuwa mbona narudia rudia msemo wangu, nina maana kabisa, viache kama vilivyo”
“Sawa mama nimekuelewa”
“Na sitoki tena saivi,ngoja nikapumzike tu. Nipikie ugali na samaki, nitakula nikiamka”
Moza alienda jikoni kuandaa huo ugali huku akiwaza kuwa amepona ila aliwaza ameponapona vipi bila kubambwa ingawa alizimia kwa karibu lisaa lizima, pia akawaza kuwa huyu mama kapata vipi taarifa huko alipokuwa kwamba ule mlango ulishikwa? Hapo kidogo akapatwa na uoga, akawa tu anajisemea mwenyewe
“Mimi Moza mimi jamani nitulie tu, kwetu nakupenda pia. Nitakuwa sirudi mmmh”
Alipomaliza alienda chumbani mara moja.
Alipoingia chumbani alijiweka kitandani, mara usingizi ukampitia. Akaanza kuona kama anaingia tena kwenye kile chumba, kisha anafungua mlango wa kile choo ila mule aliwakuta wadada watano wakiwa wamechoka sana, ni wadada walewale ambao walikuwa wakimuomba msaada kwenye ndoto ya jana yake. Kwahiyo ndoto hii ilikuwa kama muendelezo wa ile ndoto ya usiku ila ndoto hii ilikuja kivingine. Wakati anawashangaa wale wadada, halafu akawa kama anataka kuwahoji, mara gafla akasikia sauti ikiita…
“Moza, Mozaa…”
Akashtuka kutoka usingizini na aliposikiliza vizuri ilikuwa ni sauti ya Ana, ikabidi atoke haraka kwani alitambua itakuwa Ana amerudi shuleni. Moza alivyofika sebleni akamkuta Ana amekaa na amevimba kwa hasira, ilibidi Moza aanze kwa kumuomba msamaha
“Nisamehe Ana, nilipitiwa na usingizi kidogo”
“Umekuja kulala au kufanya kazi, yani mimi nakuita muda wote huitiki, haya piga magoti”
Moza hakubisha alipiga magoti, kisha Ana akamwambia,
“Nivue viatu”
Moza alimvua Ana viatu, kisha akanza kumsikiliza ujumbe mwingine
“Begi langu la madaftari nimeliacha pale getini kwa mlinzi kalichukue unipelekee chumbani.”
Moza alienda kwa mlinzi kuchukua begi, Yule mlinzi akamwambia Moza
“Usisubiri siku nyingine akukumbushe, yani akirudi tu uje uchukue begi lake. Yeye hawezi kubeba eti ni zito”
Moza aliondoka na lile begi hadi chumbani kwa Ana akagonga na kuruhusiwa kuingia, kisha akaenda kuliweka lile begi. Ana akamwambia Moza,
“Nipikie tambi na mayai, nataka kula hivyo leo”
Moza aliitikia kisha akaenda jikoni kuandaa huku akiwaza moyoni,
“Hivi mimi ni mfanyakazi wa ndani au ni mfanyakazi wa hotelini? Mmmh hii nyumba unaweza kujikuta siku nzima unapika tu”
Aliwaza Moza huku akifikiria kutoweza kufikisha hata miezi miwili humo ndani,
“Kazi za humu ni za kitumwa sana, yani mwezi huu ukiisha tu nipate mshahara wangu nirudi kwetu nikaangalie ustaarabu mwingine”
Alipika na alipomaliza, alitoka nje na moja kwa moja alienda getini kwa mlinzi, kisha akamuuliza
“Kaka samahani, hivi wewe una muda gani toka uanze kulinda hapa?”
Huyu mlinzi akacheka kwanza, kisha akamwambia
“Ni kitambo sana, kabla huyo Ana hajazaliwa. Mimi nipo hapa, yani huyo Ana anakuwa namuona”
“Kheee kumbe! Mbona nasikia wafanyakazi wa hapa hawakai yani wanafukuzwaga”
“Ni wa huko ndani sio mimi, ni sababu hawawezi kufatilia sheria za huyu mama. Mfanyakazi ambaye alikaa hapa kwa muda mrefu ni mmoja tu, ambaye anaitwa Ashura. Yeye peke yake ndio alikaa hapa kwa muda mrefu na aliondoka mwenyewe ila ni mtu mwenye siri nzito sana”
“Yuko wapi huyo Ashura?”
“Dada, tambua kwamba unaongea na mwanaume. Nimekaa kwa muda mrefu kwenye nyumba hii sababu mimi ni mwanaume. Mambo ya umbea sifanyi. Naomba kaendelee na kazi zako”
Moza aligeuka nyuma akamuona mama mwenye nyumba amesimama, ikabidi Moza aende upesi kumsikiliza,
“Kule getini unatafuta nini?”
“Nilikuwa namuuliza mlinzi masoko yalipo kwa hapa”
“Yule mwanaume na mambo ya masoko ni wapi na wapi? Moza, chunga sana nakuangalia ujue nakuangalia sana, huo mwenendo wako sijui kama tutawezana. Haya kaniwekee chakula mie”
Moza aliingia ndani, kisha Yule mama alienda kwa mlinzi, inaonyesha alienda kumuuliza pia kilichompeleka Moza pale getini.
Moza alipomaliza kuandaa, Yule mama aliingia na kukaa mezani, kisha akamwambia Moza
“Una bahati sana, Yule mlinzi kaniambia ni kweli ulikuwa unamuuliza kuhusu masoko. Vinginevyo ungenitambua. Haya kaniitie kipenzi changu Ana nije kula nae”
Moza aliondoka kwenda kumuita Ana huku akijiuliza, Yule mlinzi kama amepanga nae vile, imekuwaje nae amesema kama yeye kuwa alikuwa anaulizia masoko, yani kama alikuwa kwenye akili ya Moza.
Kma kawaida aligonga kwa Ana na kumuita ambapo aliitikia wito na kwenda sebleni, kisha akamwambia Moza amletee chakula chake, ambapo Moza akafanya hivyo. Rose alipoona mwanae ameletewa kile chakula akasema,
“Oooh kipenzi changu leo umetaka tambi na mayai”
“Ndio mama, kuna sehemu nimeona picha nikatamani”
Kisha Rose akamuita Moza na kumuuliza,
“Wengine umewaandalia chakula gani?”
“Dada Sara amesema nimuandalie chapati na rosti ya maini, wale mapacha wamesema niwaandalie chakula chochote kizuri. Kwahiyo nao nimewaandalia chapati na rosti ya maini. Ila kuhusu baba nilimuuliza Dada Sara akasema anapendeleaga ugali kwahiyo nae nimemuandalia ugali”
“Wewe Moza wewe, hizo habari sijui za dada Sara sijui mapacha sitaki kuzisikia, sijui baba sitaki kusikia. Hao wote wanakula chakula ninachosema mimi. Mwenye amri humu ndani ni mimi tu, na Ana. Kwahiyo chakula ukiambiwa ukiandae na Ana, fanya upesi au mimi nikikwambia uharakishe ila usiniletee hayo madudu mengine.”
“Lakini si watoto wako pia?”
“Wewe, wewe, weeee msichana wewe usitafute maneno yani naona unachokonoa chokonoa mambo. Kwani wakiwa watoto wangu ndio nini sasa? Wawe na amri kwani nyumba yao hii? Tena sitaki kusikia. Mwenye amri humu ndani ni mimi na Ana tu nimemaliza”
Moza aliitikia na kwenda zake jikoni huku akijiuliza maswali mengi sana bila ya majibu, na haswa ni kuhusu baba mwenye nyumba, masikini toka alipoambiwa akalale hajapewa amri ya kuamka hadi muda ule.
Moza akiwa kule jikoni, Yule mama alimuita kutoa vyombo kisha akamwambia,
“Siku nyingine sio mpaka nikuite kutoa vyombo, unatakiwa kujiongeza mwenyewe.”
“Sawa mama”
Moza alitoa vile vyombo ila alihisi kama Ana na mama yake wana maongezi ya ishara ambayo yeye hakuyaelewa moja kwa moja, na muda kidogo Ana na mama yake wakatoka yani wakaondoka kabisa hapo nyumbani ila muda huu hata hawakumuaga wala hawakumwambia kama wanatoka, kwahiyo Moza alibaki akishangaa tu mwenendo wa watu kwenye nyumba ile ila akajisemea kuwa atazoea tu.
Muda si muda akarudi Sara na alionekana kuwa amechoka sana, Moza alimkaribisha na kumpa pole
“Pole na mizunguko dada Sara”
“Asante, yani ni mizunguko haswaa. Vipi mama karudi?”
“Ndio alirudi ila ameondoka tena”
“Kheeee alirudi duh! Aliniambia kuwa leo atachelewa sana kurudi kumbe alisharudi mmmh huyu mama nae. Kwahiyo kaenda wapi sasa?”
“Sijui ila kaondoka na Ana”
“Yani mama na Ana mmh! Ngoja nikaoge mie uniandalie chakula changu”
Sara aliondoka zake ila Moza alitamani amdadisi na Sara pia ili aujue undani wa familia ile.
Kwenye mida ya saa tatu usiku, wale mapacha nao walirudi na cha kwanza kabisa waliulizia chakula ambapo Moza aliwaandalia, pacha mmoja akaulizia kuhusu mama yao na Moza aliwapa taarifa kama aliyompa Sara, kisha Yule pacha akamuuliza kuhusu baba yao, mwenzie akamkatisha
“Sasa unamuulizia wa nini huyo?”
“Ni binadamu mwenzetu Kulwa, eti baba yuko wapi?”
“Kalala”
“Kalala saa hizi?”
“Hapana, ni tangu asubuhi mama alipomwambia akalale hajaamka tena”
“Duh”
Yule pacha akainuka pale mezani, Moza alitulia tu akiangalia picha inavyoendelea, baada ya muda Yule Dotto akarudi na Mr.Patrick na kumkaribisha mezani pia, ambapo Yule mzee alikula kama anakimbizwa, baada ya hapo Yule pacha akaongozana na Yule baba na kumrudisha tena chumbani kisha yeye akarudi sebleni. Yule Kulwa nae alikuwa ameshamaliza kula, akamwambia mwenzie
“Mama akigundua hili sijui utamwelezaje?”
“Vyovyote vile, Yule ni mwanaume mwenzetu, najua hata wewe hupendi kufanyiwa vile ila sababu unamuogopa mama”
Wakaondoka na kuelekea chumbani, Moza alitoa vyombo haraka haraka ili aende dirishani akawasikilize pia, na kweli alipoenda dirishani aliwakuta bado wana mada za Yule baba,
“Nimekuuliza Kulwa, unapenda anavyofanyiwa Yule baba?”
“Sipendi, lakini sina cha kufanya”
“Cha kufanya kipo ila hatujakifikiria”
“Kipi hicho?”
“Nahisi tutakigundua pindi huyu baba akifa”
“Hivi unadhani mama atamuachia huyu baba afe? Anamtesa tu, hajafikia hali ya ukatili kiasi hicho”
“Ila kwa nini mama yetu yupo hivi? Yani nawazaga hata sipati jibu”
“Hata mimi mwenyewe sijui halafu sasa yani mimi na wewe ni kwavile tu ni watoto wake ila mama hatupendi pia, labda baba yetu alimfanya vibaya mama. Yeye kipenzi chake anaanza Ana halafu anafatia Sara, yani mama sisi hatupendi kabisa”
“Ila kuna kitu nahisi kuhusu mama”
“Kipi hicho?”
Sauti ya Sara ikasikika akimuita Moza, naye Moza aliamua kwenda kimya kimya kwani alijua akiitika tu atawashtua wale mapacha.
Alivyofika kwa Sara,
“Inamaana mama bado hajarudi?”
“Hajarudi ndio”
“Nilitaka nimpe taarifa”
“Taarifa gani?”
“Leo nimekutana na Ashura, humjui wewe yani Yule mdada mama anamtafutaga sana. Ngoja nikuonyeshe picha yake nimepiga nae leo”
Sara akatoa simu yake na kumuonyesha Moza picha ya Ashura, ila Moza alishtuka kidogo sema alijigelesha ili Sara asigundue mshtuko wake.
Kisha Sara akamwambia Moza,
”Yani huyu Ashura alikuwa mzuri sana, halafu hata hakufanania na kazi za ndani. Alikuwa mpole na mkimya. Ni yeye tu aliweza kuishi kwa muda mrefu kwenye nyumba hii akifanya kazi za ndani ila baada yeye kuondoka hakuna tena msichana aliyeweza kuishi kwa muda mrefu hapa. Mmmh halafu sijui hata ni kwanini nakuambia yote haya, nenda kaendelee na shughuli zako Moza”
Moza alitoka pale na kwenda jikoni kusafisha vyombo huku akifikiria kuhusu Ashura,
“Mbona namjua Yule, alikuwa akifanya kazi za ndani duh! Si nimefanya kazi kwao Yule! Hapa lazima kuna kitu”
Moza alimaliza shughuli zote, kwenye saa sita kasoro ndipo Rose na mwanae Ana walirejea na kama kawaida Moza alipewa amri ya kwenda kutandika kitanda cha Ana.
Wakati anatandika kitanda cha Ana akasikia kama sauti inamwambia afunue godoro, wakati anataka kufunua mara Ana akaingia ndani na kumuuliza kwa ukali,
“Unafanya nini?”
Moza alipatwa na bumbuwazi tu, alishikwa na kigugumizi asiweze kujibu, mara Ana akamsogelea na kumzabua kofi.
Itaendelea kesho usiku……………!!!!!!!!!!!!!!!!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: