SIMULIZI YA KUSISIMUA... Ndoa Yangu Inanitesa part 2 Nilipofika kazini, nilikabidhi pesa kwa Tajiri yangu Mzee Jophu tukiwa katika maongezi ya mabadiliko ya kibiashara. Tulisikia mlango ukigongwa kwa nje, bila kujali wala kujua ni nani mtu huyo, Mzee Jophu aliamuru aingie, Aliingia na alikuwa sekretari wa Mzee Jophu. “Boss, samahani kuna wageni wa Sweedy wanamuhitaji” sekretari aliongea akijikanyaga kanyaga na kuuma vidole.Alionekana kumuogopa sana bosi wake. “Sawa waambie wasubiri kidogo” Mzee Jophu alijibu kwa kifupi na kuendelea na mazungumzo nami. Tuliongea na kumaliza, Mzee Jophu alikuwa wa kwanza kutoka kinyume na mashariti yake, tuliongozana kujua nani alikuwa ananiita. Kwenye viti vya mapokezi ya wageni, nilimuona baba na mama, mama mwingine wa makamo ambaye simfahamu, pembeni ya yule mama nisiye mfahamu nilimuona binti mwingine mrembo. Kwa haraka ubongo ulifanya kazi yake kwa bidii na kukumbuka kuwa niliwapa kazi wazazi wangu kunitafutia mchumba baada ya kuzunguka kila kona ya dunia bila mafanikio. Kumbukumbu hiyo iliutesa moyo wangu kwani nilishapata mchumba mwingine, tena mzuri kuliko yule niliyeletewa na wazazi, japo nae alikuwa mzuri lakini kamwe asingefurukuta kwa Jennifer.Ndivyo nilivyo hisi moyoni na wasiwasi ukawa umejidhatiti akilini. “Baba shikamoo, mama shikamoo!, Mama shikamoo!, Dada habari yako! Niliwasalimia wote nikipita kwa mstari huku nikiwashika mikono. Pia mzee Jophu naye alifanya hivyo hivyo nilivyofanya mimi. Lakini cha ajabu aliposhikana mkono na binti yule akabaki amemshika muda mrefu, macho ya upendo yakiwa yanatambaa usoni mwake. Nilishtuka pale yule binti alipovuta kujinasua mikononi mwa Mzee Jophu. Baba hakupenda kufanya mambo kwa siri, alizungumza yote mbele ya mzee Jophu mama na yule mama mwingine na binti yule. “Mwanangu unayemuona pembeni ya mama yako ni mama mkweo na msichana unae muona hapo ni mkeo kazi uliyotutuma tumeikamilisha. Sidhani kuna la ziada zaidi ya kuhitimisha ndoa kanisani” Baba alizungumza na alitegemea kuona furaha, lakini furaha yangu ilifunikwa na uzuri wa Jennifer niliyeonja penzi lake Nchini Thailand. “Mbona huongei wala huonyeshi furaha” Baba aliniuliza kwa mshangao. “Baba ningeomba tuzungumze faragha kidogo. Kuna mambo mengine hayafai kuzungumza mbele ya mama na watu wengine, nilipoongea hivyo baba alikiri na kujikuta akitikisa kichwa kuafiki yale niliyoyasema. Tuliondoka eneo lile na kulizunguka nyuma ya jengo la kazini. “Baba nimekuita mazungumzo ya pembeni nina jipya lililojitokeza” “Jipya lipi zaidi ya hili nililo kuletea? Baba alizidi kunikazia macho ya ukali. “Ndio hilo ni jipya ulilolileta wewe nashukuru. Lakini hata mimi nina jipya nililopata nikiwa Nchini Thailand kikazi”Baba alionekana mwenye furaha iliyotoka moyoni, alihisi pengine nimemletea zawadi, kumbe asijue ni ujumbe wa kumkataa binti walionitafutia. “Umeniletea suti nini mwanangu Sweedy?” Baba aliuliza huku akiwa ametoa tabasamu zito la kupokea zawadi. “Hapana baba, ila ninaomba radhi kwa usumbufu.” “Usumbufu gani?. Sema” “Nimewasumbua kunitafuti mchumba. Baba nikiwa Bangkok Nchini Thailand nimebahatika kupata mchumba ninayetegemea kufunga naye ndoa.” “Eti nini”? usinichezee naona unataka radhi ya wazazi, hatuelewi kila kitu tumemaliza. Mahari tumeshalipa tunachosubiri ni ndoa tu. Halina mjadala” Baba aliongea kwa ukali, mishipa ya shingoni ilimtoka, ghafla macho yake yalibadilika rangi na kuwa mekundu. “Naomba uniambie sasa hivi. Unamuoa yule binti au laa! Sitaki uniambie nikupe muda” Baba alizidi kufoka kwa sauti. Sauti yake ilienda mpaka alipokuwa mama na mama wa yule binti na binti. “Baba nisamehe sauti hiyo inasafiri naomba yaishe”Mara anakuja mama akikimbia huku kanga zikimdondoka alikwapua kanga na kufika pale nilipokuwa na baba. “Baba Sweedy kuna nini? Mama aliuliza kwa kudadisi . “Mwanao anataka kututia aibu.”Baba alisema akinikazia jicho la ghadhabu. “Aibu gani tena?”Mama akauliza akiwa anamtumbulia macho Baba. “Mwanao hataki tena kuoa.Anasema binti tuliyemtafutia hajampenda.Na ameshapata mchumba huko alikotoka” Baba aliongea kwa sauti ya taratibu iliyojaa uchungu. “Hakuna pingamizi lazima aoe la sivyo atazunguka hii dunia wakumwoa hatamuona. Hata huyo anayesema amempata pia atamkataa. Kama sisi sio…… nilimkatisha mama aliyekuwa anaongea kama kuniachia radhi. “Mama sasa naona mnaniachia laana, basi nitamuoa binti huyo.” Muda mfupi niliona maneno hayo yalirudisha furaha zao. Hawakupenda nichelewe kuoa, mipango ya harusi ilifanyika na tarehe ya harusi ilipangwa. Wiki tatu kabla ya kusafiri kwenda nchini Thailand. Nilipokubali wazazi wote walirudi kule tulipowaacha mama wa binti, binti mwenyewe ambaye ndiye mke wangu mtarajiwa na mzee Jophu. Lakini tukiwa katika mazungumzo mimi na wazazi wangu, huku nyuma Mzee Jophu alikuwa akiongea na mama wa binti aliongea kuwa anamuhitaji yule binti amuoe yeye na sio mimi tena mambo hayo yalifanyika haraka na kwa siri, si tu kwa maneno bali Mzee Jophu alimpatia hela nyingi kuliko zile za wazazi wangu walizolipa. “Mama kamata laki tano hizi ni zako bado nitakuongeza” kwa shida ya mwanamama yule alizipokea na kuziweka kibindoni kwa haraka huku akimuahidi kuvunja ndoa isifungwe, aliniamini angetumia njia yoyote ya kukwamisha ndoa. Ni mambo ya kusikitisha, mzee Jophu pamoja na kuwa baba wa familia ya watoto watatu, bado alihitaji mke wa pembeni aliamini kwa pesa zake nisingeweza kufurukuta “Pesa inazungumza. Pesa ni kila kitu.Haki pasipo haki kwa tajiri ni haki” mzee Jophu alizidi kuzungumza. Tuliporudi pale nilishangaa kumuona Mzee Jophu akiwa na hasira alikunja ndita aliponiona tofauti na mwanzoni. Nilijiuliza nina kosa gani, kama ni mazungumzo yetu yalikuwa mazuri nimemfanya nini boss mbona ananitupia jicho la ukali, nilishindwa kujua kilichoendelea kwa wakati huo.Mama mkwe mtarajiwa nae alipindua midomo yake na kuibetua kama iliyoteguka jicho la dharau lilinitizama kuanzia chini ya unyayo hadi juu ya nywele, kisha kabla ya yote nilisikia akisema “Kijana wenu hana hadhi ya kumuoa mwanangu. Kwa jinsi ninavyomuona” nilistaajabu kusikia sauti iliyoambatana na kusonywa. “Kwa nini mama Getu?. Amefanya nini mwanangu?” Mama alimuliza kwa sauti ya chini. “Mwanao hana nidhamu. Uso wake umetawaliwa na dharau. Hawezi kumuoa mwanngu” aliongea kama kawaida alinitupia macho ya kunitazama kama mtu aliyejinyea japo maneno yake niliona na niliyasikia yakinichoma moyoni mwangu. Nilikabwa na fundo kali la ghadhabu nikaamua kumuheshimu tu, kama si heshima basi ningeropoka neno lolote baya nae limkere moyoni. Mzee Jophu alikuwa kimya pembeni , macho yakipepesa kwa kuibia na furaha iliyojificha ilionekana usoni mwake, lakini sikuweza kugundua kwanini mama yule alibadilika yeye na Mzee Jophu. Mama na baba walimuomba radhi awasamehe kuzaa mtoto asiye na nidhamu na anisamehe, walijua pengine hasira ile ni kile kitendo cha mimi kumuambia baba siko tayari kumuoa mwanae kwani nilipata mchumba Thailand. Lakini mama mkwe mtarajiwa msimamo wake ulikuwa pale pale, hakutaka nimuoe mwanae, na alitaka arudishe mahari, kwa kile kitendo cha kusema “Mtoto wenu hana nidhamu” hata alipoulizwa nidhamu gani alishindwa na kubaki akisema. “Sitaki nasema basi. Chukueni hela zenu na ng’ombe zenu nne, sikotayari kumuozesha mwanangu” Aliendelea kuwa na msimamo wake. Kwa maneno ya mama yule yalikuwa ni furaha kwangu, kwani ningemkosa basi ningeenda kumuoa Jennifer na kwa upande mwingine yalinikera sana, hasa alipozidi kusema sina hadhi ya kumuoa mwanae. Eti nina dharau, nilishindwa kumuelewa alikuwa na maana gani?. Baba na mama yangu walinivuta pembeni na kuzungumza kama dakika takribani tatu, kisha wakarudi na kuomba waondoke wakayazungumze nyumbani. Waliondoka wote, baba, mama, mama Getruda na Getruda. Hawakutaka kuyazungumza pale kwani ilikuwa sio sehemu yake. Tulibaki mimi na mzee Jophu, lakini sikumuona akiwa na furaha kama nilivyomzoea, hakutaka kuongea na mimi. “Boss mbona unaonekana una hasira nini hasa nilichokukosea. Nimeona umebadilika” kimya kilitanda sikupata jibu lolote zaidi ya kunitazama na kuondoka zake. Kesho asubuhi nilipowasili kazini, nilifanya kazi vizuri kama kawaida nikiwa naongea na baba na mama kwenye simu. Mara Boss Mzee Jophu anaingia na wakati huo nilimaliza maongezi na kukata simu, nilipomsalimia hakuitikia salamu yangu, bali alinitupia barua mezani, na kusema “Sina shida na salamu yako. Barua hiyo na unijibu haraka iwezekanavyo.Nakupa nusu saa” aliondoka na kufunga mlango kwa kishindo kikubwa. Nilishindwa kumuelewa, lakini kwa matendo yake nilihisi na kuamini barua ile ilikuwa ya kufukuzwa kazi, lakini nilishindwa kuelewa kosa hasa lilikuwa lipi?. Homa ya kufukuzwa kazi ikaniingia, nilishindwa kuisoma ile barua, niliinamisha kichwa nikiwaza. “Hivi kama nitakuwa nimefukuzwa kazi nitaenda wapi? Nitamuonaje Jennifer tena? Nauli sina ya kwenda Bangkok” Ghafla mawazo yakanijia nilikumbuka kuwa boss alinipa muda wa nusu saa kuijibu barua yake. Ndipo nilipoanza kuifungua barua huku mikono na vidole vyote kwa pamoja vikitetemeka kama mgonjwa wa degedege. Nilifanikiwa kufungua Barua. Kitu cha kwanza kukutana nacho ni maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa. YAH: UPIMAJI WA AFYA KWA AFISA MAUZO, JOPHU MINING TRANSPORT CO.LTD. Moyo wangu ulipasuka kwa furaha “nilihisi ni ridandasi kumbe ni kupima afya hilo halina shida. Ngoja niendelee kusoma” nilijisemea kimoyomoyo. HUSIKA NA KICHWA CHA HABARI HAPO JUU, TUMEPATA BARUA KUWA WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YETU WANAHITAJIKA KUPIMA AFYA ZAO, HASA UKIMWI NA AFISA MAUZO AWE WA KWANZA . BODI ILIPANGA KIKAO CHA SIRI. MKURUGENZI WA KAMPUNI JOPHU KUNDY. Nilimaliza kusoma barua, lakini hata hivyo moyoni nilijiuliza “Kwanini Mzee Jophu na msalimia haniitikii, halafu akanipa barua ya kwenda kupima afya yangu, au anahisi nina virusi nini?. Ama anataka kunitafutia kosa ili anifukuze kazi nini?. Kwanini ananikasirikia, ni kwa vile wazazi wangu wamekuja kuongelea maswala ya kuoa hapa kazini au ni nini?.” Nilizidi kutumbukia kwenye kisima cha mawazo kem kem, bila kupata jibu muafaka. Kwa ujumla nilishindwa kuelewa wazo halisi la Boss kunitaka nikapime afya yangu, na nikiwa mtu wa kwanza kazini kupima virusi na kwa nini alinikasirikia. Muda niliopewa na Mzee Jophu ulitimia, hakupenda kupoteza muda, aliingia ofisini kwangu na kuniuliza, “Sweedy umeisoma barua niliyokupatia?. Naomba majibu. Utaenda kupima au hutakwenda?” “Nitakwenda boss, lakini kwani ni lazima kupima?” “Ndio, ni lazima hasa wewe” Mzee Jophu alinijibu kwa uhakika. “Kwa nini mimi iwe lazima, asiwe mfanyakazi mwingine. Boss unanitisha sana hasa unaposema ni lazima mimi, na cha kushangaza boss hutaki kuitikia salamu zangu. Nimekukosea nini, naomba uniambie, ndipo nami nikujibu kuhusu jibu la kupima” Niliongea nikilalamika kidhaifu kwa boss, niliogopa mabadiliko ya boss. “Ok, usihofu kuhusu kutoitikia salamu yako. Nilijaribu kukutingisha tu unajua Sweedy mimi na wewe dam dam. Pia watu wanatufananisha kama mtu na mdogo wake, wengine wanajua dhahiri kuwa wewe ni mdogo wangu wa toka nitoke. Nilikuwa nakupima imani yako, hivi wewe hushangai toka nikuajiri kazi hatujawahi kukasirikiana iwe sasa? Wewe ndiye ninaye kuamini katika kampuni yangu, hata nikifa leo, wewe ndiye utakaye shikilia mali mpaka watoto wangu watakapokomaa kiakili. Umenielewa Sweedy? Ondoa shaka yale yote ni matani.” Mzee Jophu aliamua kuficha ukweli uliopo moyoni mwake, alinichukia mno! kwa muda mfupi tu toka amuone Getruda, binti mrembo, hakutaka nijue nini kilichotaka kuendelea, alizidi kunifumba kwa maneno ya uwongo na kunifanya nimuamini kuliko siku za nyuma. Nilipandisha pumzi na kushusha kwa nguvu “oophhhh!” “Ni kweli boss lakini ilinifanya niwe na alama ya kuuliza ndani ya ubongo wangu, hata hivyo sikuamini kuwa ni wewe ulinibadilikia kiasi hicho. Kuhusu kupima nani kakupa wazo hili?”. “Ok, swali zuri, nilipata barua kutoka mamlaka ya Uhamiaji, kwamba si ruhusa mtu kutoka nje ya Nchi bila kupima afya, hivyo wewe kama Afisa mauzo bila kupima hutaenda Nchini Thailand lakini utakapopima utaendelea na kazi yako kama kawaida.” “Hakuna shida boss mimi nitapima virusi najiamini sina kitu, mimi sio mkware” Nilimjibu. Furaha yangu nikutaka kwenda nchini Thailand nikaonane na Jennifer . “Kesho asubuhi watakuja Daktari kukutoa damu. Hutaenda huko hospitalini, cheo chako kinakulinda na sitaki uhangaike. Watakuja na kukupima na wiki ya tatu utaenda Nchini Thailand kama hutakuwa na virusi. Sio sheria yangu hapana ni serikali”Akasema Boss akizunguka zunguka pale ofisini.Alionekana mwenye furahabaada yakukubali kuopimwa. “Nitakuongezea mshaharaasilimia hamsini wa mwanzoni”Alizidi kunipa motisha. “Nitafurahi Bossi” . Tukiwa kwenye maongezi nilisikia simu ikiita. Nilipoitoa mfukoni niliona namba za baba juu ya kio cha simu. Niliipokea na kuanza kuongea . “Shikamoo baba.Mama hajambo?” “Marahaba!. Wote wazima wanakusalimu. Jiandae kwa harusi yule mama amekubali umuoe mwanae. Ni baada ya kwenda kwenye mila na desturi, amepewa faini ya kutaka kurudisha mahari. Umenielewa mwanangu?” “Ndio baba. Kweli amekubali nimuoe mwanae?. Hata siamini nitajitahidi kukusanya mchango wa harusi” “Sawa jitahidi mwanangu” Tulimaliza maongezi na kukata simu. Nilipomtizama Mzee Jophu alinitupia macho ya lawama, lakini hata hivyo nilichukulia usemi wa kupima imani kumbe yeye maneno ya yule mama kukubali nimuoe mwanae yalimuumiza roho sana, na alikiri kumuua mama Getruda kwa kumsaliti na kumchukulia laki zake tano, lakini kwa upande wa mama Getruda hakula wala hakuzitumia hata senti tano yoyote, alipanga kumrudishia baada ya kushindwa kuzuia ndoa isifanyike. By brayton starpoz

at 9:02 AM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top