Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 11 Wakati anaendesha gari akasikia sauti, “Rose, umenigonga nimekufa halafu kwenye maizishi yangu unakimbia!” Rose alishtuka na kusimamisha gari kwa haraka huku akiwa amejawa na hofu iliyomfanya ashindwe hata kutazama nyuma ya gari kuwa hiyo sauti inatoka wapi. Akiwa amejawa na hofu zaidi, ile sauti ikajirudia tena, na kumfanya Rose ashuke kabisa kwenye gari ile, alipokuwa chini akatazama kwenye kioo cha gari gafla alimuona kama Yule babu yupo ndani ya lile gari. Uoga ulizidi kumshika Rose na kujikuta akiacha gari kisha kuanza kukimbia hovyo, alikimbia sana hadi akachoka kwakweli. Alifika kwenye mti mmoja na kukaa chini yake huku akiwaza kuwa alikuwa anaota au ni vipi maana yale mambo yalikuwa kama ndoto. “Hivi ni kweli au naota? Lakini mimi uoga umeanza lini kwangu? Hivi mi naweza kuwa na uoga wa namna hii kweli? Ningeweza kuwafuga wale wajinga wangu? Hapana kwakweli, mimi ndio mimi uoga kwangu ni mwiko” Akainuka na kuanza safari ya kurudi kwenye gari yake ila aligundua kuwa ni mbali sana ameiacha hiyo gari. Alitembea kwa umbali mrefu sana hadi kuifikia, alivyofika alikuwa amechoka vilivyo, akafungua na kuingia ndani ya gari yani ingawa milango ya gari hakufunga na funguo ila ilionyesha wazi hakuna mtu aliyeingia kwenye gari ile kwani kila kitu alikuta kama kilivyo. Aliendesha gari na kwenda moja kwa moja hotelini, hakutaka kwenda nyumbani kwake kwanza kwahiyo aliamua kwa wakati huo akalale hotelini kwanza. Kwa upande wa nyumbani kwa Neema, ilipofika usiku Salome aligoma kwenda kulala na mamake mdogo Ashura, kitendo hiko kilimshangaza sana Neema kwani kwake ilikuwa ni ajabu, “Kwahiyo, Salome unataka ukalale wapi?” “Nataka leo nikalale na wewe mama” “Una nini lakini Salome jamani?’ “Sina chochote mama ila nataka nikalale na wewe” Neema hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali tu vile alivyoambiwa na mtoto wake ila Ashura nae kwakweli alimshangaa sana Salome ila hakusema chochote. Muda wa kulala ulipofika, moja kwa moja Salome alikwenda na mama yake chumbani ila walipotaka tu kulala, Salome akaanza kumwambia vitu Neema vilivyomshangaza sana, tena muda mwingine akamuuliza maswali ambayo Neema hakufikiria kama kuna siku Salome atamuuliza maswali ya namna hiyo, “Mama, baba yangu yuko wapi?” “Mmmh Salome, ndio maswali gani hayo?” “Kila mtu kwenye ulimwengu huu ana baba yake, mimi je baba yangu yuko wapi?” “Jamani, Sa lome kwanini kutaka kunikumbushia machungu yaliyopita? Wewe ni mwanamke pia, ukikua vizuri utatambua nazungumzia nini” “Mama, mimi ni mkubwa tayari au unataka nikue mara ngapi? Nataka kujua baba yangu alipo” “Baba yako alishakufa” ‘Si kweli mama” “Sasa ukweli ni upi? Baba yako alishakufa, wewe huna baba” “Sawa, baba yangu alishakufa. Je baba wa hawa wadogo zangu je nae alikufa? Maana nae sijawahi kumuona na wote tunatumia majina ya babu!” “Salome, tafadhali niache nilale, wala sitaki maswali zaidi” Neema aliona maswali ya Salome yanamchanganya kichwa tu, ila Salome hakuendelea na maswali zaidi halafu akajifanya muda huo huo amelala ila kumbe alikuwa kijicho kimoja akimchungulia mama yake kila alichofanya kwa muda huo, kwani Neema nae hakulala tena maswali ya Salome yalimkumbusha mbali sana hivyo hakuyataka tena, Ila kabla hajalala aliinuka pale kitandani na kupekua vitu kwenye kabiti lake, kuna kitu alikitoa kilikuwa kama daftari dogo, akakiangalia sana kisha akakirudisha na kurudi kitandani halafu akalala sasa. Salome akainuka pia na kwenda pale alipokuwa anapekua Neema, akapata kile kitu kumbe ilikuwa ni kadi ya kliniki ya miaka ya nyuma, iliandikwa jina la mtoto Maria Patrick. Alitazama vizuri ile kadi kisha akairudisha na kwenda kulala pia. Leo usiku ilikuwa sokomoko pia nyumbani kwa Patrick kwani bado Sara ilionyesha hataki kulala mwenyewe ingawa kuongea alikuwa hawezi ila kila walipotaka kumpeleka akalale aliangusha machozi, “Mmmh hapa kazi ipo, ila Sara mbona mchana ulikubali. Kwanini usiku huu unakataa?” Sara alizidi kutokwa na machozi hivyo kufanya maamuzi ya kubaki sebleni ila Ana alitaka kwenda chumbani kulala, “Kheee Ana, wewe si ndio ulitakiwa kubaki na dada yako hapa!” “Hivi nyie vipi, humuoni kuwa mimi ni mtoto mdogo. Halafu huyo anagoma kwenda kulala kwa misingi ipi? Ngoja niende nikalale mie, huyo akilala mkamlaze” “Sasa humuonei huruma kwani?” “Namuonea huruma ila inabidi nikalale kwanza ndio huruma yangu ifanye kazi” Ana aliwaacha pale kisha yeye akaenda chumbani kwake ila Muda huo huo Sara alianguka na kuhisi kuwa amezimia ila walipomuangalia alikuwa kwenye usingizi mzito sana. Ikabidi wambebe na kwenda kumlaza chumbani kwake, kisha na wao kwenda chumbani kwao kulala. Ila Patrick yeye aliamua kukaa sebleni, muda kidogo akafatwa na Ana na kumwambia, “Nenda kalale” “Mmmh nini tena mpaka unanilazimisha nikalale Ana!” “Sasa sebleni unabaki kufanya nini?” “Namsubiri mama yenu” “Harudi leo ni hadi kesho, kwahiyo wewe nenda kalale” “Hivi kwa mfano nikigoma kwenda itakuwaje?” “Goma uone” “Mmmh!” Patrick mwenyewe aliinuka kwenye kochi na kuelekea chumbani kwani hakutaka makubwa ukizingatia huyu mtoto alikuwa na kauli sana tena kuzidi hata mama yake, kwahiyo Patrick aliona ni vyema atumie busara kuliko kugombana na huyo mtoto mdogo. Kulipokucha, wale mapacha walikuwa wa kwanza kutoka sebleni ila harufu ya sebleni iliwashangaza sana yani ilionekana kama kuna kitu kilikuwa kimechomwa hapo, Doto akamuuliza mwenzie, “Hivi na wewe hii harufu unaisikia?”: “Ndio nilitaka kukuuliza na wewe ndugu yangu, ila ni harufu ya nini?” Hawakupata jibu ila badae wakamkumbuka dada yao ambaye haongei chumbani ikabidi waende kumuamsha na kumtoa sebleni ila hali yake iliwashtua tena kwani kwasasa dada yao hakuweza kuongea wala kufumbua macho. “Mmmh kamuamshe baba Doto, tumpeleke huyu mtu hospitali. Mbona mambo yanazidi kuwa makubwa” Basi Doto akenda kumuamsha baba yao ambaye nae alishangazwa na hali ya Sara kuzidi kuwa mbaya, wakakubaliana pale kuwa suluhisho ni kumpeleka hospitali tu hakuna kingine. Wakati wanajiandaa ili kumpeleka hospitali, Ana nae aliamka na kwenda sebleni kisha akawauliza, “Mnataka kufanya nini?” “Tunataka kumpeleka Sara hospitali” “Hakuna kumpeleka” “Kheee unaongea kwa kujiamini kabisa!” “Ndio najiamini” “Halafu mtoto, unanyodo wewe. Hebu tupishe huko tumpeleke Sara hospitali” “Nimesema hamna kumpeleka” “Unaongea hivyo kama nani?” “Naongea kama Ana, hakuna kumpeleka popote” Kaka zake walitazamana pamoja na Patrick bila kumuelewa huyu Ana anamaanisha nini au ni kitu gani anakitaka hadi kusema vile. Ila Patrick akajikuta akiwataadhalisha wenzie, “Jamani, Ana kashakataa tutulie tu” “Kwani baba, Ana ni nani kwenye nyumba hii hadi tumuheshimu? Ana sauti gani kwenye nyumba hii? Ni bado kinda tu huyo, ana ukubwa gani huyu! Anajua matatizo ya mtu huyu? Sara anaumwa na hakika anajisikia vibaya sana, hospitali ndio suruhisho la pekee kwa matatizo yaliyompata kwani watachunguza kinywa na macho yake yamepatwa na nini. Achana na huyu Ana baba, tushirikiane tumpeleke Sara hospiatali” Ana akacheka, kisha akasema “Kwani Ana ndio nani? Ana sauti gani kwenye nyumba hii? Nadhani wote mnataka kunua nina sauti gani kwenye nyumba hii na mimi ni nani. Sasa endeleeni kung’ang’ania kumpeleka hospitali niwaonyeshe kuwa mimi ni nani” Kaka zake walimuangalia kwa gadhabu sana, kisha wakaanza kumbeba Sara ili amtoe nje na wakampakize kwenye gari waende hospitali ila gafla wote walipiga miyeleka na kuanguka chini tena walianguka vibaya sana, halafu cha kushangaza ni kuwa kila aliyejaribu kuinuka alishindwa na kila aliyejaribu kuongea alishindwa pia. Wakabaki chini tu wakiugulia maumivu. Ila Ana alikaa na kuwacheka sana, kisha akaenda kuchukua juisi na kunywa huku akiwaangalia na kucheka. Neema alikuwa wa kwanza kuamka ila kabla hajatoka nje, mtoto wake alimuuliza “Mama, Maria Patrick ndio nani?” Neema akashtuka sana kwa swali lile, “Eeeh Salome unasemaje?” “Maria Patrick ndio nani?” “Hata salamu hakuna? Si ndio tumetoka kuamka jamani mwanangu!” “Ndio mama, shikamoo ila nijibu Maria Patrick ndio nani?” “Ni mdogo wangu wa mwisho” “Wewe mama huyo mdogo wako ni wa wapi? Kwanini hutaki kusema wazi tu kuwa Maria Patrick ni mimi” “Salome, niache tafadhali niache. Wewe mtoto usinitafutie makubwa jamani. Wewe ni Salome, hiyo Maria imetoka wapi tena. Niache wewe mtoto nipumue” “Mama, nahitaji kwenda kwa baba yangu” Neema akapumua kwa hasira na kutoka nje, kisha akamuita Ashura halafu Salome nae alienda pembeni akisikiliza maongezi yao, “Huyu mtoto mwenzangu anataka kuniletea balaa” “Lipi tena dada?” “Eti anataka kumjua baba yake” “Mmmh hilo balaa kweli, mwambie alishakufa” “Nimemwambia, ila sijui katoa wapi jina la Maria Patrick na amesema anataka kwenda kwa baba yake” “Khee dada, hapana bhana usithubutu kufanya hivyo” “Sasa nitafanyeje mimi?” “Ngojea, nitajua cha kufanya dada ila usithubutu kumueleza kuhusu baba yake” Neema aliondoka zake kujiandaa ila salome alishaelewa kinachoendelea hapo. Rose alipoamka hotelini, alijiandaa kwa safari ya kurudi nyumbani kwake, kwakweli alikuwa anajihisi uchovu sana ingawa alilala hotelini ila bado mwili wake uligubikwa na uchovu wa hali ya juu. Aliendesha gari yake hadi nyumbani kwake, ambapo getini alifunguliwa mlango na mlinzi kama kawaida. “Vipi, ndani humu wote wazima?” “Nadhani, ila leo sijamuona yeyeto akitoka nje” “Itakuwa wananisubiria” Aliingia ndani na kukuta wote wapo chini, tena kila mmoja na pozi lake ila kwa muda huo walikuwa wamepitiwa nausingizi. Wakati anataka kuwaamsha mara akatokea Ana na kumwambia mama yake, “Usiwaamshe waache hao” “Vipi tena imekuwaje?” “Ni viburi sana hao mama” Rose hakuelewa bado, ila Ana alimvutia mama yake chumbani na kumueleza alichowafanyia ndugu zake. “Jamani mwanangu kumbe wewe ni fundi hivi jamani!” “Nilikuwa sizijui vizuri nguvu zangu ila saivi nimezijua” “Aaah wewe ni kiboko, ila mwanangu watu hawa inabidi warudi kwenye hali ya kawaida maana ndio wanaotusaidia” “Nitawarudisha wengine ila sio dada Sara” “Hapana mwanangu, Yule ni dada yako” “Hata kama, labda aone tu ila kuongea ni no, Yule mdada ni mbea sana” “Ila kwanini hatukuweza kumziba mdomo Moza?” “Achana na habari za huyo mtu mama hakuwa wa kawaida ila cha msingi hatuponae tena hapa” “Sawa mwanangu, ila waachilie ndugu zako” Ana akaenda chumbani kwake kufanya dawa, na muda kidogo tu pale sebleni waliamka na waliweza kuinuka na kuzungumza ila kila mmoja aliogopa kuzungumza kuhusu kitu kilichotokea. Sara nae aliweza kuangalia ila kuzungumza hakuweza. Wale mapacha, walipoinuka kitu cha kwanza kilikuwa ni kuondoka hapo nyumbani kwao, na kumuacha Patrick na Sara hata hawakutaka kujua kama mama yao karudi au la. Salome alikuwa makini akifatili mambo ya Ashura kwani alijua ni wazi angewasiliana na Rose kumwambia ile mada na kweli Ashura aliingia chumbani na kumpigia simu Rose kumbe Salome alikuwa amejibanza akisikiliza, “Yani dada, ule wasiwasi ambao ulikuwa nao kipindi chote sasa unaenda kutokea. Kwa kifupi haka katoto kameanza kumchachafya mama yake kuhusu baba yake na kanataka kuja kwa baba yake” Ashura akawa kimya sasa akisikiliza maelekezo ya Rose, ila Salome nae alikuwa makini kabisa kwani alijua ni wazi baada ya maelekezo hayo Ashura angeongea tu. “Kwahiyo ndio wakati wa kuitumia ile dawa eeeh! Sawa dada nimekuelewa, si nimuwekee kwenye chakula! Sawa dada nitafanya hivyo. Lakini si siyo ya kuua? Sawa maana ingekuwa ya kuua ningeogopa kwakweli maana kesi hizi” Kisha Ashura akakata simu na kwenda kwenye begi lake ambapo alionekana kama akipekua kitu kisha akatoa kichupa kidogo na kutoka nacho. Muda kidogo akamuita Salome na kumwambia, “Njoo ule Salome mzuri weee” Salome alifika na kumuuliza, “Sasa nakula peke yangu?” “Hapana, tunakula wote. Chakula change si hicho hapo. Halafu cha kwako ni hiki” “Sawa, ila wadogo zangu wako wapi nao waje nile nao bhana” “Kawaite basi” “Mi naona uvivu” “Yani wewe mtoto loh!” Kisha Ashura akaenda kuwaita wadogo zake Salome, ila kwa muda huo huo Salome aliweza kubadilisha zile sahani za chakula. Ashura aliporudi akaenda kuwapakulia chakula chao watoto, kisha kwa pamoja wakaanza kula mara gafla Ashura akadondoka huku akitapatapa na povu likimtoka mdomoni. Itaendelea kesho usiku……!!!!!! By, Atuganile Mwakalile.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: