BOTI LA VALENTINE NO:02 Nilikuja kukutana tena na James baada ya miaka minne, yaani mwaka 2015 mwezi wa tatu. Kwa bahati baada ya kuachana naye nilikuwa nimepata kazi nyingine mkoa wa Mwanza miezi kadhaa baadaye, na pia nilikutana na mwanaume (huyu tulisoma naye chuo kikuu lakini hatukuwahi kuwa karibu sana), ambaye tulijenga urafiki na kisha ndiye nikaolewa naye. Wakati nakutana na James, nilikuwa ni mjamzito wa miezi mitatu, hivyo nilikuwa nimeongezeka kidogo na nimenawiri. Nakumbuka siku nakutana naye nilikuwa natokea kazini mchana. Siku hiyo sikuwa najisikia vizuri hivyo niliomba nitoke ofisini mapema. Pia ofisi yangu haikuwa mbali na kwangu kwahiyo mara kadhaa nilipendelea kwenda kwa miguu ili pia nifanye mazoezi Tulikutana uso kwa uso, na yeye alikuwa wa kwanza kunitambua na kuniita. Sikutamani kukutana tena na huyu kaka kwani sura yake ilinikumbusha siku tuliyoachana, lakini hata hivyo kwa sasa nilikuwa nimeshamtoa akilini mwangu siku nyingi. Nilimuona kama tu mwanaume yeyote niliyefahamiana naye, lakini mwenye mambo ya kichawi. James hakuwa kama yule wa awali niliyemfahamu. Alikuwa amechoka na amekonda. Alionekana kama hali yake ya uwezo ni tofauti na ile niliyomuacha nayo. Pia hakuwa tena mwanaume mwenye kujiamini na mtanashati kama alivyokuwa kabla Kwa kiasi niliingiwa na huruma. Tulisalimiana na kisha aliniomba sana tukae kwenye mgahawa ulokua jirani, tuongee. Sikumficha James kuwa amebadilika sana, na kwajinsi nilivyoonesha kumshangaa nadhani alijua ni kweli amebadilika sana. Muda tuliokaa haukuwa mwingi sana ila ulitosha yeye kunieleza yaliyotokea kwenye maisha yake tangu tulipoachana “Siku tuliyoachana baada ya kutoka baharini ni siku ambayo niliumia sana sana. Katika maisha yangu hakuna mwanamke nilimpenda kama wewe. Kwangu ulikuwa ni mwanamke pekee nimewahi kuwa naye mwenye ndoto, maono makubwa na misimamo thabiti ya maisha. Pia muonekano wako nadhani ni mzuri kuliko wanawake niliowahi kuwa nao kabla yako, na jambo jingine, mara zote nilikuwa nikianzisha mahusiano napata presha sana ya kuoa kutoka kwa msichana nnayekuwa naye, lakini kwako haukuwahi kunisumbua”, alizungumza James huku akionekana kama mtu anayetamani kuurudisha nyuma wakati, kisha aliendelea. “Nikiwa kijana wa miaka 21 nilianza mahusiano ambapo nilikutana na binti mrembo sana nikiwa mwaka wa kwanza chuo. Naye pia alikuwa mwaka wa kwanza, lakini hakuwa mtu anayejali sana masomo na mara kadhaa hakuonekana darasani. Msichana huyu alionesha kuvutiwa sana na mimi, na ni yeye aliyenishawishi tuwe wapenzi. Kwa kiasi nilijiona mwenye bahati kwani wakati huo sikuwa bado najitambua, na nilianza mapenzi na yule binti kwa kasi kubwa mno. Alikuwa amenizidi umri kidogo ila kikubwa cha ajabu alikuwa na pesa sana. Alinidanganya kuwa wazazi wake ni watu wenye uwezo. Tulikula raha sana kwa muda wa miezi kadhaa ambapo ilinipelekea kuanza kuharibu shuleni. Hiyo haikunisumbua sana kwani nilikuwa nimeingia kwenye mapenzi na mtu asiyejali masomo na maisha na pia alinihakikishia kuwa kuna nafasi kibao duniani za kufanikiwa hata bila elimu. Wakati huo alikuwa amenipa hela nyingi na kunambia naweza kufungua miradi nikaanza biashara huku naendelea na chuo. Nilianza kukosa kufikia kiwango kwa mitiani kadhaa na kupata ‘sapu’ ambazo zilinikatisha tamaa kabisa na shule. Mwaka wa pili nilifeli na kushindwa kuendelea na shule (nili disco), hivyo nikaacha shule. Wakati haya yote yanatokea nyumbani walikuwa hawajui chochote na niliwaficha hata nilipoacha shule kwani baba alikuwa mkali sana. Baada ya kuacha shule nilifungua biashara na kuanza kuisimamia mwenyewe. Mapenzi yetu na huyu binti (nitamuita Love) yalinoga sana kiasi kwamba tuliamua tuanze kuishi pamoja. Hapo ndipo nilipojua ukweli kuwa binti huyo hakuwa mtu wa kawaida. Alikuwa hana familia ya kawaida na alikuwa akiniacha mara kadhaa usiku wa manane na kutoka. Sikuwa na cha kumfanya kwani kila nilipojaribu kumfatilia alikuwa mkali lakini pia aliniahidi siku moja nitaujua ukweli, na kwa wakati huo yeye ndo alikuwa ameshikilia maisha yangu kwa kiasi kikubwa. Ilibidi niwe mpole hasa ukizingatia nilikuwa Napata kila ninachohitaji na zaidi. Tuliendelea na mapenzi kisha siku moja alinipeleka baharini tulikoenda siku ile. Ilikuwa siku ya valentine na tulienda kwa namna ile ile niliyoenda na wewe. Nilikuwa na hofu sana pia kama wewe, lakini nilijivika ujasiri hasa kwa kuwa kuna baadhi ya vitu nilishavihisi. Love aliponifikisha kule chini niligundua ni mtu anayeheshimika sana kama malkia. Aliongea na mimi mambo mengi huku akinisisitiza lazima niwe naye siku zote. Sikuweza kumuacha Love hata baada ya kujua ukweli hivyo nilikubaliana na masharti yake likiwemo sharti la kuwa mpenzi yeyote nitakayekuwa naye baada yake ni lazima apate kibali kutoka kwake ili nimuoe. Alinambia ye hataweza kuwa mpenzi wangu wa muda wote kwani ana majukumu mengine na hivyo itabidi aniache tuwe tunaonana siku maalumu. Iliniuma lakini ye ndo alikuwa mwamuzi wa mwisho. Baada ya kuachana naye nilianza kuwa na kila msichana mrembo niliyetamani kuwa naye, lakini sikuwahi kuwa na zaidi ya mpenzi mmoja kwa wakati. Nilikaa nao kwa muda mfupi na kuwaacha. Sikuwahi kukaa na msichana kwa mwaka mzima mfululizo, mpaka nilipokupata wewe. Love alinifanya kuwa na pesa nyingi na kupata kazi ninayoitaka, hivyo haikuwa tatizo kuwa na msichana yeyote mjini. Sharti lake la kupeleka msichana kabla sijamuoa ili ampitishe lilinipa shida sana hasa nilipokuwa na wewe. Uliponiacha niliumia lakini sikuwa na namna zaidi ya kuendelea kuwa mtumwa wa Love. Nilipata msichana mwingine ambaye hatukudumu sana lakini baadaye nilipenda tena msichana ambaye alinifanya nifanye maamuzi magumu. Iliponibidi nimpeleke kwa Love, nilimueleza ukweli. Yule msichana aliniacha kabla hatujaenda na sasa ndipo niliamua kuachana na Love. Tulipoonana naye tena nilimwambia kuwa nimeamua kumuacha na kila kitu chake. Alicheka sana na kunambia nitarudi tu. Niliumia kuona kuwa hana hata huruma na mimi na hivyo nikajiambia kuwa ni bora nikahangaike na maisha kuliko kuwa kwenye kifungo hiki miaka yote. Sasa ni miaka karibu miwili imepita, mambo yamekuwa magumu kwani hata elimu yangu ni ndogo na katika kuhangaika nimekuja huku Mwanza kwa biashara Fulani. Nimegundua kuwa miaka niliyodhani nina maisha mazuri na kujidai kwa pesa na nafasi nilivyopata kwa yule mwanamke nilikuwa natengeneza hasara ya muda wangu na maisha yangu”. James alimaliza kunipa stori yake iliyonisisimua na nilijikuta nimetoa machoni. Nilimshauri mambo kadhaa ambayo naamini yalimsaidia baadaye. Natumai vijana wenzangu mmejifunza jambo kuhusu maisha, elimu na mapenzi, kutokana na simulizi langu. MWISHO

at 8:27 PM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top