Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 36 Rose akalamba ile dawa na kutoka nje, ila kabla hajalisogelea gari lake akashangaa kumuona mwanae Ana akiwa amemfata kule kwa mganga, alishangaa sana na kujikuta akisema, “Ana!” “Ndio ni mimi mama, nimekufata nata……” Ila kabla Ana hajamaliza sentensi yake, Rose alianguka chini na kuanza kutapatapa. Ana alipatwa na hofu sana baada ya kumuona mama yake katika hali ile ila gafla alijikuta akipata wazo la kutoa lile jiwe la dhahabu ila hakujua kuwa afanye nalo kitu gani. Akalitoa lile jiwe la dhahabu na kujikuta akilishika na kuliweka kwenye kifua cha mama yake na gafla wakatoweka mahali pale. Mganga alikuwa pembeni akiwaangalia na akiangalia kinachoendelea kwahiyo alishangazwa sana na kuona kuwa gafla watu wale hawaonekani ila gari ya Rose ilibaki pale pale na mwili wa mama Jack ulibaki mule mule kwenye gari, mganga alishangaa sana na kumwambia msaidizi wake, “Mwanamke mshenzi sana Yule, ananiletea uchawi wake kwenye nyumba yangu pia! Kaacha maiti yake hapa, akimaanisha nini? Na nitamkomesha kwakweli yani nitamkomesha haswaa” Msaidizi wa mganga alikaa kimya kwani hata yeye hakuelewa kitu chochote kile kinachoendelea, na pia hakuelewa kuwa yeye na mganga watafanya nini na maiti ambayo imeachwa ndani ya gari. Nyumbani kwa mama Jack napo hawakuelewa kabisa kuhusu mama yao, walijaribu kuulizia sehemu mbali mbali ila hakuna mahali walipopata jibu la kueleweka, ila wakakumbuka tu kuwa mara ya mwisho mama yao alimsindikiza Yule binti aliyemuokota na kuamua kumpeleka kwao, watoto wake walijiuliza kuwa bora hata wangeenda na mama yao kumsindikiza ila kwavile waliona ni mtu mzima basi wakamuacha aende mwenyewe ila kitendo cha kutokupata mawasiliano yake na kitendo cha kutokurudi nyumbani kiliwapa hofu kubwa sana, walijiuliza maswali mengi bila majibu na mwisho wa siku walipanga kuwa wakatoe taarifa polisi maana walihisi kuwa huenda mama yao ametekwa na watu wenye lengo la kumuibia gari sababu aliondoka na gari, basi wakakubaliana kufanya hivyo ila walipotoka nje walishangaa kuona gari ya mama yao iko pembeni kama vile alirudi na kuondoka tena bila ya gari, “Jamani gari imerudije?” “Lazima alirudi jamani, inawezekana vipi gari lirudi lenyewe?” Wakalisogelea gari lake na kulichunguza, funguo za gari zilikuwa mlangoni na kila kitu kwenye gari kilikuwepo kasoro tu mama Jack ndio hakuwepo, ila kwavile waliona gari wakajipa matumaini kuwa atarudi tu na kuacha kwenda kutoa ripoti polisi, “Maana kama karudisha gari basi yupo hapa hapa mtaani atakuja tu, na akiona tumeenda kutoa taarifa polisi atatuona sisi ni wajinga sana. Bora tumeona gari kidogo mioyo imetulia” “Hivi lakini mama arudishe gari halafu asiingie hata ndani?” “Labda sehemu aliyokuwa anaenda ni ya muhimu sana, atakuwa kwa majirani tu huko sidhani kama kaenda sehemu ya mbali aache gari” Wakakubaliana kuwa atakuwa mazingira hay ohayo na kuwafanya hofu iondoke kwenye mioyo yao kuwa mama yao yupo. Wakina Rose waliamua kwenda kulala sababu usiku ulishafika, ila Salome aliwaaga kuwa anaondoka muda huo. “Kheee mbona usiku tayari?” “Aaah kuna umuhimu wa mimi kuondoka muda huu, natakiwa niwahi nyumbani” “Kwanini usingelala hapa ukaondoka kesho asubuhi?” “Hivi mmeshaniona nikilala hapa toka siku mama yenu alipotaka kufanya mambo ya ajabu kwenye chumba change? Mi naenda kulala nyumbani kwetu” Wakatazamana ila hakuna aliyemjibu la zaidi, kisha Salome akaondoka zake na kuwaacha wakijadiliana, huku Doto akiuliza kuwa ni mambo gani ya ajabu ambayo mama yao alitaka kuyafanya chumbani kwa Salome. “Jamani mimi kama nilisikia sikia tu kuwa eti mama alitaka kuzini na mlinzi wetu” Wote wakashangaa na kuuliza kwa makini huku wakimfikiria mama yao na Yule mlinzi wao, “Hivi kweli mama anaweza kufikia hatua hiyo ya kutaka kuzini na mlinzi wetu? Yule mlinzi si yupo sawa na sisi tu?” “Hivi kama mama ameweza kutaka kututoa kafara sisi atashindwaje kutaka kuzini na mlinzi? Mama yetu kawa na mambo ya ajabu, tutakataa hilo ila ndio ukweli huo, mama amekuwa na mambo ya ajabu” “Mimi naona tusiendelee kujadili tena mambo hayo, jamani tunataka kwenda kulala na mkumbuke kuwa mimi nalala peke yangu” “Hivi unaweza kwenda kulala chumbani kweli leo?” “Basi nawaomba jambo moja, tulale wote sebleni jamani” Wakakubaliana na Sara kuwa wote walale sebleni kwa usiku wa siku hiyo. Swala la Neema kukuta simu ya Ashura kwenye begi la Neema ni swala lililompa wasiwasi zaidi, akajikuta akitoka nayo kwa Patrick na kumueleza kuwa ile ni simu ya Ashura na ameikuta chumbani kwa Salome. “Hivi umesema kuwa tangia Ashura aondoke umekuwa ukiwasiliana nae kwa njia ya ujumbe” “Ndio, hata nikashangaa kusema kuwa eti umeona picha ya maiti yake ikiwa imeoza ila nimeshangaa zaidi kukuta simu ya Ashura kwenye pochi ya Salome na kunitia uwoga zaidi kuwa huenda Salome anajua kuhusu kifo cha Ashura au huenda ndio yeye mwenyewe aliyekuwa akiniandikia ujumbe mimi. Tuseme….” Akafikiria kidogo kuwa Salome ndio kamuua Ashura, akajikuta akitikisa kichwa chake na kusema, “Hapana, mwanangu sio mkatili kiasi hicho. Mwanangu hawezi kuwa amemuua Ashura, kwanza kwa lipi baya alilofanyiwa na Ashura hadi amuue? Hapana kwakweli, haiwezekani yani haiwezekani kabisa” Patrick akamshauri Neema kuwa awashe ile simu ya Ashura ili wajaribu kuangalia kuwa ni namba gani zimewahi kupigwa na ujumbe mingapi iliyowahi kujibiwa kwenye simu hiyo. Basi Neema akajaribu kuwasha simu ile ila haikuwaka na kugundua kuwa haikuwa na chaji kwahiyo ikabidi aiweke kwenye chaji huku wakiwa na hamu ya kujua kuwa ni watu gani wamekuwa wakiwasiliana nae kwenye simu ile. Muda kidogo alijaribu tena kuiwasha ila iliwaka na ilipowaka tu kuna ujumbe ambao inaonyesha ulikuwa unasubiri kuingia kwahiyo uliingia muda huo huo, ilionekana ni namba mpya ambayo haijatunzwa kwenye simu hiyo ndio imemtumia huo ujumbe, ujumbe ule ulisema, “Umeona mambo uliyoyafanya sasa Ashura yani umenivurugia kila kitu, huyu Salome amekuwa mtihani mkubwa sana katika maisha yangu. Nilikutuma umamalize ila ukakimbia bila ya kummaliza, sasa huyu mtoto amekuwa na nguvu za ajabu na anataka kunimaliza mimi. Je utafurahi ukisikia ndugu yako nimemalizwa na huyu mtoto wa laana? Sijapendezewa kabisa na ulichofanya” Neema na Patrick walitazamana kwani kuelewa huo ujumbe moja kwa moja ilikuwa ngumu kabisa ukizingatia mtumaji wa ujumbe ule hawakumfahamu, hivyo wakaamua kufatia mazungumzo kwa namba hiyo na jumbe zilizotumwa, mwishowe waligundua kuwa mtuma ujumbe alikuwa ni Rose na walishangaa sana kwani waliona hadi jinsi Rose alivyopanga mipango ya kummaliza Salome kwa kushirikiana na Ashura yani hadi walijikuta wakishindwa kuangalia jumbe zingine zaidi ya zile kwani ziliwatisha kwakweli, “Yani kumbe Ashura nilikuwa naishi nae halafu anajuana na Rose! Kumbe alipanga mipango ya kumuua mwanangu! Sielewi kabisa sielewi” Patrick alikuwa kimya tu kwani yeye ndio hakuelewa zaidi, muda kidogo walisikia mlango wa sebleni ukigongwa kisha Neema kwenda kufungua, alikuwa ni Salome ila Neema alishindwa hata kumfokea Salome kwa kurudi usiku huo nyumbani kwani jumbe za kwenye simu ya Ashura zilikuwa zimemtisha sana, badala yake alijikuta akimkaribisha ndani na kumuuliza kuhusu Ashura kama ana mpango wa kumuua yeye alijuaje na je imekuwaje hadi simu ya Ashura ipo kwake, “Mama na Baba naomba niwaeleze kwa ufasaha kabisa, kama mmesoma hizo jumbe mtakuwa mmapata maana kuwa Ashura alikuwa ni mtu wa aina gani katika maisha yetu. Mama ulimchukulia Ashura kama mdogo wako ila kiukweli kuna kazi alipewa ndiomana alikuja kukaa hapa, Ashura na Rose hawakumuweza Salome sababu alikuwa na kinga thabiti kutoka kwa marehemu mama yake na Patrick” Walimshangaa kuwataja majina yao ila kwavile walitaka kujua zaidi ndiomana walikuwa wakimuuliza tu maswali kuhusu Ashura, “Eeh mwanangu hebu nieleze vizuri, ilikuwaje tena yani ilikuwaje hadi kutaka kukuua wewe na ilikuwaje hadi simu yake ipo kwako?” “Mama, nilimsikia kwa masikio yangu akiongea na simu kuhusu dawa ya kuweka ili wanimalize, ndipo akaandaa chakula na kuniwekea hiyo dawa kwenye chakula ila mimi nilifanya mchezo wa kumbadilishia sahani ya chakula na ndipo alipokula alianza kutoka povu na kutapatapa na akawa kimya hapo hapo kumbe ilikuwa ni sumu kali sana ya kuua kwa muda mfupi. Nikachukua simu yake na kugundua kuwa kuna vijana alizungumza nao kuja kubeba mwili wangu, kwahiyo nikampakia yeye kwenye viroba na kuwatumia wale vijana ujumbe kuwa waje wabebe tayari ila mimi niliondoka kwani nilipata pesa kwenye begi la Ashura na kuja kutafuta nyumba. Kwahiyo wale vijana walijua wameenda kunitupa mimi. Nilifanya hivyo kwasababu ni kesi kukutwa na maiti tena imeuwawa kwa sumu, nilifanya hivyo kuficha ushahidi kwani hata yeye alipanga kufanya hivyo” Neema alishindwa kuwa alie au acheke kwani hakujielewa kabisa, siku zote alimchukulia Ashura kama mdogo wake ila hakuelewa kama Ashura alikuwa akimzunguka, ndipo akaelewa jinsi alivyoulizia habari za Ashura kwa mamake wa kambo na kuambiwa kuwa huyo mtu hawamtambui kabisa, alijaribu kuunganisha picha ya jinsi alivyokutana na Ashura na kupata jibu ya maswali aliyokuwa akimuuliza na kujua kuwa Ashura alitumwa katika maisha yake. Salome akawaeleza vingi sana kuhusu Ashura na kuwafanya wabaki wameduwaa tu na hawakuelewa chochote kile, yani Neeema hakujua alie kwa kupata uhakika wa kifo cha Ashura au acheke sababu mwanae kanusurika na kifo, walijikuta wakikaa kimya tu wakitafakari kuhusu Ashura na kutumwa na Rose, yani Patrick alijikuta akijutia maisha yake, “Najuta kumfahamu Rose, najuta kuanza kufanya biashara na mwanamke huyu. Alinifanya niifukuze familia yangu, amefanya nisiwathamini wanangu, amefanya mamangu auwawe kikatili, amenifanya niwasahau ndugu zangu, amefanya niwe kama ndondocha kwenye mali zangu mwenyewe. Najuta, amefanya niamini maneno ya Ashura kuwa ni ya ukweli sababu ni ndugu yako kumbe ni mtu ambaye amempanga kuja kuharibu maisha yetu, huyu mwanamke sijui nimfanye nini? Yeye ni mchawi ila mimi nitamfanyia kitu cha kawaida tu ambacho hatokisahau maishani mwake” Patrick alionyesha kutokufurahishwa kabisa na mambo ya Rose, waliinuka na kwenda kulala ila si Patrick wala si Neema waliopata usingizi, kwani usingizi haukuwajia hata kidogo, muda wote Neema aliwaza alivyokuwa akiishi na Ashura jinsi alivyokuwa akishauriana nae halafu kumbe alikuwa na mipango ya kuuwa mtoto wake, ila tu alijiuliza kuwa kama alikuwa na mpango huo kwanini hakuweza kumuua mtoto wake wakati akiwa mdogo kabisa ndio kutaka kumuua mkubwa vile, aliwaza sana bila ya jibu la aina yoyote ile. Kwa upande wa Patrick nae alikuwa akiwaza tu toka siku ya kwanza alivyomfahamu Rose na jinsi alivyotelekeza familia yake. Asubuhi ilipofika walikuwa palepale sebleni yaani Sara, Doto na Kulwa. Waliamka na kusalimiana, mara wakashangaa kumuona mama yao akitoka chumbani, wakajikuta kwa pamoja wakisema, “Mama!” Muda kidogo wakashangaa kumuona na Ana nae akitoka chumbani, na kujikuta wakisema tena kwa pamoja, “Ana!” Ila Ana na mama yao walikuwa wakishangaa pia kwani ilionyesha kuwa nao hata hawakujijua kama wapo hapoa nyumbani, ikabidi Rose atoke nje ili akaangalie kama gari yake ipo, alipotoka hakuiona ile gari ambayo alienda nayo ikamfanya ajiulize sana kuwa imekuwaje yeye amerudi ila gari yake haijarudi? Halafu akakumbuka kuhusu rafiki yake aliyetakiwa kumzika wakati mwili ulikuwa ndani ya lile gari, hapo bado hakuelewa, akarudi ndani na kumtazama Ana kisha akamwambia, “Mara ya mwisho nakumbuka nilikuona wewe ila kilichoendelea sikumbuki, imekuwaje mwanangu nimerudi nyumbani?” “Hata mimi sielewi mama, nakumbuka ulianguka na kuanza kutapatapa. Kuna jiwe la dhahabu nililiokota mtoni, nikachukua na kukuwekea kifuani ila kilichoendelea sijui, ninachojua ni kuwa nimeamka asubuhi hii nipo chumbani mwangu” “Unasema jiwe la dhahabu? Liko wapi hilo?” “Sijui lilipo, yani mara ya mwisho ni kulitoa na kuliweka kwenye kifua chako ila sikumbuki limekwenda wapi” “Unasema uliliweka kifuani mwangu?” “Ndio mama” Rose alikaa chini na kuanza kulia, watoto wake wote wakamshangaa kuwa anacholilia ni kitu gani maana wao hakwakuona cha kushangaza na kumfanya mama yao hata alie, walimuuliza kuwa analia nini, “Ana mwanangu umenimaliza, yani umenimaliza kila kitu” “Kivipi mama?” Mara akaanza kuulizia kuhusu Salome na kuacha mada ya kuwa anamalizwa, “Salome yuko wapi?” “Yupo kwao” “Sio Salome Yule, wanangu Yule ni Moza” “Moza!!!” Waliuliza wote kwa mshangao wa hali ya juu, “Ndio ni Moza” “Kivipi mama?” “Nyie nieleweni tu, Yule sio Salome ni Moza” “Mmmh kwahiyo Salome yuko wapi?” “Sijui ila Yule ni Moza anatumia tu mwili wa Salome” Wote walikuwa wanashangaa ila gafla wakasikia mtu akicheka na mara kidogo akatoka sebleni, na kusikia sauti ya Moza ikisema sasa, “Unasemaje Rose?” Kila mmoja alikuwa anatetemeka na hakuna aliyeweza kumtazama Moza machoni. Itaendelea
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: