KURUDI KWA MOZA: 22 Rose alijua Salome ataanguka chini ila ilikuwa kinyume maana Salome hakuanguka chini, Rose akamsukuma tena ila Salome alisimama kamavile mlingoti. Muda huu Rose alipotaka kumsukuma tena Salome alishangaa mkono wake ukianza kutetemeka. Kila mmoja ndani ya nyumba yake alimshuhudia Rose akitetemeka mkono, Ana akainuka kwani aliona mama yake asije akaumbuka yeye kisha Ana akamsukuma yeye Salome ila kwake ndio ikawa kinyume kabisa kwani mkono wake uliganda kwenye mwili wa Salome, kila mmoja alikuwa akishangaa na kati ya wale mapacha na Sara hakuna aliyeweza kuongea neno lolote. Mara Salome alianza kuelekea vyumbani ila Ana ambaye mkono wake uliganda kwa Salome alikuwa akimfata nyuma, halafu Rose naye ambaye mkono wake ulikuwa ukitetemeka alikuwa akimfata nyuma pia, kitendo hiko kiliwafanya wale mapacha na Sara wafate nyuma kwani walitaka kujua ni nini kinaendelea au ni kitu gani huyo Salome anataka kufanya. Salome aliongoza moja kwa moja mpaka chumbani kwa Rose na kufungua mlango, kila mmoja alikuwa akimfata nyuma huku wengine hawaelewi elewi, alikutwa Patrick akiwa amelala chini sakafuni, Salome akamuangalia Rose na kumuamuru, “Muamshe” Rose akiwa anatetemeka, alisogea kwa Patrick na kujaribu kumuamsha. Alimuamsha kwa muda akashindwa, akainua kichwa chake na kumtazama Salome kwa uoga kisha akamwambia, “Nakuomba basi wanangu watoke humu chumbani nimuamshe” “Unashindwa nini kumuamsha hivyo hivyo?” “Tafadhali usinidhalilishe, nakuomba watoke kwanza ndio nimuamshe. Nipeni dakika chache tu nitakuwa nimemuamsha” Salome akatoka nje na wengine wote walimfata nyuma hadi sebleni kwahiyo walimuacha mama yao akiwa chumbani na Patrick. Kila mmoja alikuwa akimshangaa tu Salome na wala Ana hakuweza kuutoa mkono wake kwenye mwili wa Salome maana uligandia alipotaka kumsukuma, kwahiyo walikuwa wamesimama tu na hakuna yeyote aliyethubutu kukaa wala kusema neno lolote kwa wakati ule kwani wote walijikuta wakimtazama tu Salome. Baada ya muda kidogo, mama yao alirudi na Patrick sebleni na muda huu hata Ana akaweza kuutoa mwili wake kwenye mwili wa Salome, basi Salome alienda kumfata Patrick na kumkalisha kwenye kiti kisha akapitisha mkono wake machoni pake na kusema, “Nataka uone yote na zaidi ya yote amabayo mkeo amekuwa akikutendea kwa miaka yote hii” Ikawa kama akili ya Patrick imefunguka kiasi hivi kwani alianza kujishangaa na kuhoji kuwa yuko wapi, “Nikowapi hapa?” Ni Salome pekee aliyekuwa na ujasiri wa kumjibu, “Unatakiwa kutulia kwanza maana ndio umetoka kifungoni ni ngumu kujua kwa mara moja ulipo. Tulia kwanza tuliza akili halafu utajua ulipo na kila kitu ingawa kuna baadhi ya vitu utavitambua badae sana” Patrick alikaa kimya kwani alikuwa kama haelewi elewi vile. Walitamani kumuhoji Salome lakini hakuna aliyekuwa na ujasiri wa kufanya hivyo, kisha Salome akainuka na kwenda zake ndani kisha akawaacha wote pale sebleni. Yani kama kuna siku ambayo Rose aliwaonea wanae aibu basi ilikuwa ni siku ya leo maana nae hakuweza tena kukaa pale sebleni bali aliondoka na kwenda chumbani kisha Ana nae akafata na kwenda chumbani kwake. Kwahiyo sebleni walibaki wale mapacha, Sara na Patrick. Muda kidogo Patrick alimuangalia Sara na kumuomba jambo, “Naomba kaniletee simu yangu na funguo za gari chumbani” Sara hakubisha wala nini, alifanya hivyo na kwenda chumbani kwa mama yake ambapo aligonga na mama yake alimkaribisha kwani alijua ni Ana, akashangaa kumuona ni Sara. Akamuuliza kwa mshangao, “Vipi tena?” “Baba kanituma funguo za gari na simu yake” “Chukua hivyo hapo mezani mpelekee” Yani siku ya leo hata kuhoji hakuhoji zaidi ya kusema funguo zilipo na simu ya mumewe, simu ambayo mume wake ana kitambo sana hajaishika wala kuwasiliana na watu. Sara alichukua na kwenda kumpelekea baba yake huyo wa kambo. Alipompa tu Patrick alitoka nje na kuondoka zake, tena hakuna aliyemuaga kuwa anaenda wapi. Wale mapacha waliangaliana na dada yao Sara, halafu Sara akawaambia, “Yani kwa matukio haya naogopa hata kulala peke yangu” “Sasa utalala na nani?” “Sijui yani” “Basi kalale na Ana au Salome” “Mmmh hao watu ni bora uniambie nikalale getini na mlinzi, nawaogopa hao watu kama kitu gani” Mara Salome akatokea, Sara akajikuta tu akimwambia “Baba kaondoka tena bila kuaga, halafu leo kachukua na simu yake” “Ungekuwa ni wewe ungeweza kuaga?” “Kivipi?” “Unajifanya hujui ambayo baba yangu alikuwa akitendewa kwenye nyumba hii? Sasa anatambua kila kitu, maswala ya kumfanya mwenzenu kama ndondocha mwisho” Sara aliwaangalia wenzie, halafu Salome alitoka nje kabisa na alionekana akielekea getini ambako alitoka na kuondoka. Sara aliwauliza wenzie, “Jamani mnamuelewa huyu mtoto?” “Simuelewi na sitaki kuongea sana” “Hata mimi pia simuelewi na naogopa kuongea sana” Kisha wale mapacha wakaondoka zao na Sara akaondoka zake. Rose alipoona mwanae Ana hajaenda chumbani kwake ikabidi yeye mwenyewe ndio aende chumbani kwa Ana, aliingia na kumuuliza mwanae, “Hivi wewe umeweza kumuelewa huyu Salome?” “Mama naomba tuzungumze usiku kwenye muda wetu sio muda huu” “Hata tukisema tuzungumze usiku hatatusikia kweli?” “Mama, mimi ndio nimekwambia na bado natafakari maana sipo sawa kabisa. Amewezaje Yule kugandisha mkono wangu mama? Yule msichana ana majini sio bure” “Ndiomana nakwambia tujadili sasa hivi, unajua ile majuzi nilienda kwa mganga mwingine halafu ndani kwa mganga nilimkuta Moza” “Moza!” “Ndio nilimkuta Moza” “Si amekufa huyo mama” “Mwanangu hatuna uhakika na kifo cha Moza, kumbuka maiti yake ilitoweka kaburini” “Ndio ilitoweka ila nikajua utafanya jambo, na imekuwaje hadi Moza awe hajafa kweli?” “Sijui mwanangu, ila kama ile dawa iliyomuua Moza ilichomwa moto basi tumeisha” “Unamaana gani mama?” “Ile dawa mwanangu nilipewa na ilikuwa hairuhusiwi kuonekana na mtu yeyote halafu sitakiwi kuiweka mbali na nyumba yangu ndiomana nikaifukia kwenye ua ili nijue ni ua gani nimeifukia. Ni ya muda mrefu sana ile dawa na ilikuwa hairuhusiwi kuonekana na mtu yeyote wala kuungua na moto ndiomana hata kuunguza mboga humu kwenye nyumba yangu huwa sitaki. Sasa kama imechomwa moto sijui itakuwaje, ndiomana tulitakiwa kumzika nayo Moza” “Sasa mama kama imechomwa moto imechomwa na nani wakati Moza alikuwa amekufa nayo mkononi” “Kwamaana hiyo inawezekana ipo mahali eeh! Lakini mbona tuliitafuta bila kuiona popote” “Mi nadhani mama tufanyie usafi kile chumba cha Moza tuitafute kabla hayajawa majanga” “Sasa lile shetani linalolala kwenye chumba kile tutalifanya nini?” “Yani huyo mtu ananiumiza kichwa balaa, ila mama na wewe kwanini dawa ya maana hivyo ukaenda kuifukia kwenye ua? Mbona mimi dawa yangu ile ipo chini ya godoro” “Ni masharti ya ile dawa, kwanza haikutakiwa kuwekwa ndani ya nyumba ila inatakiwa iwe karibu na nyumba halafu haitakiwi mtu aione.” “Basi mama nitatumia dawa yangu kufanya kitu ili tuweze kupekua kile chumba cha Moza” “Sawa mwanangu, ndiomana nilikuwa nakufata tujadili. Sasa wewe unataka tufanye kwenye muda wetu, unadhani mambo yalivyotinga hivi tutakumbuka kujadiliana kweli! Ni ngumu mwanangu” “Kweli mama ila chanzo cha mambo yote haya ni mwanao Sara, yani simpendi Yule mdada simpendi kabisa” “Kweli mwanangu ni chanzo cha yote lakini ni mwanangu, kumbuka hilo. Yule ni dada yako mpende tu” Rose akajiribu pale kumshawishi mwanae ili ajende upendo kwa ndugu yake maana alikuwa anapenda watoto wake wapendane. Salome alienda nyumbani kwa mama yake na kumkuta kama kawaida akiwa na wale wadogo zake John na Joseph. Aliwasalimia kisha mama yake akamuomba chumbani kwake ili wakazungumze “Kwanza imefurahi umerudi nyumbani maana mambo yako siku hizi siyaelewi kabisa. Halafu ngoja nikuulize, hivi una simu” Salome akacheka, “Sio unacheka Salome, nijibu una simu?” “Ndio nina simu” “Umeitoa wapi?” “Baba yangu kaninunulia ili niweze kuongea nae” “Haya, wadogo zako wameniambia Ashura hakuja huku kwenye nyumba mpya, halafu wewe na Ashura kuna mchezo mlikuwa mnacheza kisha Ashura akaanguka. Unajua sijaelewa naomba nieleweshe maana huyo Ashura hata nikimpigia simu zangu hapokei zaidi ya kunitumia ujumbe tu” “Hivi hat nikikueleza unaweza ukanielewa!” “Nieleze tu, kwanini nisikuelewe?” “Acha tu ufahamu unavyofahamu, Yule Ashura si ndugu yako? Uliza kwa ndugu zenu alipo” “Hivi wewe mtoto unaongelea nini mbona sikuelewi?” “Huyo mamdogo Ashura yupo kwenye kijiji cha baba yenu amesema anaenda kuangalia kaburi la baba yenu kwahiyo ungeenda na wewe kijijini ili uulize vizuri kuhusu Ashura” “Tutaenda na wewe?” “Hapana, mimi nitabaki ila utaenda na wadogo zangu. Mimi nabaki na baba yangu.” “Haya nitafikiria kwenda” Salome akainuka, na kumfanya Neema amuulize tena, “Sasa mbona unaondoka kabla hata sijamaliza maongezi na wewe” “Subiri nakuja sasa hivi” Salome aliondoka zake, Neema nae alitoka ila kiukweli hakumuelewa kabisa mwanae na mambo aliyokuwa anayafanya. Alipokaa muda kidogo mwanae alirudi kisha akampa mama yake tiketi, “Nimeshakukatia tiketi, wewe na wadogo zangu ya kwenda kutembelea kaburi la babu” “Kheee kwahiyo ndio unataka tusafiri!” “Ndio, si mnaenda kukaa wiki tu mnarudi” “Kwahiyo tiketi umekata ya kuondoka lini?” “Kuondoka kesho” “Kheee Salome hebu acha masikhara, tutaondokaje kesho wakati hatujajipanga!” “Unataka mjipangaje?” “Sijapanga nguo za watoto, sijawanunulia mama zangu vitenge” “Ni hayo tu au kuna mengine?” “Ni hayo ndio” “Basi nitakusaidia, yani wewe tulia tu nitakusaidia kupanga ila tiketi ni ya kesho” Neema alimshangaa sana Salome kuwa mtoto wake amebadilika sana na amekuwa na maamuzi ya haraka haraka, akawa anaziangalia tu zile tiketi ambazo alikuwa amekatiwa na Salome. Usiku kwenye mida ya saa tatu, Neema akiwa amejipumzisha kidogo akamsikia Salome akiingia ndani kwake na kumwambia, “Mama kila kitu nimekupangia kwahiyo kesho safari” “Na nguo zangu, na za wadogo zako umepanga?” “Ndio tayari” “Ila vitenge bado sijanunua” “Nilishaenda kununua” “Kheeee hebu tuvione” Salome alimtolea Neema vitenge ambavyo aliviangalia na kushangaa tu kuwa Salome amewezaje kwenda mjini kwa muda mfupi vile na kuchagua vitenge bvizuri vile, akainuka na kuangalia mabegi ni kweli yalikuwa yamepangwa vizuri kabisa kwahiyo hakuwa na cha kubisha kuhusu safari ya kesho, swala hilo hata likamsahaulisha kuwa alishauriwa mwanae ampeleke kwenye maombi. “Nishaongea na dereva tax, kwahiyo atakuja kuwachukua kesho asubuhi” “Kwahiyo nyumba nani atafunga?” “Mimi nitafunga, na mkiwa mnarudi mtanikuta maana nitakuwa narudi mara kwa mara” Neema alimuangalia mwanae Salome hakummaliza maana kwa kawaida Salome wake ni muoga ila leo hii anakubali kuachwa mwenyewe nyumbani na anasema atakuwa anaenda mara kwa mara hata wakirudi watamkuta, alimshangaa kwakweli ila akajisemea labda ndio kukua kumemfanya abadilike. Usiku wa manane, Rose alichukuana na mwanae kwenda kufanya msako kwenye chumba cha Moza kutafuta ile dawa iliyomuua Moza maana walihisi bado ipo ndani. Basi walipekua na kupekua lakini hawakufanikiwa kuiona, ndipo walipoanza kupekua nguo moja moja ya Moza ila Ana akamwambia mama yake, “Mama, tutajichosha bure. Ngoja twende chumbani kwangu nikachukue ile dawa yangu ituonyeshe” Rose aliafikiana na mwanae na kujilaumu kuwa kwanini walikuwa wakijichelewesha wakati kuna njia rahisi ya kufanya, basi wakatoka mule chumbani kwa Moza na kuelekea chumbani kwa Ana walipofika walishangaa kumuona mtu amekaa kitandani kwa Ana halafu mtu huyo akawaangalia na kuwafanya wagundue kuwa ni Moza. Itaendelea kesho usiku…….!!!!!!! By, Atuganile Mwakalile.

at 4:44 PM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top