Home → simulizi
→ KURUDI KWA MOZA: 33
Alivyofika mtoni alimwaga dawa ile kwenye mto, ni kweli kikatokea kitanda pembeni na alipoangalia aliyelala kwenye kitanda hicho hakuwa Doto bali alikuwa ni Moza.
Rose aliogopa na mkono wake kuanza kutetemeka hata akashindwa kukisukuma kile kitanda mtoni badala yake alikimbia haraka haraka kurudi nyumbani kwa Yule mganga.
Alifika anahema sana, ila alimkuta mganga amechukia vilivyo,
“Umefanya nini wewe?”
“Nimemwaga dawa ila hakutokea Doto, bali alitokea Moza”
“Hata kama ungemsukuma mtoni hivyo hivyo, yani ushaharibu kila kitu”
“Nisamehe”
“Nikusamehe nini na ushaharibu”
“Sasa hutotoa kafara mtoto wako mmoja, itabidi utoe wawili”
Rose alishtuka sana kusikia atoe kafara ya watoto wake wawili ukizingatia huyo mmoja tu alikuwa anafikiria sasa kuhusu wawili ataweza kweli, ikabidi amwombe mganga akafikirie kwanza.
“Hili si jambo la kufikiria ila ni jambo la kufanya maamuzi”
“Mganga nina watoto wane tu, watoto wangu wote ni wa muhimu kwangu”
“Kwahiyo wanao ni wa muhimu kuliko maisha yako?”
“Sikia ndugu yangu, yani watoto hawa ndio wamefanya siku zote hizi nihangaike sababu yao. Yani yote haya ninayoyafanya kwenye maisha ni sababu yao, yani leo nikawatoe kafara kweli?”
“Chagua moja, kuwatoa watoto wako kafara au wewe kuumbuka”
Yule mganga akainuka na kumuacha Rose akiendelea kuwaza kuhusu kuwatoa kafara watoto wake, aliwaza sana bila ya kupata jibu na kufanya kama akili yake kukosa uelekeo.
Yule mganga alirudi tena na kumuuliza Rose kuwa amechagua jambo gani sasa,
“Hapana kwakweli, siwezi kuwatoa kafara watoto wangu”
“Yani hapo watoto wawili tu unasema huwezi, je ukiambiwa wote?”
“Hapana siwezi”
“Basi wewe ndio utolewe kafara”
Rose akashtuka na kuuliza kwa makini,
“Nitolewe kafara kwanini?”
“Umekiuka masharti yangu, na mimi sipo tayari kufa kwaajili ya ujinga wako kwahiyo nitakutoa kafara wewe”
Katika vitu ambavyo Rose alikuwa anaviogopa katika maisha yake basin i kifo, yani kwake ilikuwa ni rah asana kusikia wengine wamekufa ila yeye hata akianza kuumwa tu basi hofu ya kifo humkaa kichwani, kwahiyo swala la kuambiwa kuwa atolewe kafara yeye lilimchanganya akili vilivyo hadi akajikuta anakubali kuwatoa kafara watoto wake.
“Nitawatoa hao wanangu wawili kafara”
“Kwahiyo utamtoa yupi na yupi?”
“Wale mapacha”
“Mapacha hata ukiwatoa wote bado utaonekana umemtoa mmoja sababu wale wamezaliwa siku moja, kafara yao inabidi iwe ya siku tofauti ili iwe na nguvu ila kwa siku moja itakuwa haina nguvu na kafara ninayoitaka mimi ni ya siku moja. Mweke mwingine wa kumtoa kafara hapo”
“Ana najua haiwezekani ila Sara, jamani yani nimtoe mwanangu Sara kifungua mimba wangu! Nampenda Sara jamani, tafadhari nisimtoe Sara”
“Unatakiwa kumtoa, ndiomana nimekwambia kama huwezi basi kafara tukutoe wewe”
Kwa kuhofia kifo akajikuta anakubali kuhusu kuwatoa watoto wake kafara, kwahiyo kilichofatia ni mganga kumpa masharti ya kafara anavyoitaka iwe, kwahiyo Rose alikuwa makini kabisa kusikiliza mlolongo wa kafara.
Mr.Patrick alimuaga Neema kuwa anaenda kumchukulia kitu Fulani ila hakutaka kumtajia, ukweli ni kuwa alijiona mwenye bahati sana kupokelewa tena na Neema na alimuona Neema ni mwanamke mwenye upendo sana juu yake.
Aliondoka nyumbani hapo kwa Neema na alienda kwenye nyumba nyingine aliyowahi kujenga ili aiangalie kama inafaa kumuhamishia Neema hapo, ila wakati yupo kwenye ile nyumba mara wakaja vijana watatu na kumsalimia kisha wakajitambulisha kuwa wao ni wafanyakazi wa Rose, kwahiyo Patrick alitulia akiwasikiliza kwa makini kuwa wana jambo gani wanalotaka kuongea nae,
“Sikia tukwambie, kuna kazi mama alitupa ila kazi yenyewe sijui alipanga yale mazingira tumekuta mambo hayaeleweki kabisa, halafu tunamtafuta hewani hatumpati”
“Hata siwaelewi mjue”
“Hutuelewi kivipi kwani kazi za mkeo huzijui?”
“Bado siwaelewi”
“Sisi tunamtafuta hewani tumpe habari kuwa ile maiti tuliyoendaga kuitupa tumeenda kuifukunyua tumekuta imeoza na ananuka vibaya ila sura ni ya Yule ndugu yake aliyetupa kazi”
“Maiti? Bado siwaelewi”
“Huyu mzee vipi jamani, hatuelewi nini? Hebu toa simu yako umuonyeshe picha za ile maiti tulivyoikuta”
Mmoja akatoa simu na kumfungulia picha Patrick aione, kwakweli Patrick alitamani kuruka, picha ilionyesha maiti kaoza oza ila sura yake inatambulika bado na ilikuwa ni sura ya Ashura. Kwakweli Patrick hakuweza hata kuitazama mara mbili na kuamua kuwauliza tena,
“Inamaana mmemuua Ashura?”
“Hapana ila sisis tulipewa kazi tu ya kutupa ile maiti na tuliambiwa ni maiti ya mtu mwingine halafu tulikuwa tunawasiliana na huyo huyo Ashura nahisi kuna mtu katuzunguka kamuua Ashura halafu kataka sisi tubebea maiti tukijua ni yeye kumbe ni Ashura”
“Mtu gani huyo?”
“Sisi tulitumwa kubebe maiti ya binti mmoja anaitwa Salome, na tulivyobeba tulijua ni Salome kumbe ni Ashura”
Yani hapo ndio walizidi kumchanganya kabisa Patrick kwani hakuelewa kitu chochote kile, halafu wale vijana wakaanza kumueleza kwa utaratibu sasa jinsi ilivyokuwa ambapo kwa mujibu wa maelezo ya wale vijana inaonyesha wazi mtu aliyemuua Ashura atakuwa ni Salome.
“Hapana, hapana kabisa haiwezekani, mwanangu Salome hawezi kuwa muuwaji”
“Kumbe ni mwanao!”
“Ndio ni mwanangu”
“Kama ni mwanao kwanini mkeo alitaka tumuue?”
Patrick hakuwa na jibu kwani muda huu akili yake kama ilipoteza majira hivi, alikuwa haelewi kitu chochote kile hakuendelea hata kuangalia nyumba aliamua tu kuondoka zake eneo lile.
Rafiki wa Rose, leo aliamka na kumkuta Yule binti aliyemkaribisha kwake akiwa ameamka pia huku akifanya shughuli za mule ndani hadi mama Jack akashangaa kuwa huyu mgeni ni wa wapi kiasi cha kufanya shughuli za nyumbani kwake, kwahiyo alisalimiana nae na kumsikiliza kuwa anataka amsaidiaje,
“Mimi naomba unipeleke kwa mama yangu”
“Lakini kwa mama yako si unakujua, kwahiyo nitakupakiza tu gari uende”
“Nakuomba twende wote, napenda mama asikie mtu aliyeniokoa alinikuta kwenye mazingira gani. Naomba unipeleke, mama yangu ana hela na atakulipa kwa shukrani ulizomfanyia”
Mama Jack akasikiliza maneno ya Yule binti ila muda mwingine kama moyo wa imani ulimshika kwahiyo akamuomba waende mchana mchana na Yule binti alionyesha kufurahishwa sana,
“Asante sana mama yangu, nitakumbuka ukarimu wako siku zote za maisha yangu”
“Usijali binti mzuri”
Kwahiyo mama Jack alijikuta akisaidiana na Yule binti kwenye kila kitu hadi muda ulipofikia wa kwenda nyumbani kwa binti, ila wakiwa njiani binti alimuomba mama Jack amsindikize hospitali kumuona ndugu yake nae alifanya hivyo bila hiyana yoyote, walifika hospitali na kumuomba mama Jack amsubiri nje ya wodi, huyu mama alikubali ila hakuelewa kitu chochote wala hakumuelewa huyu binti sababu hakumjua ila alimsaidia, baada ya muda kidogo Yule binti alitoka huku akimsaidia mgonjwa wake kujikokota na kusema kuwa karuhusiwa, sababu mama Jack alikuwa na usafiri hakuona hiyana ya kumsaidia Yule binti kumrudisha na huyo anaedai ni kaka yake nyumbani.
Rose alitulia akisikiliza dawa anazopewa na Yule mganga, ambapo alianza kwa masharti,
“Hakikisha siku ya leo hakanyagi rafiki yako yoyote nyumbani kwako”
“Hata hivyo hakuna rafiki yangu anayepajua nyumbani kwangu”
“Sawa, ukifika tu getini utapuliza dawa hii”
“Sawa, baada ya hapo”
“Utaingia ndani bila kuongea na yeyote ila cha kwanza kabisa, utaanza kumuita jina mwanao aliyeko hospitali maana ukifanya hivyo tu mwanao kule atakufa. Kisha unajifanya ulikosea unaanza kumuita mwanao mwingine wa Kafara, ataanguka alipo na kufa. Hakikisha unaita majina wakati ushaingia ndani kabisa na kwenye kochi umekaa, yani ita kamavile huna wasiwasi na kilichopo au kitakachotokea. Ukipata habari ya msiba wa watoto wako, jifanye umechanganyikiwa na upotee nyumbani kwako yani uje huku mpaka watakapozika. Utakaporudi watakuonyesha tu makaburi ya watoto wako ila baada ya hapo, kila mtu mjini atakujua wewe ni nani maana mali zako zitaongezeka maradufu na utazidi kuheshimika”
“Nimeipenda hiyo ingawa wanangu wananiuma ila hiyo ya mali zangu kuongezeka nimeipenda sana”
“Ila hakikisha nyumbani kwako asifike mgeni wa aina yoyote”
“Haiwezekani mganga, kwanza saivi watoto wote wanapaogopa pale nyumbani kwahiyo hata kualika rafiki zao ni ngumu”
“Sawa, na rafiki zako pia wasifike”
“Hawatofika, yani hakuna anayepafahamu pale”
Rose alijiaminisha vilivyo kuwa hakuna anayepajua nyumbani kwake, mganga alimpaka dawa nyingine ya kumkinga akimwambia kuwa hiyo itamsaidia zidi ya Moza kwani hatomuona tena kwenye macho yake na hatoweza tena kumsumbua.
Mama Jack alifika nyumbani kwakina Yule binti na kukaribishwa vizuri sana, mama Jack hakuelewa kuwa alikuwa mtegoni maana Yule binti alikuwa ni Salome ambapo alipitia hospitali kumchukua Doto kwahiyo mama Jack alifika kwenye nyumba ya Rose bila kujua kuwa pale ni nyumbani kwa Rose, na kwavile mama Jack hakuwazoea watoto wa Rose kwahiyo ilikuwa vigumu sana kwa yeye kugundua kuwa wale ni watoto wa Rose, mtoto pekee wa Rose aliyemfahamu alikuwa ni Ana na muda huo aliofika Ana alikuwa bado yupo shuleni.
Walimkaribisha vizuri sana huku Salome akiwaambia kuwa Yule mama kamsaidia sana bila ya kusema kuwa kamsaidia vitu gani, ila Salome alimuomba huyu mama asubiri mama yao atarudi nyumbani muda sio mrefu, Sara alimuuliza Salome,
“Una uhakika mama atarudi leo?”
Salome alimuangalia kwa jicho kali Sara na kumfanya Sara ainuke tu pale alipokuwa amekaa kanakwamba alimwambia kuwa aondoke, kisha Salome akabadilisha mada na kuanza kuongea na Doto habari za hospitali na jinsi anavyojisikia, kwavile habari ilibadilika kidogo, Sara alijikuta akirudi tena sebleni huku akiwa ameongozana na Kulwa ambaye alifurahi kusikia kuwa Doto ametoka hospitali.
Patrick alirudi moja kwa moja kwa Neema na kujikuta akimueleza Neema kile ambacho kaelezwa na vijana aliokutana nao, kwakweli Neema alishangaa sana na kuuliza kwa makini
“Kwahiyo Ashura amekufa?”
“Ndio, nimeona hivi picha akiwa ameanza kuoza kwakweli sijui kama ile picha itatoka akilini mwangu ila siamini kama Salome anaweza kutenda kitu cha namna hiyo”
“Nimeumia sana, ingawa kuna mengi nimeyagundua kijijini lakini Ashura niliishi nae kama ndugu yangu kabisa, alikuwa kama mdogo wangu na aliwapenda wanangu. Ila siamini kama Salome anaweza kutenda kitu cha namna hiyo, hapana kwakweli. Salome ni mwanangu, namjua vyema sana, hawezi kufanya jambo la namna hiyo. Salome hawezi kuua”
“Hata mimi nimekataa kuwa Salome hawezi kuua”
“Naomba hao vijana watupeleke huko nikaone jambo alipotupiwa ndugu yangu Ashura jamani nimeumia sana, sasa mbona nilikuwa nawasiliana nae jamani aaah haiwezekani”
Akajikuta akikumbuka kuwa wanae hawa wadogo wamewahi kumwambia kuwa mama yao mdogo Ashura alianguka na povu kumtoka halafu Salome akawaambia ni mchezo wanacheza, akajikuta anasema,
“Ina maana……”
“Ina maana nini?”
“Aaah tuachane na habari hizo, jamani Ashura ndugu yangu hapana jamani. Hata kama hakuwa ndugu yangu, hakustahili kuzikwa kinyama hivyo”
Alichukua simu yake na kujaribisha ile namba aliyokuwa anawasiliana na Ashura ila hakuipata hewani na kumfanya hadi tumbo limuume na kuzidi kuamini kuwa itakuwa kweli ashura kauwawa ila bado moyo wake ulikataa kuwa kauliwa na Salome kwani hakutegemea kama mwanae anauwezo wa kuua.
Rose aliondoka kwa mganga na kwenda nyumbani kwake, alifika getini na kumwaga ile dawa kisha kuingia ndani, kwanza alishangaa kumuona mlinzi getini kwake wakati alimshuhudia akiwa anaondoka ila hakuweza kuongea nae kwa kuhofia kuharibu masharti ya dawa, alisalimiwa lakini hakuitikia kiasi kwamba Yule mlinzi alifikiria kuwa Rose hajapenda kumuona tena.
Rose aliongoza hadi ndani kwake na kuingia sebleni, alishangaa kumuona rafiki yake akiwa amekaa sebleni, halafu pembeni yake yupo Doto, Sara, Kulwa na Salome ila kabla hajaita hata jina moja alishangaa kuona rafiki yake akianguka chini na kuanza kujipigiza kama mtu mwenye kifafa huku mapovu yakimtoka.
Itaendelea kesho usiku……!!!!!!
By, Atuganile Mwakalile.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: