Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 25
Akajikuta tu ameachiwa na kuanguka kisha akainuka upesi na kuanza kutoka chumbani kwake kwa uoga na kufanya haraka haraka, kufika sebleni akamkuta Salome amekaa kwenye kochi, hapo ndipo akili yake ikapoteza dira kabisa.
Akashtuka ila Salome akacheka na kumuuliza,
“Unashtuka nini sasa?”
Rose alikuwa kimya kabisa na kushindwa kujibu kwani kadri alivyomuona Salome ndivyo uoga ulivyokuwa ukimshika, kisha Salome akamwambia tena,
“Wewe si ulikuwa unataka mimi niuwawe wewe, eti unamwambia Ashura aniwekee sumu kwenye chakula, sasa unashtuka saivi umeona mzimu au nsyuka? Si kila siku unaniona hapa, sasa unashtuka nini? Pona yako wewe ni kuachana na mambo unayoyafanya, kwanza kabisa uwafungulie wale uliowafungia”
Rose alikuwa akitetemeka tu, ila Salome aliendelea kuongea,
“Nipe ahadi utawafungua lini?”
“Nisamehe kwa hilo sitaweza kufanya, naogopa kufa”
“Kama wewe unaogopa kufa mbona unaua wenzio bila huruma? Kwani Moza alikukosea nini hadi ufurahie kifo chake?”
“Sikufurahia na wala sikutaka afe ila Moza alikuwa mbea ndio kitu ambacho sikukipenda”
“Mbea wa kuchunguza mambo yako mabaya unatyoyafanya, uliona nini kuacha baada ya kugundua ni mbea? Na hata hivyo, sababu mbea ndio utake afe? Angekuwa muongo je? Unajua tofauti ya mbea na muongo? Muongo huongea vitu vya uongo, ingawa kuna uongo wa aina mbili wa kubomoa na kujenga. Ila mbea anaongea vitu vya ukweli, tofauti ya ukweli na uongo ni moja tu, ukweli unauma ndiomana mtu mbea anaonekaga kuwa mbaya kuliko muongo. Ila siku ukikutana na mtu muongo na mnafki ndio utasema bora ya mbea.”
“Unanichanganya Salome, sipo hapa kuulizia tofauti ya mbea na muongo ila nipo hapa ili nipumzike kidogo, uwepo wako unanifanya nisiweze kupumzika”
“Toka lini wewe ukapumzika usiku? Huu si ndio muda wa kufanya mambo yako yasiyofaa? Halafu unataka mimi niende wapi nikapumzike pia?”
“Si kule chumbani kwa Moza”
“Chumba ambacho ulitaka kufanyia uchafu! Mimi niko makini kuliko wewe, niingie kwenye chumba ulichotaka kuzini na mlinzi wako!”
Kumbe Sara aliposikia mabishano sebleni alitoka, na muda huo ndio akasikia kuwa chumba cha Moza, mama yake alitaka kuzini na mlinzi wao. Alijikuta akisema kwa nguvu,
“Mama azini na mlinzi!”
Salome alijibu kanakwamba alitambua kuwa Sara angekuja na kuuliza hilo swali,
“Ndio, mama yenu alitaka kuzini na mlinzi kwenye chumba cha Moza. Muoneeni huruma mama yenu, kaeni nae chini muongee nae anapoelekea atazini hadi na maiti ili arekebishe nyumba yake. Rose nyumba imebadilika hii kama kitumbua tayari kimeingia mchanga, swala ni wewe tu kuachana na hayo unayoyafanya”
Rose aliinama chini kwani hapo ataliweza kudhihilika wazi kuwa anafanyaga mambo ya ajabu yani hata kujitetea hakuweza kabisa, alimuangalia mwanae kwa macho ya kuibia ila cha kushukia Salome alinyoosha mkono wake juu kisha Rose na Sara walijikuta wakilala pale sebleni.
Ilikuwa ni siku nyingine, siku hii Neema alikuwepo kwenye kijiji cha mama yake na kuamua kwenda kutembelea kaburi la baba yake kisha kwenda kumsalimia aliyekuwa mama yake wa kambo, na hapo akakumbuka kuhusu Ashura na kuamua kuuliza.
“Eti mama, nilikuwa na ndugu yangu mwingine kwa baba?”
“Mmmh atoke wapi?”
“Eti alizaliwa na mama mwingine”
“Neema, baba yako alikuwa na mtoto mmoja tu ambaye ndiye wewe ila hakuwahi kuzaa tena mtoto mwingine”
Ikabidi Neema amueleze mama yake huyu jinsi alivyokutana na Ashura na jinsi alivyojitambulisha kwake kuwa ni ndugu yake, ila huyu mama alionekana kushangaa sana na kumwambia Neema,
“Sikia Neema, wewe ni mtoto wa pekee wa marehemu baba yako. Hajawahi kuwa na mtoto mwingine sehemu yoyote, alipatwa na ugonjwa wa ajabu baaa tu ya kuzaliwa wewe na hakuweza kuzalisha tena, hata mimi sijazaa nae sababu ya matatizo hayo. Sasa hizo habari za huyo ndugu yako wa kuitwa Ashura sizijui, ningekuwa simjui vizuri mume wangu sawa, ila nilimjua vizuri sana na alipenda watoto balaa kwahiyo ingekuwa huyo mtoto wake lazima ningejua. Labda huyo Ashura ni ndugu yako kwa mama yako huko ila baba yako hajawahi kuwa na mtoto mwingine zaidi yako”
Neema alishangazwa sana na ile habari na kukumbuka jinsi Ashura alivyoonyesha kumfahamu, na jinsi alivyoishi nae kama ndugu yake hadi ilifikia hatua ya kumpa hadi siri zake, alishangaa kusikia baba yake hakuwa na mtoto mwingine kwahiyo Ashura hakuwa ndugu yake ila akajiuliza kama ni kweli hakuwa ndugu yake sasa kwanini kamdanganya? Hakupata jibu ila huyu mama yake wa kambo alimsisitizia kabisa kuwa hakuwa na ndugu wa dizaini hiyo.
Ana ndiye aliyemuamsha mama yake baada ya kumkuta anakoroma sebleni,
"Mama, mama imekuwaje tena?"
Rose aliamka ila alikuwa akishangaa shangaa tu, mara wale mapacha nao walikuja na kumuamsha Sara maana waliona mama yao akiamshwa na Ana. Walimuuliza dada yao kuwa kapatwa na nini hadi kalala sebleni, hakukumbuka kwa wakati huo, wakamsogelea na mama yao ila mama yao akawaambia wamuache na alitaka kwenda chumbani kwake ila aongozane na Ana, basi akaondoka na Ana na kuwaacha wale wengine pale sebleni.
Walibaki wakiendelea kumuuliza tu Sara kuwa ni kitu gani ila bado Sara hakuweza kuwajibu kwani hakuwa na jibu la imekuwaje kwa wakati huo, akili yake ilikuwa kama imesizi hivi kwa kiasi fulani, basi kaka zake wakamshauri kuwa akajiandae ili waondoke pamoja, nae Sara akainuka ili akafanye hivyo alivyoshauriwa na kaka zake.
alipofungua mlango wa chumbani kwake alishtuka sana kwani alimkuta Salome akiwa kitandani kwake amejilaza,
"Kheeee Salome!"
"Ndio ni mimi, mbona umeshtuka sana?"
"Sikutegemea kukukuta chumbani kwangu, umeingiaje bila ruhusa yangu!"
"Na wewe kwako kunataka ruhusa? kwani mama yenu kabla ya kufanya yote aliyoyafanya aliomba ruhusa?"
Ndio hapa Sara akajikuta akikumbuka mambo ya usiku na kujikuta akiuliza kwa makini,
"Ni kweli mama yangu alitaka kuzini na mlinzi?"
"Nadhani itakuwa vyema kama ukimuuliza mwenyewe"
Sara hakuendelea tena kuuliza chochote bali alitoka na moja kwa moja akaenda chumbani kwa mamake, na kugonga mlango ila alimkuta mama yake ndio alikuwa anatoka na Ana,
"Kheeee mama unaenda wapi?"
"Ndio salamu hiyo?"
"Hapana mama, shikamoo"
"Sina haja, Ana twende mwanangu"
Wakatoka na kumuacha Sara akiwa palepale mlangoni, ila alijaribu kuwafata nyuma ambapo aliwashuhudia tu wakiondoka bila hata kuwaaga wale mapacha waliokuwepo pale sebleni. Sara aliwasogelea kaka zake, ila na wao wakamshangaa kuwa hajajiandaa toka muda ule,
"Vipi bado hujajiandaa tu!"
"Jamani, si muda huu huu jamani!"
"Muda huu huu! Tumekusubiri hapa karibia lisaa limoja, unasema muda huu huu, kwakweli tunaondoka Sara"
"Jamani acheni masikhara, lisaa limoja limepita saa ngapi wakati ni muda huu huu!"
"Utatukuta ukija"
Na wao wakatoka na kuondoka kwahiyo wakamuacha Sara pale sebleni.
Muda kidogo Salome alitoka na kumwambia Sara,
"Ulitaka kuniacha peke yangu, hapana leo utashinda na mimi hapa"
Sara alimuangalia Salome na kuona kama mtu anayefanya mambo ya ajabu kwenye nyumba yao, ila hakumuuliza chochote zaidi ya kwenda chumbani kwake ili ajiandae na atoke hivyo hivyo.
Basi Sara akajiandaa na alipomaliza alitoka sebleni ilia toke nje na aondoke zake ila pale sebleni alikuwepo Salome ambaye alimwambia Sara,
“Si nimekwambia leo tunabaki wote!”
“Tunabaki wote kivipi? Mimi nina safari zangu bhana”
“Usiwe mbishi Sara, leo tunabaki wote humu ndani. Mimi leo siendi popote na wewe leo huendi popote. Tunabaki wote”
“Na wewe Salome aaah usinibabaishe bhana”
Sara akafungua mlango na kutoka nje, ila gafla akajikuta yupo chumbani kwake,
“Jamani si nimefungua mlango wa kutoka nje, iweje nimerudi tena chumbani?”
Hakuelewa aliona kamavile ni mchezo wa kuigiza, akatoka mule chumbani kwake na kwenda tena sebleni ambako alimkuta Salome amekaa kama kawaida na kuwaza kuwa mwanzoni laba ilikuwa ni mawazo yake ila si kweli kuwa alifungua mlango na kutoka nje, basi akajikuta akimuuliza Salome,
“Hivi tumeongea mimi na wewe muda si mrefu?”
“Ndio tumeongea, kwanini umeuliza?”
“Ulinikataza kutoka nje na ukasema tutabaki wote leo?”
“Ndio, leo tutabaki wote. Mimi siendi popote na wewe utabaki hapa na mimi”
Sara akamuangalia Salome bila ya kummaliza, kisha akaenda tena kufungua mlango wa nje na kujikuta yupo chumbani kwake tena. Akili yake sasa ikaanza kuchanganyikiwa kwani aliona kamavile ni mazingaombwe kabisa ukizingatia mambo hayo yalikuwa ni ya ajabu sana kwake, alijiuliza kuwa ule mchezo anafanyiwa na nani, kama ni Salome basi Salome ni mtu wa aina gani mwenye uwezo wa kukurudisha chumbani wakati ulikuwa ukitoka nje? Alifanya hivyo kama mara tano, na mar azote alijikuta akirudi chumbani. Uoga ukamshika na kuamua kukaa chini pale chumbani, akachukua simu yake na kumpigia mama yake.
“Mama, nipo ndani nataka kutoka ila nashindwa, eti kila nikitoka najikuta nimerudishwa chumbani”
“Mbona sikuelewi Sara, hebu nieleweshe”
“Sijui nikueleze vipi ila kutoka ndani ya nyumba siwezi”
Sara aliamua kama kumuelekeza mama yake kwenye simu ila bado ilikuwa ngumu kwa Rose kumuelewa mwanae, ikabidi Sara akate tu simu ya mama yake na kujibaza kwenye kitanda chake.
Rose muda huu alikuwa mwenyewe akielekea kwa Yule mganga, siku ya leo alimuacha Ana aende shule kama kawaida halafu yeye ndio alienda tena kwa Yule mganga, na njiani nio alipigiwa simu na mwanae Sara akimueleza jinsi hawezi kutoka ndani ya nyumba. Hiki kitu kilimstaajabisha sana Rose ila alijisemea kuwa atamwambia na swala hilo mganga kwani bado hakukata tamaa kuwa ameshindwa kupambana na alioamini kuwa ni mzimu ndio unasumbua ingawa mganga alimuhakikishia kuwa sio mzimu.
Alifika kwa mganga na kama bahati leo hakukuta foleni kubwa kama alivyoena mara ya mwisho. Yule mganga kama kawaida alianza kwa kumuelezea yeye matatizo yake,
“Najua kuwa umekosea masharti, tatizo lako mdomo, yani huwezi kunyamaza kimya”
“Nisaidie mganga nifanyeje?”
“Sasa inatakiwa nitume kombora la kushambaratisha nyumba nzima, yani kila kilichopo ndani kombora langu litaenda kusambaratisha”
“Ndani ya nyumba yangu?”
“Ndio nyumbani kwako, natakiwa kutuma kombora yani kila kitu kinasambaratika mule nani. Nyumba inakuwa nyeupe kabisa”
“Sasa mwanangu Sara yupo ndani”
“Yeye hajatoka? Mpigie simu na umshawishi atoke”
“Ametoka kunipigia simu na amesema kuwa kila akijaribu kutoka anashindwa”
Yule mganga akaanza kuangalia kibuyu chake, kisha akatikisa kichwa na kumwambia Rose,
“Ndani kwako kuna mtu yani yeye anajua mipango yetu kabla hata hatujapanga, kwamaana hiyo amefanya makusudi mwanao asitoke ili kombora likitumwa basin a mwanao adhurike”
“Huyo mtu ni nani?”
“Namuona binti mdogo, mwenye sura ya kipole ila ana roho ya kikatili”
“Anaitwa Salome huyo mganga, sijui ni mchawi”
“Najaribu kuangalia nguvu alizonazo huyu binti nashindwa”
“Mwanzoni huyo binti niliweza kumdhibiti lakini saivi siwezi, nilikuwa najua tunasumbuliwa na Moza kumbe ni Yule Yule Salome. Je Moza yuko wapi?”
“Naona kuna nguvu za Moza zikifanya kazi kwenye nyumba yako ila alipo simuoni, sema sijajua huyu binti ana nguvu za aina gani. Nadhani ni vyema kama nitakuja kwako”
“Dah utakuwa umenisaidia sana, huyo mtoto Salome sikumpenda toka mdogo ila kila nikijaribu kumuua nashindwa”
“Basi tutafanya kitu, nitakuja nyumbani kwako”
Rose alifarijika sana kusikia kuwa huyu mganga atafika nyumbani kwake, na aliamua kumuomba kuwa waende nae siku hiyo hiyo. Alimuomba sana na hatimaye Yule mganga akakubali.
Rose na mganga walijiandaa kisha wakaianza safari ya kwena nyumbani kwa Rose, walienda vizuri njia nzima hadi walifika getini kwa Rose na kufungua mlango na kuingiza gari ndani. Rose alimuonyesha Yule mganga alipo mlinzi wake, Yule mganga alitikisa kichwa tu.
“Basi jana alitoweka ndani huyo”
“Ni mazingaombwe tu hayo, ila usijali maana sasa kila kitu kinaenda kufika mwisho”
Basi wakashuka kwenye gari na kwenda kufungua mlango wa sebleni ili waingie nani, ila walipofungua tu walishangaa kujikuta wapo kibandani kule kule kwa mganga walipotoka.
Itaendelea kesho usiku…….!!!!!
By, Atuganile Mwakalile.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: