Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 21
Sara akaanza kusogea akitaka kufungua, ila gafla akashtuliwa na sauti iliyotokea nyuma yake ilikuwa ni sauti ya mama yake.
“Unafanya nini hapo?”
Sara aligeuka na kumtazama mama yake ambaye alikuwa amemkazia sura vilivyo, ila cha kushangaza alivyoangaza huku na huku hakumuona Salome.
Sara alishangaa sana kwa kutokumuona Salome hadi mama yake akamuuliza,
“Mbona unashangaa hivyo?”
Akataka kumwambia mama yake kuwa alikuwa na Salome ila akashangaa mdomo unakuwa mzito kupita maelezo, akabaki tu kimya na mara akamuuliza mama yake,
“umeingiaje humu?”
“Badala nikuulize wewe umeingiaje humu eti unaniuliza mimi! Badala uniulize utatokaje humu unauliza nimeingiaje? Hujui kama humu ni ndani kwangu, popote nina uhuru wa kuingia. Haya umeingiaje humu? Na umefuata nini”
Sara alikuwa kimya tu akimuangalia mama yake kwani kiukweli hata yeye mwenyewe hajui humo amefuata nini maana alikuwa akimfuata tu Salome ndiye aliyempeleka humo ingawa hakumuona tena, mama yake alimuangalia tena kwa hasira na kumuuliza,
“Ulikuwa unafata nini humu? Unashida gani humu wewe mtoto lakini? Yani yote uliyonitendea leo unaona hayatoshi zaidi ya kuendelea kunichokonoa chokonoa? Ngoja nisiongee kwanza humu tutoke kwanza”
Rose alimvuta mwanae mkono kisha akafungua mlango tu kawaida kanakwamba haukufungwa na funguo halafu akatoka nae ila Sara alimchoropoka mama yake kwani bado alikuwa akijiuliza kuwa Salome yuko wapi, alienda moja kwa moja kwenye chumba ambacho huwa analala Moza na kufungua mlango ilia one kama Salome yupo ila alifungua mlango na hakumuona yoyote, mama yake alikuwa nyuma yake na kumuuliza,
“Sasa unatafuta nini?”
Sara alitamani kumwambia mama yake kuwa kwenye chumba kile aliingia na Salome na hakumuona tena kwahiyo alitaka kumuangalia kama chumbani kwake yupo, ila mdomo ulikuwa mzito kusema hayo na alishindwa. Mama yake alipoona mwanae anabung’aa bung’aaa akamvuta tena mkono na kupita nae sebleni, halafu akaenda nae kwenye sebule nyingine ambayo wale mapacha hupenda kuitumia. Akakaa nae na kumuuliza,
“Sara, mimi ni mama yako au sio mama yako?”
“Wewe ni mama yangu”
“Kwanini huniheshimu sasa?”
“Mama sio kwamba sikuheshimu ila linapokuja kwa wewe kuhusishwa na habari za kichawi ndio huogopa”
“Una uhakika kama mimi ni mchawi?”
“Mbona Ana ni mchawi mama”
“Kwahiyo kama Ana ni mchawi huo uchawi nimempa mimi?”
“Hapana mama sijamaanisha hivyo”
“Na kama nimempa Ana uchawi basi nyie wote kwenye nyumba hii ni wachawi, unaponaje kuwa mchawi wakati mama yako mzazi ni mchawi? Uchawi unaujua wewe? Kwanza nani aliyekuambia kama mimi ni mchawi?”
“Sijui mama”
“Sara mwanangu, acha fikra mbaya. Wewe ni mwanangu wa kwanza na mambo mengi nafanya kwaajili ya maisha yenu, kumbuka baba yako alikukataa wewe toka upo tumboni mwangu. Je alikukataa kwavile nilikuwa mchawi? Nimehangaika mimi nimeteseka, nikawapata kaka zako nao wakakataliwa na baba yao. Sasa mimi kumpata mtu na kumdhibiti asifurukute kwenye himaya yangu na awajali nyie na kuwapenda na kuwapa chochote mtakacho ni uchawi huo? Kumtafuta mtoto kama Ana ili kuongeza upendo kwa mwanaume niliyempata, ni uchawi huo? Unaacha kujiuliza kwanini huolewi na umri umeenda umekazana kutafuta uchawi wa mama yako. Sitaki yakukute yaliyonikuta mimi, usiamini maneno au vitendo vya kusema mimi ni mchawi ila nafanya vitu kwaajili na maisha yenu yani wewe na wadogo zako. Sina tatizo na Ana, ni wa tofauti na nyie Yule. Sahau katika maisha yako kama utakuja kuolewa, na kaka zako wasahau maishani mwao kama watakuja kuoa, ila Ana ataolewa na ataolewa sababu nataka amtese mume wake. Mimi sio mchawi mwanangu, na sitaki unifatilie tena. Nadhani tumeelewana!”
“Nimekuelewa mama na ninakuahidi sitakufatilia tena, ila kwanini unasema kuwa mimi sitaolewa wala kaka zangu hawataoa?”
“Nitakwambia sababu ila sio leo, nyie mtaishi name miaka yote”
Rose aliondoka na kumuacha mwanae kwenye dimbwi la mawazo, alikosa jibu kuwa kwanini hatoolewa ila aliweza kuolewa kuwa ni kwanini kila mwanaume anayemleta mama yake anampinga mwanaume huyo, yani hapo ndio akaelewa kuwa mama yake hataki yeye aolewe, akasema lazima awataarifu kaka zake kuhusiana na hicho alichoambiwa na mama yao.
Kisha Sara aliinuka pale na kutoka.
Wakati Sara anatoka kwenye ile sebule aliamua kupitia jikoni, alishangaa kumuona Salome anapika na kumuuliza kwa mshangao,
“Kheee Salome unapika?”
“Ndio napika, unafikiri sijui kupika? Mamangu amenifundisha kupika”
“Sio kwamba nashangaa unapika ila nashangaa ulivyotoweka kwenye kile chumba”
“Nimetoweka!”
“Ndio umetoweka, wewe Salome ndio mchawi na sio mama yangu”
Salome akacheka kisha akamuuliza Sara,
“Lini nimekwambia kuwa mama yako ni mchawi?”
Sara akajaribu kuvuta kumbukumbu lakini hakupata siku ambayo Salome alimwambia kuwa mama yake ni mchawi, akajiuliza tena kuwa kuhusu mama yake ni mchawi ni nani amemwambia, lakini hakupata jibu.
“Mbona umenyamaza? Ni kuwa huna jibu ya kuwa lini nimekwambia kuwa mama yako ni mchawi, wewe mwenyewe umekuwa ukisema kuwa mama yako na mdogo wako ni wachawi”
“Ni kweli nilisema mwenyewe”
“Haya sasa, mimi nitajulia wapi uchawi wa mama yako? Kumbuka kuwa mimi ni mtoto wa mama mwingine na ninatokea mbali, sijawahi kuishi na mama yako ila wewe uliyeishi nae ndio ulisema hivyo. Jibu ni kuwa sijawahi kukwambia hivyo ila kuwa makini sana na maamuzi yako”
Sara akaondoka na kuacha kumuuliza tena Salome kuwa ni kivipi alitoweka na vipi anapika, je ameambiwa afanye hivyo. Ila Sara siku ya leo alikuwa akisubiria kwa hamu kaka zake warudi na awape ujumbe wa mama yao.
Muda kidogo alimsikia Ana akirudi nyumbani ila Salome alimfata Ana chumbani kwake. Kitendo hiko Sara alikiona na kufanya aende taratibu kwenye mlango ili asikilize maongezi ya salome na Ana. Kwa upande wa Ana kitendo cha kumuona Salome chumbani kwake kilimchukiza sana na kumfanya aulize kwa hasira,
“Kwanini umenifata tena bila ya hodi?”
“Nahitaji kuzungumza na wewe”
“Ila mimi sihitaji kuzungumza na wewe”
“Na ujue kwamba sikulazimishi na ukigoma jua nitazungumza na wewe kwa lazima kwa muda wangu”
“Unaniambia hivyo wewe kama nani?”
“Ninakwambia hivi nikiwa kama mtu niliyekushuhudia kitendo ulichofanya leo, Ana muachilie Yule mwalimu lasivyo nitakuumbua mbele ya wanafunzi wenzio na walimu wote”
“Hivi unanitishia mimi unanijua vizuri au Kitendo nilichofanya mimi unakijua wewe? Najiamini na hakuna chochote utakachoweza kunifanya wewe. Tena utoke chumbani kwangu kabla sijachukia”
Salome akacheka sana, kisha akamwambia Ana,
“Subiri sasa utakachokiona”
Kisha Salome akatoka na kumkuta Sara mlangoni ambaye alikuwa amepigwa na butwaa tu kwa maneno ambayo Salome alimwambia mdogo wake, kisha yeye akaingia ndani kwa mdogo wake ili kumuona vizuri na kujaribu kumuuliza mawili matatu,
“Ana vipi?”
“Vipi nini, nani amekwambia na wewe uingie chumbani kwangu bila ruhusa?”
“Jamani Ana”
“Jamani nini? Naona na wewe unanitafuta kama huyo mtoto wa kuokota uliyemleta humu ndani eti aje atupe vitisho, sikiliza wewe mdada usiyejielewa na akili zako mbovu hizo. Usitake na leo nikufanyie kitu kibaya”
“Kwani wewe Ana ni mchawi?”
“Ndio mimi ni mchawi ulikuwa hujui eeeh! Mimi ni mchawi wa wachawi na huwa sibabaishwi na vikaragosi kama wewe na huyo mwehu mwenzio”
“Kheee kumbe kweli wewe ni mchawi sasa umepata wapi uchawi?”
“Nimepata wapi? Usinichekeshe na wewe, uliona wapi mtoto wa paka akawa mbwa?”
“Inamaana mama naye ni mchawi?”
“Usiniulize maswali mwehu nini wewe, tena usinikere sasa hivi. Nina uwezo wa kukugeuza hata mende namuonea huruma tu mama yako. Ondoka chumbani kwangu upesi”
Sara aliondoka ila ndio akapata maswali mengi zaidi kuwa ni kweli mdogo wake na mama yake ni wachawi.
Mr.Patrick hakuonekana kabisa lakini Salome alielewa kitu gani kimempata Mr.Patrick na alihitaji kumsaidia bila yaw engine kuwa na mashaka, akajifanya kumuita mama yao sebleni maana alijua muda huu ni karibia wale mapacha walikuwa wanarudi, ni kweli baada ya kumuita tu wale mapacha nao walikuwa wamerudi, Salome alianza kwa kumuuliza,
“Yuko wapi baba yangu?”
“Sijui”
“Hujui!”
“Ndio nimekwambia sijui, halafu wewe mtoto sitaki maswala ya kunipanda kichwani kwenye nyumba yangu mwenyewe sitaki unipande kichwani”
“Sawa sitakupanda kichwani ila kila mmoja humu ndani ataona baba alipo leo”
“Unamaanisha nini?”
“Si hujataka kusema baba yuko wapi, basi nitamuonyesha kila mmoja alipo baba”
“Hivi wewe msichana una nini na kwanini unajiamini hivyo?”
“Unaogopa kujiamini kwangu eeh! Najiamini sababu najua hakuna wa kunishinda, baba yangu yuko wapi? Nimekuwa mpole sana kwa siku zote hizi ila hujiongezi wala nini. Subiri tena nakwambia kila mmoja nitamuonyesha baba alipo leo”
kisha Salome akaondoka zake na kwenda chumbani kwake, kwakweli Rose alimshangaa sana Salome kuwa anajiamini na nini mpaka anafikia kumwambia yeye maneno yale wakati watu wengi sana wanamuogopaga yeye, ikabidi aonoke aende chumbani kwa binti yake Ana kuzungumza nae basi na yeye akamueleza mama yake vitisho alivyopewa na Salome,
“Hivi anajiamini nini Yule?”
“Hata mimi mwenyewe namshangaa mama sijui anajiamini nini?”
“Tunatakiwa kufanya jambo mapema iwezekanavyo”
“Ndio mama”
“Sasa tutafanya nini?”
“Tumuingize kwenye kile chumba”
“Sawa sawa mwanangu”
Wakaanza kukubaliana pale namna watakavyomtokomeza Salome, bila ya kujua kuwa mbinu nyingi Salome anazijua.
Muda huu Sara alienda kuwafata kaka zake na akaongea nao namna ambavyo mama yake alimwambia mchana, ila wale mapacha wakapinga vikali kauli ya mama yao,
“Haiwezekani, kwakweli haiwezekani kabisa. Mimi nitaoa labda wewe Doto ndio hutooa”
“Mimi pia nitaoa, labda wewe mwanae wa kwanza ndio hutaolewa. Sisis tusioe kwa misingi gani? Kwanza mchumba wangu yupo tayari, ni kitendo tu cha kumleta nimtambulishe”
“Mmmh msiwe wabishi, mwenzenu mchumba wangu amepotelea humu kwenye nyumba”
“Kivipi?”
Sara aliwaeleza jinsi Ommy alivyopotea kiajabu ajabu, na kuwaambia kuwa kitu hiko amekiona kwenye ndoto.
“Mmh kwa staili hii simleti tena Yule mchumba wangu”
“Mimi nitamleta tu bila kujali chochote, Yule ni mama yetu lakini hatakiwi kuingilia kwenye mahusiano yetu. Kwanza tusioe kwanini? Au wewe usiolewe kwanini? Hebu acha hizo bhana.”
Mmoja akajikuta akikumbushia ishu ya Salome,
“Jamani huyu dogo Salome mnamuelewa kweli?”
“Jamani Yule mtoto kaka zangu ni ana mambo ya ajabu yani ya ajabu sana, nimejaribu hata kulala nae nimchunguze ila cha kushangaza nikilala nae nakuwa kama mzigo yani nikilala sishtuki hadi kunakucha yani hata chooni siendi. Yule dogo mi mwenyewe simuelewi”
“Ila wewe Sara una moyo, hata kulala na mtu asiyeeleweka vile unaweza mmmh! Mtoto haeleweki Yule, sijawahi kumuelewa toka siku ya kwanza amekuja humu ndani”
“Ila kuna kitu nahisi kuhusu huyu dogo”
“Kipi hicho doto?”
Gafla wakasikia sauti ya mama yao akimuita Salome kwa ukali sana, ikabidi nao waende kushuhuia kuwa kuna nini mbona ameitwa hivyo.
Kufika sebleni walimkuta mama yao akiwa na Ana halafu muda kidogo Salome nae alifika ila kabla hakijaongelewa chochote walishangaa kumuona mama yao akimsogelea Salome na kumsukuma kwa nguvu. Rose alijua Salome ataanguka chini ila ilikuwa kinyume maana Salome hakuanguka chini, Rose akamsukuma tena ila Salome alisimama kamavile mlingoti. Muda huu Rose alipotaka kumsukuma tena Salome alishangaa mkono wake ukianza kutetemeka.
Itaendelea kesho usiku…….!!!!!
By, Atuganile Mwakalile.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: