HOUSE GIRL DIARY; NAITWA RAYA NI HOUSE GIRL MSTAAFU—SEHEMU YA TATU (ILIPOISHIA SEHEMU YA PILI; Raya anarekodi Video ikimuonyesha yule Mama akimtesa mtoto wake wa kambo, akimpiga na kumfanyisha kazi. Anamkabidhi Baba Jack ili aone kinachoendelea. Je nini kitatokea ENDELEA.. Kama hujasoma sehemu ya pipi basi bonyeza hapa; Iddi Makengo Dada alimuona namna Baba anavyobadilika, namna ambavyo uso wake alikua anaukunja, ghafla nilimuona Baba machozi yanamtoka, nikitegemea kama atapandwa na hasira kama nillivyokua mimi na kuanza kumtandika Dada makofi niliona anamgeukia taratibu, alimuangalia kwa uchungu kama vile alikua anataka kusema kitu lakini maneno hayatoki. “Ni…ni nini hiki?” Alijitahidi kuuliza, wakati huo Dada alikua kimya akiangalia chini kwa aibu. “Nisamehe mume wangu ni hasira tu, huyu mtoto wakati mwingine ananiudhi nalazimika kumpiga…” Alijitetea. Mimi bado nilikua nashangaa ni kwanini Dada hakua amelala chini akitokwa damu kwa kipigo. “Hasira ndiyo unwe unampiga mtoto namna hii, hizi ni hasira gani?” Hapa Baba aliuliza kwa hasira kidogo, nilipata faraja labda atamtandika makofi lakini haikutokea. Dada alianza kulia, “Hata mimi sijui mume wangu, sijui hata nini kilinitokea siku hiyo nikampiga mtoto, mimi sina mkono wakupiga kabisa, wewe mwenyewe unanijua labda ni hii mimba…nikiwa katika hali hii nakua tofauti sana…” “Muongo, ni kila siku anampiga, hata haya anayoita mapele ni yeye. Hata chakula anamnyima, anamtukana, anamfanyisha makazi kama Mbwa, huyu si mwanamke ni shetani!” Niliongea huku nikinyanyuka kwa hasira, Baba alikua kama zezeta flani hivi, baada ya kutajiwa neno mimba ni kama alisahau kuwa yule mwanamke alikua ni shetani. Nilikua nasikia mambo ya limbwata lakini nilikua sijawahi kuona mtu kalogwa akalogeka. Kwa namna ile video ilivyokua mtu yeyote mwanye akili timamu hata kama asingekua mzazi wa Jack angekasirika na asingemsikiliza yule mwanamke. “Una mimba mke wangu, ina miezi mi ngapi? Mbona hukuniambia?” Alisahau kabisa kuhusu Jack na kuanza kuulizia upuuzi mwingine ambao nilijua kabisa ni uongo. “Hakluna cha mimba wala nini, hivi wewe huoni kama anataka kukuchota akili!” Niliongea kwa hasira, pale nilikua kama mfanyakazi ila kwa wakati ule nilijua kazi sina hivyo ilikua ni lazima kumtetea Jack na kuhakikisha haki inatendeka. Nilipiga kelele na harakaharaka nilitaja karibu kila kitu ambacho mimi nilikishuhudia Dada akimfanyia Jack. “Mume wangu unaona, huyu binti ndiyo sababu ya kila kitu. Hataki kufanya kazi, nyumba ikakua chafu na kamjaza mwanao kiburi, mbona kabla ya kuja tulikua tunaishi salama. Jack namfundisha kazi na ananisaidia kufanya kazi za ndani, kwa hali yangu hii siwezi kufanya chochote, wewe mwenyewe unakumbuka kilichotokea kipindi kile. Unajua namna tulivyohangaikia huyu mtoto, hivi kweli kumfundisha mtoto wa kike kazi za nyumbani ni kosa? Au kumchapa akikosea ni kosa? Au kwakua mimi sina kazi nipo hapa nyumbani, au kwakua mimi ni Mama wa kambo ndiyo mnaniona kama shetani. Huyu binti anajazwa maneno na Mama yake, kila siku wanaongea na ndiyo wanataka kutuvuruga. Mimi siwezi, mimi siwezi kama umenichoka niambie tu niondoke zangu!” Aliongea huku akilia, kila kitu kilikua ni uigizaji, wakati anaongea alianza kunyanyuka, alinyanyuka huku akishika tumbo kama vile ana maumivu tumboni. “Nini? Kuna nini kimetokea, tumbo linauma?” Baba alimuuliza lakini hakujibu zaidi ya kumuambia niache kama umeamua kumsikiliza huyo baki naye mimi naondoka. Alinyanyuka kwa kupepesuka kisha taratibu alidondoka chini. Niliona kabisa kafanya makusudi kwani hakudondokea sakafuni, alipiga jicho pembeni kisha akapepesa macho na kudondokea kwenye sofa, akawa kama kakaa kiupende kisha ndiyo akafika chini. Baba alipaniki, alianza kuhaha, simu alitupa pembeni na kuacha kuangalia, watoto wake nao walikuja kulia na kumlilia Mama yao. Ilikua ni kama maigizo flani, Baba alianza kuongea habari za Hospitali ndipo alijifanya kufungua macho na kulazimisha kupelekwa chumbani. Aliniambia nimsaidie kumnyanyua lakini sikua tayari, nilimshika Jack mkono na kuondoka naye mapaka chumbani, nilimuacha Baba akihangaika kumnyanyua ili kumpeleka chumbani, alisahau kabisa ishu ya mwanae. **** Usiku mzima sikulala, nilijua nafukuzwa lakini suala la kumuacha Jack pale halikuingia akilini. Nilimuambia Jack nimpeleke kwa Bibi yake lakini alikataa katakata. “Watakuja tu kunichukua, hata nikisema nini hakuna mtu wa kunisikiliza. Wewe dada ondoka tu uniache hapa, nimeshazoea kila dada anayekuja anachoka na kuondoka mimi naendelea tu kubaki. Baba hawezi kuruhusu niondoke, alishagombana na Bibi mara nyingi lakini anasema ananipenda na hawezi kukaa mbali na mimi. Kumbe sikua mimi peke yangu niliyeona yale mateso na kukerwa nayo, kulikua na wafanyakazi wengine wawili nyuma ambao walishafukuzwa kwaajili ya Jack ndiyo maana alikata tamaa. Mmoja alisema kwa Bibi yake Jack na mwingine alimpa chakula na alikua anawasiliana na Mama yake Jack. Asubuhi Baba aliamka kama kawaida, ni kama kulikua hakuna kitu kilichotokea, Dada alijifanya kuamka na kumuamsha Jack kwaajili ya shule, alijidai kumuandaa na kujifanya hana kinyongo. Waliwaaandaa na kuwapeleka shule, alipoondoka tu Dada aliniambia nikusanye kila kilicho changu na kuondoka. Alinitukana sana kwa kutaka kuingilia nyumba yake akiniambia kuwa pale hawezi kuondoka. Alitaka kunipiga lakini kwakua sikuwa nikihitaji kazi tena na nilishajua siwezi kubaki tena pale kumlinda Jack niliamua kumtolea hasira. Baba alishaondoka kwenda kazini hivyo tulibaki wawili tu, pamoja na mwili wangu mdogo lakini nilipitia mengi, maisha ya kupigana mtaani nilishayazoea. Nilimsubiri aliponipiga kofi la kwanza na la pili. Nilimuacha anogewe ndiyo nikaanza kumtandika, hakuamini. Nilimtandika kama vile mtoto mdogo, nilimpiga sana akapiga kelele lakini hakukua na mtu wa kumsikia. Baada ya hapo nilichukua kilicho changu na kuondoka. Nilimuambia naondoka lakini nitarudi, nitarudi kwaajili ya Jack. Alinyamaza kimya bila kusema chochote. Kumbe mtu mwenyewe alikua mayai mayai halafu anajifanya kuonea watu. Niliondoka na kwenda kwa kijana mmoja, huyo alikua ni X wangu, tulizinguana kitambo kabla sijaacha kazi nilipokua nikifanya mwanzoni, yeye alikua ni Kondakta wa daladala hivyo mchana alikua kazini. Mlango wake nilikua naujua vizuri hivyo niliufungua hata bila funguo. Sikua na pakwenda kwani sikua na ndugu Dar, ingawa sikuachana naye vizuri lakini nisingelala mtaani. Jioni alirudi na kunikuta, hata hakukasirika, alianza kucheka na kunitania kama siwezi kuishi bila yeye. Nilimuambia ishu yangu, nikamuonyesha ile video katika simu yangu, hata yeye pamoja na Bangi zake hakuamini kama kuna mtu anaweza kufanya vile tena kwa mtoto mdogo kama yule. “Huyo mwanaume kashatengenezwa, cha kufanya hapo ni kwenda Polisi, mbona siku mbili huyo akikaa ndani anakaa sawa…” Aliongea huku akinigusa, najua alitaka mapenzi lakini sikua katika mood kabisa, ila aliongea jambo amaalo sikuliwaza kabisa hapo awali. “Baba yake anaweza asijali lakini sidhani kama Polisi hawatajali.” Niliwaza kufanya hivyo lakini ulikua ni usiku, niliamua kusubiri mpaka asubuhi. Lakini niliwaza kama itakua vizuri nikienda na Jack kwani nilijua kuwa wakiangalia makovu yake basi utakua ni ushahidi tosha na watamuonea huruma. Lakini ningempataje wakati yuko shuleni, niliamua kwenda nyumbani kwao kumsubiri wakati anatoka shule. Wakati wanashushwa na gari kabla ya kuingia ndani nimchukue na kuondoka naye. Mchana muda wa wao kutoka shule nilichukua Bajaji, nilimuambia Dereva kupaki karibu na geti kabisa, Gari la shule lilipokuja na kuwashusha nilishuka na mimi. Wote waliniona, wale wengine walikimbilia ndani lakini Jack ambaye alikua anaogopa alisimama na kuniambia niondoke kwani atapigwa. Sikumsikiliza wala sikusubiri kumuelezea. Nilimshika na kumvuruta mpaka kwenye Bajaji, nikamuingiza kwa lazima kisha nikamuambia Dereva tuondoke. Kwakua nilishamuambia kila kitu aliwahsa Bajaji mpaka kituoni. Kule nilienda mpaka mapokezi, hakukua na watu wengi, nilianza kuelezea kila kitu, nikawaonyesha na Video. Kila askari aliyeiona alikasirika, tulipewa askari wa kike ambaye alienda kumkagua Jack. Alikua ni Mama mtu mzima, wakati anamkagua alianza kutokwa na machozi ingawa alijizuia sana. Mwanzoni Jack alikataa kusema lakini baada ya kuhakikishiwa usalama wake lielezea kila kitu. Niliandikisha maelezo kisha tukapewa PF3 ili akatibiwe, askari mmoja alitupeleka hospitalini na gari yake binafsi. Baada ya hapo ilitolewa RB, Dada na Baba wote walikamatwa na kufikishwa kituoni. Wote walikua na kesi, haikua ni ya mtu mmoja tena. Polisi waliwasiliana na ndugu wengine kwaajili ya kumchukua Jack na kukaa na wale watoto wengine kwani wote hawakupewa dhamana. Mimi niliondoka lakini nilikua naenda Hospitalini kumuangalia Jack mara kwa mara. Alilazwa kupatiwa matibabu kwa muda wa wiki moja hivi, Mama yake alikuja na baadaye kukabidhiwa mtoto wake. Baba na Dada walikaa mahabusu kwa wiki moja na kutoka kwa dhamana lakini cha kushangaza hawakupelekwa mahakamani. Sijui nini kilitokea lakini binafsi naamini walitoa pesa nyingi kwani Baba Jack alikua na pesa na kacheo flani. Kesi iliisha chinichini na mimi sikuweza kufuatilia, baada tu ya Jack kurudi na kukabidhiwa kwa Mama yake kwangu hilo lilitosha hayo mengine yalikua hayanihusu. Hela yenyewe ya kula ilikua ni shida nisingeweza kufuatilia maisha ya wengine. Sasa hivi imepita kama miaka miwili hivi tangu hili tukio litokee, nipo hapahapa Dar lakini nimehama mtaa. Sifanyi tena kazi za ndani, nimefungua Genge langu ambalo nauza mbogamboga na matunda. Bado nawasiliana na Jack kupitia Mama yake na anaendelea vizuri, wanaishi maisha ya kawaida sana lakini yenye furaha. Katika kazi yangu hii ya kuuza Genge wateja wangu wengi ni wadada wakazi ‘House Girl’ mengi wanayokutana nayo katika nyumba za watu ni kubwa. Kwa wa mama ambao ndiyo mabosi wetu kumbukeni hata sisi ni wanadamu kama nyinyi. ***MWISHO MAMA KWANI BABA YETU NDIYO HUYU HUYU AU SISI NI MAYATIMA? Baba yao ndiyo alikua na kila kitu, mali zote zilikua za kwao lakini kila akisafiri walikua wakiishi kama mashetani, Shangazi zao na Baba zao wadogo waliungana kuwachukia, Mama yao alikua akinyanyaswa na kutukanwa. Kila siku walimuambia yeye ni mzigo na hawezi kuchukua mali za Kaka yao. Bibi yao ambaye alitegemewa kuwa upande wao naye walimjaza maneno. Walimuambia huyu mwanamke kama Kaka akimuacha watagawana mali na Kaka akifa basi atachukua mali zote. Kilichopo hapa ni kuhakikisha Kaka hawi na kitu chochote cha yeye kuchukua…. JE UNATAKA KUJUA KISA HIKI KINAHUSU NINI…Kama kisa kilichopita kilikutoa machozi hiki kitakupigisha mayowe… Lakini nacho kimetokea niseme kinaendelea kutokea, unaweza kuwa na mali nyingi na wanao wakaishi kama mashetani hata kabla hujafa. Kama unataka kuwa wa kwanza kukisoma basi hakikisha umelike ukurasa

at 2:14 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top