Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 23
Rose aliafikiana na mwanae na kujilaumu kuwa kwanini walikuwa wakijichelewesha wakati kuna njia rahisi ya kufanya, basi wakatoka mule chumbani kwa Moza na kuelekea chumbani kwa Ana walipofika walishangaa kumuona mtu amekaa kitandani kwa Ana halafu mtu huyo akawaangalia na kuwafanya wagundue kuwa ni Moza.
Kwa mara ya kwanza Ana alishikwa na uoga ambao hajawahi kuupata kabla, wakafunga mlango haraka haraka na huku wakihema juu juu, hakuna aliyeelewa kwa wakati ule ila wakajikuta tu wanaenda tena chumbani kwa Moza, ila kwa wakati huu napo walimkuta amekaa kitandani, katika siku zote leo mkojo ulimtoka Ana kwa uoga walifunga tena mlango na kukimbilia sebleni huku wakihema juu juu na wakikumbatiana mama na mtoto, kwa wakati huo hakuna uchawi walioweza kuufanya maana uwepo wa Moza uliwachanganya kuwa ni mzimu au ni kitu gani. Hata sebleni hawakuweza kukaa sana kwa uoga wakafungua mlango na kukimbilia nje. Kitendo hiki kilimshtua pia mlinzi aliyekuwa kalala, aliamka na kwenda kuwauliza kuwa tatizo ni nini, Ana alijikuta akiropoka,
“Kuna mzimu ndani”
“Mzimu!”
“Ndio, kuna mzimu wa Moza”
Gafla wakahisi kama eneo hilo linatingishwa yani kama mtu anatingisha ardhi, kisha wote wakazimia. Rose, Ana na mlinzi wao.
Kulipokucha, wale mapacha waliamka na kujiandaa kutoka kama kawaida na wazo lao walihisi kumkuta mama yao sebleni ila hawakumkuta, muda kidogo Sara nae akatoka na kuwauliza kaka zake,
“Eti mama ameshaondoka?”
“Sijui, sisi wenyewe hatujamkuta hapa sebleni”
“Nimeenda kumuangalia chumbani kwake nimemkosa, sijui atakuwa wapi”
“Sie tunaondoka bhana”
“Nisubirini, yani jumba lote hili mniache peke yangu”
“Mbona zamani ulikuwa unaweza kubaki peke yako!”
“Ushasema zamani, siku hizi mambo yamebadilika. Nisubirini bhana”
Wakamsubiri dada yao ajiandae, alipomaliza akatoka kisha wakatoka nje ili kuondoka ila wakashangaa walipotoka kumuona mama yao, mdogo wao na mlinzi wakiwa chini wamelala maana walipowaamsha waliamka na kushangaa sana, Sara alimuuliza mama yake,
“Imekuwaje mama?”
“Sina jibu kwasasa”
Yule mlinzi aliinuka na kwenda kwenye lindo lake, kisha Rose na Ana waliinuka na kwenda ndani. Ila muda huo Rose aliwaomba wanae wasiondoke wamsubiri kwanza, ikabidi wamsubiri kwani hakuna aliyekuwa anajua kuwa mama yao amepatwa na nini.
Wakati ameenda kujiandaa walienda kumuuliza mlinzi kuwa ni kitu gani kimetokea,
“Hata mimi sielewi”
“Huelewi kivipi?”
“Yani sielewi sijui hata imekuwaje mpaka nimelala pale”
“Kwahiyo hujui ni kitu gani kilitokea?”
“Sijui kweli yani sijui kabisa”
Wakamuacha na kurudi ndani wakimsubiri mama yao na Ana. Baada ya muda kidogo mama yao akatoka, na swali la kwanza alimuuliza Sara,
“Salome mbona sijamuona kaenda wapi?”
“Aliondoka jana na hakurudi tena”
“Aaah sawa, jamani leo mkitoka nawaomba muda wa kurudi msubiri hadi niwapigie simu, asirudi yeyote hapa ndani hadi niwapigie simu. Mimi na Ana kuna mahali tunaenda”
Watoto wake wakatazamana maana hawakuona kama lile jambo lilikuwa na umuhimu kiasi cha wao kurudishwa wasiondoke kwa muda huo na wasubirie maana angeweza hata kuwapigia simu na kuwapa ujumbe huo, baada ya maongezi hayo nyumba nzima wakatoka, kwakweli Rose hakuwa hata na muda wa kuulizia kuhusu Patrick kwani kadri siku zilivyoenda mbele ndivyo akili yake ilivyozidi kuchanganyikiwa.
Rose alikuwa na mwanae kwenye gari na safari ilikuwa ni kwenda kwa mganga,
“Kwahiyo mama tunaenda kwa mganga yupi?”
“Kuna mganga alikuwa ananisaidia sana, ila yupo mbali yani gari haifiki kule anapoishi. Hapa itabidi tuache gari mahali halafu tuanze kukanyaga kwenda, huyo ni kiboko najua atatusaidia na hili jinamizi la Moza”
“Kwahiyo mama kwa huyo mganga ni mbali hivyo, bora ungeenda mwenyewe tu mi nitachoka kutembea”
“Mwanangu usichoke, nitawaomba hata watu wakubebe maana ukiwa na pesa kila kitu kinawezekana”
“Sawa mama, ila una uhakika atatusaidia huyo? Hivi mama hukuwahi kufikiria mambo kama haya?”
“Kwanza sijawahi kufikiria kama kuna mtu angeiona ile dawa niliyoichimbia chini kwenye lile ua ukizingatia nilikuwa nataka kila siku limwagiliwe maji ili palowane na pasiunguzwe na jua. Yani Yule mwehu Yule dah sijui nafanyaje kumuepuka, ila twende huko mwanangu”
Wakaenda hadi wakafika mahali pa kuacha gari na kuanza kutembea kwa miguu,
“Kheee mama, lile daraja nitawezaje kuvuka?”
Wakati anafikiria namna ya mwanae kuvuka hapo darajani, akamuona kijana na kumuomba ili amvushe mwanae ila Ana machale yakamcheza na kukataa kuvushwa na yule kijana kisha akamwambia mama yake ambebe tu mgongoni,
“Jamani mwanangu, unajua umekua sasa”
“Ndio nimekua mama ila kuvushwa na huyo kijana hapana, nibebe tu mwenyewe univushe. Nitakwambia kwanini nimegoma kuvushwa na Yule kijana”
Basi Rose akaamua kumbeba mwanae mgongoni na kuvuka nae, lile daraja lilikuwa na mwendo kidogo ila walimaliza kuvuka na kufika ng’ambo ya pili.
Rose alimuuliza mwanae kuwa kwanini amegoma kuvushwa na Yule kijana,
“Hakuwa mtu wa kawaida Yule mama”
“Kivipi?”
“Mama, kumbuka ulivyonielezea kuhusu kule kwa mganga ulipoenda unajua kwanini yalikukumba maswahibu?”
“Kwanini?”
“Kwasababu uliliokota lile begin a kuliweka kwenye gari lako halafu ukatembea nalo kila mahali, yani Yule kijana angenivusha pale darajani asingekubali anishushe na tungeenda nae mpaka kwa huyo mganga halafu yangetupata maswahibu”
“Mmmh mwanangu!”
“Ndio hivyo mama”
Wakaendelea na safari yao, mahali ambako Ana alichoka alimwambia mama yake ambebe na alitembea nae, walitembea kwa takribani lisaa limoja, kwakweli Ana alichoka sana ila alivumilia sababu yeye na mama yake walihitaji tiba haswaa kwa muda huo.
Hatimaye walifika kwa mganga waliyemtaka na walikuta foleni ya watu kama watatu hivi, nao wakaunga foleni. Huyu mama akamuuliza wa mbele yake
“Hivi hakuna njia rahisi ya kutuleta huku?”
“Njia ipo ila ni mbali sana, unazunguka sana mpaka kufika huku yani unaweza kutumia siku nzima”
“Kheee lakini gari si linapita?”
“Gari linapita ndio, ila inatakiwa kuwa makini sana huko. Ila hata huku sio mbali kivile ni daraja tu ndio linaharibu njia lakini boaboda zipo”
“Mbona hatukuziona?”
“Hamkuziona? Labda zilikodiwa zote ila huwa zipo”
Kidogo Rose alishukuru alivyosikia bodaboda zipo maana kwa huyo mganga alikujaga muda mrefu sana, kwahiyo hakujua kama kuna maendeleo ya kuwepo bodaboda ingawa hawakuziona na mwanae muda walipokuwa wanaenda hata njiani hawakukutana na bodaboda ya aina yoyote.
Siku ya leo wale mapacha na dada yao walienda sehemu moja ila njiani wakakutana na Salome akidai kuwa anaenda nyumbani,
“Ila hakuna mtu nyumbani”
“Kuna nguo yangu naenda kuichukua”
“Unawezaje kwenda kwenye nyumba ya watu bila ya wenyewe kuwepo?”
“Leo unaniuliza hivyo Sara, hivi siku ile ningeogopa kuja ungepona macho yao hayo?”
“Ila mama amekataza kwenda nyumbani amesema hadi apige simu?”
“Amewakataza ninyi sio mimi”
“Mmmh kasema mtu yeyote”
“Jamani nina uhakika hata nikiwauliza sababu ya kukataza mtashindwa kunijibu, Ngoja niende zangu tu.”
Sara akawa kimya kwa muda basi Salome akawaaga na kuondoka, wakati Salome anaondoka tu kabla hawajaongea chochote alitokea rafiki yake na Sara, kisha aliwasalimia na kuwauliza kuwa Salome ni nani yao,
“Yule aliyeondoka ni nani yenu?”
“Ni ndugu yetu”
“Aaah kumbe siku zile alipona?”
“Siku gani?”
“Siku ile aliyoangukia kaburini”
Wote wakamshangaa kwani hakuna aliyekuwa na wazo kuwa ni Salome ndio aliangukia kaburini,
“Mbona hatukuelewi?”
“Siku ile wakati anazikwa Yule mdada wenu wa kazi basi huyu msichana ndio aliangukia kaburini na akawa kama amepigwa shoti”
“Mmmh au umemfananisha?”
“Hapana sijamfananisha, zile nguo ndio zile zile alikuwa amezivaa siku ile. Halafu nilimshuhudia hadi anapakizwa kwenye gari ili apelekwe hospitali. Nikataka kwenda na mimi ila wakanikatalia. Tena nakumbuka hata dereva aliyembeba ni mtu ambaye anafahamiana na mtu ninayemfahamu, ngoja tukamuulize vizuri ila ni yeye”
“Mmh wewe rafiki yangu wewe Jesca, acha maneno yako”
“Jamani mimi ule umbea mlinifukuzaga kwenu pale nisikanyage nimeshaacha na wala huu ninaoongea sio umbea ni ukweli kabisa. Yule msichana alitumbukia kaburini na akakauka kama amepigwa shoti ya umeme”
Wale mapacha hawakuyaamini maneno ya rafiki wa Sara na kuomba wapelekwe kwa huyo dereva kwa uthibitisho kwani lazima dereva aliyembeba alikuwa anajua, na Yule msichana aliamua kuacha mambo yake aliyokuwa anafanya kwa muda huo na kwenda kumtafuta huyo dereva.
Zamu yao ilifika ya kuingia kwa Yule mganga, waliingia na kumkuta ambapo kabla hawajamueleza matatizo yao Yule mganga aliwaambia,
“Najua kila kitu, yani kitu pekee kinachowasumbua ni Moza”
Walishtuka na kuangaliana sababu huyu mganga amejua kabla hata hawajamueleza, Rose akamuitikia Yule mganga,
“Tawile baba, yani hata hatujui tufanye nini”
“Hapa ndio mwisho wa matatizo, yani mimi ndio kila kitu. Mimi ni tishio la vitu vyote vya ajabu, Yule Moza amerudi kwa lengo moja la kukukomesha wewe. Yule msichana alijua siri zako mapema sana kabla hata hujajua kuwa anafatilia siri zako, na kitendo chake cha kupata ile dawa ndio kila kitu kimekuwa wazi kwake”
“Kwahiyo inamaana Moza ni mzimu?”
“Moza ni zaidi ya mzimu ambao unajua wewe, Moza ana nguvu za ziada kwani ana nguvu za kutoka kwenye mzimu wa bibi yake na ana nguvu za ile dawa yako maana ilichomwa”
Rose alishtuka sana kusikia kuwa dawa yake ilichomwa kwani hapo alihisi kila kitu kimeharibika, kwakweli alihisi nguvu kumuisha akauliza kwa upole,
“Sasa kama ile dawa yangu ilichomwa, aliichoma nani na je nifanye nini?”
“Ile dawa ilichomwa na mume wako”
Rose na Ana walishangaa sana kuwa ile dawa imechomwa na aliyeichoma ni Patrick, kwahiyo walijiuliza kuwa Patrick alipata wapi ujasiri wa kuchoma ile dawa na kwanini alifikia uamuzi wa kuchoma ile dawa,
“Kama nilivyowaambia, Moza anaongozwa na mzimu wa bibi yake na mzimu huo ndio ulimtuma Patrick akachome ile dawa halafu Moza aliongezeka nguvu mara mbili. Nyie mnahisi Moza amekufa ila kiuhalisia Moza hajafa na amerudi kwaajili yenu”
“Sasa tufanyaje?”
“Cha kufanya hapa ni kimoja tu”
“Kipi hiko?”
Akamuangalia Rose na kumwambia,
“Unatakiwa ulale na mlinzi wako”
“Nilale na mlinzi wangu?”
“Ndio, unatakiwa ulale nae”
“Kheee nitawezaje kulala na mlinzi wangu?”
“Nitakupa dawa ya kukusaidia, na ukilala nae kwa hakika kila kitu utaona kimebadilika”
“Jamani mganga sikuelewi, kwanini mlinzi wangu nilale nae?”
“Yule mlinzi alikuwa anampenda sana Moza yani alikuwa na mapenzi ya dhati na Moza. Unatakiwa kulala nae ili kutimiza ile azma ya mapenzi yake kwa Moza kisha ndio tutamuweza Moza. Tena unatakiwa ulale nae kwenye chumba alichokuwa analala Moza”
“Mmh mbona umenipa mtihani mkubwa sana, je litawezekana hilo?”
“Nitakupa dawa na itawezekana”
Rose alijifikiria sana namna ya kulala na mlinzi wake maana siku zote amekuwa akimdharau sasa leo anatakiwa alale nae, kwakweli aliona ni mtihani mkubwa sana ila kwavile alichoshwa na vimbwanga vya hapa na pale akajisemea ni lazima afanye hivyo ili aepukane na vimbwanga vile.
Kwahiyo akakubali kuchukua dawa aliyopewa na mganga, kisha kuuliza kuwa baada ya kulala nae afanyaje.
“Baada ya kulala nae tu, yani kwanza mumeo atarudi na kuwa chini yako halafu Moza atakufa kweli. Nitakupa tu maelekezo ya hii dawa, ukifika getini iweke mdomoni usiongee chochote na mlinzi wako, yani wewe mshike mkono tu hadi chumbani kwa Moza halafu lala nae”
“Hawezi kuniletea shida?”
“Usiongee kitu chochote, na kukataa hawezi hata usijali”
Basi Moza akachukua ile dawa na kuanza safari ya kuondoka akiwa na binti yake Ana, ila muda huu walipata usafiri wa boaboda hadi darajani.
Salome alifika na kumkuta mlinzi akiwa getini, basi Salome akamuomba kitu Yule mlinzi,
“Kuna mahali nataka nikuagize”
“Mmmh yani niondoke niache lindo langu? Hapana kwakweli”
“Katika maisha yako, umewahi kupewa hela ipi nyingi kwa mkupuo”
“Nimewahi kupewa laki tano”
“Basi mimi nataka nikupe milioni mbili ila tu ukiniahidi kwenda ninapotaka kukuagiza”
Yule mlinzi aliposikia milioni mbili, kwakweli akili yake iliruka kidogo na kusikiliza anapotaka kuagizwa,
“Sio sehemu mbaya, nakuagiza hotelini alipo mzee Patrick uende ukamshawishi hadi urudi nae hapa. Jitahidi kwa ujui wako wote umshawishi arudi”
Yule mlinzi hakuona kama ile ni kazi ngumu, ila alihitaji kupewa hizo hela kabisa na kuuliza tena,
“Na hapa getini atakaa nani?”
“Mimi nitakaa hapa getini kwa siku ya leo na siendi popote, unajua Yule ni baba yangu. Nahitaji aje nyumbani”
Kisha Salome akamkabidhi pesa Yule mlinzi na kumuelekeza mahali alipo mzee Patrick halafu Yule mlinzi akaondoka zake, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Yule mlinzi kuondoka kwenye lindo lake hilo wakati mama mwenye nyumba hayupo.
Muda kidogo alirudi Rose na binti yake Ana, ila walimkuta mlinzi yupo getini amesinzia. Rose alikunywa dawa yake na kuanza kumvuta mlinzi mkono ili waelekee nae ndani, ila mlangoni akakutana na Salome. Rose akashtuka kwani hakutegemea kukutana na Salome mlangoni, halafu Salome akamuuliza,
“Vipi huyo mlinzi unampeleka wapi?”
Rose alitamani kumjibu Salome ila akakumbuka masharti aliyopewa na mganga kuwa asiongee kabisa akimeza ile dawa, hakujibu ila akataka kuingia ndani ila Salome akamzuia mlangoni na kumfanya Rose achukie sana akatamani hata mwanae Ana angekuwa karibu apambane na Salome kwani muda huu Ana alikuwa ameachwa getini akisubiria mama yake amalize kwanza shughuli na mlinzi.
Rose akawa anang’ang’aniza aingie ndani,
“Sikupishi hadi uniambie huyo mlinzi unampeleka wapi?”
Rose alipambana na Salome pale mlangoni hadi akajikuta akimwambia,
“Nipishe bwana weee”
Salome alimpisha huku akicheka sana, Rose alikuwa na hasira sana na alijiuliza kama dawa itafanya kazi kama alivyoambiwa na mganga maana kashakosea masharti na kuongea wakati aliambiwa asiongee chochote.
Aliingia na Yule mlinzi kwenye chumba cha Moza na kumuweka kitandani, kisha yeye akainuka na kuanza kuvua nguo zake ila alipomaliza tu kutazama kitandani hakumuona mtu yeyote.
Itaendelea kesho usiku……..!!!!!!
By, Atuganile Mwakalile.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: