Home → simulizi
→ MOYO USINIDANGANYE
NO :01
Mara yangu ya kwanza kuja Dar es Salaam, rafiki yangu Tonny alinizungusha kariakoo. Mwanza pamechangamka lakini mji huu ni hatari. Kuna kila aina ya bidhaa, na nyingi hupatikana kwa bei rahisi kuliko Mwanza, hasa za madukani. Tulipita sehemu moja, kununua nguo za ndani maarufu kama boxer, mtaa wa DDC. Niliona boxer nzuri zilizouzwa kwa bei nafuu, nikachanganyikiwa kidogo lakini Tonny akanipeleka duka ambalo alidai ni mteja hapo. Nilitegemea angemchangamkia muuzaji, ama kuonesha anamfahamu, lakini ilikuwa tofauti. Walisalimiana kama watu wasiojuana kabisa, huku mimi nikiwa nimetoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango.
Nilishindwa kujizuia kumkodolea yule dada muuzaji, kiasi cha yeye mwenyewe kujistukia, hivyo akanitazama na kutabasamu, na kunipa salamu ambayo kwa mara ya kwanza ni kama sikuisikia japo niliisikia. Mara ya pili akanistua tena kwa kuniita, “Kaka, habari yako?”. “Oh, nzuri, za kwako mrembo?”, nilijibu kwa aibu.
Tonny alimuulizia mwenye duka, nikaelewa kumbe yule mrembo hakuwa mwenye duka au muuzaji wa awali.”Ametoka kidogo, ameenda kuniulizia boxer fulani kwa rafiki yake, hapa zimeisha. Lakini naweza kuwauzia chochote mnachohitaji, hakuna shida, pia kama hamniamini, jirani yake huyo anamlindia”. Alizungumza huku akionesha tabasamu mahiri. Hakujua muonekano wake usingefanya mtu yeyote kutomuamini. Kusikia hayo maelezo, moyo wangu ulisononeka kidogo, kwani maelezo yake yalionesha aidha ameolewa ama yuko kwenye mahusiano imara. Baada ya muda mfupi, alikuja muuzaji, aliyezoeana vizuri na Tonny, akampa yule dada mzigo wake, kisha binti akaondoka.
Tulinunua tulichohitaji kununua, tukaondoka, akilini nikiwa na mawazo utadhani nimepoteza hela. Tonny alianza kunicheka, jinsi nilivyomshangaa yule binti ambaye kwa bahati mbaya hata jina au namba ya simu yake sikufanikiwa kuuliza. Tonny ananijua kuwa mimi si kijana ninayezuzuka na mabinti, na nina misimamo yangu fulani kuhusu mahusiano. Hata kwangu pia ilikuwa ni ajabu kuvutiwa na msichana kiasi kile, kwa mara ya kwanza tuu namuona. Miezi miwili iliyopita tuliachana na aliyekuwa mpenzi, bila sababu ya msingi naweza sema, kwani chanzo cha kukosana kilikuwa kidogo sana, kikapelekea kukorofishana mpaka kuachana. Nadhani ni kama nilimsukuma aliyechuchumaa, kwani kabla ya hapo viliwahi kutokea visa kadhaa kuniashiria kuwa Anitha, mpenzi wangu huyo, hakuwa ananipenda tena. Hata hivyo si lengo langu kuelezea sana uhusiano wangu uliopita.
Nilirudi Mwanza, wiki mbili baadaye. Nikaendelea na biashara zangu za kusambaza bidhaa za kula kwenye maduka na supamaketi mbalimbali pale Mwanza. Huwezi amini, akili yangu ilishindwa kupuuza sura ya mrembo niliyekutana naye kariakoo, kwa muda wa miezi kadhaa. Siku ile nilipomtazama kwa kuduwaa, niliona uzuri wa ajabu kwa binti yule. Rangi yake ni ya kahawia, si nyeusi lakini si mweupe pia. Ngozi laini kama ya mtoto, yani utadhani hajawahi hata kung’atwa na mtu. Alipotabasamu, (nadhani anajijua ana tabasamu la kuvutia sana), meno yake meupe sana yalionekana, na kama pengo dogo upande wa kushoto wa kinywa chake pia nililiona kwa mbali nalo liliongeza mvuto. Zaidi ya hayo, mrembo huyu aliongezewa kionjo cha dimpoz katika uumbaji wake, mashalaah, Mungu fundi jamani! Macho yake meupe, makubwa kiasi, niliwaza akilini mwangu, akiwa ndio yuko mikononi mwangu ananitazama kwa mahaba itakuaje? Sitaki kuongelea umbo lake kwani sikupata fursa kulitazama kwa ufasaha, lakini kwa sekunde chache nilizomtizama akiondoka pale dukani, naweza sema ile ni namba sita ndefu, nadhani unanielewa.
Kwa jinsi alivyoiteka akili yangu, haikuwa ajabu kumuota mara kadhaa. Niliota nimekutana naye tena, na mara hii nikamuomba namba yake. Lakini mara ya pili niliota niko naye eneo zuri, kama wapenzi, huku tukifurahia kila mmoja wetu hiyo fursa. Asubuhi kuamka, Kumbe! Ni mawazo na hisia zangu hunipeleka mahala ambapo hakuna matumaini ya kufika. Kumuwaza yule mrembo mara zote kulinisaidia kumsahau kabisa Anitha, kwani mpaka wakati huo nilikuwa nikijaribu kumbembeleza kwa simu turudiane, huku nikiambulia vichambo na matusi. Basi maisha yaliendelea hivyo, kwa miezi kadhaa, nikamkatia tamaa Anitha kabisa, nikawa mpole, nikifarijiwa na hisia zangu hewa za binti mrembo, ambaye hakuna matumaini hata tone ya kumuona tena.
Miezi kadhaa mbele nilipata wazo la kupanua biashara yangu, huku nikiangalia fursa ya kutoa nguo Dar es Salaam kuuza Mwanza. Niliamua nitalenga nguo za ndani, hivyo nilitembelea baadhi ya wadau wangu wenye maduka ya nguo na kuwaonesha sampo za hizo nguo nilizotaka kuuza. Nilipata muitikio mzuri sana, labda kwa sababu ya uzoefu wangu katika biashara, na uwezo wa kutumia lugha vizuri. Niliamua kuanza biashara kwa kusafiri tena ili kupata mzigo. Nilipomshirikisha Tonny alinishauri kwa mzigo wa mwanzo tutachukua kwa yule rafiki yake huku akijaribu kumuuliza wapi anapopata mzigo, na kupata muongozo. Nilianza biashara, nashukuru dada muuzaji hakuwa na hiana, wala hakuogopa kupoteza wateja au kutengeneza ushindani. Alitupa ushirikiano mkubwa, hatimaye mzigo wa tatu niliufata nchini Uganda. Biashara ilinoga haswaa, huku nikiendelea na ile ya awali, kwani ilikuwa imethibitika kwa muda mrefu na yenye wateja wakudumu. Sasa maisha yangu yalikuwa bize sana kiasi cha kutonipa nafasi ya kuwaza chochote kuhusu mapenzi. Sikumkumbuka tena mpenzi hewa niliyekutana naye kariakoo wala Anitha ambaye ninauhakika naye alishanisahau kabisa.
Mwaka mzima ulipita, na wa pili, nikiwa singo kama wanavyosema vijana wa mjini. Biashara zilichanganya, kuna wakati nilipigwa, yaani niliibiwa kidogo na vijana wangu, lakini si kiasi cha kunitia hasara. Niliongeza mtandao, na marafiki katika biashara, kwani nilianza kuwa mkombozi katika upatikanaji wa nguo za ndani kwa urahisi na kwa bei nafuu pale Mwanza. Baada ya muda nilikutana na binti mwingine, tukaanza mazoea na kuwa kama wapenzi. Nadhani nilichoshwa na upweke na kuamua kuwa kwenye mahusiano, japo sikuwa nimemaanisha sana. Mungu anisamehe, kwani mpaka leo nahisi sikumtendea haki yule mpenzi wangu mwingine baada ya Anitha. Utanielewa baadaye.
Miezi michache tena ikapita, nikiendelea na biashara zangu na uhusiano wangu wa kupotezea muda. Nakumbuka siku moja, nikiwa Dar es Salaam, nikisubiri safari yangu kufata mzigo Uganda, siku moja kabla ya safari. Nikiwa kwa rafiki yangu Tonny, tunakula chakula cha mchana kilichoandaliwa na mkewe mpya (walikuwa na mwaka tangu waoane), Tonny alipigiwa simu na jamaa yake fulani akimualika kwa chakula cha jioni. Ni rafiki yake, walisoma naye miaka sita ya sekondari, waliishi naye chumba kimoja, kwa wakati huo walikuwa wamepotezana kama miaka miwili huku huyo jamaa akiwa jeshini ambako hakutakiwa kuwa na mawasiliano na watu. Alipopokea simu, alipata msisimko na hakutaka kutakaa kabisa ule mualiko. Alianza kutushawishi mimi na mkewe twende naye, lakini mke wake aliyekuwa na mimba changa hakutaka kusumbuka kabisa. Nilitaka kumkatalia pia, ili nijiandae na safari kesho yake, lakini alinishawishi sana, nikashindwa. Tukamuacha mkewe, na binti wa kazi, tukaondoka.
Tulikutana hoteli moja nzuri mjini Dar es Salaam, maeneo ya Posta, inaitwa Ramada. Tulifika, na kuongoza kwenye meza moja yenye watu wawili, mwanaume na mwanamke, walioonekana ni wapenzi. Lahaula! Sikutaka kuamini macho yangu kile nilichoona mbele yangu. macho yangu yaligonga moja kwa moja katika sura ninayoifahamu, ya binti aliyewahi kunivutia kuliko wanawake wote kabla. Msichana niliyemuota na kutamani kuwa naye kuliko mwanamke mwingine yeyote. Ghafla akili yangu ilihama, nikajihisi kuchanganyikiwa, nikatamani tungeipita ile meza, yani wasiwe ndio hao watu ambao tutakaa nao. Lakini nikiwa katika lindi la mawazo, nilijikuta tayari tumekaa kwenye meza hiyo hiyo, na muhudumu ameshafika kutusikiliza. Tonny na rafiki yake walisalimiana kwa furaha, Tonny akanitambulisha, huku nikiwa kama mtu aliyenyeshewa. Tukatambulishwa pia huyo mrembo, aliyeitwa Ninah, ambaye jamaa alisema ni mkewe mtarajiwa. Rohoni nikajisemea,”bora ni mtarajiwa”, huku nikijipa matumaini kwa mbaali kwamba kama bado hawajaoana pengine bahati inaweza kunigeukia.
INAENDELEA...
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: