MOYO USINIDANGANYE NO :02 Marafiki wawili walifurahiana, wakipiga gumzo za hapa na pale, huku kwa namna fulani wakijaribu kutufanya mimi na yule mchumba wa jamaa tusijisikie wapweke. Kiukweli akili haikuwa hapo. Kila wakati nilimtupia Ninah jicho la wizi, huku nikitamani azungumze. Kuna wakati alizungumza kidogo, basi nikamuitikia kwa shamra mpaka nikajistukia. Tuliendeleza zogo kwa muda, lakini nilijihisi nahitaji kwenda kupata pumzi, nikainuka kwenda uani. Yaani muda wote niliokaa pale pezani nilihisi hewa hainitoshi. Nilikuwa na hisia mchanganyiko, furaha ya kumuona mrembo wangu kwa mara ya pili, ambaye sikutegemea, lakini pia sikuwa na namna ya kumuiba mrembo huyo kwa jamaa hivyo niliishia kujisikitikia. Niliinuka na kwenda uani, nikajiangalia kwenye kioo, huku nikijiambia,”Ni sawa tuu Balongo, sio wako. Inatosha kumuona kwa mara nyingine na walau kukaa naye meza moja”. Nilirudi, na haikuchukua muda tukaondoka. Kesho yake nilisafiri, nikimuwaza Ninah akilini, lakini walau nilifanikiwa kumuona kwa mara nyingine, kujua jina lake na zaidi kujua anafanya wapi kazi. Akilini mwangu hakuondoka kuanzia wakati huo, japo nilijilazimisha kumtoa. Sijawahi kupenda hivi, wala kuhisi kama naweza kumpenda mwanamke ghafla kiasi hiki. Ninah aliingia akilini mwangu, aliingia moyoni mwangu, alichukua nafasi ndani yangu kiasi ambacho sikutegemea. Sauti ya maneno machache aliyoongea usiku ule ilijirudia kichwani mwangu kana kwamba yalinihusu mimi. Sura yake haikuniacha akilini hata dakika moja. Hisia hizo zilinipa raha kiasi, kwani niliiruhusu akili yangu imuwaze, iwaze uzuri wake na kila kizuri kumuhusu. Lakini wakati huo huo zilinipa mawazo, na huzuni pia kwani ni kama nilijaribu kujenga ghorofa hewani. Nilifarijika kwa kumuwaza tuu, hivyo safari nzima nilimuwaza binti huyu aliyeuteka moyo wangu kwa kasi. Maisha yaliendelea kwa miezi kadhaa, nikaendelea na biashara zangu. Kila nilipowasiliana na Tonny nilimuuliza kuhusu rafiki yake. Sikutaka kumwambia kuwa Ninah ndiye binti aliyenipagawisha siku ile kariakoo kwani Tonny hata hakukumbuka ile sura. Nilijaribu kuulizia habari zake za kuoa, huku nikimdodosa kujua kama anamaanisha kumuoa Ninah, japo sikutaka kudodosa sana kwani Tonny angenistukia. Haikupita muda mrefu, nilitafuta tena safari ya Dar es Salaam, kama kawaida nikaenda kwa Tonny ambaye hata baada ya kuoa hakuwa ananiruhusu nifikie hotelini. Siku moja usiku, mkewe akiwa amelala nasi tuko sebuleni kuzungumza kidogo, niliuliza tena habari za jamaa na kama ana nia kweli ya kuoa. Alistuka kidogo, akaniuliza kwanini nafatilia sana habari za huyo jamaa yake. Sikumwambia, lakini nilikazana kuuliza, akaniambia, “Jamaa si muoaji. Labda kama amebadilika sasa hivi, lakini kipindi chote namfahamu huwa, kila binti anayenitambulisha ni kama atamuoa mwezi ujao, lakini ukikutana naye wakati mwingine unamkuta na msichana mwingine”. Kwangu hiyo ilikuwa habari njema sana, hakujua tuu. Niliacha kuuliza habari hizo tena kwa muda, lakini nikaamua kufanya jitihada zangu binafsi kumtafuta Ninah. Kipindi hicho nilikaa Dar kama mwezi mzima, kiasi cha Tonny kushangaa imekuaje, lakini sikumwambia nini hasa kimenikalisha. Kwa asili, sipendi kuonesha udhaifu wangu juu ya wanawake, hivyo japo Tonny ni rafiki yangu wa ndani sana, sikutaka kumuonesha kiasi gani Ninah aliiteka akili na moyo wangu, hasa kwa kuwa bado hakukuwa na mwanga wowote wa kumpata. Nilimfatilia alipofanya kazi, nikafanikiwa kumpata, lakini sikujionesha kwake. Niliamua kutumia mbinu fulani kumvuta karibu kwanza, kabla hajanifahamu. Nilianza kumtumia zawadi, huku nijitambulisha kama secret admirer yaani akupendaye kwa siri. Nilifanya hivyo, kwa ujanja, mara kadhaa. Nikaondoka na kurudi Mwanza, na kuendelea kutuma zawadi kadhaa zenye hamasa ya mapenzi. Sikujua anazichukuliaje, labda sikutaka kujua kwa wakati huo. Kiasi, naogopa kukataliwa, pengine nina moyo muoga wa maumivu, hivyo nilijaribu mbinu ambayo ingenipa nafasi ya kukubalika kiurahisi. Kwenye mizigo au parcel nilizomtumia, niliambatanisha na jumbe fupi, nikimsifia, kumwambia namna nilivyohisi mara ya kwanza namuona, na mambo mengine mengi. Sikumpa anuani wala kumpa fursa ya kunijibu. Nilifanya hivyo kwa miezi mitano mfululizo, ndipo nikapanga kuonana naye. Nilimtumia mzigo wa mwisho wenye ujumbe wa kumuomba kumuona, na namba yangu ya simu, nikimsihi sana anipigie ili tuonane. Hapa nilikuwa narusha kete zangu nikiwa na matumaini kidogo kuwa angenipigia. Hatima ya mimi na huyu mrembo kuwa pamoja ilikuwa juu yake, kama angepiga simu. Nilipata mawazo sana tangu nilipotuma ile parcel kwani hapo ndipo nilielewa nilishapenda kiasi gani. Kitendo cha kukaa siku kadhaa nikisubiri anipigie huku nikishindwa kufuatilia kama kweli atapiga au la, kilinipa mawazo kiasi cha kunipungua uzito. Siku zilipia, tofauti na matarajio yangu ukapita karibu mwezi mzima, kiasi cha kunifanya nikate tamaa kabisa. Lakini nakumbuka siku kama ya 27 au 28 hivi tangu nitume ule mzigo, nikasikia simu inaita nikiwa bafuni. Nilitamani kutoka na povu kichwani, kwani kwa wakati huo wote sikuwa najiruhusu kukosa simu hata moja. Nilipotoka haraka sana nilishika simu yangu na kuona namba mpya. Lahaula, moyo ulistuka, nikasema ndio nshamkosa hapa. Nilishika simu kupiga huku moyo ukienda kasi kama treni ya umeme, na sijui kwanini akili yangu yote iliniambia ndiye, kwani kama mfanyabiashara haikuwa kitu cha ajabu sana kupokea simu mpya. Lakini nadhani siku hiyo moyo wangu uliamua kunielekeza kwa Ninah. Nilijaribu kupiga lakini haikupokelewa, hapo nikakata tamaa kabisa. Lakini baada ya kama nusu saa simu iliita tena, namba ile ile, nikiwa nimejilaza kitandani kwangu na kuitizama kana kwamba nimeambiwa nisubirie. Niliipokea nadhani kabla aliyepiga hajajua kama imeanza kuita. Ikasikika saauti ya kike Kwenye simu: Halo! Mimi: Halo, habari? (nikajibu huku nikiisikilizia sauti, na kujaribu kuwa na sauti nzuri ya kiume na ya upole) Kwenye simu: Nzuri, naongea na Maxwel? (mzigo wa mwisho kumtumia uliokuwa na namba ya simu, nilijitambulisha kwa jina hilo moja) Mimi: Ndio, hujakosea, nani mwenzangu? (hapo sasa nilibakiza hatua moja kuhakikisha kwamba huyu ndiye. Sikungoja tena kusikiliza sauti, ilibidi nimuulize) Kwenye simu: Naitwa Ninah Sikusubiri aendelee kuzungumza au kujieleza zaidi. Nilipiga kelele, bila hata mimi mwenyewe kujua imekuaje nimepiga kelele kubwa namna hiyo. Lakini nilijikuta nashangilia kwa sauti, huku nikimshukuru sana kwa kupiga nisijali kwamba amepiga kukubali wito au pengine kunionya nisiendelee kumtumia zawadi. Nilianza kumshukuru sana kwa kunipigia, nikimwambia jinsi gani nimekuwa nikisubiria simu yake. Nilitumia kama dakika mbili nzima kujieleza jinsi gani simu yake imekuwa ya maana kwangu. Baadaye nikajistukia, ikabidi nimwambie,”Hata kama umepiga kunionya au kunigombeza lakini kitendo tuu cha wewe kunipigia simu nafsi yangu imefurahi sana”. Alicheka kwa sauti kidogo, nikavuta pumzi nikiwa na matumaini kwamba kwa cheko lile basi kuna shwari. “Nimekuwa nikipata parcel zako, nashukuru”, alianza kwa kusema hivyo, nami nikamjibu kwa haraka,”Asante wewe mrembo, kwa kupokea”. “Kwani ulinipa nafasi ya kukataa?” alitania, “Hapana lakini kitendo cha kunishukuru sasahivi kimenipa amani kwamba ulizipokea. Sasa niambie kama naweza kukuona tafadhali. Hata kama huna cha kuniambia, au kwenye simu hii ulitaka kunitukana basi utafanya hivyo huku umenitazama sura”, nilijipendekeza na kujihami huku nikimsihi tuonane. Alicheka kidogo na kuniambia, ni sawa. Nadhani unapata picha ni furaha kiasi gani nilikuwa nayo kupata hiyo fursa. Alitaka kuanza kuuliza maswali kuwa naishi wapi na tutaonana wapi nikamkatiza na kumjibu kwa haraka,”Niambie ratiba yako tuu mrembo, lini na saa ngapi ungetaka tuonane. Wapi pa kuonana tafadhali niachie mimi, nitakuchukua ofisini kwako au popote utakapotaka nikuchukue siku hiyo tutakayo onana”. Aliguna na kukubali kwamba tungeonana siku mbili baadaye. INAENDELEA...

at 8:31 PM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top