Home → simulizi
→ KISA CHA MAPENZI:
Neema alitoka kijijini kwao akiwa binti mdogo sana, alichukuliwa na kulelewa na shangazi yake.
Alipofika kidato cha pili, hapa ndipo maluweluwe ya usichana yalipomuanza.
Akapata ushawishi kutoka kwa rafiki yake kuwa awe anaenda kujisomea kwao yaani Neema awe anaenda nyumbani kwao na rafiki yake aliyejulikana kwa jina la Rhoda. Kumbe rafiki yake huyo alitaka kumuunganisha Neema kwa kaka yake, na ikawa hivyo hakuna kusoma ni kutongozana tu. Mwisho wa siku Neema akajikuta amefeli masomo yake ya kidato cha pili kwahiyo akashindwa kuingia kidato cha tatu.
Shangazi yake akachukia sana, na hakujua afanye nini na Neema kwa wakati huo.
Ndipo kaka yake na Neema ambaye ni mtoto wa shangazi yake akaamua kumchukua Neema na kumpa kazi katika duka la jumla, kwahiyo Neema akawa anauza duka hilo.
Akiwa pale dukani kuna kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Adamu.
Kijana huyo alikuwa anaenda mara kwa mara dukani hapo kuchukua mzigo.
Adamu akajikuta amevutiwa na Neema, ikabidi amwambie ukweli.
Adamu akamweleza Neema kuwa yeye ana duka lake na mzigo anaochukua hapo huwa anaupeleka dukani kwake, Neema akamkubali Adamu baada ya kusikia hivyo.
Mwanzoni kabla ya kuwa na mahusiano, Adamu alikuwa ni kijana rafu sana, alikuwa anavaa ilimradi tu. Ila walipoanza mahusiano Adamu akawa mtanashati na nadhifu sana yote ni kumuonyesha Neema kuwa yeye ana pesa. Muda wote alikuwa akimwambia Neema ishu za pesa tu.
Siku ya siku ikafika, Adamu akamchukua Neema na kumpeleka anapokaa, kwakweli Neema akapagawa sana kwani alipelekwa kwenye chumba kilichojaza vitu vyote vya msingi ndani.
Neema akajitoa kwa Adamu na tamaa ya maisha bora ikamchukua, hakuona tatizo kupata mimba ya Adamu kwani alijua atahudumiwa vile inavyotakiwa.
Na kweli ukitakacho utapata tu, Neema akapata mimba.
Hapo ndio utata ulipoanza, baada ya kaka yake kugundua kuwa Neema ni mjamzito akaamua kumtimua dukani kwake, kufika kwa shangazi nako ikawa hivyohivyo kwani shangazi yake akamwambia aende kwa aliyempa ile mimba.
Neema hakuwa na jinsi kwani mimba ilishaanza kuonekana, ikabidi aende kwa Adamu.
Kufika kwa Adamu akakutana na mtu mwingine ndani aliyejitambulisha kuwa ni rafiki wa Adamu aliyeitwa Maiko.
MAIKO: Kwahiyo wewe ndio demu wa Adamu?
NEEMA: Ndio na nyumbani nimefukuzwa, ndio nimekuja hapa kwa Adamu.
MAIKO: Sikia nikwambie shemeji, Adamu hakai hapa na wala hapa sio kwake, hata mimi sio kwangu ila ni kwa kaka angu. Kaka mwenyewe hayupo kasafiri. Adamu anakaa kwao, nitakupeleka.
Neema alijikuta akishangaa na kutokuamini kuwa muda wote aliokuwa anakwenda pale na Adamu kumbe sio kwake.
Maiko akamchukua Neema na kumpeleka nyumbani kwao na kwakina Adamu, kwakweli Neema hakudhania kama kwakina Adamu kutakuwa vile kwani palionekana ni maisha ya chini sana sio yale aliyofikiria.
Walipouliza Adamu alipo, wakaambiwa kuwa yupo kwenye kazi yake.
MAIKO: Sasa shemeji, mi naenda zangu. Hapa ndio kwao na jamaa wee msubiri tu.
NEEMA: Ndio unaniacha hapa jamani?
MAIKO: Sio nakuacha, hapa ndio kwao. Labda nikakuitie jamaa alipo.
NEEMA: Kwani dukani kwake ni wapi?
MAIKO: Dukani kwake? Hana duka bhana ila kuna duka la tajiri flani hivi alikuwa anambebea mizogo.
NEEMA: (Alitamani achimbe shimo ajifukie), kwahiyo Adamu anafanya kazi gani?
MAIKO: Ina maana hujui? Yuko hapo barabarani anachoma maindi.
Kwakweli Neema alijikuta machozi yakimtoka kwa mfululizo kwani alichokifikiria hakikuwa vile kilivyo.
Maiko akaondoka na kumuacha Neema mahali hapo.
Baada ya muda, Adamu akafika mahali pale. Akamkuta Neema akilia, ikabidi ambembeleze. Neema alikuwa na hasira sana.
NEEMA: Kwanini ulinidanganya Adamu?
ADAMU: Ningekwambia ukweli usingenikubali Neema.
NEEMA: (Huku akizidi kulia kwa hasira), bora ungeniambia ukweli. Ona sasa nimefukuzwa kwetu.
ADAMU: (Huku akishtuka), umefukuzwa kwenu?
NEEMA: Ndio nimefukuzwa sababu ya hii mimba.
ADAMU: Jamani Neema unadhani tutaishije?
NEEMA: Kivipi sasa? Wakati mimba umenipa mwenyewe?
ADAMU: Najua ndio kama hiyo mimba ni yangu ila mimi nina maisha magumu sana na familia nzima inanitegemea mimi.
NEEMA: Adamu jamani, hata siamini kabisa. Hebu niambie ukweli umesoma hadi kidato gani?
ADAMU: Sikufanikiwa kufika sekondari Neema, mwenzio niliishia darasa la nne.
Neema akalia sana, na Adamu akazidi kumbembeleza
ADAMU: Pole Neema ila itabidi ukubaliane tu na maisha halisi ya sasa.
Maisha yakawa magumu sana kwa Neema alijikuta akilia kila siku, hakuweza kupata zile huduma muhimu kwani familia yote ya Adamu ilitegemea ile ile biashara ya Adamu ya kuchoma mahindi.
Miezi tisa ilipofika, Neema akapatwa na uchungu wa kwenda kujifungua ila hakukuwa na pesa ya kutosha kumpakia kwenye tax au kibajaji kumpeleka hospital, ikabidi wapande daladala. Neema uchungu ulimzidi ndani ya daladala ikabidi abiria wamuombe dereva apeleke daladala hospitali kwanza, yule dereva hakuwa na kinyongo, akawafikifa hospital Neema na wifi yake halafu daladala likaondoka.
Hawakuwa na pesa za huduma, Neema alijikuta akipata huduma hafifu sana.
Akafanikiwa kujifungua watoto mapacha ila kwa bahati mbaya watoto wale wakafa.
Neema alilia sana, akajikuta akimchukia Adamu kwa maisha yake yote.
Walipotoka hospital, Neema hakuona sababu ya kuendelea kuishi kwakina Adamu, akaamua kurudi kwa shangazi yake na kumuomba msamaha.
Shangazi yake akamuhurumia Neema. Ila hakuweza kuishi nae tena pale mjini, akaamua kumkatia tiketi na kumrudisha kwao kwa wazazi wake kijijini.
~Hiki ni kisa cha kweli kabisa.
<3 Mapenzi yapo, yalikuwepo na yataendelea kuwepo cha msingi ni kufanya kitu sahihi kwa wakati sahihi. Usipende kukurupukia mambo katika maisha, YATAKUSHINDA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: