Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 19
Rose alishtushwa na sauti ya huyu mganga kwani ilikuwa ni sauti ya mtu anayemfahamu, akajikuta akisema kwa mshangao,
“Mozaa!!!”
Yule mganga alifunua sura yake na kumfanya Rose ashtuke zaidi kwani ni kweli alikuwa ni Moza.
Kwakweli Rose alitetemeka sana na kupata ujasiri wa gafla wa kutoka mule ndani na kuanza kukimbia yani kila mtu aliyekuwa pale alimshangaa, alikimbia sana kufika mbele akakumbuka gari yake na kujiuliza kurudi tena kuifuata, leo Rose alipatikana yani alipatikana haswaa kupita siku zote anazopatikana. Alichoka sana na kuanza kurudi kufata gari yake.
Alipofika kwenye gari yake alifungua na kuingia ndani ya gari, watu wapale karibu walimfata na kumuuliza kuwa ana tatizo gani lakini hakuna aliyemjibu zaidi ya kuondoa gari yake na kuondoka zake. Njia zima aliona kilichotokea kamavile ni ndoto tena ndoto haswaa, hadi hakujielewa jinsi anavyoendesha gari. Akapata wazo la kuangalia lile begi la hela aliloliokota kama lipo ila aliliona pale pale alipoliweka, kidogo akapata nafuu moyoni mwake kuwa begi lipo huku akiendelea na safari ya kurudi nyumbani kwake.
Salome alikuwa amekaa sebleni kwa Rose ila Patrick alitoka chumbani na kushangaa kumkuta tena Salome kwenye nyumba hiyo, alimuuliza kwa mshangao
“Wewe tena umefuata nini kwenye nyumba hii?”
“Jamani baba si nimekuja kwako, kuishi kwa baba yangu!”
“Kwani wewe ni mwanangu?”
“Ndio mimi ni mwanao, naitwa Maria”
“Maria!! Ndio yupi?”
“Mama yangu ni Neema na alinipa jina la mama yako ambaye ni bibi yangu”
Patrick alikuwa kama akitafakari jambo na alionyesha kumkumbuka sana mama yake, kisha akainuka na kumkumbatia Salome,
“Jamani kumbe ndio wewe mtoto ambaye mama aliniambia kuwa natakiwa kumfahamu, masikini mama yangu nilimkuta amekufa”
“Pole sana baba, ila mimi ndio Maria”
“Naomba uishi hapa siku zote, mama alinihusia nikupende na nikutunze ila mama yangu alikufa na sikujua kama mwanangu huyo alikuwepo”
Yani akili za Patrick zilikuwa zinakuja na kuondoka kiasi kwamba alikuwa anashindwa kutambua jambo lolote kwa wakati mmoja yani mara nyingine ilimlazimu kutafakari kwanza.
Waliongea mengi sana, Patrick alijikuta akimwambia Salome kuhusu familia yake.
“Lakini mama yangu ndio alikuwa mke wako wa ndoa!”
“Ni kweli mama yako alikuwa mke wangu wa ndoa ila alinitendea jambo bay asana siwezi kusahau ila sikutaka tu kumfungulia mashtaka mama yako, na siku zote sikujua kama wewe upo yani kulikuwa na kauli mbili kuwa ni kweli nina mtoto kwakwe ila kauli nyingine ilikuwa mtoto si wa kwangu ila ana baba mwingine”
“Alikufanyia jambo gani baya?”
“Unajua mama yako niliishi nae kwa muda mrefu sana bila kupata mtoto, hivi unafikiri ni nani anayeweza kuvumilia muishi kwa miaka karibu ishirini bila mtoto! Ni nani anayeweza kuvumilia hilo? Niliondoka takribani miaka mitatu, kurudi kidogo tu mamako akasema amepata mimba yangu, unafikiri ni rahisi kwangu kuamini hilo? Nilimfukuza nakiri hilo kabisa, na nilimfukuza kwa hasira kwani sikuwa na imani hata kidogo kuwa amepata mimba yangu. Baada ya miezi kadhaa nikapata habari kuwa anaishi kwa mamangu na mama akasema mtoto anafanana sana na mimi na wamempa jina lake. Nilifurahi kusikia hivyo na nikawa na lengo moja kwenda kumchukua mamako kwa mamangu na wewe tuishi pamoja. Cha kushangaza siku niliyoenda nilimkuta mama yangu ameuwawa kikatili sana na watu wote wakasema ni Neema tu ndiye amehusika na kifo cha mama yangu. Kiukweli niliumia san asana, yani niliumia kupita maelezo. Nilitaka kumtafuta Neema nimfungulie mashtaka akaozee jela huko ila mke wangu Rose akanishauri kuwa nisifanye hivyo na nisahau habari za Neema, nimejitahidi kuzisahau hata na mtoto aliyemzaa habari zake zilipotea kwenye akili yangu ingawa kuna baadhi ya ndugu zangu walikuwa wananishauri nimtafute mwanangu, ila napenda sana kusikia ushauri wa mke wangu na aliniambia nisifanye hivyo kwani hakuna ushahidi wowote kuwa ni mwanangu. Ila leo umenikumbusha mbali sana, kwakweli Maria mwanangu nakumbuka kifo cha mama yangu. Naomba unikutanishe na mama yako aniambie kwanini alimuua mama yangu kikatili kiasi kile”
Salome loe alimuangalia kwa makini huyu mzee aliyeonyesha anaongea kwa kujiamini kabisa halafu anaonyesha kamavile akili yake ipo salama kabisa kwa siku hii, Salome alijikuta akisema,
“Sasa huyu ndio mzee Patrick ninayeweza kuongea nae kwasasa”
“Sikuelewi”
“Utanielewa tu, kwanza tambua kuwa mama yangu hakuhusika na kifo cha bibi ila ukweli wote utaupata kwenye ndoto”
“Kwenye ndoto?”
“Ndio kwenye ndoto”
“Kivipi?”
“Subiri”
Salome alitoka nje na baada ya muda kidogo akarudi ndani na kitu kidogo kama kipande cha mkaa kisha akampa Patrick atafune naye akafanya hivyo halafu akamwambia,
“Leo ukilala utaona kila kitu kama sinema jinsi mama yako alivyouwawa”
“Mmmh kwani wewe mwanangu ni mganga wa kienyeji?”
Salome akacheka na kumuuliza,
“Mbona nilivyokupa dawa utafune hukuniuliza chochote? Mimi si mganga baba, ila fanya vile nilivyokuelekeza”
Patrick alitamani hata aende akalale muda huo ili kama hiyo ndoto aipate muda huo kwani miaka yote alikuwa akifikiri kuwa Neema ndiye aliyemuua mama yake ndiomana hakupenda hata kumuona na wala kile kitendo cha kwenda kwa Neema hakijui maana kilifanyika kwa namna nyingine. Patrick aliinuka pale sebleni na kumuacha Salome peke yake kisha yeye akaelekea chumbani.
Siku ya leo hii Neema alitoka nyumbani kwake na kwenda kumtembelea rafiki yake, ambaye alimshangaa kwa mabadiliko ya muda mfupi,
“Mmmh nipe siri ya mafanikio shoga maana sio kwa kung’aa huko, halafu pale kwako mbona umehama bila kusema?”
“Ndiomana nimekuja nikuhadithie”
Kisha akamuelekeza jinsi yeye alivyokuta wameshahama na jinsi Ashura alivyomtumia ujumbe,
“Mmmh kumbe Yule mdogo wako ana upendo hivyo!”
“Ndio, nakushangaa tu wewe ulikuwa na mashaka nae”
“Kwakweli nisiwe mnafki, sijawahi kumuelewa Yule mdogo wako na sijawahi kumuamini kabisa. Yani kila alichokuwa akiongea nilikuwa nakitilia mashaka, eti leo hii ndio amekutafutia nyumba nyingine ya kukaa mmmh”
“Na zaidi ya yote baba yake Salome yani Yule alikuwaga mume wangu, amejirudi yani kawa mpole huyo balaa. Aminiomba msamaha na amesema yupo tayari kumlea mtoto wake”
“Ila wanaume bhana, kaona mtoto amekuwa ndio kujifanya yupo tayari kumlea mtoto wake. Ila napo ni vizuri, halafu kitu kingine, mbona Salome simuoni shule?”
“Na hilo ndio jambo lingine limenileta ili unipe ushauri, Salome hataki shule kwasasa, unaweza kuamini hilo? Salome amesema anataka kupumzika kwahiyo nimuombee ruhusa ya ugonjwa, kwa kifupi Salome wangu hataki shule kwasasa”
“Kheee makubwa hayo, utaniletea niongee nae”
“Sawa nitakuletea maana wewe ndio mshauri wangu, na wakina Pendo wako wapi?”
“Wameenda kanisani”
“Kheee watoto wale kwa kanisa loh!”
“Ila ndio vizuri, na hakika hata wakina Salome wangependa kusali sidhani kama angekataa shule”
“Basi saivi hizo ibada ndio kama kituo cha polisi, mtoto hataki kabisa kuongelea habari hizo”
Mara akafika mgeni mwingine pale kwa mama Pendo ila huyu mgeni baada ya salamu kama alionyesha kumfahamu kidogo Neema yani ilikuwa kama kuna tukio ambalo alilifanya Neema halafu yeye analijua.
“Mmh hivi sio wewe ambaye mwanao alitumbukia kwenye kaburi!”
Neema nae alishtuka kuona kuna mtu anagundua kuhusu hilo jambo kwani yeye na Sa
lome kwenye msiba ule hakujua kama kuna watu wangetokea kuwafahamu,
“Kwani na wewe ulikuwepo kwenye ule msiba?”
“Ndio nilikuwepo, na lile tukio lilikuwa la kushangaza sana. Nakukumbuka vizuri sababu mimi ndiye ulinikuta pale njiani na nikakwambieni tunaenda kwenye msiba wa Moza, mkashangaa pale kuwa Moza amekufa kisha tukaaanza kuongozana kuelekea makaburini’
Ndio Neema nae alipoanza kukumbuka hilo tukio na kuona ni kweli kabisa kama ni yeye lazima awe anamkumbuka vizuri,
“Vipi mwanao hali yake maana kila mtu alipigwa na bumbuwazi pale msibani”
“Mwanangu amepona wala sikutaka kurudi tena kule zaidi zaidi kwenda na mwanangu nyumbani”
“Hata mngerudi kule kuna kilichokuwa kinaeleweka basi! Yalitokea makubwa sana, mwili wa marehemu ulitoweka na hadi leo hakuna anayejua kilichoendelea labda ile familia tu. Ulitokea upepo wa gafla pale makaburini na kila mmoja akikimbia na lwake. Kwakweli hali ilikuwa mbaya sana”
“Duh poleni sana, kwahiyo marehemu hakuzikwa?”
“Azikwe vipi na hata mwili wake haujaonekana”
Mama Pendo ikabidi aingilie kati maana haya maelezo hata yeye yalimchanganya kabisa,
“Unataka kuniambia Salome alitumbukia kwenye kaburi”
“Ndio alitumbukia halafu akazimia”
“Yani Neema umekaa tu na mtoto na alipatwa na makubwa kiasi hiko, anakataa shule unakaa nae tu hujiulizi! Mlete nimpeleke kwenye maombi”
“Nitajaribu kumwambia kama atakubali”
“Wewe ni mama yake bhana, atakubali tu”
Neema aliitikia pale ila hakuwa na namna ingawa Salome alimwambia kuwa wafanye siri ila atafanyaje na mambo yameshakuwa kama hivyo yani kuna watu wanamkumbuka vyema. Aliaga muda huo na kuondoka zake.
Rose alikuwa amevurugwa kabisa akili na gari alikuwa anaendesha ilimradi tu, kitendo hicho kilimfanya afike nyumbani kwake saa tano za usiku, aliingiza gari ndani na kushuka kisha akaenda sebleni kwake ila akakumbuka lile begi lenye hela akaamua kwenda kulichukua kwanza kabla na lenyewe haljachukuliwa. Cha kushangaza muda huu alienda kuliangalia mule kwenye gari hakuliona na kumfanya achanganyikiwe tena,
“Jamani, begi langu limeenda wapi tena?”
Akamuuta mlinzi kwa nguvu na kuanza kumuuliza kama ameona begi ila mlinzi alikuwa akimshangaa tu maana ni muda huo huo ameingia sasa huyo mlinzi alione begi na kulichukua aende nalo wapi.
“Mi sijaona begi mama”
“Inamaana limeibiwa na nani sasa?”
“Labda huko huko ulipotoka mama lakini hapa hakuna hata mtu mmoja anayeweza kufungua gari na kuiba”
“Hebu niondokee hapa”
Rose alijikuta akifoka tu kisha kwenda tena ndani na akiwa na mawazo lukuki kuwa begi limepotea tena kwa mara nyingine, hakukaa sana sebleni kwani watu wote kwenye nyumba yake walikuwa wamelala hivyo akaamua kwenda chumbani kwake na kumkuta mumewe akiwa amelala hoi,
“Huyu nae kalala kama mzigo leo, na wala simuamshi atajijua mwenyewe saivi nina mawazo yangu”
Akawaza pale cha kufanya kwa usiku ule ila hakupata jibu kabisa na alijiona kama sijui kitu gani ila wazo lingine likamtuma kuwa aende chumba alichokuwa analala Moza ili akapekue kitu Fulani, hakutaka kupuuza wazo hilo na moja kwa moja akaenda chumba alichokuwa analala Moza ila alipofungua mlango alimuona mtu amekaa amempa mgonga, kwa mashaka zaidi Rose aliuliza,
“Wewe ni nani?”
“Ni mimi”
“Ni nani wewe?”
Yule mtu akageuka na kumfanya Rose aanguke na kuzimia, na ilikuwa ni mara ya kwanza katika maisha yake kuzimia kwa muda mrefu kama siku hiyo.
Kulipokucha Rose alijikuta kitandani kwake na kuanza kujiuliza kuwa mara ya mwisho alikuwa wapi na mbona amepatwa na kitu ambacho hakijawahi kumpata maishani mwake,
“Yani na mimi Rose nalogwa? Haiwezekani yani haiwezekani kabisa”
Rose akakumbuka mara ya mwisho alienda kwenye chumba alichokuwa analala Moza na alimuona mtu ila sura ya Yule mtu alipogeuka hakuiona vizuri zaidi ya kuzimia. Hasira zikampanda na kujiuliza kuwa ni nani anayecheza na akili yake, akataka kuita familia yake yote sebleni siku hiyo ili ajue kinagaubaga kuwa ni nani anacheza na akili yake. Akatoka sebleni ila akagundua kuwa watu wake wote bado hawajaamka ukizingatia hata Patrick amemuacha kwenye usingizi wa hali ya juu, alianza kuita mmoja mmoja na waliokuja sebleni kwa muda huo walikuwa ni wale mapacha na Ana, akauliza kwa hasira
“Wengine wako wapi?”
“Wakina nani mama?”
“Sara na baba yenu?”
“Kuhusu Sara sidhani kama amelala hapa nyumbani jana”
“Mnasemaje nyie?”
“Hatukumkuta mama, sidhani kama amelala hapa nyumbani jana”
Rose akashikwa na hasira na kwenda chumbani kwa Sara, akafungua ila hakumkuta Sara na kumfanya apate jibu kuwa ni kweli Sara hakulala nyumbani kwa siku ya jana,
“Huyu mtoto ameanza kunichezea akili eeeh! Atalalaje nje ya nyumbani, atalalaje nje ya nyumba yangu!”
Akarudi tena sebleni kwa hasira, na kuuliza
“Ni nani alilala chumba cha Moza jana?”
“Mmmh mama, nani anayeweza kulala mule zaidi ya Yule binti Salome. Na toka ameondoka siku ile hajaja tena”
Akawaangalia wale wanae mapacha na kuwauliza,
“Ni nini mnajua kuhusu mimi?”
“Hatujui chochote mama”
“Mna uhakika?”
“Ndio hatujui chochote”
“Haya mnaweza kuondoka, na wewe Ana mwanangu unaweza kwenda kujiandaa na kwenda shule najua hata wewe unachukizwa na hali hii mwanangu”
Rose akaondoka na kuelekea chumbani, ila wale mapacha kabla nao hawajaondoka walishangaa kumuona Sara na Salome wakitokea njia ya vyumbani, na kushangaa
“Inamaana dada Sara ulikuwa chumbani?”
“Ndio, jana nililala na Salome chumbani kwa Moza”
Wale mapacha wakatazamana maana mama yao aliwauliza kuwa ni nani alilala kwa Moza jana na hawakuwa na jibu.
Kwa upande wa Rose, aliingia chumbani kwake na kumuamsha Patrick ila la kushangaza leo Patrick alivyoamka aliinuka na kumuwasha kibao Rose kisha akamwambia,
“Yani wewe mwanamke umeniulia mama yangu!”
Kabla Rose ajajitetea, alishangaa akipigwa kofi jingine.
Itaendelea kesho usiku…….!!!!!!!
By, Atuganile Mwakalile.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: