Home → simulizi
→ MAPENZI YA FACEBOOK.
*🅱 professional love*
Phidelis anasimulia;
Nakumbuka nilifahamiana naye kupitia Facebook, alikuwa ni rafiki yangu, nilipenda sana kulike pamoja na kukomenti picha zake. Alikuwa ni msichana mrembo sana, alijaaliwa kila sifa zinazoweza kumshawishi mwanaume yoyote rijali atamani kuwa naye. Alikuwa akijulikana kwa jina la Cleopatra Mushi ila kwa facebook alikuwa akitumia jina la Precious Girl, sijui kwanini aliamua kutumia jina hili ila pengine ni kutoka na uzuri aliyokuwa nao.
Alikuwa akipenda sana maisha ya starehe, picha zake alizokuwa akipost katika akaunti yake ziliweza kuakisi maisha halisi ambayo alikuwa akipendelea kuishi. Alionekana kuwa msichana wa maisha ya kitajiri sana.
Nilitamani sana kuwa naye kimapenzi ila sikuwa na maisha kama aliyokuwa nayo hivyo niliona sikustahili kufanya hivyo, niliogopa kumwambia.
Picha zake alizokuwa akizipost akiwa na mwanaume zilizidi kuniweka katika wakati wa maumivu sana, nilikuwa nikiumia kwasababu nilikuwa nikimpenda sana. Nilitamani siku moja afahamu ni kwa jinsi gani nilivyokuwa nikimpenda lakini muda haukuweza kuruhusu hilo.
“Nampenda sana huyu demu ila tatizo ana mtu wake,” niliamua kumueleza ukweli rafiki yangu Juma juu ya Cleopatra alivyokuwa ameniteka akili yangu.
“Sasaunachoogopa hapo ni nini?” aliniuliza Juma huku akionekana kutojali lolote.
“Tatizo ana mtu wake.”
“Mbona mimi sioni tatizo hapo kama unampenda mwambie ukweli halafu akikataa basi unakula kona,” aliniambia Juma.
Kwa kweli kila nilipokuwa nikizitazama picha za Cleopatra zilizidi kuniweka katika wakati mgumu, nilikuwa nikimpenda sana. Nilitamani afahamu ukweli wa moyo wangu. Ulikuwa ukimpenda japo mpaka kufikia wakati ule sikuwa nafahamu historia ya maisha yake.
“Umependeza mdada,” niliamua kukomenti picha yake moja aliyokuwa ameipost muda mfupi. Alikuwa amevalia sketi fupi iliyoyaacha vyema mapaja yake wazi yaliyoonekana kunona huku juu akiwa amevaa kishati kilichokuwa kimembana kisawasawa, kilimkaa vyema na kuzidi kuonekana msichana wa kisasa. Alipendeza sana tena na kwa weupe aliyokuwa amejaaliwa ndiyo kwanza alizidi kunoga.
“Asante mkaka,” alinijibu kitendo ambacho kilinishangaza sana, sikutegemea kama angeweza kunijibu kwa wakati ule.
Ngoja nikuambie kitu ndugu yangu, nilikuwa nikipenda sana kulike na kukomenti picha zake, nilikuwa nikijaribu kujiweka karibu naye ili japo niweze kupata nafasi ya kuzungumza naye lakini mara zote alikuwa ni mtu wa kunitolea nje, hakuwa akinijibu lolote.
Siku ile nilipoamua kukomenti picha yake na yeye kunijibu hakika nilikiona kuwa nikitendo cha kipekee. Niliitazama kwa muda wa dakika tatu lile jibu lake huku nikitabasamu. Nilikuwa nahisi furaha isiyokuwa na kifani.
Sikutaka kupoteza muda nikaamua kumfuata inbox.
“Mambo mrembo,” nilimtumia ujumbe mfupi lakini alikuwa kimya hakuweza kunijibu lolote. Sikukata tamaa, niliamua kumtumia tena ujumbe mwingine lakini hakuweza kujibu kitu. Tukio hili lilizidi kuniumiza sana, alikuwa akionekana kuwa online lakini hakuwa akizijibu meseji zangu jambo ambalo lilizidi kunifanya nianze kumuona alikuwa akijisikia.
Kila nilipokuwa nikiziona picha zake pamoja na mwanaume aliyekuwa akimpost katika akaunti yake nilikuwa nikijisikia vibaya sana, kuna kipindi sikutaka kabisa kumuona Cleopatra katika macho yangu. Niliamua kutoka facebook na kufanya mambo mengine lakini ajabu haikupita siku nilijikuta nikitamani kumuona msichana huyo hivyo niliingia facebook na kumuangalia. Nilijikuta nikifurahi mara baada ya kumuona. Alikuwa akivutia sana machoni mwangu.
“With my baby!” haya yalikuwa ni moja kati ya maelezo yaliyoambatana na picha aliyokuwa amepiga yeye pamoja na mwanaume mmoja aliyekuwa na asili ya kiarabu. Walikuwa wakionekana kuwa wenye furaha sana.
Nilizidi kuumia sana kila nilipokuwa nikimuona mwanaume huyo, nilimchukia sana katika maisha yangu japo sikuwahi kuonana naye.
Sikuchoka kumtumia ujumbe mfupi kila nilipopata nafasi niliamua kumtumia huku nikiamini kuna siku angeweza kunijibu jambo ambalo lingeweza kuufurahisha moyo wangu.
Baada ya kupita siku kadhaa aliweza kunijibu.
“Poa Phidelis, mzima wewe? Samahani nilikuwa bize ndiyo maana ukaona kimya.”
“Usijali, mimi niko salama kabisa sijui wewe mrembo.”
“I’m oky.”
“Nafurahi kusikia hivyo mrembo.”
“K,” alinijibu kwa kifupi kwa kuandika herufi “K” akimaanisha neno Ok.
Kwa kweli nilijisikia vibaya sana, niliona kama alikuwa amenidharau. Nilijaribu kumtumia ujumbe mwingine lakini hakuweza kunijibu lolote japo nilimuona kuwa online. Hilo lilizidi kuniumiza sana moyoni mwangu.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Kesho mahali hapa hapa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: