Home → simulizi
→ MREMBO HIMANA
(Full story )
Jana usiku niliamka mida ya saa nane, na kama kawaida yangu, nikalia sana. Ni ajabu kwa mwanaume kulia, lakini kwangu imekuwa kitu cha kawaida sana. Nadhani ninapolia huwa najihisi nafuu kiasi, na kwa namna fulani napunguza uchungu ulio ndani yangu. Nimekuwa nikifanya hivyo kwa muda wa mwaka mzima sasa, lakini usiku wa jana ulikuwa tofauti kidogo. Baada ya kulia sana, niliamua kwamba huu ndio utakuwa mwisho.
Mwaka 2007 tarehe kama ya jana nilikutana na binti mmoja nikiwa masomoni Arusha. Huyu binti ni mmang’ati kwa kabila, ana urefu wa wastani, rangi ya ngozi nyeupe inayofanana mwili mzima, yaani si kama rangi za mabinti wa siku hizi za kuchanganya na kutafutiza. Ni mzuri mno kwa sura, kama unavyojua wadada wengi wa mkoa huo. Ngozi yake ni laini na nyororo kama ya mtoto mdogo, na ni mwenye macho mazuri. Yaani kwa kifupi hana kasoro ya kuonekana kwa macho.
Tulikutana kituo kimoja cha daladala wilayani Monduli, mimi nikiwa naelekea Arusha mjini. Nilimkuta amekaa, kama ana huzuni, japo hilo halikuficha uzuri wake. Nilimsogelea na kumuuliza kwa kuonesha kujali, “Mrembo, nini tatizo? Unaonekana una huzuni”. Alinitazama na kujibu kwa upole sana,”Hapana, niko sawa”. Niliamua nitatumia fursa hiyo kuongea naye, na kweli alinionesha ushirikiano mzuri tuu. Tulizungumza kwa kifupi, nikimuuliza maswali ya hapa na pale, kasha likaja gari tukapanda. Uelekeo wetu ulikuwa mmoja, na kwa nasibu tulikaa siti moja. Tuliendelea na mazungumzo na huyo binti, aliyejitambulisha kwa jina la Himana, na kiukweli niliifurahia safari yangu.
Kufika mjini, mahala ambapo sote tulishuka, tayari tulishajenga urafiki kiasi cha kukubaliana kuonana tena na hata kupanga siku ya kuonana. Sidanganyi, wakati huo nilikuwa tayari kwenye mahusiano, na binti ambaye tulipendana sana. Huyo mpenzi wangu naweza sema hatukuwahi kukosana kwa miaka mitatu yote tuliyokuwa pamoja, ukiacha mikwaruzo kidogo sana ya mara chache. Nilimpenda sana mpenzi niliyekuwa naye, Hilda, na nilimuahidi tungeoana mara tuu baada ya kumaliza masomo yangu ya muda mfupi huko Arusha. Tayari nilishajitambulisha kwao, na kwa uwezo wa wastani niliokuwa nao, nilijitoa kwake kwa kiwango kikubwa kiasi cha kumuaminisha kwamba mimi ndiye mume wake. Sikuwahi kuvutiwa na msichana mwingine yeyote zaidi ya Hilda, mpaka nilipokutana na Himana.
Tulianza mawasiliano ya kasi sana na Himana, kiasi cha kunifanya nianze kumpuuza Hilda. Nilijihisi kuvutiwa na Himana, na kila mara mawazo yaliponijia kuwa nina mpenzi anayeniamini na kunithamini, akili yangu haikunipa hiyo fursa kwa muda mrefu bali ilinielekeza kwa Himana ambaye wakati huo penzi kubwa lilianza kushamiri kati yetu. Binti huyu, aliyepata umri wa miaka 21 tu wakati huo, alinionesha mapenzi nisiyowahi kuona kabla. Hapa niwe muwazi zaidi, kwa miaka mitatu niliyokuwa kwenye mahusiano na Hilda, hatukuwahi kukutana kimwili, isipokuwa mwezi mmoja kabla ya safari yangu ya kwenda Arusha. Hilda alikuwa na misimamo binafsi ya kutofanya mapenzi kabla ya ndoa, na niliweza kumvumilia kwa miaka mitatu huku nikiwa muaminifu kwa asilimia 100. Baada ya kujitambulisha kwao rasmi, na kuanza hatua za kuoana, ndipo alikubali tukutane kimwili, na alifanya hivyo kunihakikishia kuwa hata ninapokwenda kusoma, nijue kwamba mimi ndiye mwanaume wake pekee, na alinipenda kwa dhati, hivyo nisimpe msichana mwingine moyo wangu.
Kwa bahati mbaya sana, Himana alinisahaulisha hayo yote. Tuliingia kwenye mahusiano kwa kasi sana, alinifuata popote, aliniletea vyakula, alizungumza nami maneno ya mahaba na hakutaka kujua kama nina uhusiano au la. Alinipa raha kiasi cha kupuuza ahadi zote tulizowekeana na Hilda, na sikukumbuka tena gharama nilizoingia kwa ajili yake wala heshima niliyokuwa nayo kwa familia yake. Hilda alianza kulalamika kuwa nimepunguza mapenzi kwake, lakini nilimpuuza. Sikujali tena hisia zake, nilidharau hata bikira yake ambayo mimi ndiye niliitoa, na sikuona tena uthamani wake kama hapo awali.
Mapenzi na Himana yalishamiri sana, nikamaliza shule yangu lakini sikutamani kurudi Dar es Salaam nilipoishi. Niliamua kufatilia uhamisho kazini kwangu, na kwa vigezo ambavyo nilitoa, haikuwa ngumu kupata. Nilijaribu kutoa vigezo vya msingi kuhusu uhutaji wa mtu wa taaluma yangu katika ofisi zetu za Arusha. Sikumjulisha Hilda juu ya uamuzi wangu wa kuhama, isipokuwa nilipopata uhamisho nilimwambia kuwa ofisi imeamua kunihamisha. Mara kadhaa nikiwa nasoma na hata baada ya kumaliza masomo alinitaka tuonane, kwa kuniomba niende Dar es Salaam walau mara moja, au hata yeye aje Arusha, lakini nilimpa sababu kadhaa na kumkatalia. Mawasiliano kati yetu yalizidi kuwa hafifu na muda nilioahidi tungeoana ulipita. Hilda alikuwa na asili ya ukimya, lakini nilimfanya awe mtu wa kulalamika. Hata hivyo, malalamiko yake hayakuisumbua akili yangu ngaa kidogo. Nilimpuuza, na kuendeleza mahusiano yangu motomoto na Himana.
Siku zilipita, miezi ikasogea, nikaona nahitaji kuwa na huyu binti Himana, kwenye maisha yangu yote. Nilimueleza kuhusu suala la kumuoa, akakubali, lakini akawa kana kwamba ananipiga chenga kunipeleka kwao. Baada ya kulazimisha kwa muda mrefu, alinipeleka kwa familia aliyoitambulisha kama ya wazazi wake, familia inayojiweza kiasi. Alinitambulisha kwa binti mwingine mkubwa ambaye alisema ni dada yake wa pekee. Wakati huo tayari tuliishi pamoja, na pamenzi yalizidi kushamiri kati yetu. Hilda aliendelea kunitafuta, na mara hii ni yeye ndiye alisababisha tuwasiliane kwani bila kunipigia basi nisingethubutu kumtafuta. Tulipanga harusi ndogo na Himana, tukaamua tuifanyie huko huko Arusha, nikaenda kwao kutoa mahari, lakini nilishangaa kwamba hakukuwa na shamrashamra za mahari au za kuolewa kwake tofauti na familia nyingi za kitanzania.
Tulioana, nikafanya kuwaalika wazazi ambao mwanzo walipingana namimi sana juu ya suala hilo, lakini hawakuwa na namna zaidi ya kumkubali yule niliyemchagua. Taarifa zilimfikia Hilda kuwa nimeoa, na naumia sana ninapoandika hii habari kuwa mpenzi wangu aliamua kujiua kwa kunywa sumu. Moyo wake mdogo haukuweza kustahimili kusalitiwa na mwanaume aliyemuamini sana. Labda kwa miaka mitatu yote nilimuonesha mimi ni malaika, hivyo ikawa vigumu kwa akili yake kuamini kuwa malaika amekuwa shetani. Habari ya kifo chake ilinifanya nimwambie Himana ukweli kuhusu mimi na Hilda, lakini cha kunishangaza, hakujali bali alinipa pole na kunifariji sana.
Baada ya harusi, mapenzi yalizidi kushamiri, tukapata mtoto mmoja wa kike. Tumekaa kwenye ndoa miaka sita, lakini sikuwahi kujua ndugu zaidi wa Himana mpaka mwaka huo wa sita ambapo alikuja nyumbani kwetu mzee, aliyedai kuwa ni baba yake. Huyu ni tofauti kabisa na mzazi wake niliyemfahamu kabla. Mzee yule alikuja akilia na kumuomba binti yake arudi kwao japo akamuone mama yake mzazi aliye kwenye hali mbaya ya afya. Hata hivyo Himana hakukubali na aliishia kumfukuza kama mbwa. Miezi michache baadaye walikuja wanaume wawili, mmoja alijitambulisha kama kaka yake na mwingine kama mume wake. Niliogopa sana, nikaanza kuhisi kuna mengi yamejificha, japokuwa baada ya tukio la yule mzee, Himana alikataa katakata kuwa ni baba yake. Mara hii tena aliwakana hawa wanaume, akidai hawajui wala hajawahi kuwaona, jambo ambalo nililitilia mashaka sana.
Nilianza kufanya uchunguzi wa chini kwa chini, bila mke wangu kujua. Kuna mengi nilianza kugundua mabayo singependa kuyaeleza, lakini kikubwa niligundua kuwa ile familia aliyonipeleka Himana haikuwa yake bali ya rafiki yake. Niligundua pia kuwa aliolewa, kijijini alipoishi, akiwa na miaka 18 tena kwa hiari yake mwenyewe, kwani kabla ya kuolewa alijiingiza kwenye mahusiano kadhaa pale kijijini. Mwanaume aliyemuoa hakuwa wa kijijini, hivyo alimleta mjini, lakini mwaka mmoja tuu baada ya ndoa yake hakuwa anashikika tena. Alichukuliwa na mwanaume mwingine mtu mzima na kuishi naye, na mpaka tunaonana alikuwa kwenye mahusiano na huyo mtu mzima.
Nilijitahidi kutomuonesha kuwa nimejua ukweli huo. Ilinigharimu kufanya utafiti wa kina, kusingizia safari kadhaa, kuonana na rafiki zake na hata kwenda nyumbani kwao pasipo yeye kujua. Nakumbuka siku moja, baada ya uchunguzi wangu kukamilika, nilikusudia kuwa ningemwambia ukweli. Moyo wangu uliuma mno, nilimpenda sana huyu mwanamke na nilitamani kuwa yale yote niliyoyajua juu yake yawe ni uongo. Nilitumai kuwa huenda angekana na kunipa uhakika kuwa yote ni uongo, lakini haikuwa hivyo. Alinisikiliza nikiongea naye, na kasha kunijibu kwa kujiamini kuwa ni kweli yote ninayosema. Niliumia, kupita kiasi, nikatamani ajitetee lakini hakufanya hivyo. Nilitamani hata aniombe msamaha lakini pia hakufanya hivyo na badala yake aliendelea kuishi kana kwamba hakuna kilichotokea.
Nikiwa bado naugulia maumivu, na wakati huohuo najaribu kumsamehe ili tuendelee kuishi kwa amani, siku moja usiku aligonga hodi mwanaume mmoja pale nyumbani. Tulimkaribisha ndani, lakini mke wangu alionekana mwenye kustuka sana. Yule mwanaume alimsalimia Himana kama watu wanaofahamiana, kisha alianza kumlaumu na kumuhukumu mbele yangu. nilibaki nashangaa, sijui nini cha kufanya, na mke wangu akabaki kimya kabisa, asiyeweza kujitetea. Baada ya muda yule mzee alitoa pisto ndogo kiunoni na kwa hasira alimpiga mtoto wangu aliyekuwa amejilaza miguuni mwa mama yake, akampiga na Himana mwenyewe kichwani.
Nikiwa nimechanganyikiwa, nilipiga nilikaa chini na kuanza kulia. Yule mtu alinipiga mimi pia risasi maeneo ya shingoni ambapo nilipoteza fahamu na kuja kujikuta niko hospitali. Hapa ninapoongea nina mwaka mzima, siwezi kutembea, mwili umepooza kuanzia miguuni kwani inasemekana nilijeruhiwa mishipa inayohusika na uwezo wa kutembea, ya uti wa mgongo. Nimeshatibiwa sana bila mafanikio. Mbaya zaidi nilikuja kupata fahamu na kupewa taarifa kuwa mke wangu na binti yangu walifariki na kuzikwa nikiwa sijitambui. Yule muuaji alijisalimisha polisi na sasa anatumikia kifungo cha maisha, lakini haiondoi uchungu niliopitia na ambao ninao mpaka sasa.
Najilaumu, najuta, naumia lakini sina cha kufanya. Inavyoonekana jamaa alifiwa na mkewe, na aliamua kumuoa Himana ambaye alikuja kumtoroka baada ya kukutana namimi.
Himana, binti mwenye kila sifa ya kuitwa mrembo, ameujeruhi moyo wangu. Sasa namkumbuka Hilda, aliyenipenda kwa dhati, aliyejitoa kwa ajili yangu. najutia kumfupishia maisha yake, naona Mungu amenilipa mara mia. Nimepoteza binti yangu kipenzi na wa pekee, nimepoteza familia na mbaya zaidi nimepoteza thamani ya maisha yangu. nimelia kwa muda wa mwaka sasa lakini imefika mahala nimefika mwisho wa kulia, na hapo nikaamua niandike hadithi hii fupi kunihusu iwe fundisho kwa wengine. Si kuwa ni kosa kubwa kuachana na mpenzi wako na kuwa na mtu mwingine, lakini Je, unamuachaje? Alikuamini kiasi gani? Na sababu hasa ya kumuacha ni ipi? Ulimpa ahadi zipi? Machozi tunayowaliza wapendwa wetu ipo siku nasi tutayalia. Namuomba Mungu anisamehe, na ninaamini kuna siku nitainuka tena.
……………………….MWISHO………………………..
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: