KURUDI KWA MOZA 2: Usiku wake Moza alishangaa yule mama akimuita kwa ukali sana, "Wee Moza wewe" Moza alishangaa kuitwa kwa ukali vile na kwenda kwa haraka sana, alivyofika pale tu cha kwanza alipigwa kofi hadi chini, akamtazama yule mama aliyeonekana na hasira sana, kisha yule mama akamuuliza Moza, "Maswali gani ya kijinga hayo unamuuliza mwanangu?" Moza alikuwa kimya alishindwa kujibu maana hakujua ubaya wa swali lake kwa yule mtoto ukizingatia anaonekana ni binti tayari wa karibia miaka kumi na mbili. Moza alibaki akishangaa tu, mara kibao kingine akapigwa, kasha Yule mama akamwambia, “Si nilishasema mambo ya udadisi kwenye nyumba yangu sitaki, huyu mtoto asipoweza kutandika kitanda wewe inakuhusu nini? Inamaana wewe ndio unajua kulea sana au, mambo ya mtoto wangu hayakuhusu. Kama hajui kufanya kazi yoyote mwache tu kama alivyo, nimekuajili wewe sio uje kukaa tu na kuuliza uliza maswali ya kijinga. Sitaki, na ninakwambia sitaki kabisa huo upuuzi na nisisikie tena” Ikabidi Moza amwombe msamaha mama huyu, “Nisamehe mama, kwakweli haitajirudia tena. Naomba nisamehe. Nisamehe sana” “Mimi sio wa kuniomba msamaha, nenda kamuombe msamaha Ana huko” “Lakini Ana nilishamuomba msamaha” “Mpaka kaniambia mimi inamaana hajakusamehe, nenda kamuombe msamaha tena mpaka akusamehe ndio uje hapa. Na asipokusamehe jiandae kurudi kijijini kwenu” Moza akaondoka taratibu mpaka chumbani kwa Ana akaingia na kumuamsha kasha kuanza kumuomba msamaha, Ana akamuangalia Moza akamsonya kasha akamwambia, “Hivi unaingiaje chumbani kwangu bila ya hodi, hujui kugonga hodi au? Halafu unaniombaje msamaha huku umesimama kama mlingoti? Toka nje huko, ugonge mlango nikuruhusu kuingia kasha uje na magoti ndio uniombe msamaha” Moza akatoka nje na kugonga mlango, aliporuhusiwa na Ana alipiga magoti, akaingia chumbani kwa Ana na magoti kisha akamuomba msamaha, Ana alicheka kasha akamwambia, “Nimekusmehe ila siku nyingine usirudie tena. Nilijua na wewe ni kiburi kama waliopita. Haya ondoka zako” “Asante Ana” Moza alitoka huku macho chini, alienda kumalizia kazi zake kasha akaenda kulala. Alipokuwa chumbani aliwaza sana, na kujisemea “Jamani umasikini huu loh, yani mimi kweli wa kudhalilishwa na yule mtoto mdogo jamani? Yule si sawa na mtoto wa dadangu jamani, yani kanidhalilisha nimpigie magoti nimuombe msamaha, yote haya ni sababu ya umasikini tu. Ningekuwa na uwezo au kwetu kungekuwa na uwezo yasingenipata yote haya, ila wadada wengi wa kazi tunateseka sababu ya umasikini.” Alijifikiria sana, ila aliamua kulala ili kesho awahi kuanza usafi na shughuli zingine. Akiwa kwenye usingizi mzito wakati panakaribia na kukucha akajikuta yupo kwenye ndoto nzito sana, alijiona yupo mahali halafu kuna wadada kama watano wapo pande ya pili wakimuomba msaada, akawa anasikia kelele, “Moza tusaidie, Moza tusaidie tafadhari,Moza ni wewe tu unaeweza kutusaidia” Wakati anataka kwenda kuwasaidia akashtuka kutoka usingizini, alikaa akitafakari kuwa ni ndoto ya aina gani ile. Lakini alipoangalia saa aliona karibu panakucha, alitoka chumbani na kwenda kuanza shughuli za usafi, alishangaa kumkuta baba mwenye nyumba yani Mr.Patrick akiwa sebleni muda ule amesinzia, hakutaka kuhoji kwani taratibu za nyumba ile bado hakuzijua vizuri kwahiyo alianza tu kufanya kazi zake hadi muda wanaamka wengine na kujiandaa kutoka huku wengine wakisubiria chai mezani ikabidi awaandalie. Siku hiyo Ana alichelewa kuamka, ila kwavile hakujua taratibu za nyumba ile alijua ndio kawaida, mama mwenye nyumba aliamka na kumfata Moza jikoni, “Umeshamuamsha mtoto aende shule?” “Mtoto yupi mama? Kwanza shikamoo” “Nitolee uwendawazimu wako mie, inamaana humuoni Ana kuwa ni mtoto! Kwahiyo hujamuamsha hadi muda huu unategemea nini? Mwanangu haendi shule, au ulijua hasomi kama watoto wa kijijini kwenu? Haya nenda kamuamshe na utaenda nae shule, wewe ndio utamtetea kuchelewa kwake” Moza hakubisha ila alienda hadi chumbani kwa Ana, ila alipofika mlangoni akasita kuingia maana jana yake huyo Ana alimfokea kwa kitendo cha kuingia bila ya hodi. Ikabidi aanze kugonga hodi, aligonga na kugonga na kugonga ila hakuitikiwa akawa anajishauri tu kuwa afanyaje, wakati anajishauri, Sara alipita pale na kumkuta anagonga, “Weee huyo mtoto analalaga kama pono, yani hapo utagonga hadi vidole viote sugu. Ingia tu umuamshe” Moza akamwambia Sara, “Lakini jana alinikataza kuingia chumbani kwake bila ya hodi” “kitoto kina amri sana hicho sijui kwanini, ila ingia tu. La sivyo atazidi kuchelewa shuleni” Ikabidi Moza aingie huku akiwa na hofu ya kufokewa na Ana. Akaanza kumuamsha kwa utaratibu, “Ana, amka uende shule mtoto mzuri” Ana alimka, kasha akatabasamu baada ya kuamka, na kumwambia Moza “Kaniwekee maji ya kuoga nioge halafu niandalie na sare kabisa” Moza alimuandalia huku akimsikiliza kuwa ni nguo gani amuandalie kasha Ana akaenda kuoga na kuvaa, baada ya kumaliza ilitakiwa Moza ndio ampeleke Ana shuleni, akatoka sebleni na kumkuta mama na baba, “Mama, ndio nataka kumpeleka Ana shuleni” “Si umpeleke, unataka mimi nifanyeje?” “Nampelekaje mama?” “Hivi si uzembe wako, gari ya shule imemuacha? Mpeleke sasa utajua wewe utampelekaje” Moza akajifikiria akakosa jibu, mjini kwenyewe hajawahi kuishi kivile sasa ni njia gani atampeleka huyo mtoto shuleni ikiwa hata shule ilipo hajui, wakati anawaza hayo akamsikia Yule baba mwenye nyumba akisema, “Naomba niwapeleke mke wangu, nipe ruhusa yako.” “Si mafuta yako hayana kazi” “Ila mke wangu, huyu mdada bado ni mgeni” “Bhana wee wapeleke ila ndio ajifunze sio kesho tena amuache mtoto alale mpaka muda huu. Na hakikisha unaenda kumtetea mtoto kwa walimu. Tumeelewana Moza?” “Ndio mama” Kisha, Moza, Ana na Mr.Patrick wakatoka na kuelekea kwenye gari la Mr.Patrick halafu safari ya shule ikaanza. Walipofika shuleni, Moza alishuka na Ana hadi kwa walimu wake, ambapo mwalimu mmoja akasikika akisema “Ana umechelewa na leo ila kama kawaida yako umeletwa na mtetezi. Haya dada tunashukuru kwa kumleta Ana, nenda tu. aAna nenda darasani” Moza alimshukuru pale kasha akarudi kwenye gari na safari ya kurudi nyumbani ikaanza, huyu baba alimuuliza Ana, “Hivi kitu gani kilifanya uje kufanya kazi pale kwetu?” “Nilikuwa natafuta kazi tu ndio nikapata pale” “Unajua kama ukiingia pale hutoki?” “Sitoki kivipi?” “Yani huwezi kurudi kwenu” “Kivipi baba mbona sijakuelewa?” “Ile nyumba nilijenga mwenyewe kwa mikono yangu, kwa hela zangu ila hata mimi kutoka siwezi. Nafahamu vingi ila sina ufahamu wa kutoka” Moza akajikuta akivutiwa sana na mazungumzo haya, huku akimuuliza Yule baba kwa makini, “Hebu nieleweshe vizuri baba, nasikia wafanyakazi waliotangulia mama aliwafukuza sasa sijui walifukuzwa kwa nini?” “Hawajafukuzwa ila walipo hata mimi sijui na mke wangu hajanipa nafasi ya kujua. Nimechagua leo kukusindikiza ili nikwambie haya. Nakuona huna hatia, ila umeingia sehemu sio yenyewe. Mimi ni baba mwenye akili zangu timamu kabisa lakini zipo kama hazipo. Nina mtoto ambaye ni damu yangu kabisa, naamini ni damu yangu ila mke wangu huyu ananiaminisha kuwa Yule mtoto si damu yangu” “Yuko wapi huyo mtoto? Je ni mmoja kati ya waliopo nyumbani?” “Hapana si mmoja wao, yupo kwa mamake anaitwa. Yani Yule mtoto ni damu yangu kabisa ila mke wangu hataki kumuona wala hataki niwasaidie. Ujana umeniponza mimi, mwanangu anapata shida huko alipo ila kumsaidia siwezi. Kwa wale waliopo nyumbani, siamini hata mmoja kuwa ni mwanangu, wale watatu nilimkuta nao mke wangu ila huyu Ana amezaa akiwa na mimi. Ila siamini kama ni mwanangu kwani kuna mwanaume alishaletwa nyumbani, na mke wangu alikuwa anamuita baba Ana halafu Ana nae alikuwa anamuita huyo mwanaume baba” “Baba, yani sielewi kabisa. Na kwanini umeniambia yote haya?” “Nimejisikia tu kukwambia, kisha kuwa makini sana. Ila mke wangu sijue kama nimekwambia, usithubutu kuongea chochote na kumuonyesha kama kuna jambo nimekwambia. Mimi siendi sehemu nyingine mpaka aniruhusu yeye. Ningepata mtu wa kunisaidia, kunitoa kwenye hiki kifungo ningefurahi sana” “Pole sana baba” “Tafadhali usiseme, nakuomba usiseme. Utapotea” Gari ikaingia ndani, kisha kimya kilitanda na wakashuka garini, moza alipoingia ndani alimkuta Yule mama akijiandaa kuondoka ila kabla hajatoka alimwambia, “Haya mume wangu umesharudi naomba ukalale hadi nitakapokuja” Yule baba hakupinga, alienda moja kwa moja chumbani kisha Yule mama akamuangalia moza na kusema, “Kama nilivyokwambia, kuwa makini. Mambo ya umbea kwenye nyumba yangu sitaki” Yule mama akatoka zake, na Moza akaenda kwenye shughuli zake zingine. Akiwa jikoni, walikuja wale mapacha na kumuaga pia, “Sie tunatoka, sasa ukipika vyakula kama vya kijijini kwenu utakula mwenyewe” Wakaondoka zao, na muda kidogo akaja Sara nae na kusema, “Leo nina hamu na maini rosti na chapati na juisi. Tafadhali nitengenezee hivyo, nikirudi nitakula maana nataka kutoka” “kwahiyo ndio niandae chakula hicho leo?” “Sijui wengine wanapenda nini, kwani mama hajakwambia anachotaka leo?” “Hajasema” “Basi mkaangie samaki, mwekeena viungo. Mama anapendaga samaki sana” “Na chakula gani sasa?” “Utamuwekea na hizo chapatti, anapenda pia. Ila Ana anapenda wali, yani fanya ufanyavyo ila wali usikose. Halafu baba anapenda ugali, ila baba usimjali sana maana atakachosema mama atakula tu. Mimi ndio natoka hivyo, tuitaonana badae” Sara akaondoka zake, yani moza kabaki tu anajiuliza, “Humu ndani kama hotelini, yani kila mtu anaagizaa chakula anachotaka yeye yani nitakonda humu. Ila umaskini huu loh, ndio umesababisha yote haya. Ila wale mapacha hawajasema ni chakula gani, natumaini nao watakula maini rosti na chapati.” Moza alianza kuandaa mapishi yake huku akijikuta anamfikiria sana Yule baba, yani maisha ya Yule baba yalimsikitisha sana, hakuwa na kauli yoyote kwa mkewe na alimsikiliza mkewe kwa chochote alichomwambia. Wakati anaendelea na mapishi, roho yake ikamtuma aende kwenye kile chumba ambacho kinaonekana kina choo ndani kilchofungwa, “Mmh mama akinikuta kwenye kile chumba, nitamwambia nilikuwa nafanya usafi. Ngoja niende” Alipomaliza tu kuandaa chakula, moja kwa moja akaenda kwenye kile chumba na kuchukua ufunguo juu ya mlango kisha akafungua na kuingia ndani. Ila mawazo yake yalikuwa ni kwenye mlango wenye kufuri basi huku akijiuliza kama ule mlango unatoka nje mbona kwa nje hauoni? Akajisogeza moja kwa moja huku akihisi kuwa huenda akishika kufuli unaweza kufunguka, basi Moza akasogelea na kushika lile kufuli gafla alipigwa na shoti ya ajabu na kutupwa kabisa. Hapo akazimia, na lilipita lisaa limoja akazinduka akiwa amechoka sana, akajaribu kuinuka akaweza, kisha akatoka na kufunga mlango halafu funguo akazirudishia pale pale juu. Akaelekea sebleni sasa, Mara akakutana na mama mwenye nyumba nae anaingia sebleni kutoka nje akiwa na hasira sana. Itaendelea kesho usiku………… Nitakuwa naipost usiku kutokana na majukumu yangu wadau.... Napata muda usiku kwa sana.

at 2:29 AM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top