Home → simulizi
→ JAMANI BABA
SEHEMU 01
Mume wangu leo nataka kukiri jambo moja
kwako, naamini litakukera sana lakini naanza
kuomba radhi nikiwa chini ya miguu yako, ”
alisema Zainabu akimwambia mume wake ,
Masalanda. ..
“Ipi hiyo? Mbona unanitisha mke wangu, mwaka
wa tatu sasa tangu tumeoana hujawahi
kuniambia hivyo .”
“Oooh ! Siku zote nilikuwa nafikiria namna ya
kukwambia mume wangu .”
“Sasa niambie basi .”
Zainabu alianza kuporomosha machozi na
kumfanya mume wake huyo kushangaa na
kukifikiria zaidi hicho kitu ambacho kimemfanya
mkewe aamue kukisema...
“Labda ameamua kuachana na mimi sasa
anashindwa kuniambia ?” aliwaza Masalanda .
“Utanisamehe kweli mume wangu ?”
“Nitakusamehe mke wangu, we niambie tu.”
“Unajua ... unajua wakati unanioa nilipokwambia
nilizaa mtoto akafa na nikawa sipati mimba
nilikudanganya mume wangu ... ”
“Ooo! Kumbe hukuwahi kuzaa kabisa?”
“Hapana, ila... ”
“Ila nini mke wangu hebu kuwa muwazi jamani!”
“Nina mtoto... ”
“Hee! Una nini ?”
“Nina mtoto mume wangu, nisamehe sana
sikukwambia nilikuficha kwa sababu nilijua
utaniacha wakati nakupenda sana mume
wangu,” alisema Zainabu huku akiendelea kulia.
Kwa mbali , Masalanda alianza kumuonea
huruma mkewe . Ni kweli walioana ukubwani
sana kwani Masalanda alikuwa na mke akafariki
dunia na mpaka kifo mwanamke huyo hakuwahi
kumzalia mtoto.
Wakati anakutana na Zainabu, aliamini atadumu
naye kwa sababu wote ni watu wazima tayari.
Aliamini kwamba kwa sababu alishazaa mtoto
akafa , basi watamtafuta mtoto wao kwa kudura
za Mungu mwenyewe.
“Zainabu, ” aliita Masalanda akitumia sauti ya
unyonge.
“Abee .”
“Hebu nijibu maswali yangu kadhaa
nitakayokuuliza.”
“Sawa .”
“Huyo mtoto ana umri gani ?”
“Miaka ishirini na moja .”
“Anaishi wapi ?”
“Yupo kwa shangazi yake, Tanga.”
“Anaitwa nani?”
“Mwaija .”
“Baba yake yuko wapi?”
“Alishafariki dunia , si nilikwambia. ”
“Hebu fanya mpango aje hapa, tumlee sisi . Mimi
nitakuwa baba yake.”
Zainabu alishtuka kusikia agizo hilo la mumewe
kwani siku zote , shangazi wa mtoto huyo
amekuwa akimwambia afanye juu chini
amchukue binti yake kwani ameanza
umachepele, anahofia asije akapata ujauzito
akiwa nyumbani kwake ikaonekana amemtuma .
“Kweli mume wangu?”
“Kweli , imetoka moyoni mwangu , sina kinyongo
na wewe. ”
Zainabu aliachia tabasamu kavu huku akijifuta
machozi kwa kanga. Mumewe alimkumbatia,
akampiga busu wakakaa sawasawa .
***
Ilikuwa siku ya tatu, Mwaija alikuwa ndani ya
basi la Raha Leo lenye maandishi nyuma
yanayosomeka; Tanga wadeka. Kila mara
alimtumia meseji mama yake akimjulisha
alipofikia. ..
“Mama sasa tunapita Segera .”
Mama yake alimjibu sawa , akamtakia safari
njema.
Moyoni Mwaija alikuwa na furaha iliyopitiliza ,
alitaka sana kuishi na mama yake, hasa
akizingatia kuwa anaishi katika Jiji la Dar es
Salaam ambalo aliambiwa lina kila aina ya raha
na karaha !
Alipofika Chalinze , mama yake alianza safari ya
kutoka Kigogo kwenda Ubungo kumpokea binti
yake huyo ambaye ilikuwa inamuuma sana kuwa
naye mbali .
Basi lilifika, Mwaija akashuka, mama akashtuka
moyoni maana mara ya mwisho alimuacha akiwa
na miaka kumi na nane . Alimshangaa kumuona
amenenepa, amenawiri , ametakata ile mbaya.
Kikubwa zaidi alimshangaza nguo alizovaa.
Mwaija alivaa suruali ya kubana, wenyewe
wanaita skintaiti na t- shirt juu. Kwa umbo
alilokuwa nalo Mwaija , kila mwanaume
alimuangalia kwa uchu wa mapenzi. ..
“Ha mama jamani ,” alichangamka Mwaija na
kumkumbatia mama yake kwa furaha. ..
“Shikamoo mama.”
“Marahaba mwanangu, lakini Mwaija hizo nguo
kweli ni za kuvaa mbele ya watu , si za kulalia
hizo?”
“Hamna mama, ndiyo fasheni yenyewe ya siku
hizi. Mama upo Dar es Salaam lakini hujui
mitindo?”
“Mimi sidhani kama nitapenda mwanangu , hata
baba yako niliye naye siamini kama atakukubali
kwa mavazi haya . Hapa natamani nikupeleke
wapi sijui ukabadili nguo ndiyo twende
nyumbani.”
“Jamani mama , basi nimekuelewa , twende tu
nyumbani nitavaa kanga nikifika. ”
Walianza safari ya kwenda nyumbani Kigogo .
Moyoni mama Mwaija alikuwa anaomba
mumewe achelewe kurudi nyumbani ili wao
watangulie kufika na Mwaija abadili nguo haraka
sana.. .
“Hivi na huyo shangazi yako ina maana alikuwa
hakuoni unavyovaa ?”
“Alikuwa ananiona . ”
“Sawa ? Akawa anakuacha tu unaharibika
hivihivi?”
Mwaija hakujibu swali hilo alihisi halimuhusu
yeye zaidi ya shangazi yake .
Kufika nyumbani, mlango ulikuwa wazi ...
“Mswalie mtume, keshafika huyu , sijui itakuaje?”
alisema moyoni mama Mwaija , wakaingia ndani .
Sebuleni alikaa Masalanda , alipomuona Mwaija
akashtuka.. .
“Karibuni. ..karibuni sana. ”
“Asante , shikamoo, ” alisalimia Mwaija huku
akikaa kwenye kochi kwa adabu .
“Marahaba, za safari?”
“Nzuri .”
“Karibu sana, karibu mwanangu, ” alisema
Masalanda huku akimkazia macho Mwaija na
kumshangaza mkewe kwani uchangamfu
ulikuwa mkubwa tofauti na alivyofikiria.
ITAENDELEAA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: