at
4:54 PM
Home → Tanpa Kategori → KURUDI KWA MOZA: 37
Wote walikuwa wanashangaa ila gafla wakasikia mtu akicheka na mara kidogo akatoka sebleni, na kusikia sauti ya Moza ikisema sasa,
“Unasemaje Rose?”
Kila mmoja alikuwa anatetemeka na hakuna aliyeweza kumtazama Moza machoni.
Ila sauti ya Moza iliendelea kusema,
“Waambie yote watoto wako sio unawaambia tu kuwa Yule si Salome ni Moza, sasa Moza nimekuja mwenyewe na uzungumze yote mbele yao”
Hakuna aliyeweza kuinua uso wake wala hakuna aliyeweza kusema kitu chochote na kumfanya Moza aendelee kuongea,
“Najua hapa nitakapoondoka kila mmoja atatafuta pa kwenda na kuogopa kurudi tena kwenye nyumba hii, ila niwaambie kuwa hakuna mtakapoenda nisiwarudishe. Yani mkienda popote pale mtajisumbua tu kwani mimi nitawarudisha ndani ya sekunde. Mnashindwa kuuliza kitu au kuongea chochote sababu mnaniogopa eeh! Naondoka ila kuanzia sasa, mkinitaja tu nakuja”
Kimya kikatanda na wote walikuwa kimya kila mmoja akiogopa kunyanyua kichwa chake na kutazama kwani hofu ilishatanda kwenye mioyo yao. Sara aliuliza wenzie huku bado kainamisha sura yak echini,
“Jamani, ameshaondoka?”
Hakuna aliyejibu ila ikabidi Sara ainue kichwa chake na kutazama, akaona kweli ameondoka na kuwahakikishia wenzie kuwa ameondoka, hakuna aliyeweza kucheka wala kusema neno lolote kwa muda huo kwani kila mmoja alikuwa na mashaka na nafsi yake.
Kisha aliinuka mmoja mmoja na kuelekea chumbani kwake na kuwaacha Rose pamoja na Ana kwani walikuwa kama ni watu waliopigwa na shoti vile maana ni kitu ambacho hakikutarajiwa kabisa kwa siku hiyo.
Walikaa kaa pale sebleni kisha Rose aliinuka na kwenda ndani kwake, kisha akachukua simu yake na kuiwasha yani ziliingia jumbe mbali mbali kwenye simu ile kanakwamba zilikuwa zikimsaubiri awashe tu simukwahiyo ziliingia jumbe nyingi hata akashindwa aanze na ujumbe upi na kumalizia na ujumbe upi, wakati anataka ajiweke sawa sasa asome akashangaa simu yake inaita, ilikuwa ni namba ngeni ila alipopokea ndio akagundua kuwa ni wale vijana wake wa kai ndio walikuwa wanapiga,
“Mama mbona hujibu ujumbe tunakutumia, hupatikani tatizo ni nini?”
“Yani nisameheni bure vijana wangu, simu ndio naiwasha leo. Nilikuwa na majanga mengi sana”
“Basi mama, ule mzoga tulioenda kutupa tumejaribu kuufukunyua ili tuone ni nini, mama ni maiti ya Ashura, yani aliyeuwawa na tuliyemtupa ni Ashura”
“Nini?”
“Ndio hivyo mama ni maiti ya Ashura, nadhani tulifanyiwa mchezo ndiomana namba ya Ashura tukipiga alikuwa haongei anatuma tu meseji”
Rose alihisi kushikwa na tumbo kabisa na kumwambia Yule kijana kuwa atampigia tena, aliinuka na kwenda chooni kuendesha yani tumbo lilimvurugika kabisa kwani alipewa habari ambazo hakuzifikiria kabisa, yani alihisi kuwa ni vitu vingine vimetupwa ila hakufikiria kama ni Ashura ndio alikuwa amekufa. Alitulia chooni kwa muda kadhaa kwani tumbo lilimvurugika vilivyo ingawa hakuna chakula kinachoeleweka alichokula ila tumbo lake lilivurugika, alirudi tena chumbani kwake na kujitupa kitandani huku akiwaza bila ya kupata jibu,
“Yani Ashura ndio amekufa!”
Hakujua kuwa aanze kupiga kelele za msiba au afanye kitu gani, alichukua tena simu yake na kupigia wale vijana kisha akaomba wakutane nae ili akaonyeshwe hapo ambapo walimtupa Ashura, nao wakakubaliana nao. Kwakweli leo Rose alichanganyikiwa kabisa, kwani aliona kama likitoka hili basi linaingia lile na kuzidi kumchanganya.
Alijiandaa na kutoka sebleni ambako aliwakuta tena wanae muda huu wamekaa sebleni kasoro Ana ndio alikuwa bado chumbani, kisha akawaaga na kuwaambia,
“Jamani natoka, nadhani badae tutaongea vizuri”
Alikuwa ni mtu mwenye hofu na mashaka halafu machozi yalionekana kumlengalenga, kitu hicho kilifanya wanae wamuulize kuwa mama yao anaenda wapi na kulikoni yani ni kitu gani kilichomsibu,
“Wanangu, Ashura amekufa”
“Ashura amekufa?”
“Ndio amekufa”
Machozi yalikuwa yakimtililika na kuondoka huku akiwaacha wanae wakijadiliana pale.
Walijiuliza kuwa huyo Ashura amekufa kivipi yani taarifa zimeletwaje maana mama yao alionekana kuchanganyikiwa kabisa na taarifa hiyo, Kulwa alijikuta akiwauliza wenzie,
“Sasa kama mama ni muoga hivi wa kifo hadi amechanganyikiwa kwa kifo cha Ashura, mbona alitaka kututoa kafara sisi? Angeweza kweli kuvumilia wakati watoto wake tumekufa kwa kutolewa kafara nay eye?”
“Unajua hata mimi mwenyewe namshangaa sana mama, kama anashtuka hivi na kifo cha Ashura je kifo chetu sisi angefanyaje!”
“Mi nadhani kwasababu kifo chetu alikuwa anakitarajia kwahiyo kisingemshtua sana, ila kifo cha huyo Ashura hakukitarajia. Sijui kafa vipi nay eye mmmh!”
Walijadiliana sana bila ya majibu yoyote yale ya moja kwa moja.
Patrick siku ya leo aliomba asafiri kwani aliona ana ulazima wa kufanya hivyo ili aende kwa ndugu zake, Neema hakumpinga hata kidogo zaidi zaidi akamsaidia kujiandaa na kisha kumsindikiza kwenda kupanda magari ya kusafiri kwenda mkoa mwingine. Patrick hakuondoka na gari badala yake aliliacha gari lake nyumbani kwa Neema kwahiyo waliagana kisha Neema wakati wa kurudi akapitia tena kwa rafiki yake mama Pendo ambaye baada ya maongezi mafupi bado alimsisitizia kuwa mtoto wake ampeleke kwenye maombi,
“Sasa ndugu yangu Yule si mtoto mdogo kusema nitambeba mgongoni kwenda nae huko kwenye maombi”
“Ushawahi kuongea nae lakini kuhusu maombi?”
“Sijawahi yani kila nikitaka kuongea nae yanatokea mambo mengine najikuta sijaweza kuongea nae, yani usinione hivi nina makubwa ndugu yangu hata siju nianzie wapi na niishie wapi”
“Inatakiwa na wewe uende kwenye maombi”
“Nitakuja unipeleke, yani akili yangu haipo sawa kabisa”
Akaongea ongea nae pale kisha akaagana nae na kwenda kupanda daladala ili aweze kurudi nyumbani kwake, alipokuwa kwenye lile daladala kuna vijana pembeni akawasikia wakiongea,
“Yani muvi zingine za ajabu kweli yani, eti mtu anakufa mara mtu huyo anarudi kwenye mwili wa mtu mwingine sasa huyu mtu mwingine wanamshangaa kuwa anafanya mambo ya ajabu ambayo hajawahi kufanya kabla, unashangaa mtu alikuwa hanywi mara gafla anakuwa mlevi kupitiliza. Yale mambo ingekuwa kweli sijui ingekuwaje!”
“Lakini kuna baadhi ya vitu ni kweli sema tu tunapuuziaga vitu hivi”
“Mmmh hivi inawezekana kweli mtu akarudi kwenye mwili wa mtu mwingine? Hapo ikitokea itakuwaje?”
“Kwani hiyo picha iliishia wapi?”
Mara wale vijna kituo chao kikatangazwa na kushuka, kwa jinsi Neema alivyovutiwa na maongezi yao ni hakika kama ingekuwa ni kituo cha kushuka yeye basi angepitilizwa ili aendelee kusikiliza walichokuwa wakizungumzia. Akajiuliza mara mbili mbili kuwa inawezekana vipi kwa mtu mwingine kuingia kwenye mwili wa mtu mwingine, kisha akaanza kuwaza jinsi mtoto wake Salome alivyobadilika yani anatenda mambo ya tofauti kabisa na aliyokuwa anayafanya awali, na mara nyingine anapika chakula kinachoendana na alichokuwa akipika Moza, akaanza kujiuliza,
“Inamaana Moza… Hapana haiwezekani, ile walikuwa wanasimuliana ni muvi tu. Haiwezekani mwanangu Salome akawa Moza, Yule ni Salome na wala sio Moza, halafu Moza alishakufa”
Akawa anawaza huku akikataa majibu yake mwenyewe anayoyawaza kwani aliona akichanganyikiwa tu, kuja kushtukia kapitilizwa kituo chake sababu ya mawazo, kwahiyo akashuka na kupanda gari nyingine ili aende nyumbani kwake.
Alipokuwa kwenye gari nyingine alisikia sauti ya mtu ikimwambia,
“Pole kwa mawazo mama”
Sauti hiyo ilimchanganya vilivyo kwani ilikuwa ni moja kwa moja sauti ya Moza, kwahiyo akashindwa hata kugeuka kumtazama mtu huyo kwani hofu tayari ilikuwa imeanza kuingia kwenye moyo wake, alifika kituo chake na kushuka ila alihisi Yule mtu ameshuka nae, na kila alipotembea kwenda nyumbani kwake alihisi kuwa Yule mtu yupo nyuma. Alipatwa na uoga kadri alivyoongoza mwendo mpaka anafika kwenye geti la nyumbani kwake, bado alihisi Yule mtu yupo nyuma yake, akagonga geti kwa nguvu huku akijaribu kugeuka nyuma ili kama akikutana na maajabu basi apige kelele, ila alipogeuka nyuma hakuona mtu yeyote, kidogo moyo wake ukatulia na kujiona kuwa ni muoga sana ambapo alikuwa anaogopa kitu cha mawazoni.
Akajiona ni mjinga zaidi kugonga geti lake wakati linakuwaga wazi muda wote, akalifungua na kuingia ndani, aliwakuta wale wanae mapacha wakiwa sebleni na kuwauliza,
“Dada yenu yuko wapi?”
“Amerudi muda sio mrefu yani nadhani mliongozana mama, maana muda huu huu kaingia ndani. Yupo jikoni”
Neema bado aliganda kwani alikuwa kama haelewi elewi kitu vile, alikaa kwenye kochi huku akihema kwa nguvu ili kujitoa hofu kwanza.
Rose alikutana na wale vijana wake na moja kwa moja wakampeleka kule wakikotupa ule mwili, nay eye aligundua tu nguo za Ashura,
“Jamani ni kweli Ashura wangu”
“Ndio mama, ni Ashura kumbe ndio tulimtupa na tukajua ni kile kitoto”
“Jamani nani kamuua Ashura wangu?”
“Mama itakuwa ni kile kitoto tu ndio kimetuchezea mchezo mchafu, labda ndio kamuua Ashura halafu akatuma ujumbe kuwa tukambebe na kumtupa”
Yani Rose hakujua cha kufanya kwa muda huo kwani vitu hivyo vilikuwa vikimchanganya sana, hawa vijana walimuuliza kuwa ni kitu gani kifanyike kwa mwili wa Ashura ulioharibika na kuwaomba kuwa wachimbe hata shimo na kumzika kwani hakuelewa kuwa hata wafanyeje,
“Sisi tutachimba mama ila mshiko ndio tunaouhitaji”
“Nitawapa jamani, naomba tu mchimbe bora kidogo niwe na amani kuwa ndugu yangu hata alizikwa, yani roho inaniuma sana kumuona Ashura katiaka hali hiyo.”
Wale vijana hawakupoteza muda na kuanza kuchimba shimo, ila wakati wanataka kumzika Ashura lile shimo lilijaa maji na kumfanya Rose ashangae kuwa shimo limechimbwa vizuri halafu lijae maji tena, akawaomba wale vijana wachimbe tena. Walichimba mashimo kama matatu na yote yalijaa maji wakamwambia,
“Nadhani tuzike hivyo hivyo tukisema tuchimbe chimbe tutabambwa hapa, ujue vitu vya magendo hivi tunafanya? Na tukikamatwa ni kifungo cha maisha hakuna atakayetuelewa, tutaonekana tuliua na ndio tumeamua kuja kuzika mtu tuliyemmaliza”
Rose hakuwa na jinsi ikabidi wazike hivyo hivyo kwenye mimaji na kufukia, roho ilimuuma sana kuona ndugu yake amezikwa kama mnyama, ndugu yake kazikwa kikatili na ameuwawa ingawa bado hakuelewa kuwa dawa aliyoweka ili auwawe Salome ndio dawa hiyo hiyo iliyomuua Ashura.
Walimaliza, akawalipa wale vijana na kuondoka, alikuwa anarudi nyumbani kwake huku ana mawazo mengi sana haswaa akiwaza kuwa afanyaje na huyu mtu wa kuitwa Salome ilihali kashaujua ukweli kuwa huyo Salome ndio Moza ila huyo Moza akija kwenye umbile lake la Moza asilia anatisha sana bora akija kama Salome, na hapo akajiona mapambano ya kupambana na Salome yakimshinda kabisa.
“Natakiwa nimtafute Patrick nimwambie ukweli kuwa mwanae Salome ni mtu mwingine”
Alipanga kumtafuta Patrick ila alijaribu kupiga simu za Patrick kwa wakati huo hakuzipata hewani zilikuwa hazipatikani.
Neema alikuwa pale sebleni ila ndani ya muda ule ule, Salome alikuja kumwambia kuwa chakula ni tayari na kumfanya uoga umshike zaidi kuwa amekipika saa ngapi ikiwa watoto wale wamemwambia kuwa karudi muda sio mrefu, ila kabla hajamuuliza chochote Salome akamwambia,
“Mama unajiuliza kuwa chakula nimepika muda gani, unafikiri nimekipika sasa hivi basi? Nilikiacha jikoni, na mimi nilienda dukani”
Kidogo alivyosema hivyo hofu ilimuisha Neema na kujikuta akiinuka kwenda kula, ila macho yake hayakuisha kumuangalia Salome, alikuwa akimuangalia kwa jicho la wizi lakini alikuwa akimuangalia haswa wakati anakula alimuangalia sana, kwa kawaida Salome hakuwa na utaratibu wa kula ila alishangaa Salome wa sasa hivi alikuwa na utaratibu wa hali ya juu hata wakati anakula hakuwa akiongea wakati Salome hadi alikuwa akipaliwa kwa mtindo wake wa kula na kuongea.
Walipomaliza kula aliamua kuzungumza na Salome kuhusu swala aliloambiwa na mama Pendo la maombi,
“Sawa nitaenda, ila nipe sababu ya kunipeleka mimi kwenye maombi?”
“Salome umekataa kusoma, sasa unafikiri nisikupeleke kwenye maombi kweli!”
“Kusoma sijakataa ila nimekwambia nimechoka kwa kipindi hiki na nitasoma mwakani, kwani mbali jamani mwakani si hapo tu. Halafu kitu kingine kwani mtu asiposoma ndio ana matatizo hadi aombewe? Wangapi hawajasoma na maisha yao ni mazuri tu”
“Hatakama Salome, ila mimi ni mama yako naomba twende kwenye maombi”
“Sawa mama tutaenda”
“Kesho jiandae nikupeleke kwenye maombi”
Salome alimuitikia Neema bila ya pingamizi lolote ila muda wote Neema alikuwa akijiuliza maswali bila ya majibu huku akijaribu kuhusisha stori za wale vijana na jinsi alivyo Salome wake, ila alijikuta akipinga kuwa Salome wake hawezi kuwa amevamiwa na mzimu ila ni Salome Yule Yule sema kabadilisha matendo yake.
Kwa Yule mganga ambapo Rose aliacha lile gari likiwa na mwili wa mama Jack, mganga akataka afanye jambo la kichawi ili mwili ule urudi kwa Rose kisha Rose angejijua mwenyewe, mganga alimchukua msaidizi wake na ule mwili kisha wakauweka kwenye kile chumba cha mganga na kuanza kufanya dawa zake ili ule mwili uende nyumbani kwa Rose, basi alifanya dawa zake kwa muda kama wa nusu saa na ule mwili ukatoweka machoni mwao, mganga alijisifia,
“Mimi ndio kiboko wa kila kitu”
Mara gafla ule mwili ulirudi kibandani kwake na kumfanya mganga na msaidizi wake wabaki wanashangaa,
“Imekuwaje tena?”
“Nadhani kuna mtu anacheza na akili yangu, ila sikubali”
Akafanya tena dawa zake kama kwa nusu saa hivi, na mwili ukatoweka kweli. Sasa muda huu alitaka kujua kuwa ulipo mwili ni kitu gani kinatokea, akachukua kioo chake na kuangalia alishangaa sana kuwa muda huo mwili wa mama Jack ulionekana nyumbani kwa mama Jack na watu kwenye nyumba hiyo walikuwa wakishangaa tu.
Itaendelea
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: