KURUDI KWA MOZA: 20 Wale mapacha wakatazamana maana mama yao aliwauliza kuwa ni nani alilala kwa Moza jana na hawakuwa na jibu. Kwa upande wa Rose, aliingia chumbani kwake na kumuamsha Patrick ila la kushangaza leo Patrick alivyoamka aliinuka na kumuwasha kibao Rose kisha akamwambia, “Yani wewe mwanamke umeniulia mama yangu!” Kabla Rose ajajitetea, alishangaa akipigwa kofi jingine. Kitendo hicho kilimchanganya sana rose na kila alipotazama sura ya mume wake ilionyesha kuwa na hasira za wazi wazi, Patrick aliendelea kwa kusema, “Mwanamke wewe ni shetani tena shetani mwenye mapembe, yani siku zote hizi nilikuwa sijui kama naishi na shetani, yani wewe wa kuniulia mimi mama yangu!” “Patrick sikuelewi mume wangu” Patrick akamzabua kibao kingine Rose, cha safari hii kilikuwa cha hali ya juu hadi Rose akajihisi kizunguzungu na kuanguka chini akaona akimchekea Patrick atamuumiza, vile alivyoanguka Patrick akamsogelea na kutaka kumpiga tena ila kuna dawa Rose akampulizia machoni Patrick na muda huo huo kizunguzungu kikasmshika Patrick na kuanguka chini. Rose alimuacha Patrick pale chini kisha yeye akatoka sebleni. Alipofika sebleni akashangaa kumuona Salome akiwa na Sara pamoja na wale mapacha, alimuangalia Sara kwa hamaki na kumuuliza kwa kumfokea, “Leo umelala nje eeeh!” “Hapana mama” “Hapana kitu gani, mbona nimekuja chumbani kwako sijakukuta” “Nililala na Salome kwenye chumba cha Moza” “Nini?” Sara alirudia yale maneno ila Rose alionekana kuchukizwa zaidi, ila wakati huu huu Sara alimuuliza mama yake, “Kilichonifanya nilale na Salome ni kuwa nilikuwa naogopa peke yangu, mama Ommy yuko wapi?” Rose hakujibu ila aliwaangalia wale mapacha wake na kuwafokea, “Nyie, si niliwaruhusu kuondoka” Nao walitoka haraka haraka kwani waliogopa mama yao asije akabadilisha mawazo maana huwa hakawii. Walivyotoka alimuangalia Salome na kumuuliza, “Na wewe nani amekuruhusu kuja tena humu ndani?” “Yani kuja humu sitangojea ruhusa maana ni kwa babangu” “Wewe mtoto nitakuja nikufanye kitu mbaya sana” “Najua huwezi kunifanya lolote” Salome akatoka pale sebleni na kwenda tena chumbani kwa Moza maana muda huo alikuwa amechukia na angeweza hata kubadilika. Sasa Rose alibaki na mwanae Sara kisha akamwambia mwanae atoke tu amuache nae Sara akafanya hivyo na moja kwa moja alienda tena chumbani kwa Moza akazungumze na Salome. Rose alitoka tena nje kujaribu kuangalia lile begi la hela ila hakuliona bado yani hapo ndio akaamini kweli hadi yeye kafanyiwa kiini macho. “Atakuwa ni Moza tu, na nitapambana nae. Ila nitaweza kupambana na mzimu? Mmmh! Cha kufanya ni kuwa nihakikishe haingii kwenye nyumba yangu, ngoja nizunguke nyuma” Rose alizunguka nyuma ya nyumba ili aangalie cha kufanya na mzimu wa Moza usiingie kwenye nyumba yake. Sara alienda kumuuliza Salome kwani yeye bado moyo ulikuwa unamuuma sana kuhusu kusalitiwa na Ommy, “Ni kweli nimeona kuwa Ommy alitoweka, tena inawezekana ni mama kamficha Ommy ila kila ninapotaka kukazana kumsaidia Ommy naiona sura ya Mishi yani naona kama namsaidia Mishi kumpata mpenzi wake” “Unaongozwa na wivu Sara, yani ni wivu ndio unakusumbua kwenye moyo wako. Kumbuka hata wewe Ommy unampenda, na akirudi atasema ukweli kuwa kati yako wewe na Mishi anampenda nani” “Mfano akimchagua Mishi je?” “Sioni kama ni tatizo hilo, atakuwa amekusaidia maana hutojiumiza tena moyo kwa kumfikiria mtu asiyekupenda. Mara nyingine kujua ukweli ni bora zaidi, mfano Ommy akifa huko wewe utapata faida gani? Utasema tu Mishi kakosa na mimi nimekosa, ila kuna faida yoyote unapata? Hakuna, mara nyingine kujua ukweli ni bora zaidi. Kuna watu wanakupenda wanakufataga ila unawakataa sababu upo na Ommy ila ukweli umeujua hakuna tena kusumbuliwa akili badala yake utaangalia unayempenda kati yao na kumkubali. Na hata ukiwa nae usiruhusu mapenzi yatawale akili yako yani akili yako isiendeshwe na hisia za kimapenzi maana ukiendeshwa na mapenzi, sehemu kubwa ya moyo wako itabebwa na wivu na utajikuta ukifanya jambo baya bila kutarajia. Fanya mapenzi ni sehemu tu ya maisha ila sio kila kitu katika maisha” “Unajua Salome, wewe ni mtoto mdogo sana ila unayachambua mapenzi vilivyo. Kwani ushawahi kuwa na mpenzi na udogo huo?” Salome akacheka kisha akamwambia dada yake, “Tuachane na habari hizo ila tuangalie jinsi gani unaweza kumuokoa Ommy, tambua kwamba Ommy anatakiwa kuokolewa” “Sawa nitafikiria na ushauri ulionipa, nitaongea na mama amuachie Ommy maana mama yangu ni mchawi kabisa ni mchawi sijui nifanyaje aache” “Unataka mama yako aache uchawi?” “Ndio, na mdogo wangu Ana aache uchawi tuwe watu wa kawaida tu na tuishi maisha ya kawaida” “Ila uchawi wanakula viapo, unadhani ni rahisi hivyo kuacha?” “Sijui” “Uchawi inatakiwa mtu aache kwa ridhaa yake mwenyewe ila kwa kulazimishwa haachi, nitasaidia na mama yako ataacha uchawi kwa ridhaa yake mwenyewe” Sara alikuwa anamuangalia Salome bila ya kummaliza, kisha Salome akamuomba Sara ampishe muda huu anahitaji kuvaa. Sara aliondoka na kwenda chumbani kwake, akampisha avae ila akajiuliza ni kwanini Yule Salome hawezi kuvaa mbele yake wakati yeye ni mwanamke mwenzie, “Mmmh kila akitaka kuvaa anasema nimpishe, halafu Yule mtoto mbona anaongea mambo ya kikubwa sana!” Akajiuliza sana, na kuamua kwenda dirishani kwake kuchungulia yani akili ilimtuma tu kufanya vile, wakati anachungulia gafla akamuona mama yake kapiga magoti kwenye ua, Sara alishangaa sana na kuamua kutoka ili amfate na kumuangalia vizuri maana uchawi wa mapema vile ulimuogopesha hata yeye kwani aliamini tu kuwa mamake ni mchawi ila hakufikiria kama uchawi unaweza kufanywa peupe vile. Rose alikuwa kwenye maua akifanya dawa kwaajili ya mzimu wa Moza usifike kwenye nyumba yake maana alianza kupata hisia kuwa huenda mzimu wa Moza ndio unaosumbua akili yake, basi alipiga magoti kwenye lile ua ambalo moza aliwahi kulifukua na kutoa kile kimpira kilichopelekea mpaka kifo chake, kwa upande wa Rose hili ua lilikuwa na maana kubwa sana kwake na lilikuwa likimsaidia vitu vingi sana kwahiyo alipiga magoti na kuanza kusema maneno ambayo hayatakiwi yakatishwe akianza kuyasema mpaka ayamalize, akiwa katikati yay ale maneno alishikwa bega na Sara, “Mama, mama” Rose hakumjibu chochote Sara na aliendelea na kusema maneno yake ila Sara nae hakuacha kumuita mama yake hadi akawa anamtingisha, “Mama, mama jamani mama ndio uchawi gani huu sasa mpaka umeanza kufanya peupe ili tujue kama mama yetu ni mchawi jamani!” “Mama, namuhitaji Ommy wangu, nirudishie Ommy mama. Nipo tayari kuachana nae ila nirudishie Ommy mama” Alipoona mama yake hamjibu chochote zaidi ya kuendelea na kitu anachofanya, akapata wazo la kuchukua maji na kumwagia hivyo akafanya kama wazo lake lilivyomtuma. Akafungua bomba na kukinga maji kwenye ndoo kisha akaenda kummwagia mama yake. Kwakweli hakuna siku ambayo Rose aliwahi kuchukia kama siku ya leo maana aliinuka kwa hasira halafu alimpiga mwanae hadi alizimia yani kipigo alichompiga haikuwahi kutokea, mlinzi alisikia kelele tu na kumfanya azunguke nyuma ambako kelele zilitokea ila akaona Sara akipigwa na mama yake hadi kuzimia kisha mama yake alimuacha Sara hapo na kwenda ndani, yani Rose hakujali kama mwanae amezimia au nini alikuwa na hasira zilizopindukia. Mlinzi alijaribu kumuinua Sara pale, sema sababu alikuwa na nguvu kwahiyo aliweza kumuinua na kumuweka pembeni kwenye kivuli kisha akaanza kumpepea ila hakuzinduka kwa muda huo. Salome nae alitoka ndani na kukuta yale yaliyopo kisha akachukua maji na kummwagia Sara, yale maji yalimfanya Sara azinduke ila alikuwa na maumivu makali sana ya kupigwa na mama yake, kisha Salome na mlinzi wakasaidiana kumshika Sara na kumtembeza hadi chumbani ambako walimuweka kitandani apumzike. Mlinzi alitoka na kumuacha Salome akiwa na Sara chumbani, kwakweli Sara alikuwa na maumivu mwili mzima kiasi kwamba hata alivyopigwa pigwa na mama yake hakukumbuka vizuri huku akijiuliza mwenyewe, “Hivi kilichonipeleka nyuma kule na kuanza kumfanyia fujo mama ni nini? Hivi kilichofanya nichungulie mama anachofanya ni nini?” “Usijilaumu kwa chochote Sara, katika maisha kila kitu huwa kinapangwa na kinakuwa na maana yake kwahiyo usijipe lawama za bure” “Hapana Salome, nimejitakia mwenyewe. Mwili wote unaniuma yani wote unaniuma. Mama yangu hajawahi kunipiga kiasi kile, mama yangu hajawahi kuwa na hasira na mimi kiasi kile. Hata kama mama yangu ni mchawi ila sikutakiwa kumfanyia fujo kiasi kile” Salome alimuangalia Sara kisha akaondoka na kumuacha Sara mwenyewe chumbani akijilaumu tu kwanini amemfanyia fujo mama yake maana mwili wote ulikuwa unamuuma, “Eti nampigia kelele mama amrudishe Ommy wa kazi gani sasa Ommy, janaume Malaya vile la nini? Kama limewekwa msukule na liwe tu msukule, ona nilivyopigwa na mama, huyu Salome nae sio wa kumsikiliza ushauri wake. Hivi yeye anaweza kufanya kwa mama yake ujinga kama huu! Mama ni mama hata akiwa mchawi, natakiwa kwenda kumuomba msamaha mama” Sara aliinuka kwa kujikongoja akajivuta hadi chumbani kwa mama yake ambapo aligonga bila kufunguliwa, ikabidi afungue mwenyewe. Alishtuka na kushangaa mama yake akiwa mtupu kabisa ila Rose alizidi kupatwa na hasira kwa mwanae na kuongea kwa hasira, “Hivi wewe mtoto una nini wewe? Unataka upate laana yangu au?” sara aliondoka kwa aibu hata hakuweza kuzungumza na mama yake kwani hakutegemea kama angemkuta mama yake akiwa mtupu kabisa, Sara alirudi chumbani kwake huku akijiongezea makosa aliyomkosea mama yake kwa siku hiyo na kujiona ni mtoto mpumbavu asiye na maadili halafu ndio mtoto wa kwanza wa mama yake halafu maadili hana anafanya mambo ya ajabu kama yale. “Nimemdhalilisha mama yangu, sifai mimi yani sifai kabisa” Alikuwa akijilaumu tu kwa wakati huo. Kwa upande wa Neema aliamini kuwa mwanae angeenda nyumbani kwa siku hiyo na angechukua ushauri aliopewa na mama Pendo wa kumpeleka Salome kwenye maombi, “Ila mwanangu atachukia akijua nimewaambia watu kuhusu yaliyomkuta, ila sikuwa na jinsi maana Yule mtu alituona” Akawaza ila uhakika wa Salome kufika siku hiyo hakuwa nao, wanae wale wadogo nao walikuwa wamerudi na wametulia sebleni kwao wakimuangalia mama yao akiwa na mawazo sana, mmoja akamuuliza “Mama mbona una mawazo hivyo?” “Nawaza kuhusu dada yenu Salome sijui leo atakuja” “Si umpigie simu mama” “Salome hana simu” “Mbona anayo, huwa tunamuona nayo akiongea na watu na akiitumia” Neema akashangaa kusikia kuwa mtoto wake ana simu maana yeye aliamini kuwa mwanae hana simu, aliwauliza wanae kwa mshangao. “Hebu achene maneno yenu, lini mmemuona dada yenu na simu?” “Kila siku tunamuona nayo mama, tena muda mwingine anakuwaga anaitumia sana. Toka tumehamia huku anayo” “Mmh sijui alinunuliwa na nani? Au Ashura?” “Sijui ila mamdogo Ashura toka siku ameanguka wakati tunakula ndio hatujamuona tena” Neema akazidi kushangaa na kuwauliza vizuri watoto wake, “Mbona siwaelewi?” “Dada alituambia tukacheze eti yeye na mamdogo wanacheza michezo ya kutaniana, na tulipoondoka badae akatuita na kutupakiza kwenye gari halafu tukahamia hapa” “Inamaana hapa hamkuja na Ashura?” “Hatukuja nae, dada Salome alisema mamdogo kaondokea kule kule. Ila mimi nilifurahi maana ona huku tunaishi kwa amani sana” Wakatoka nje na kucheza huku wakimuacha Neema kwenye maswali mengi sana, akajiuliza na kama Ashura aliondokea kule kule ni kwanini Salome alimdanganya kuwa aliondokea kwenye nyumba mpya waliyohamia? Na michezo gani hiyo ya kuanguka wakati wa kula? Alijiuliza maswali mengi sana bila ya majibu, na kubwa zaidi ni kuhusu kumiliki simu kwa Salome. Alijiuliza sana na mwishowe akaamua kuchukua simu yake na kumpigia Ashura ila namba haikupatikana, alipiga na kupiga lakini aliambiwa haipatikani. Sara bado hakuwa na raha kwani alijiona ni mkosaji sana kwa mama yake akawaza namna ya kumuomba msamaha mama yake, muda huu akatoka chumbani ila alimkuta Salome kwenye korido yao halafu Salome akamwambia Sara nifate, Sara hakujiuliza mara mbili zaidi ya kwenda kumfata Salome. Alimfata taratibu hadi kwenye chumba ambacho Salome alichukua ufunguo juu na kufungua kisha akaingia nae ndani na kufunga mlango kwahiyo ndani wakawa wawili tu, halafu akamwambia Sara huku akimuonyeshea mlango mdogo wa kwenye chumba kingine ndani ya chumba hiko, “Fungua ule mlango” Sara alikuwa akishangaa maana hajawahi kuingia kwenye chumba kile na wala hakuelewa kama kuna chumba kidogo ndani yake kama choo. Ila kwa muda huu aliamriwa na Salome kuwa afungue kile kimlango, Sara akakataa, “Hapana Salome, unataka nifunguie ili iweje? Sijawahi kuingia humu ndani, sijawahi kujua kama chumba hiki kina chumba ndani yake halafu leo unaniambia nifungue hapana sifungui” “Kama hutaki basi, ila mimi lengo langu ilikuwa ni kukusaidia” “Kunisaidia kivipi?” “Wewe kafungue tu halafu utaona nitakusaidiaje” Sara akaanza kusogea akitaka kufungua, ila gafla akashtuliwa na sauti iliyotokea nyuma yake ilikuwa ni sauti ya mama yake. “Unafanya nini hapo?” Sara aligeuka na kumtazama mama yake ambaye alikuwa amemkazia sura vilivyo, ila cha kushangaza alivyoangaza huku na huku hakumuona Salome. Itaendelea kesho usiku……!!!!!! Jumapili huwa situmi sababu huwa natingwa sana, yani siku yangu hii inakuwa na mambo mengi. Ila leo afadhali kidogo nimeweza hata kujivuta vuta nakutuma. Asanteni kwa maombi yenu. By, Atuganile Mwakalile.

at 11:01 AM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top