Home → simulizi
→ RIWAYA: HIGH SCHOOL
SEHEMU YA KUMI NA NANE.
Lilikuwa ni jambo la kumshukuru Mungu katika maisha yangu alijibu maombi yangu ulikuwa ni wakati ambao furaha yangu ilikamilika kwa kiasi kikubwa.
Niliona ya kwamba hatimaye naweza kuachiliwa kwa hiyo kesi. Kwa tuhuma nilizokuwa nimepewa kwa mauaji ya Candy.
Tumaini lilirejea kwa kasi na tabasamu pia, ingawa nafsi yangu haikuacha kujuta kwa kumpoteza Martin nilijuta kwanini nilibadilisha laini, Martin ungekuwepo ungekamilisha furaha yangu.
“Kama kweli ungenipenda usingejali kuhusu mtoto huyo ambaye sio wa kwako” niliendelea kuwaza
Ilikuwa ni furaha sana kukutana tena na baba yangu na shangazi yangu.
Niliwakumbatia kwa nguvu sana, baba alilia kama mtoto,
“pole mwanangu hii ndiyo mitihani ya maisha” alisema baba.
Nilishindwa kumjibu chochote nilibaki nikitoa machozi,
“tunamshukuru sana wakili Happiness kwa kukusaidia”
Nilimgeukia mwanamama yule nilishindwa hata kutamka neno la shukrani kwake kila neno niliona halifai hakika alistahili shukrani nyingi sana.
Nilimwachia baba na kwenda kumkumbatia wakili wangu Happiness
“Mungu azidi kukutunza”,
alisema “usijali binti yangu”.
Nilimwangalia na kisha nikaachia tabasamu, alitabasamu pia, hakika alionekana kuguswa sana na mimi nilimwona kama malaika aliyoshuka kutoka mbinguni, asante mungu kwa kumleta malaika wako duniani.
“Sasa” alisema
“tuelekee nyumbani”, wakili yule aliongea kwa sauti yake nzito.
Tuliingia kwenye gari na safari ya kuelekea nyumbani, Kapri point alipokuwa akiishi ilianza.
Tulikuwa tuna furaha sana vicheko vilisikika mule garini tuliongea mambo mengi na stori za hapa na pale hadi tulipofika.
Tuliingia sebuleni kulikuwa kuna hafla fupi ilikuwa imeandaliwa, tulikunywa tulikula na baadhi ya watu walialikwa.
“Nashukuru Mungu nimeweza kufanikiwa kumtetea huyu binti ingawa bado kesi haijaisha lakini yapo matumaini makubwa sana ya yeye kuachiwa katika kesi inayomkabili kwasababu hahusiki na Mungu amemtetea” alisema mwanamama yule ambaye anaonekana ana imani kali ya Mungu.
Nilitoa uchozi.
Niliitwa kutoa neno lolote nilitoa neno la shukrani huku nikimwombea baraka tele Happiness kwangu alikuwa ni mama yangu mwingine.
“Mama umerudi tena kupitia huyu kiumbe wako, ulikuwa ukinitetea na kunipigania siku zote mama yangu sasa nafasi yako Happiness ameichukua”, niliwaza kwa furaha ndani ya moyo wangu.
Usiku nililala kwa amani zote huku ndoto nyingi tamu zikiniijia.
Nafsi yangu sikuacha kuwa na majuto kwa kumpoteza Martin nafsi iliniuma sana.
Kwa njia zote nitahakikisha nakupata nilisema.
Siku ziliendelea na kesi yangu ilihairishwa ili kupisha kujifungua kwa maana siku za kujifungua kwangu zilikuwa zimekaribia.
Nilikuwa nachoka sana, na ilinilazimu kufanya sana mazoezi ili isilete shida wakati wa kujifungua ukizingatia sikuwa na umri mkubwa sana.
Nilikuwa nikiamka asubuhi na kukimbia nusu kilometa, kisha kurudi, baada ya hapo ningefanya kazi mbali mbali pale nyumbani. Hakika nilikuwa mchapakazi sana. Wakili happy alinipenda.
Baba aliniita siku moja,
“huyu mwanamama ana roho nzuri sana, ujue tangu nilipoondoka nililazwa hospitali kwa muda mrefu sana, nilikuwa sipati nafuu yoyote nilihisi ningekufa wakati wowote.
Wewe pekee ulikuwa tumaini langu na kukamatwa kwako na polisi nilijua utaishia gerezani.
Ndipo siku moja huyo mama alinipigia simu aliniambia amesikia habari zako na anataka kukutetea.
Hivyo kila kitu kitakuwa katika mikono yake kiasi fulani ilinipa faraja na amani nilijitahidi sana kupata unafuu nilijitahidi kula na kufanya mazoezi ili kuwaridhisha madakatari kuwa nimepona ili nije huku Mwanza niendelee kuisimamia kesi yako.
Nilimwambia kwamba nitakuja Mwanza.
Alinikaribisha hapa kwake tangu nimefika mimi na shangazi yako tunaishi hapa, tunaishi vizuri anatuhudumia kama ndugu zake.”
“Ukweli huyu mama ana roho ya upekee sana”, aliongea baba kwa huzuni.
Maneno ya baba yalinitoa machozi nilishindwa jinsi ya kusema nilishindwa kuongea chochote kumhusu mwanamama huyu ambaye kwangu alikuwa kama malaika.
“Baba yote ni mipango ya Mungu zaidi ya yote tumshukuru Mungu kutufikisha hapa Mungu alishamuandaa wakili Happiness kwa ajili ya hili”,
“ni kweli mwanangu” aliongea baba akinikumbatia.
Tuliishi kwa amani kama ndugu wa wakili Happiness.
Siku moja aliniita,
“Catherine unampango wowote wa kumwambia Maloya kwamba huyu ni mtoto wake”
“hapana nitamlea mwanangu mwenyewe” alitabasamu,
“haya sawa” alicheka kabisa.
“Mbona unacheka” nilimuuliza na mimi nikicheka.
“Hamna, nilitaka kujua msimamo wako, uko vizuri sana”
Alipenda sana ucheshi nilimpenda kwa hilo.
Siku zangu za kujifungua zilikaribia, ilikuwa kiasi kama mwezi mmoja tu ili nijifungue.
Siku moja jioni baada ya maongezi mafupi ya hapa na pale nilianza kusikia maumivu makali.
“Baba tumbo linaniuma” nilimwambia baba.
“Nenda kapumzike mwanangu unywe na dawa.”
Nilinyanyuka nilijitahidi kutembea lakini nilishindwa baba alinisaidia kunipeleka chumbani kwangu,
“baba tumbo linaniuma sana” nilimwambia.
“Ngoja nipige simu wakili Happy” ambaye wakati huo alikuwa ofisini kwake.
“mwite shangazi” nilisema.
Shangazi aliitwa “Mungu wangu anataka kujifungua huyu.”
Nilishtuka “mmmh!!”
Maumivu yake yalikuwa makali sana ambayo hayawezi kusimulika.
Wakili alipigiwa simu haraka sana alirudi na kunipakia kwenye gari kisha kunipeleka hospitali ya bungando nilipokelewa na kuingizwa leba.
Uchungu wa kuzaa ulikuwa mkali sana kwangu nililia sana mpaka nilihisi kuishiwa nguvu, manesi walikuwa wakinitia moyo kwamba niendelee kusukuma kwa nguvu na mimi nilijitahidi kusukuma mtoto kwa nguvu ili mtoto atoke.
Wakili happy alikuwepo humo ndani ili kunisaidia.
Nilisukuma, hatimaye mtoto aliweza kutoka nilifurahi sana kumpata mwangu kifungua mimba changu.
Nilipelekwa chumba cha kupumzika muda mchache baadae nesi aliingia,
“hongera sana Catherine umejifungua mtoto wa kiume”.
Hakika moyo wangu ulijawa na furaha sana lakini kila nilipomkumbuka Maloya roho iliniuma sana. Naomba huyu mtoto afanane na mimi asifanane na Maloya maana roho itaniuma sana naweza nikamchukia nilipeleka maombi yangu kwa Mungu.
“Mtoto yuko salama mzima na pia ana afya njema, mda si mrefu utaletewaa mtoto wako umuone” nesi aliongea huku akiachia tabasamu.
“Asante Mungu kwa zawadi ya mtoto” nilisali tu hivyo,
Baada ya muda mfupi nililetewa mtoto wangu. “Mungu wangu!!” nilijikuta nikisema kwa mshangao.
<<<<<<<<<<<<<<<< ITAENDELEA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: