Home → simulizi
→ RIWAYA: HIGH SCHOOL
SEHEMU YA KUMI NA SABA.
Walikuwa ni askari wawili ambao sura zao zilionekana hazitaki masihara,
“samahani” waliongea kabla sijawasalimia,
“bila samahani”, niliongea huku nikitetemeka,
“hatuna shaka kuwa wewe ni Catherine Kindamba” alisoma kwenye karatasi lake na kisha kuniambia.
Nilijua mwisho wangu umefika, nilijibu kwa kitetemeshi,
“ndio, ndio mimi.”
Walitikisa vichwa wakaangaliana na kisha kunigeukia,
“uko chini ya ulinzi kwa kuhusika na mauaji ya Candy Carry jijini Mwanza.”
Waliongea.
Nilishusha pumzi nzito, nilishindwa la kuongea, waliichukua mikono yangu kisha kuifunga pingu.
“Naombeni basi nimuage baba yangu” nilisema huku nikitetemeka kwa woga huku machozi yakianza yakinitiririka,
“apewe taarifa kuhusu kukamatwa kwangu.”
Walinisukumiza ndani, na kisha kugonga mlango wa ndani, shangazi alifungua alishangaa kunikuta na pingu mkononi.
“Kakaaa!!” aliita kwa woga.
“Njoo uone!!”
Baba alitoka kwa uchovu.
“Hatuna shaka wewe ndiyo mzee Kindamba”
“Ndiyo, ndiyo mimi”
“Mwanao Catherine anatuhumiwa kwa kuhusika na mauaji ya mwanafunzi mwenzie katika shule ambayo alikuwa akisoma Hanspop Academy Mwanza, hivyo tunamweka chini ya ulinzi na mara moja tutamsafirisha kuelekea mwanza kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo.”
Baba aliishiwa nguvu alidondoka na kuzimia papo hapo, bila kujali polisi wale walinitoa nje na kunipandisha kuelekea katika difenda lao na safari ya kuelekea kituo cha polisi cha kati ilianza.
Nilikuwa nikilia njia nzima mungu wangu naomba uniokoe katika shimo la simba hawa.
Nilifikishwa pale kituo cha kati cha polisi, nikaandika baadhi ya maelezo kuhusu mimi na baada ya hapo nilianza safari ya kuelekea mwanza mji ambao sikutamani tena kurudi.
Machozi yakinibubujika njia nzima nilibaki nimetulia tu nikitafakari jinsi ninavyoenda kufia gerezani, niliwaza mtoto wangu aliyeko tumboni moyo uliniuma sana.
Tulifika mwanza usiku wa siku hiyo ulikuwa ni usiku sana nilipelekwa moja kwa moja kituo cha polisi na kisha kufungiwa kwenye chumba kilichokuwa na giza. Nilianza kulia upya nililia sana.
“Mtoto mdogo muuaji.”
Polisi mmoja wa kike alisema kwa dharau.
“hebu acha kelele huko unasumbua masikio yetu”, alisema.
“Eee Mungu naomba uniokoe”
Nilipiga magoti na kuanza kusali.
“Mungu naomba unisaidie, wewe unajua sikuhusika na kifo cha Candy naomba niokoe” nilisali sana.
Baada ya hapo kesi yangu ilipelekwa mahakamani.
Nilisimama mahakamani siku ya kwanza na sikutakiwa kujibu chochote hadi nitakapopata wakili wangu.
Nilimaliza kusema hayo huku nikilia, wakili alikuwa mbele yangu ambaye nilikuwa namuhadithia mkasa mzima wa maisha yangu, alikuwa akilia pia. Mwanamama huyo mrefu mweusi hakusita kuonesha huruma aliyokuwa nayo kwangu,
“pole sana binti yangu.”
“Asante”
“Umekaa hapa mahabusu kwa muda gani?”
“Nina miezi miwili”
“Pole sana”
“Asante”
“Ujauzito wako unaweza ukawa una miezi mingapi?”
“Mara ya mwisho kuhudhuria hospitali ulikuwa na miezi mitano, unaweza ukawa na miezi saba kwa sasa.”
“Pole sana”
“Nashukuru”
“Nitakusaidia, nitahakikisha unatoka hapa”
“sina hata cha kukulipa zaidi ya kushukuru”,
“labda tu nikupe taarifa za wazazi wako.”
“Baba yako anaendelea vizuri na muda wowote anaweza akafika hapa kwa ajili kufuatilia kesi yako pamoja na shangazi yako, ninawasiliana nao mara kwa mara na ninawajulisha kuhusu hali yako. Nakuhahakishia kuwa utatoka hapa uwe na imani na usiache sana kuomba”.
Alizidi kunitia moyo mwanamama huyu.
Nilifuta machozi, na kumshukuru sana mwana mama huyu.
“Usijali binti yangu haya yote ni mambo ya dunia yataisha tu”, alisema
“Asante mama yangu” nilijibu kwa sauti ya kukauka.
“Sasa ngoja mimi niondoke nikaandae mpangilio mzima wa kesi yako kwa sababu una ujauzito mkubwa nitaomba rufaa ili utolewe humu. Kwasababu mazingira ya humu hayawezi kuruhusu wewe kuendelea kukaa na ujauzito mkubwa hivyo. Hivyo basi naomba urudi nikajaribu kuongea nao nakutakia wakati mwema.”
“Asante sana”
Aliongea yule mama na kisha kuondoka mahali pale, polisi walikuja kunikokota na kunirudisha kwa wenzangu, sikupenda kujichanganya nao.
Mara nyingi walikuwa wakinisema,
“daa aisee unaweza kukutana na watu na usiamini, kabinti kadogo hivi kauaji bora mimi limama lizima nimekamatwa kwa kesi ya kuiba. Huyu mtoto mdogo hivi kaua mtu akija kuwa mmama kama mimi huyu si gaidi kabisa”
Maneno yao yaliniumiza sana ila sikutaka kujali ukweli wote nilikuwa naujua mwenyewe na nisingeweza kukaa kumwadithia kila mtu.
Nilidumu katika kuomba siku zote, sikuacha kuomba kwa ajili ya maisha yangu na kwa ajili ya kesi iliyokuwa ikinikabili.
Baada ya wiki moja yule mama alirejea tena,
“Cathe” aliniita baada ya kufikishwa mbele yake.
“Unamfahamu Edwin?”
“Edwin!! Hapana”
“Humfahamu Edwin Maloya?”
“Namfahamu sikuwa najua kama anaitwa Edwirn”
“Ahaa, Yeye atatoa ushahidi kuhusu kesi yako kwamba unahusika.”
“Mimi naona kama anaweza kumaliza kwa kutoa ushahidi huo”
Nilivuta pumzi na kuishusha.
“sijui itakuaje wakili.”
“Lakini ulisema mara ya mwisho alikuwa akikutafta Candy na ulipofika chooni mlianza kuzozana kabla hajadondoka”
“Ndio”, nilimjibu.
“Utaongea hivyo kisha utasema alishikwa na kizunguzungu kabla ya kudondoka sawa”
“Ndio” nilijibu kwa unyonge
“Usijali lazima utoke, hii kesi wala haiwezi kukufunga ni kesi ndogo sana”
Najua kuwa alikuwa akinitia moyo tu.
“Naenda kuendelea kupanga kesi yako nitakuja tena pale nitakapokuhitaji uwe na wakati mwema” aliondoka.
Nilikuwa nimekaa nimejinamia kiunyonge baada ya siku nyingi kupita bila wakili kurejea.
“Moyo uliniuma sana nilihisi ameamua kuniiacha, peke yangu kwanza yule wakili ni nani na ametokea wapi mbona mi mimi simjui.”
“Atakuwa ameamua kuniacha peke yangu mimi najua mungu wewe ndio msaada wangu”.
Nilijiinamia kwenye chumba hicho ambacho hakikua na hadhi ya binadamu kuishi.
“Catherine Kindamba”
Nilisikia jina langu likitwa kwa sauti ya ukali, nilisimama
Mlango ulifunguliwa na kisha nikaamuliwa kutoka nje nilitoka, nilipelekwa hadi kwa mkuu wa gereza.
Nilishangaa kuona nakabidhiwa vitu vyangu
“Mungu wangu nini kimetokea!!”, nilimkuta wakili amesimama pembeni katika mlango wa kutokea.
“Mama nilimwita na kwenda kumkumbatia huku machozi yakibubujika”,
“Ashukuriwe Mungu” alisema tu mwanamke yule.
“Nini kimetokea?” nilimwachia gafla na kumuuliza.
“Niliomba ukae nje kwa sababu ya kesi yako, kwamba huhusiki na mauaji ya Candy, lakini pia una ujauzito”.
“Hivyo sio mahali salama kuwepo huku ukizingatia siku zako za kujifungua zimekaribia”, nilishusha pumzi ndefu na kuangua kilio.
Tuliongozana hadi nyumbani kwa mwanamama yule.
<<<<<<<<<<<<<<<< ITAENDELEA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: