Home → simulizi
→ NDOA YANGU.....
EPISODE 8
ILIPOISHIA..
Zimepita siku tano tokea nifanyiwe like tukio la kinyama ule usiku, siku tano baada ya baba kumpigia simu Tony na kumtaarifu na siku tatu tokea nitoke hospitali ya Bugando, bado Tony hajaja na hapokei simu tena....
Sina nilichobakiza kusema nitaiishi kesho, nipo radhi nife hata sasa hivi......
Sasa endelea....
Baada ya miezi mitatu ya kumpigia simu Tony bila mafanikio yoyoye hatimaye nikakata tamaa. Nikajua ndoa yangu imeshavunjika. Nililia vya kutosha, na hasira zilinifikia kiwango cha mwisho kabisa.
Nikajidharau nafsi yangu hata nguvu ya kusali ikanikimbia..sikuwa nasali tena. Nilijaribu kutafuta maana ya ukimya wa Tony kwa njia tofauti lakini jibu lake ilikuwa ni kwamba Tony hanipendi tena kiasi cha kupigania ndoa yetu.
Nilimtumia text za aina mbalimbali, lakini kwa miezi yote mitatu hakuwahi kujibu hata moja ingawa zilikuwa zikipokelewa. Sikuweza kuelewa inakuaje mwanaume anakua kimya kiasi hicho wakati amesikia kabisa mke wake kuwa amebakwa!!
Ile Ijumaa mchana Kama kawaida yake mama alikuja chumbani kwangu na kuniuliza ni nini kimetokea kati yangu na mume wangu. Alikuwa ameshaanza kugundua kuwa kuna tatizo katika ndoa yetu ila kila siku nilikua ninamkatalia na kumwambia kila kitu kipo sawa.
"Vicky, unajua nini? Mimi na baba yako tumejaribu vya kutosha. Umekaa nyumbani kwetu mwezi wa tatu huu na mume wako hata simu hapokei. Huwezi kusema hakuna tatizo huko ulikotoka. Mimi nimeolewa mwaka wa 35 sasa na ninajua mengi ya ndoa kuliko wewe uliekaa miezi 12 tu"
"Mama, please sina hata nguvu za kuanza kubishana hapa."
"Sawa, kama ndio hivyo mimi na baba yako tumeonelea kwamba huwezi kuendelea kuishi hapa. Hatuwezi kutunza mke wa mtu sisi. Na kwa kuwa wewe na mmeo mmeshindwa kutuheshimu kiasi ya kutafuta ushauri kwetu, basi ni bora urudi kwa mume wako au kokote kule utakapoona wewe panakufaa ila hauwezi kuendelea kukaa hapa na wakati wewe ni mke halali wa mtu."- mama alizungumza kwa huzuni iliyochanganyika na hasira."
Nikiwa bado nashangaa maneno mazito aliyoniambia nikamwita; "Mama?"
"Ndio mwanangu"
Nikawa sina namna nyingine tena, maji yamenifikia shingoni! Sina Plan B!!
"Mama, Tony na mimi tuna matatizo makubwa, ndoa yetu ndio kwanza ina miezi 12 na bado hatujui ni namna gani tutasonga mbele."
"Sawa mwanangu, sasa nieleze kila kitu, mimi nakusikiliza, usinifiche chochote."
Hivyo basi, nikakaa saa moja nzima nikimuelezea kila kitu kilichotokea katika ndoa yetu kuanzia ule usiku baada ya sherehe ya harusi nyumbani kwa Tony, honeymoon mpaka ile siku nimeondoka kwa Tony!
Kwa mshangao wangu mama hakuingilia kati wakati namwelezea wala hakunikaripia. Nilitegemea aanze kunifokea wakati nikiendelea kumuelezea lakini hakufanya hivyo, alitulia kimya akinisikiliza. Utulivu wake ulinishangaza.
Baada ya kumaliza kumsimulia mama akaanza kuongea...."Heheheeee Vicky weeee mwanangu"...akaanza kuongea kwa kisukuma huku ameshika kichwa (akimaanisha nimeharibu dunia)
"Mama, kipi mimi nimekosea? Inakuwaje Tony amenitelekeza hapa? Mapenzi yake ni ya mashaka mama, hanipendi kama mke wake mama!!" Nikamweleza mama huku nikiwa na hasira na kukata tamaa.
"Jambo la kwanza mwanangu lazima uhame hilo kanisa. Hiyo aina ya mama mchungaji wa kanisa lako sio mtu mwenye hekima kabisa na hukupaswa kumsikiliza. Kwanini hukunipigia mimi mwanangu? Kwanini hukuongea na mtu mwingine mbali na mama mchungaji wa hilo kanisa lako?"
"Mama, wewe ndiye uliyenieleza kwamba masuala ya ndoa yangu yawe siri."
"Hapana mwanangu, sio wakati mambo yanatuendea kombo, wote hua tunahitaji msaada"
"Sawa mama, sasa tunafanya nini? Unafikiri kuna nafasi ya Tony na mimi kurudiana tena?"
"Ndio mwanangu, mimi na baba yako tumekabiliana na vita vikubwa sana katika kipindi cha ndoa yetu. Ndoa inapigwa vita sana, tunapigana, tunashambulia, tunashinda. Na kesho tena vita mpya inaibuka.
"Kamwe hatukukata tamaa, vita hii huisha pale unapositisha mapigano. Vicky endelea kupambana mpaka ushinde hii vita, hakuna mwisho hapa. Ulifanya maamuzi ya hatari na ukachukua hatua zisizo sahihi hata kidogo."
"Mama, vipi kuhusu Tony? Nae amechukua maamuzi yasiyo sahihi pia."
"Ndio, nitaongea na Tony lakini nataka niongee na wewe kwanza. Nilikwambia usijipe pressure ya kupata mtoto. Atakuja tu! Hukutakiwa kufunga na kumnyima mume wako tendo la ndoa, sio mimi nilekwambia chakula akipendacho mume kuliko vyote ni tendo la ndoa? Mbona umeniangusha mwanangu?
Hata Biblia iko wazi kabisa katika hili, Waraka wa kwanza wa paulo mtume kwa Wakoritho 7:3-5 paulo anawaambia, "Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; Vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu."
"Vicky, mumeo hakupatana na wewe kuhusu kufunga, ulilifanya hili jambo pele yako..hata hivyo ulitakiwa umpe haki yake ya ndoa kati ya saa kumi na mbili jioni unavyofungua na mwisho saa sita siku inapoanza.
"Vilevile Vicky hukutakiwa kukimbia nyumbani kwako bila hiyari ya mumeo na kuja kujificha huku. Kukueleza ukweli, Ni mpaka Mungu aingilie kati kwa Tony kuja kulala na wewe tena."
Umesahau yale niliyokuusia kipindi unaolewa? Ngoja nikukumbushe yale maneno mwanangu nilikueleza haya;
Nilikufundisha jinsi ya kuheshimu mume, na kutokuwa na hasira zisizo na msingi. Lakini kama utafanya vinginevyo, hutakuwa binti yangu niliyekuzaa bali mwanamke mwenzangu.
Binti yangu, nilikueleza unamuona mumeo? Ni gentlemen haswa! Ila usichukulie faida ya yeye kuwa gentlemen kumletea mizengwe.
Nilikwambia Usilete ujinga dhidi yake. Mwanangu unaona hili kovu kwenye paji langu la uso? Baba yako ndio alinipa hili kovu.
Alinivumilia muda mwingi sana, ila siku moja from nowhere nilimuudhi tena, najua halikuwa lengo lake ila hasira zilimfika hapa akanipiga mara moja na kunumiza.
Mamii, Wanaume wanachukia pale unapomwambia "HUWEZI". Anajua anaweza akafanya zaidi ya hapo lakini anafanya hivyo kukulinda asikuumize. Nilikueleza Binti yangu pale kutakapokuwepo na kutouelewana, jaribu kunywa maji, huwezi ukaongea huku maji yapo mdomoni.
Nikakueleza kuwa sasa una familia mbili. Una bahati sana mamii, Vumilia na heshimu familia yako kama ulivyokua ukifanya hapa. Jifunze kuwakarimu watoto wa majirani zako, na karibuni watoto wako wataizunguka meza yenu kwa upendo mkila pamoja chakula kwa furaha.
Nikakuonesha lile hotpot langu kubwa! Nililinunua wakati bado sina hata mtoto mmoja, kabla ya kuwazaa ninyi. Lakini mara kadhaa nilipika chakula na kulijaza na kula pamoja na watoto wasio na pa kula.
Nilikifunza kuwa mkarimu, wakarimu wageni walau hata kwa maji ya kunywa. Usinyanyapae wageni, usidharau ndugu wa mumeo bali walete kwa pamoja. Jifunze ku appreciate jitihada ndogo zinazofanyika na karibuni watajifunza mengi kutoka kwako na watakupenda.
Nilikwambia Pale kutakapokuwa na kutokuelewana, usirudi hapa nyumbani. Msuluhishe wenyewe huko huko na jenga nyumba yenye furaha. Nilijenga yangu na baba yako amekuwa akifurahia mpaka kesho.
Nikakwambia wazi kabisa kwamba Mamii wanaume wanapenda chakula kizuri. Wanapenda vyakula vyote cha jikoni na cha chumbani. Usimnyime chakula cha aina yoyote eti kwa sababu hamna maelewano. Hiyo ni sumu katika ndoa!
"Wote wawili mmeharibu mambo. Hili tatizo halikutakiwa kufikia hatua hii. Jambo la kwanza kesho asubuhi , tutarudi wote Dar es salaam, tunaenda kumuona mume wako."
KAWE, DAR ES SALAAM.
NI Kweli, Jumamosi asubuhi tulipanda ndege ya saa mbili, tukafika Dar es salaam saa tatu asubuhi. Mpaka saa tano asubuhi tulikuwa tumefika nyumbani kwangu. Nilipouona tu gari ya Tony imepaki uani, moyo wangu ukaanza kudunda kwa kasi mno.
Nikatamani asiwepo nyumbani, ingawa mama alishampigia simu jana usiku kumuelezea ujio wetu. Tulipoukaribia tu mlango Tony akaja kutufungulia. Nafikiri alituona kupitia dirishani wakati tukiingia.
Akamsalimia mama kwa kisukuma, lakini mimi akanipotezea....hakunipa salamu kabisa, mama akatabasmu! Nikawaacha sebuleni mimi nikapitiliza moja kwa moja chumbani kwangu. Kila kitu nilikikuta kama nilivyokiacha na kwa uchunguzi wangu sikuona dalili yoyote ya mwanamke kuishi na Tony.
Nikamsikia mama akiniita sebuleni na haraka haraka nikaenda kujiunga nao.
"Mama, Vicky hataki ndoa. Kwa mwaka mmoja tu wa ndoa yetu ameshanionesha dharau, kiburi na kutonitii kwangu na kwa nyumba hii. Me nimechoka.kwa hayo. Hafikirii angekuwa mwanaume mwingine, asingeanza kuchepuka kwa hivyo vituko alivyokua akinionesha??"
"Mama mimi Nimekua muaminifu pale Vicky aliposhindwa kuwa muaminifu kwenye majukumu yake kwa ndoa, nimevumilia kipindi chote hicho mama sikuwahi kumsaliti hata siku moja......." Tony akawa akiongea kwa hasira huku akilengwa na machozi......
_____________________________
Je vipi kuhusu hali ya afya Vicky?, Je kwanini Tony alikaa kimya muda wote wa miezi mitatu asipokee simu wala kujibu texts za Vicky? Je vipi kuhusu mustakabali wa ndoa yao? Ama hakika maswali ni mengi...
ITAHITIMISHWA BAADAE......
Share
Jumaa mnak
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: