Home → simulizi
→ BOTI LA VALENTINE
NO:01
Watu wengi wana historia tofauti ya siku ya Valentine,japo kijumla inajulikana kama siku ya wapendanao. Kwangu hii siku ina mtazamo tofauti kwani ni siku ambayo nakumbuka hisia za tofauti sana nilizowahi kukutana nazo kwenye maisha yangu
Tangu Nina umri wa miaka 20 nilianza kutilia mkazo siku hii. Hii ilikua ni baada ya kuanza kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi. Mpenzi niliyekua naye wakati huo alihakikisha inakuwa siku maalumu sana kwetu na kwa vile alikuwa wa kwanza,niliamini hivyo ndivyo Valentine zinatakiwa kuwa
Nilipoachana na mpenzi wa kwanza kwa sababu ambazo sitaelezea, nilipata mwanaume mwingine ambaye pia tulipendana sana. Sasa nikiwa na umri wa miaka 25 nilifurahia sana kila ilipofika tarehe 14 mwezi wa pili. Kwa miaka mitatu mfululizo,mbali na kufurahia siku nyingine za mwaka kwa penzi letu, siku ya valentine ilikua na maana sana kwetu. Sikujua kwanini mpenzi wangu aliienzi sana siku hiyo mpaka valentine ya mwaka 2011
Nakumbuka ilikua siku ya Jumatatu. Siku ambayo kwa wafanyakazi inakua ni ndefu na ya kuchosha. Kwajinsi nilivyomfahamu mpenzi wangu nilijua tu atataka tutoke jioni hiyo,lakini kesho yake pia nilikua na kazi nyingi ofisini hivyo sikupanga kuchelewa kulala
Mpenzi wangu (nitatumia jina la James, japo si lake) alinifata ofisini saa 11 kamili. Alinisubiri chini kwenye parking. Nilikuwa nimemtaarifu kabla kuwa valentine hii hatutatoka lakini ye alisema tu ngoja nije tutaongea.
Alinisubiri kwa muda sana pale chini. Yeye kazi yake japo ilikua inamlipa vizuri, haikua inambana sana. Na pia James alikua mtu mwenye vyanzo vya pesa nje na kazi yake vingine hata mimi sivijui
Mara zote James alionekana kama kuna kitu kinamzuia kunioa na siku zote sikuelewa kwanini hatuoani, kwani kiukweli tulipendana. Kama binti wa kabila fulani ambao tumezoeleka kwa maringo na kujidai, sikutaka kumuonesha James kuwa nina shida ya yeye kunioa mpaka ye ndo aoneshe uhitaji. Mapenzi alonipa huyu kaka,yalinifanya pia nisifikirie sana kumsukuma kunioa kwani nilijijua na kujiamini kuwa mi ndo mwanamke pekee maishani mwake.
Saa 12.30 jioni nilitoka ofisini na kumkuta James kwenye parking. Siku hiyo alikuwa amenambia nisiende ofisini na gari hivyo alinipeleka yeye na jioni ndo alikua amenifata. Tulibishana sana kuhusu kutoka lakini hakunielewa. Baadaye nilikubali japo kwa shingo upande. Alinichukua tukaenda kisiwa kimoja kinaitwa mbudya. Kuna boti za bei rahisi lakini pia kuna boti za gharama kidogo za kwenda mbudya ambazo mnaweza kukaa wawili au wanne mkiamua
Boti ambayo James alikua amekata ticket niliishangaa nilipoiona,nikamuuliza"Ni mbudya tu tunaenda au kuna kwingine?" Alitabasamu na tukapanda kwenye boti ndogo kiasi lakini ya kifahari mno. Sikuwahi kupanda wala kuona boti ya namna hiyo. Tulikua watatu ndani (akiwemo nahodha). Nilifurahia jinsi ndani ya boti palivyokua kwani ilikua kama chumba cha kifahari sana. Nilihisi hii lazima itakua siku maalumu sana lakini pia niliona kwa safari ya mbudya ilivyo fupi, kutumia ile boti ilikua ni ubadhilifu
Nikaanza kushangaa kwanini hatufiki. Kwakua nilikua na mtu ninayemuamini sana na yeye hakuonesha wasiwasi, nilihisi labda kuna ‘sapraizi’ ameniandalia hivyo nikawa mpole. Nilipojaribu kumdadisi alinambia "tulia bebi "
Mara ghafula niliona uelekeo wetu kama unaenda chini utadhani ndege iko hewani inataka kutua. Nilistuka sana lakini wenzangu walikua kawaida tu. Kisha ghafula pia niliona anayeendesha boti amepotea na sasa ni James alikuwa akiendesha.
Mungu wangu!! Nililowa mwili mzima. Nilianza kutetemeka na kumuita James kwa nguvu nikiongea maneno nisiyoyaelewa. James aliniangalia kwa upole na kunambia nisiogope, lakini nilikua kama naona shetani mbele yangu kwa jinsi nilivyokua naogopa. Nililia na kupiga kelele huku nikimuomba James msamaha kana kwamba kuna kitu nimemkosea, lakini hakujali hata kidogo. Wakati huo tulikua na uelekeo wa kasi sana kwenda chini ambao ulichukua muda mrefu.
Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, tulifika na kutua. Wakati huo nilikua natetemeka sana na sijielewi. Sikuwa najiona kama niko na James yule niliyempenda sana, bali nilijiona niko na shetani asiye na undugu na mimi. Mlango wa boti ulifunguka, nikashangaa sana kuona tuko ndani ya maji, lakini cha ajabu hayakutulowesha. Kingine cha ajabu ni kule ndani ya maji palikuwa kama nyumba nzuri sana ya kifahari. Kulikuwa na wanawake warembo sana, kulikuwa na watu wakistarehe na pia kulikuwa na vitu vingi vya kifahari
James alitangulia kutoka nje ya boti na kunishika mkono kama mwenyeji wangu bila kusema na mimi. Nikiwa nina hofu kubwa lakini sina msaada zaidi ya kusubiri kinachofuata, tulielekea sehemu moja ambayo tulifungua mlango na kuingia ndani ya chumba. Hicho chumba kizuri tulimkuta mwanamke kijana, mrembo sijawahi kuona, na ilionekana kama James hakuwa mtu mwenye ujasiri sana mbele yake. Aliniangalia kwa dharau kisha akamuliza James,” ndiyo huyu anayekupa jeuri?”. James hakujibu kitu.
Yule mwanamke aliniangalia kwa kujiamini sana kiasi cha kunifanya nijione mdogo, japo ki umri tulikuwa kama watu tunaolingana. Alinambia kwa sauti ya kuamrisha, “Kuanzia leo utakuwa ukija huku kila mwaka siku kama ya leo. Nitakupa maelekezo ya nini cha kufanya na tutafanya kazi pamoja mimi na wewe. Hilo pekee ndilo litakupa fursa ya kuendelea na James. Vinginevyo unambie kama hauko tayari kwa hilo na leo ndo utakua mwisho wenu”.
Uchaguzi niliopewa kwa wakati huo haukuwa mgumu hata kidogo. Kichwani mwangu nilikuwa tayari nimesahau kama James ni mwanaume ninayempenda sana, na sikuwa tayari hata kidogo kuendelea kuwa naye hata bila sharti lolote. Nilimuangalia James na kumuomba kwa huruma na upole sana kuwa anirudishe. Alikaa kimya akisubiri maamuzi ya yule mwanamke ambaye aliendelea kuongea na mimi kunieleza jinsi gani nitafaidika endapo nitakubali alichotaka. Mwisho wa siku, baada ya kuona naendelea tu kulia, alimwambia James kwa hasira “MTOE”, huku akimpa maelekezo, nikiwa tayari ndani ya miezi mitatu atanirudisha.
Tuliporudi nchi kavu, sikuweza kuongea na James chochote. Alijaribu kuniomba tuongee anielezee lakini sikutaka kumpa nafasi sata ya kunirudisha nyumbani. Nilimuomba tu aniache palepale na asinitafute tena. Nilibadilisha simu na huo ndo ulikua mwisho wa mahusiano yetu, japo alijaribu kunifatilia kazini lakini sikuwahi kumpa nafasi hata ya kuongea naye tena.
INAENDELEA...
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: