KURUDI KWA MOZA: 16 Mara wakasikia sauti ya Sara ikiongea kwa nguvu tena kwa ujasiri, “Sasa huyu ndio kiboko ya Ana” Ikabidi watoke ili wakamuone huyo kiboko ya Ana, kwakweli Rose alishtushwa sana kumuona Salome. Kitendo cha Rose kumuona Salome kilimkosesha furaha na kujikuta akipatwa kama presha na kuanguka kwani mawazo yake ilikuwa ni Salome amekufa kwahiyo kitendo cha kumuona akiwa mzima kilimshangaza kabisa. Watoto wake wote walimfata pale chini na kumpeleka chumbani ambako walimuwashia feni ilia pate upepo na wazo hilo la kumuwashia feni walilipata kwa Ana, kisha wakarudi sebleni na kumuacha Ana akiwa chumbani na mama yao. Katika watu ambao walikuwa hawaelewi kinachoendelea ni Patrick maana yeye aliona kila kitu ni cha ajabu tu hapo, alikuwa akimuangalia Salome kama mgeni kabisa machoni pake ila Salome akamtoa mashaka, “Usiniangalie hivyo, mimi ni mtoto wako” “Nakuangalia sababu sielewi elewi” “Mimi ni mtoto wako, na mama yangu ni Neema” “Yeye yuko wapi?” “Sijaja nae sababu alikuwa hataki nije huku” Patrick alimuangalia Salome na kujikuta akimsogelea na kumkumbatia, “Kumbe nina binti mkubwa tu” “Ndio ni mimi mtoto wako” “Karibu sana hapa nyumbani” “Asante” Muda watoto wa Rose wanarudi sebleni ni muda ambao Salome alikuwa anaondoka na kuelekea chumbani, wote wakajikuta wakisimama na kumuangalia ataelekea kwenye chumba kipi ila alielekea kwenye chumba kile alichokuwa analala Moza. Hapo iliwashangaza sana kwani hawakutegemea kama Salome angeelekea kwenye chumba cha Moza, na baada ya muda akarudi sebleni na kuwakuta wamekaa. “Nimeshaenda kuweka begi langu” Pacha mmoja akamuuliza Salome, “Mbona chumba cha kulala umeenda bila kuonyeshwa na yeyote?” “Mbona hapa nilishawahi kuja kipindi yupo dada Moza! Nishawahi kuja hapa, najua kila sehemu. Vipi leo tunakula nini?” Wote walikuwa kimya ila huyu mgeni wa leo aliwashangaza sana kwani alikuwa na mambo ya ajabu ajabu, kafika tu mara mama yao kazimia, mara anaenda chumbani bila kuonyeshwa saivi anawauliza watakula nini, na alipoona kimya alienda yeye jikoni kupika. Kila mtu alikuwa kimya hata Sara mwenyewe alikuwa kimya kabisa. Rose alipozinduka bado alikuwa na mkaranganyiko wa mawazo kwani bado hakuelewa kitu chochote, akachukua simu yake na kuanza kumpigia Ashura lakini haikupatikana. Akachukua tena simu na kuwapigia wale vijana, kisha akaongea nao “Hivi nyie mmenifanya nini? Si mlisema Yule mtoto mmeenda kumtupa mbali na hakuna wa kumuokoa iweje anaonekana tena nyumbani kwangu” Wale vijana wakamuelezea ilivyokuwa kisha rose akawatuma waende pale alipokuwa anaishi Ashura ili kama yupo wamkamate mpaka aseme ukweli. Alipokata tu ile simu akashangaa akipata ujumbe kutoka kwa Ashura, “Samahani dada yangu, mimi sikuona kosa la huyu mtoto Salome na sikuona kama bi vizuri kumuua. Wale vijana niliwawekea mbwa kwenye kile kiroba ili wakuaminishe kuwa ni kweli nilimuua Salome ila kiukweli Salome sikumuua na mimi nimeondoka sipo kabisa mjini nimeenda kijijini kweli na sitaki tena kujishughulisha na hizo kazi zako.” Kwakweli ujumbe huu aliusoma mara mbili mbili bila ya kumaliza na akiwa haamini kile anachokisoma kuwa Ashura anaweza akamgeuka namna hiyo, akaamua amtumie ujumbe pia, “Ashura unajifanya umesahau tulivyoahidiana, hivi ningesema ukweli wa mambo yako na wewe ungeweza kukaa huko unapokaa? Mbona wewe pia una maovu mengi Ashura, umesahau Yule mganga babu ni wewe ndiye ulinipeleka? Umesahau hawa wasichana niliowafunga humu ndani ni ushauri wako, eti leo unajifanya kunigeuka Ashura! Kwanza jina lako sio Ashura wewe ila subiri nitakupata tu, mimi nina pesa” Muda kidogo akajibiwa, “Pesa zako wala hazinibabaishi hata mimi nina pesa, tena kwa taarifa yako ni mimi nimemueleza ukweli wote huyo Salome kuwa baba yake ni Patrick kwahiyo usishangae akija kuishi hapo. Ukweli wote nishamwambia, ujipange upya na hunipati ng’ooo, hao misukule uliowatunza utajijua nao mwenyewe” Rose alichukizwa sana na ujumbe huu ila kila alipojaribu kupiga simu hiyo namba ya Ashura haikupatikana, yani alichukia hadi akarusha simu yak echini. Kwa upande wa Salome ilikuwa furaha sana kwake na alijikuta akigundua siri nyingi sana za Rose maana muda wote Rose alijua anayejibishana nae kwenye ujumbe mfupi ni Ashura kumbe kuna mtu mwingine, na huyo ashura mwenyewe ni marahemu wa muda mrefu sana. Salome alikuwa ameingia na chakula chumbani na alikuwa anakula humo, mara Sara alienda kumgongea na kuingia ila alipomkuta anakula chumbani alishtuka sana, ikabidi Salome amuulize ameshtuka kwasababu ipi, “Hapa nyumbani hakuna mtu anayeruhusiwa kula chakula chumbani” “Mmmh kwanini?” “Sijui ni kwanini ila mama anakataa kabisa mtu kula chakula chumbani” “Hujui sababu kweli! Labda ungesema mama anaogopa panya watazaliana au mende watajaa. Ila ni leo tu haitajirudia kula chakula chumbani” “Na kwanini umechagua kulala chumba hiki?” “Sababu hiki ni chumba alichokuwa analala mpendwa wangu Moza, namkumbuka sana ndiomana nimekuja kulala hapa” “Ila unafikiri Moza tulimzika! Alitoweka kimiujiza” “Alitoweka!” “Ndio alitoweka, yani kuna binti alitumbukia kwenye kaburi walipompeleka hospitali basin a mwili wa Moza ulipotea” “Maskini Moza wangu, kwahiyo hakuna kaburi la Moza!” “Ndio hakuna” “Kwa staili hiyo inamaana basi Moza hakufa, labda kwa mfano hakufa!” “Mmmh usiongee habari hizo, mimi ni muoga nitashindwa kulala hapa usiku” “Basi usijali” “Ila huku ndani kuwa nako makini sana, ulisaidia macho yangu yakaona tena na mdomo wangu ukaweza kuongea ila chakula nilichopika siku ile kuna kilichopotea na sijui kimeenda wapi. Kuwa makini sana na humu ndani kuna mambo ya ajabu sana” “Usijali, nipo makini sana” Sara alijikuta akimpenda sana huyu Salome yani alimpenda sana kutokana na jinsi alivyomsaidia matatizo yake ya kurogwa na mdogo wake. Walipomaliza maongezi, Sara akamuomba Salome waende nae sebleni ambapo alifanya hivyo na pale sebleni walikuwepo wale mapacha na mr.Patrick ambae toka amerudi hakwenda kabisa chumbani kwa mke wake. Baada ya kimya kirefu pale sebleni, Salome akaanza kusema, “Hata hamniulizi jamani kuwa nimejuaje kama huyu baba ni baba yangu” Pacha mmoja akadakia, “Eeh tuambie umejuaje!” “Unajua mimi nimeishi bila kumjua baba kwa miaka yote hii mpaka sasa nilikuwa kidato cha tatu ila baba yangu simjui. Alipotokea msamalia mwema na kuniambia kuwa huyu ni baba yangu nilifurahi sana ndiomana sikutaka hata kupoteza muda zaidi ya kuja hapa ili nifurahi na ndugu zangu wengine. Jamani ndugu zangu, mimi ni ndugu yenu ni mtoto wa Mr.Patrick kama mlivyo nyie” Mmoja akahamaki, “Wewe si ulituambia pale kuwa wewe ndiye mtoto wa pekee wa mzee Patrick, haya saivi unasema na sisi ni watoto wa huyu mzee. Hapana, sisi ni watoto wake wa kambo. Labda Ana sijui” Sara akadakia, “Ana nae ana baba yake mwingine, ni hakika kabisa wewe Salome ndiye mtoto wa pekee wa baba” Mama yao akiwa ameambatana na Ana walitoka chumbani na waliisikia vilivyo kauli ya Sara na iliwakera sana. Rose kabla ya kukaa alianza kwa kumuuliza Sara, “Hivi wewe Sara una nini wewe? Kitu gani kinakuwasha mdomoni kwako?” Kisha Rose alikaa na kumuangalia Salome na kusema, “Haya na wewe nani kakukaribisha kwenye nyumba hii?” “Nimekuja kwa baba yangu” Salome alijibu kwa kujiamini kabisa. “Sikuelewi” “Mamdogo Ashura kaniambia kuwa hapa ni kwa babangu, hata ameshakwambia kuwa nakuja hapa” “Kwahiyo hapa kwangu unalala chumba gani sasa?” “Kile chumba alichokuwa analala dada Moza” Rose akamuangalia mume wake na kumwambia waelekee chumbani ana mazungumzo nae, kwahiyo sebleni walibaki watoto tu. Ambapo Ana alimuangalia Salome na kumwambia, “Utaondoka kama ulivyokuja, hakuna anayekutambua hapa. Ndiomana unalala chumba cha marehemu” Kisha akaenda zake chumbani kwake, ila Sara alimuangalia Salome na kumwambia, “Hata usijali, nitakuwa na wewe bega kwa bega” Wale mapacha wakainuka na kwenda chumbani kwao ila Sara aliinuka na Salome na kumkaribisha Salome kwenye chumba chake, “Humu ni chumbani kwangu Salome, muda wowote unaruhusiwa kuingia. Ukiwa na shida ya kitu chochote unaruhusiwa kuja kuchukua” “Asante dada” “Nimefurahi sana kupata mdogo mwenye upendo kama wewe, kwanza umeniponya macho yangu na mdomo wangu. Halafu ngoja nikuhadithie kitu bhana” Basi Sara akaanza kumueleza Salome jinsi Ana alivyokuwa akishangaa mwalimu wake amepona kimiujiza, “Niambie Salome, ni wewe uliyemsaidia Yule mwalimu” Salome akacheka kidogo, “Hapana bhana si mimi ila nimefurahi kusikia kuna mtu alifanyiwa hivyo na amepona pia” “Mmh si wewe kweli! Sasa mimi ulijuaje kama naumwa?” “Nilioteshwa na nilioteshwa dawa za kuja kukupa ndiomana nimekwambia hawatakusumbua tena” “Ila mimi nimefurahi sana umekuja kuishi hapa, naomba uishi hapa milele yote” Salome akacheka tu na kufurahi pale na Sara kisha usiku ulipoingia alimuaga na kwenda kulala kwani nyumba hiyo huwa chakula kinakuwa mezani na mwenye njaa anaenda kula mezani na kama siku hiyo hakijapikwa basi kila mmoja anajijua mwenyewe. Salome akiwa chumbani kwake aliona ujumbe kwenye simu ya Ashura ukionekana umetoka kwa wale vijana, “Sista mbona umefanya tupate lawama, ila mbona hupatikani hewani? Sasa ni mtu gani Yule tuliyemtupa kama sio Yule mtoto? Mama ametupa oda kuwa twende kwenye ile nyumba na tumalize yeyote tutakayemkuta pale” Ujumbe huu ulimchanganya sana Salome, akawaza kwanza cha kuwaambia hawa vijana kisha akawatumia ujumbe, “Basi kama nyie mnataka kuwateketeza wale wote ngojeni kwanza, msiende hivi karibuni. Subirini mpaka mwezi upite” ‘Haiwezekani sista, sisi tunataka pesa na si vinginevyo” “Hatakama mnataka pesa, kumbukeni Yule Rose ni dada yangu, kwahiyo msifanye kitu chochote bila kuwaruhusu mimi. Yule Rose ametumia hasira tu” “Kwahiyo tusubiri hadi lini?” “Subirini hadi keshokutwa” Wakamjibu tu poa, na hapo Salome akawaza cha kufanya maana ingawa kaihamisha familia yake ila waliohamia hapo watapata matatizo kwahiyo alikuwa anafikiria cha kuweza kuwasaidia na wale wengine. Ila kabla hajalala, alianza kupekua kwanza vitu vya mule ndani ambapo alipata kijitabu kidogo ambacho kimeandikwa vitu vya maelekezo yaliyokuwa kama historia hivi ya mtu aliyeonekana ameandika hicho kitabu. Kurasa ya kwanza kabisa akaona, “Nimeanza kazi leo kwenye hii nyumba ila usiku nilipolala nimegundua kuna chumba walichowekwa wadada wawili kama misukule. Natakiwa niwasaidie watoke” Salome alisoma mara mbili mbili sehemu hiyo na kuwaza jambo Fulani ila kabla hajaendelea na kile kitabu, alikuja Sara chumbani kwake ikabidi kile kitabu akiweke pembeni, Sara akaanza kumwambia Salome, “Naomba tukalale wote chumbani kwangu” Salome alikuwa anakataa ila Sara alimbembeleza sana hadi alikubali na kwenda kulala nae. Kulipokucha siku ya leo ilikuwa ni ya ajabu sana kwani Patrick aliwaita watoto wake wote sebleni kisha akaanza kuongea, “Salome, sikutambui kwahiyo naomba uondoke. Jamani hatuna undugu na huyu wakuitwa Salome, simtambui mimi” Salome akacheka kisha akamuangalia Rose na kumwambia, “Ndio mlivyohamua hivi!” “Ndio. Uondoke Salome, hakuna anayekutambua kwenye nyumba hii. Kama huyo unayedai ni baba yako hakutambui, je sisi tutakutambua?” “Basi naombeni nafasi kidogo niongee na huyu baba ndio nitaondoka” Wote walitoka pale sebleni kasoro Rose ila salome alimsihi aondoke ili yeye aweze kuzungumza na mzee Patrick halafu ataondoka, Rose alikubali kuondoka kwani alijua mzee Patrick hawezi kubadilisha maamuzi yake yoyote kutokana na alichomfanya usiku wa jana. Kwahiyo sebleni alibaki Salome na Patrick, kisha Salome akamuangalia vizuri Patrick na kumuuliza, “Hunitambui mimi!” Patrick alikuwa kimya tu, ila Salome akamsogelea karibu na kumkazia macho. Mzee Patrick akashtuka na kusema, “Aaaah kumbe Moza!” Akaanguka chini na kuzimia. Itaendelea kesho usiku………!!!!!1 By, Atuganile Mwakalile.

at 10:58 AM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top