Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 13
Kisha akaingia chumba anacholala Salome tena aliingia bila hodi, ila alimuona Salome amesimama akiwa amempa mgongo hivi ila Neema alishtuka sana na kujikuta akisema kwa mshtuko,
“Aaah Moza!!”
Salome aligeuka sasa na kumuangalia vizuri Neema, lakini Neema alijikuta anaanguka chini.
Salome akasogea na kumfata Neema pale chini, kisha akamwambia kwa sauti ya upole,
“Mama una nini jamani?”
“Mungu wangu, yani Salome ulivyosimama pale nimekuona kama Moza halafu ulipogeuka yani sura ya Moza kabisa ikanijia. Nilichanganyikiwa kabisa maana Moza ashakufa”
“Jamani mama una mawazo sana, mimi ni mwanao Salome yani hata usiwe na mashaka. Sasa mimi nawezaje tena kuwa Moza!”
“Hapana mwanangu, nahisi ni utu uzima huu”
Neema akapumua sasa hata jambo la kuongea alilokuwa nalo lilipotea kabisa kwani miguu yake ilikuwa kwenye mtetemeko wa hali ya juu, ikabidi Salome amsaidie Neema kuinuka pale kisha akampeleka sebleni ambapo alikuwa kimya kabisa akionekana kutafakari jambo Fulani. Muda kidogo wale wadogo zake Salome waliamka na kutoka pia kisha wakamsalimia mama yao na dada yao. Baada ya Salamu alianza kuongea John,
“Yani leo nimelala usingizi wa raha kweli yani!”
Salome akamuuliza mdogo wake huyu,
“Umelala usingizi war aha, hebu tudokeze kivipi?”
“Yani kule tulipokuwa tunakaa zamani, mindoo yote ya maji chumbani kwetu ila leo tumelala chumba cheupe chenye kitanda tu”
Mama yao nae akawaambia,
“Kumbe yale mandoo yalikuwa yanawakera eeeh! Mnatakiwa kuzoea maisha yote”
Kisha Salome akamuangalia mama yake na kumwambia,
“Mama unajua hawa watoto sasa wamekuwa wanatakiwa waende shule”
“Natambua hilo mwanangu, ila hela kwasasa sina”
“Sasa mama, ila nitafanya jambo na wataenda shule hawa. Wamekuwa sasa”
“Utafanya jambo gani? Wewe utapata wapi hela?”
“Mama tulia tu ila hela nitapata”
Kisha Salome akawachukua wadogo zake ili akawaandalie chai, kwakweli Neema alikuwa akimshangaa tu mwanae chauvivu alivyokuwa siku hizi.
Siku ya leo, Rose aliruhusu watoto wake kutoka pia alimruhusu Patrick kutoka kwani alikuwa na furaha sana, kasoro kwa Sara tu ambaye hakuweza kuongea ndio alikaa ndani kama mwali hivi, kwa upande mwingine wa moyo wake alimuhurumia mwanae Sara ila kwa upande mwingine aliona ni vyema apate adabu kidogo kwani ni yeye aliyevuruga mwenendo mzima wa mazishi ya Moza, hakutaka mtu yeyote kwenda nyumbani ila Sara sababu ya kiburi chake akaenda.
Akiwa ametulia zake sebleni, huku Sara nae yupo sebleni akiangalia tu Tv ila kuongea ndio alikuwa haongei, mara ujumbe mfupi ukaingia kwenye simu ya Rose, alipoangalia ulikuwa unatoka kwa Ashura,
“Dada niongezee hela kidogo, halafu huku mtandao unasumbua sana yani nitakuwa sipatikani kabisa. Ukiniongezea hiyo hela sitakusumbua tena”
Rose alisikika akisema,
“Aaah huyu nae kashafanya ndio kitega uchumi wake mimi loh! Namtumia hiyo hela na bora asipatikane kabisa maana sasa anaanza kuniudhi. Miela yote niliyokuwa nampaga halafu kazi yenyewe kaichelewesha hadi leo”
Sara alikuwa akimsikia tu mama yake huku akitamani kumuuliza kitu ila alishindwa, basi Moza akatuma hela na kumuandikia ujumbe,
“Nimekutumia hiyo milioni tano nyingine najua itakusaidia, na wewe kuwa makini huko utafute biashara ufanye maana kazi yangu huku mjini ushamaliza.”
Alipotuma kidogo tu akajibiwa ule ujumbe,
“Asante dada wala usijali sitakusumbua tena dada yangu”
Basi Rose akapumua sasa, ila kila alipomuangalia mtoto wake alimuonea huruma sana.
Muda mfupi wakapata mgeni, alikuwa ni Ommy. Rose alipomuona hakupendezewa nae wala nini ila alimkaribisha tu kwa shingo upande. Basi Ommy akamsalimia Sara pale ila Rose akajibu kwa niaba ya Sara,
“Anaumwa kifua huyo, sauti haitoki”
“Jamani hata kidogo ya kunijibu tu!!”
“Hivi Kiswahili unaelewa wewe, nishakwambia anaumwa kifua huyo sasa akujibu nini?”
“Sawa mama, ila ameshaenda hospitali?”
“Kwahiyo wewe ndiye unayejali afya yake sana kushinda mamake mzazi niliyemzaa! Yani nikae na mgonjwa mpaka muda huu nikisubiria ushauri wako tu! Naomba uondoke, kwanza sikupendagi wewe kijana basi tu”
Ommy akaomba msamaha, kisha akainuka na kuaga na kuondoka zake. Sara machozi yalikuwa yakimtoka tu, mamake akamuangalia na kumwambia
“Sasa kinachokuliza ni nini? Unafikiri mimi sikuhurumii? Mdomo wako ndio haukuhurumii ila mwanangu usijali nitamwomba Ana akirudi akusamehe mwanangu”
Halafu Rose akainuka na kwenda chumbani kwake, kile kitendo tu cha Rose kuinuka na kwenda chumbani, Sara nae aliinuka na kutoka nje.
Alipofika getini, mlinzi alimuuliza,
“Madam vipi unashida na Yule rafiki yako nimkimbilie”
Sara akaitikia kwa kichwa tu, ila mlinzi akaelewa na kuona kuwa kaitikiwa vile kutokana na mapozi ya matajiri ila alitoka na kumkimbilia Ommy, bahati nzuri hakuwa amefika mbali, naye ommy akasikia wito na kurudi ambapo Sara alitoka nje ili aweze kuzungumza na Ommy japo kwa vitendo.
Ommy alivyofika pale, alimkumbatia Sara na kumwambia,
“Nieleze Sara umepatwa na nini tena?”
Ila Sara hakuweza kumjibu ila alimuomba simu yake kwa vitendo, kisha alivyompa akafungua sehemu ya ujumbe na kumuandikia,
“Mdogo wangu ni mchawi Ommy, ndio amenifanya hivi. Kanifunga mdomo nisiongee kabisa. Nisaidie”
Ommy alishika simu na kusoma ule ujumbe, kwakweli alishtuka sana na kujikuta akimuuliza kwa sauti ya chinichini,
“Mdogo wako yupi? Ana au?”
Sara aliitikia kwa kichwa, ila muda si muda Ana nae alirudi kutoka shuleni hata wakamshangaa maana sio kawaida yake kutoka shuleni mapema hivyo.
Ana akamuangalia Sara kwa jicho kali sana, Sara alijikuta akitetemeka na kuingia ndani bila kujidhania kisha Ana nae akaingia ndani na kumuamuru mlinzi afunge geti. Ommy aliweza kuelewa kinagaubaga kuhusu kinachoendelea mule ndani, basi akaondoka zake.
Ana alimtanguliza Sara mbele na walipofika sebleni tu akaanza kufoka hadi mama yake akatoka nje.
“Vipi tena mwanagu kuna nini?”
“Mama, ndio mtu wa kumsamehe huyu!”
“Kafanyaje tena?”
“Nimemkuta nje ya geti anaongea na kale kamchumba kake”
“Khee alitoka nje ya geti, weee Sara wewe jamani kwanini lakini? Yani kwenda chumbani tu kidogo ukaamua ukifate kile kibwana chako? Na utaendelea kuwa bubu mpaka akili ikukae sawa”
Sara machozi yalikuwa yakimtoka tu na kwenda chumbani kwake huku akitokwa na machozi zidi ila bado kuongea hakuweza. Pale sebleni alibaki Ana na mama yake,
“Mwache nimkomeshe mama”
“Ila namuhurumia mwanangu jamani, ila mbona leo umewahi kurudi?”
“Nishawavuruga na huko shuleni”
“Kheee umewavuruga!”
“Ndio, mwlimu mkuu na walimu wake leo hawaelewani”
“Kwanini umefanya hivyo mwanangu?”
“Nimejisikia tu, kwahiyo wenyewe wameturuhusu shule nzima turudi nyumbani”
“Mmmh mwanangu, sasa huko siko. Wale ndio walimu wenu sasa ukiwafanyia hivyo mtafundishwa na nani?”
“Mama hujui tu, kuna mwalimu bonge huyo kanifokea leo yani yeye ndio kanifanya nijaribishe vitu vyangu. Kwanza nimemfanyia mchezo akaanguka chooni halafu nimetoa maelewano kwa walimu wote hadi wameturuhusu turudi nyumbani, nina hakika atajutia mule mule chooni maana sidhani kama atapata wa kumtoa”
“Mmmh mwanangu umekuwa kiboko, yani saivi sijui kama kuna mtu atatubabaisha tena”
Ana akacheka kisha akaelekea chumbani kwake.
Sara nae alikuwa chumbani kwake huku akiwaza cha kufanya akaamua kuwasha simu yake kwani alihisi huenda Ommy akamtafuta, na kweli alipowasha tu akakutana na ujumbe wa Ommy,
“Pole sana Sara kwa tatizo lako, ila kuna mzee nimekutana nae nimemueleza. Basi badae nitakupigia simu akuelekeze namna ya kufanya halafu utafanya na amesema utaongea tu”
Sara nae akamjibu Ommy,
“Nashukuru sana, simu niko nayo hapa kwahiyo ukipiga tu nitapokea yani nikipokea uanze kuongea kwani itakuwa tayari sikioni mwangu”
“Sawa, usijali Sara”
Basi Sara akaiweka ile simu makini kabisa ili akipigiwa na Ommy apokee.
Siku ya leo, Neema hakutoka kwenda popote alibaki tu nyumbani kwake akitafakari kisa na mkasa halafu akishindwa hata kumuuliza Salome kwani akikumbuka ule ujumbe ulimwambia kuwa asijisumbue kumuuliza Salome.
Akiwa amekaa sebelu yao hiyo mpya, kwenye mida ya jioni alikuja Salome na kumwambia habari ambayo alipoisikia hakuipenda hata kidogo,
“Mama, kesho nataka kwenda kwa baba yangu”
“Unasemaje wewe?”
“Kesho nataka kwenda kwa baba yangu”
“Hivi wewe Salome una matatizo gani jamani, baba yako unayemuongelea ni yupi!”
“Patrick mama, najua baba yangu anaitwa Patrick. Nataka kesho niende kwa baba yangu”
“Unapajua?”
“Ndio napajua, wewe subiria tu kesho nikienda kwa baba yangu”
“Salome una nini lakini mwanangu, mwenzio nakupenda sana na sitaki kukupoteza. Aliyekwambia baba yako ni Patrick nani?”
“Mamdogo Ashura aliniambia ukweli wote hadi anapoishi baba yangu alinielekeza, aliniambia kila kitu kuhusu baba yangu”
“Mmh haiwezekani, Ashura akwambie wewe haiwezekani”
“Sasa mimi nimejuaje?”
“Sijui ila Ashura, labda lakini siamini nitamtafuta badae aniambie vizuri”
“Wewe mtafute tu ila kesho naenda kwa baba yangu. Yule ni baba yangu mama utanificha hadi lini? Mimi ni binti mkubwa sasa”
“Salome tafadhali usinitafutie makubwa”
“Yani mama huna cha kunishawishi kwakweli hata useme nini ila kesho naenda kwa baba yangu”
Neema hakuongea neon la zaidi, akainuka na kwenda chumbani kwake. Muda huo Salome nae aliinuka na kwenda chumbani.
Basi Neema akaanza kupiga simu ya Ashura ila iliita sana bila ya kupokelewa mara akapokea ujumbe,
“Tuma meseji nipo kwenye kelele”
“Ashura mdogo wangu umeanzaje kumwambia ukweli Salome kuhusu baba yake jamani! Unajua ni mabalaa unayaanzisha, kumbuka Yule mama alisemaje!”
Muda kidogo ujumbe ule ukajibiwa,
“Dada, Salome amekua sasa ana haki ya kumjua baba yake ndiomana nimemwambia. Na ukae nae chini umueleze ukweli wote, amekua huyo dada tutamficha hadi lini? Nimemwambia ukweli kuwa baba yake yupo na anitwa Patrick halafu anapokaa nimemuelekeza. Mwache mtoto amtafute baba yake. Kila mtu ana haki ya kumjua baba yake”
Neema aliposoma huu ujumbe akapumua kidogo kwani siku zote aliyekuwa mkali kwa Salome kumjua baba yake ni Ashura sasa ilimradi huyo Ashura amekubali basi hakuna wa kupinga.
Kwenye mida ya jioni kabisa, Sara akiwa chumbani kwake akaingia Ana na kumuangalia dada yake. Muda kidogo simu ya Sara ikaanza kuita basi Sara akaichukua ila alienda Ana na kumpora kisha akaipokea na kuiweka sikioni ili amsikie mpigaji anasemaje maana aliona jina Ommy, kwakweli Sara aliona kabisa mwangaza wake umetoweka kwani Ana ndio alkuwa akisikiliza kila kitu ambacho mzee aliyetafutwa na Ommy alikuwa akimwambia Sara basi alipomaliza kumsikiliza akakata ile sime kisha akamuangalia dada yake na kumwambia,
“Yani wewe hukomi, hukomi kabisa eti umeamua utafutiwe mganga wa kienyeji akusaidie. Hivi hujui kuwa huyo mganga nikiamua hata yeye namfanya mbaya! Ila wewe nitakukomesha maana kinachokupa jeuri sasa ni hayo macho, na hutatazama tena”
Pale pale macho ya Sara yakajifunga na hakuweza kuangalia tena, kwakweli machozi yalikuwa yakimtoka tu.
Kisha Ana akaondoka zake na kwenda sebleni, hata kaka zao walivyorudi siku hiyo na kutaka kwenda kumtazama Sara walizuiliwwa na Ana, walitii kutokana na kile kitendo alichowafanyia siku ya kutaka kumpeleka Sara hospiatali.
Rose alijifanya kama hayupo kwenye matatizo ya mwanae huyo na wala hakuonekana kumsaidia tena, wala kwenda kumuona alivyofanywa kipofu amakweli mtu akishakuwa na roho ya kichawi anakuwa mnyama na huruma inamtoka kabisa.
Usiku ulifika na wote kwenda kulala.
Asubuhi kulivyokucha kama kawaida, watu waliondoka wote mule ndani tena na siku ya leo hata Rose aliondoka ingawa mwanae alikuwa haoni na yuko ndani.
Ila tu alimtoa na kumuweka sebleni kisha akamuacha hapo na kuondoka, kwahiyo mlinzi alikuwa anajua ndani kabakia Rose ila hakujua kama hakuwa na uwezo wa kuongea wala kuona.
Muda kidogo wakati Yule mlinzi yupo pale getini akamuona Salome na kumfanya amshangae,
“Karibu ila umekuja wakati Moza alishakufa”
“Nilipata habari ila mimi sijamfuata Moza”
“Umemfata nani kwani?”
“Kuna nani ndani?”
“Yupo Sara peke yake, wengine wote wametoka”
“Sawa, basi huyo ndio nimemfata”
Mlinzi hakuwa na jinsi zaidi ya kumkaribisha tu, ambapo Salome aliingia moja kwa moja ndani hadi sebleni na kumkuta Sara amekaa tu kwa kujiinamia huku machozi yakimtoka. Salome alimfata Sara pale alipokaa,
“Ni wewe ndiye umenifanya nije kwa wakati huu”
Sara alitamani kuongea lakini, alishindwa akaendelea tu kumsikiliza huyu Salome,
“Funua kinywa chako”
Sara alifunua kinywa na akanyunyuziwa dawa kama matone halafu gafla akajikuta akiweza kuongea, na kuuliza kwa sauti ya upole,
“Wewe ni nani uliyekuja kunisaidia?”
“Unataka kuniona?”
“Ndio nataka kukuona”
Basi Salome akachukua dawa na kunyunyiza kwenye macho ya Sara, na hapo hapo Sara akafikicha macho yake na kuona ila alipoinua macho vizuri ili amtazame aliyemsaidia alishtuka sana na kusema kwa nguvu,
“Kheee Moza!”
Itaendelea kesho usiku……!!!!
By, Atuganile Mwakalile.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: