KURUDI KWA MOZA: 17 Kwahiyo sebleni alibaki Salome na Patrick, kisha Salome akamuangalia vizuri Patrick na kumuuliza, “Hunitambui mimi!” Patrick alikuwa kimya tu, ila Salome akamsogelea karibu na kumkazia macho. Mzee Patrick akashtuka na kusema, “Aaaah kumbe Moza!” Akaanguka chini na kuzimia. Salome alihakikisha ile sauti wengine wote hawajaisikia pia alimpulizia Yule mzee maji na kumfanya azinduke muda ule ule, ila alipozinduka sasa alikuwa na swaga mpya kwani alimsogelea Salome na kumwambia, “Nisamehe mwanangu, jamani nisamehe wewe ni mwanangu. Damu yangu jamani nisamehe, nisamehe kwa kipindi chote bila kuwa karibu na wewe nisamehe sana mwanangu. Nataka unipeleke na kwa mamako nikamwombe msamaha” “Usijali nitakupeleka” Kisha Mr. Patrick akawaita tena wote sebleni, na walipokuja aliwaambia, “Jamani huyu ni ndugu yenu, naomba tumpende” Halafu akainuka na kutoka nje ya nyumba, kwakweli hichi kitendo kilimkera sana Rose yani alitamani sijui afanye kitu gani, alimuangalia Salome kwa hasira sana, ila alipotoka nje ili kumuangalia mume wake alikuta ameshaondoka, “Yani leo Patrick ameondoka bila ruhusa yangu? Nitamfundisha huyu Salome na atanijua mimi ni nani” Rose alirudi tena ndani akiwa na hasira sana na moja kwa moja akaenda chumbani kwake. Watoto wake walikuwa sebleni wakijadiliana kasoro Ana, “Mmmh nyie huyu mzee kama anakuwaga anaugua vile, kwajinsi alivyofanana na huyu dogo anaanzaje kumkataa!” Walijadiliana na kuondoka kisha wakamuacha Salome akiwa na Sara, halafu Sara akamwambia Salome “Usijali hata nyumba nzima ikikutenga jua ya kwamba nitakuwa pamoja na wewe” “Nashukuru” Kisha Salome akamuaga Sara kuwa anatoka kidogo, basi akaondoka kumbe mr.Patrick aliwekwa nje ya geti akimsubiria Salome, na alipotoka aliingia kwenye gari ya Patrick kisha safari ya kwenda nyumbani kwao ikaanza. Walifika nyumbani kwakina salome na kumkuta Neema akiwa anafanya usafi, kwakweli nae alishangaa sana kumuona Patrick akiambatana na Salome ila aliwakaribisha ndani hivyo hivyo cha kushangaza Patrick alianza kwa kupiga magoti na kuomba msamaha kwa Neema, “Nisamehe Neema, naomba unisamehe. Nisamehe sana, nimefanya makosa makubwa sana, sikumtambua mwanangu naomba unisamehe” Kwajinsi Patrick alivyokuwa anatia huruma ikambidi Neema amuhurumie kwani hajawahi kuwaza kama ipo siku Patrick atakuja na kumpigia magoti ya kumuomba msamaha. Neema akamshika mkono Patrick na kumkaribisha kwenye kochi, “Usijali Patrick, yale yamepita ni mapito tu na nimeshasahau. Mtoto amekua sasa na amekutambua” “Kwakweli moyo unaniuma sana yani sana, kumkosa mwanangu mpendwa kwa kipindi chote hiki. Nisamehe kabisa Neema” Kisha Patrick akamuuliza Neema kuhusu pale anapoishi na alimwambia kama alipanga, kwakweli Patrick alisikitika sana maana nyumba nyingi tu alikuwa nazo ila mwanamke aliyezaa nae amepanga, akamuahidi kumpa nyumba moja. “Kweli utanipa?” “Ni haki yako Neema, kila kitu change ni haki yako. Nitakuja tu nikukabidhi” Muda huu Salome alikuwa chumbani kwake ila gafla akashtuka na kusema, “Muda umeisha, itabidi nimtoe huyu mzee haraka sana mpaka kwa wakati mwingine” Basi akatoka chumbani na kumuomba baba yake kuwa waondoke, ila Patrick alitoa begi lake na kumpatia Neema pesa zote zilizokuwepo kwenye begi hilo wala yeye hakuzihesabu ila alimpa Neema pesa zote na begi lake kisha akaondoka na Salome ambapo Salome alishuka mahali na kumuacha akiendelea na safari zake zingine. Salome alienda kwanza kule walipokuwa wanaishi mwanzo na kumuomba mama mwenye nyumba asiweke mpangaji mwingine mpaka miezi miwili iishe kwani wao walikuwa na hatihati ya kurudi na ukizingatia kodi yao ilikuwa bado kuisha ikabidi mama mwenye nyumba asikilizane nao kumbe Salome alifanya vile ili kuepusha wale wakija wasikute mtu katika nyumba ile. Kisha Salome akarudi tena kwa mama yake ili akahesabu nae pesa zilizokuwemo kwenye lile begi. Rose akiwa na hasira sana, kwanza alipoingia chumbani kwao na kufanya mambo yake akagundua kitu. Akagundua kuwa Patrick aliondoka na gari yake ambapo kwenye gari hiyo aliweka begi lenye pesa ili akawalipe wajenzi kwenye saiti yao na lile begi aliliweka asubuhi ya siku hiyo akiwa na lengo la kumaliza yale mazungumzo ajiandae na kwenda saiti ila sasa Patrick alishaondoka na lilke gari lenye begi, “Mungu wangu, Patrick kaondoka na lile begi eti! Na hivi akili yake haipo sawa litakuwa limepona kweli? Ila natumai limepona maana sidhani kama anaweza kufanya ujinga.” Ikabidi Rose ajiandae haraka haraka na kuelekea saiti. Kufika kule alimkuta Patrick amekaa chini ya mti, akamshtua na Patrick alishtuka sana kama kashtuliwa na kitu gani. Swali la kwanza ambalo Rose alimuuliza Patrick, “Kwanini umeondoka na gari yangu?” “Hata mimi mwenyewe nashangaa sijui hata imekuwaje nimeondoka na gari langu” “Natumaini hujafanya ujinga” “Ujinga gani tena?” Rose akainuka na kwenda kuangalia begi la hela kwenye gari, ila lile begi halikuwepo. Kwakweli Rose alikuwa na hasira sana na kumuuliza tena Patrick, “Begi la hela liko wapi?” “Begi! Begi lipi?” “Inamaana hukuona begi kwenye gari hilo?” “Sijaona begi” “Patrick usinitanie na hela zangu, tafadhali begi langu liko wapi?” Patrick alionekana pia akishangaa yani kama mtu anayeonewa vile kwani ilionyesha wazi hajui begi la hela limeenda wapi. “Patrick, Patrick. Begi la hela limeenda wapi?” “Sijui kweli mke wangu unanionea tu” “Nakuonea kitu gani, haya sasa tutawalipa nini hawa mafundi?” “Kachukue hela nyingine benki tuwalipe” “Hivi wewe Patrick una matatizo gani? Yani unarahisisha tu. Haya twende nyumbani ndio utanieleza vizuri” Akapanda kwenye gari kisha Patrick akawa gari ya mbele akiongoza kwenda nyumbani halafu Rose akiwa nyuma yake, kwakweli Patrick alikuwa haelewi kabisa kwa muda huo kuwa begi limeenda wapi na kwenye begi kulikuwa na kiasi gani. Salome alienda tena kwa mama yake ambaye bado alikuwa akitetemeka tu kuziangalia zile hela za kwenye begi, “Usitetemeke mama, ni zako hizo” “Mmmh mwanangu ni miujiza hii” “Usiwe na mashaka mama yangu, nimekuja nikusaidie kuhesabu” Basi wakaanza kuhesabu zile hela wakakuta ni milioni thelathini na tano, kwakweli Neema alipagawa kabisa kwani hajawahi kushika hela za namna hiyo katika maisha yake kwahiyo alihisi kuchanganyikiwa. “Sasa mwanangu nafanyaje? Nizipeleke benki!” “Usiwe na haraka mama, benki tutazipeleka kwa utaratibu. Usizipeleke hivyo kwa mkupuo, na huo wasiwasi wako watahisi hata umeiba. Nitakupekea mwenyewe benki, yani wewe hata usiwe na mashaka” Haya mambo Neema hakuyaamini kabisa na kwake yalikuwa kama ndoto vile hadi alijikuta akitetemeka tu, na kumfanya ashindwe kumuuliza maswali zaidi Salome kwani aliona kama kawa mokozi wake kwa kipindi hiko. Alijikuta akimwambia, “Salome, ni kweli nimekuzaa na nimekulea ila sikutegemea kama kuna siku ungeweza kuja kufanya kitu cha namna hii. Baba yako nimemsamehe na nimefuta yote aliyonitendea, yani yote kabisa nimeyafuta. Kwahiyo mwanangu unaenda tena kwa baba yak oleo?” “Siendi leo mama, nitaenda keshokutwa hadi nikamilishe hizi hela zako kukuwekea benki. Hata usiwe na mashaka mama yangu” Neema alifurahi kusikia hivi na kisha Salome alikaa na mama yake huyo na kumueleza utaratibu watakaotumia kuziweka hizo hela benki. Patrick na Rose walifika nyumbani ila kwakweli Rose alikuwa na hasira sana kwa kile kilichofanywa na Patrick kuondoka na gari lenye begi la hela na eti kujifanya hajui begi limeenda wapi, akaenda moja kwa moja na Patrick chumbani kisha akaanza kumuuliza tena, “Patrick, hebu kumbuka vizuri begi limeenda wapi?” “Hata sijui mke wangu yani sijui kabisa” “Hebu kwanza niambie ulipotoka hapa ulienda wapi?” “Yani ninachokumbuka ni kuwa nimejikuta tu nipo kule saiti, nikaa chini nikawa najifikiria bila kupata jibu kuwa nimeenda kule kufanya nini. Na mara ukaja wewe yani sielewi kabisa” “Haya, vipi kuhusu kumkubali Salome wakati mimi nimekwambia umkatae Yule mtoto!” “Pale nakumbuka ndio, Yule mtoto nilimkataa ila nilikuja na kumkubali. Unajua ni mwanangu Yule!” “Hivi wewe Patrick una nini lakini? Yule kawa mwanao tangia lini jamani? Mwanao wewe si Ana!” “Yule ni mwanangu Rose” “Yule si mwanao, inamaana hunielewi au” Rose akampulizia kitu uoni na Patrick akapatwa na usingizi na kulala. Kisha Rose akatoka sebleni, mara akaingia ndani Sara akiwa ameambatana na ommy, kwakweli Rose alivyowaona alichefukwa sana ukizingatia akili yake ilishavurugika kwa wakati huo, “Na wewe kijana mwanga unataka nini nyumbani kwangu?” Ommy alianza kwa kumsalimia ila Rose hakuitaka salamu ya Ommy zaidi ya kumfukuza tu nyumbani kwake, ikabidi Sara aingilie kati, “Mama jamani, utamfukuzaje rafiki yangu?” “Sara, hii ni nyumba yangu sio nyumba yako unanisikia! Sitaki ujinga kwenye nyumba yangu” “Lakini mama huyu Ommy ni rafiki yangu” “Kama ni rafiki yako ishia nae huko huko sio nyumbani kwangu tena usinikere” Sara alibaki tu anamshangaa mama yake, lakini Rose alipoona wamesimama tu wakimshangaa akainuka na yeye na kumsukumia mlangoni Ommy ambaye alijikwaa kwenye mlango na kuaguka kisha damu zikamtoka ikabidi Sara ainame pale alipoangukia Ommy na kuanza kumsaidia kwenda nje ila kabla hawajafika getini Ommy alionekana akianza kuugulia kichwa ni kitu ambacho kilimshtua sana Sara na kumfanya akimbilie ndani ili akamletee huduma ya kwanza ila aliporudi hakumkuta Ommy, alimuita lakini hakumsikia sehemu yoyote ikabidi fike getini na kumuuliza mlinzi, “Eti Ommy ametoka hapa?” “Nimemuona tu akiingia ila kutoka sijamuona” “Mungu wangu jamani, Ommy atakuwa ameenda wapi wakati alikuwa anaumwa. Hivi hukumuona kama nakokotana nae pale na alilala pale chini?” “Sijawaona kabisa madam yani hata mimi unakuja kuniuliza muda huu nashangaa tu” Sara akaangalia kwa makini pale ambapo alilala Ommy kwani alijua lazima damu zitakuwa zimebaki na kama kaelekea mahali basi ataona matone ya damu ila alipoangalia hakuona damu yoyote na hadi alipoingia ndani pale alipojigonga ommy hakuona damu yoyote. Kwkweli hiki kitu kilimuumiza sana Sara kwani hakuelewa kabisa aliona kama ndoto kwa ommy kutoweka mbele ya macho yake mwenyewe. Akataka kumuuliza mama yake ila hakumkuta sebleni na alienda kumgongea mlango chumbani kwake ila hakuitikiwa na kujiuliza inamaana mama yake amelala kwa muda mfupi huo, hakupata jibu kwakweli na alibaki anashangaa tu ila bado alikazana kumuita mama yake ili ampe jibu. Rose alichoshwa na kelele za Sara, na baada ya lisaa limoja rose alitoka ndani na kumfata Sara alipokuwa kisha akamuangalia kwa jicho kali sana na kuanza kumvuta hadi chumbani kwa Sara kisha akamwambia, “Laiti kama ungejua leo ninavyojisikia au yaliyonitokea wala usingethubutu kunipigia kelele” “Sasa mama yaliyokutokea yanamahusiano gani na kupotea kwa Ommy!” “Hivi unajua leo nimepoteza kiasi gani cha pesa? Unajua! Yani wewe mtoto tafadhali niache usitake kukorofisha akili yangu kabisa” “Basi mama niambie alipo Ommy wangu” “Kwahiyo mimi huyo Ommy wako nimemla au? Wewe mtoto wewe hebu niache” Rose akatoka na kumfungia Sara mlango kwa nje ambapo alikuwa akiugonga tu bila ya mafanikio yoyote. Rose akaenda zake sebleni na baada ya muda watoto wake walianza kurudi na wote wakawa pale sebleni na kuzisikia kelele za Sara kuwa afunguliwe, wale mapacha walimuhurumia sana dada yao, “Mama jamani, msamehe dada Sara, nadhani hatorudia tena” “Hebu na nyie niacheni” Gafla ikasikika sauti kali sana ya kelele za Sara ikisema, “Mozaaaaaaaaa” Na gafla kukawa kimya kabisa. Itaendelea kesho usiku……!!!!! By, Atuganile Mwakalile.

at 10:59 AM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top