KURUDI KWA MOZA: 31 Basi wakafungua na kuingia, Rose alikuwa wa kwanza kuingia mule ndani ila alishtuka sana kwani alijiona yupo nyumbani kwake na aliyewakaribisha alikuwa ni Patrick na sio Salome. Kila mmoja alipoingia alishtuka, kisha Patrick akawauliza kwa kejeli, “Mnashtuka nini sasa? Mnashtuka kuniona kwenye nyumba yangu mwenyewe? Hapa si nyumbani kwangu, kwahiyo siruhusiwi kuja?” Wote walikaa kimya kwani kila mmoja alikuwa akijiuliza kuwa imekuwaje tena wamerudi nyumbani kwao wakati walikuwa wakiingia kwakina Salome na aliwakaribisha, Patrick aliwashangaa kuwa hawasemi chochote akajua wanamfanyia kiburi bila ya kujua kilichowasibu. “Nyie jifanyeji kiburi tu, mmenikuta kwenye nyumba yangu, hata salamu kutoa hamjatoa eti mnashangaa shangaa. Haya endeleeni kushangaa tu mkimalia mtaniambia” Patrick akakaa chini akiwaacha wao wamesimama huku bado wakishangaa tu, Rose nae alikaa chini huku akitikisa kichwa chake na kusema, “Hivi ni kweli au naota?” Alidakia Ana na kumjibu mama yake, “Ni kweli mama, tumerudishwa nyumbani tena bila ridhaa yetu. Anayetufatilia kwa hakika ana nguvu zaidi yetu” Wote walikuwa kimya tu, Rose alipumua kwa nguvu maana mambo yalikuwa yakimchanganya zaidi na kuanza kuhisi huenda swala la kumpeleka Doto hospitali ndio limeendelea kuzua hayo wanayoyaona. Alipojitafakari vilivyo akamuangalia Patrick sasa na kuanza kumuomba msamaha maana kwa hakika Patrick alihisi wamemdharau, “Tafadhali tusamehe bure ila yaliyotupata kwa siku ya leo hapana kwakweli” “Yaliyowapata yapi hayo?” “Mume wangu unanichukia bure tu ila familia yetu inafatiliwa na wachawi” “Wachawi kushinda wewe uliyemuua mama yangu!! Yani mimi naongea na wewe bure tu ila wewe Rose ni mwanamke mbaya sana, umeniulia mama yangu, umefanya niiache familia yangu iteseke, nimeacha ndugu zangu wakiteseka huku mimi nikila raha ya maisha. Nimeacha mwanangu akiteseka huku wanao nikiwalea maisha ya kifahari, wewe ni mwanamke mbaya sana Rose” “Naomba unisamehe kwanza, halafu hayo si maneno ya kuongelea mbele ya watoto” “Unataka nikaongelee wapi? Umenitesa sana wewe mwanamke, na kwa taarifa yako ndugu zangu wanakuja hapa sio siku nyingi” “Patrick! Ndugu zako wanakuja!” “Ndio ndugu zangu wanakuja hapa na watakuwa wanakaa hapa” “Haiwezekani Patrick, huwezi kufanya jambo bila kunishirikisha mimi. Humu ndani mimi ndio mama mwenye nyumba” “Mke wangu ni Neema na ndio mama mwenye nyumba” “Neema kivipi? Kumbuka Patrick, ulimuacha Neema na kunioa mimi, iweje leo useme mke wako ni Neema! Umechanganyikiwa wewe sio bure” Kisha Rose akawaangalia watoto wake na kuwaambia, “Hivi na nyie hamuwezi kwenda kufanya mambo mengine hadi make msikilize mazungumzo ya mimi na baba yenu!” Patrick akadakia, “Waonyeshe baba zao watoto wako, mimi sio baba yao. Na kibaya zaidi hata huyo mtoto wako wa mwisho nae sio wangu, nilijivunia nimepata mwanamke kumbe ananiacha ndani anaenda kuzaa na mwanaume mwingine nje” Wakina Sara baada ya kuona jicho kali la mama yao ikabidi watoke nje na kuwaacha sebleni kwani Patrick aligoma kwenda kuongelea popote pale zaidi zaidi ya hapo sebleni. “Jamani Patrick twende tukaongelee chumbani mambo hayo” “Twende chumbani ili ukaniroge? Rose umeniroga kwa miaka mingi sana, akili yangu imefunguka sasa na huwezi kunishawishi juu ya kuniroga tena, mwanamke mbaya wewe” Rose alijaribu kila njia ya kumtuliza Patrick ila leo alikuwa hatuliziki kabisa, inaonyesha wazi aliamua na alidhamilia. Kule nje walienda moja kwa moja kwa mlinzi wao na kumuhoji kuwa Yule baba yao alienda saa ngapi pale nyumbani, ila mlinzi alivyowaona alishtuka sana badala ya kumuuliza yeye aliwauliza wao, “Mmeingia muda gani humu ndani?” “Tunataka kukuuliza baba amekuja muda gani?” “Humu ndani mbona mmekuwa na mambo ya ajabu sana sijapata kuona, yani siwaoni kuingia ila gafla nawaona ndani” Basi akafikicha fikicha macho yake na kuiona gari ambayo walitoka nayo ikiwa imepaki uwani, yani hapo ndio akashangaa kabisa kuwa hata gari ilivyoingia hakuiona yani aliona mambo ya ajabu na kuhisi nyumba yote hiyo ni wachawi. “Mama akirudi namuomba mshahara wangu naacha kazi” “Usiache kazi bhana, uache kwasababu gani? Hata hivyo mama yuko ndani” Mlinzi akashtuka tena, “Yuko ndani? Ameingiaje?” “Tulikuja nae” “Hii nyumba hapana, imenishinda kwakweli yani imenishinda kabisa siwezi kuendelea kuishi humu” “Usiondoke, haya mambo yatarekebishwa tu hata usiende popote” “Hapana siwezi, yani watu unawaona wakati wa kutoka tu ila wakati wa kuingia huwaoni!” “Inamaana nae baba hujamuona wakati wa kuingia?” Ana aliuliza kwa makini swali hilo kwani alitaka kujua kama ni kiini macho wamefanyiwa au ni kitu gani, “Mzee yeye kafika vizuri, tumesalimiana nae hapa na kuuliza mko wapi na akaingia ndani kuwangoja. Yani nyie ndio mmenifanyia maajabu, na toka mzee aje sijatoka kabisa hapa getini leo, haya niambieni mmeingiaje” “Yani hata sisi wenyewe hatujui kwahiyo utakuwa unatushutumu bure tu” Ila huyu mlinzi alishikilia wazo lake tu kuwa yeye ataomba mshahara wake aondoke kwenye nyumba hiyo, wakati wanaongea na Yule mlinzi alifika mtu na kugonga geti alipomfungulia alikuwa ni Salome, walibaki wanamtazama kama dakika kadhaa ndio kumkaribisha ila Salome alitabasamu tu na kuingia ambapo moja kwa moja alienda ndani na kuwakuta Rose na Patrick wakiwa kwenye majibizano makubwa sana. Alipoingia tu kama kawaida yake aliingilia yale mazungumzo, “Wewe mama ushaambiwa usamehewi, sasa ya nini kulazimisha msamaha!” “Hata maandiko yanasema samehe saba mara sabini” Salome alicheka sana ten asana kisha akamwambia, “Hivi leo ndio unatambua maandiko yamesema hivyo, je ulipokuwa unamuua bibi wa watu asiyekuwa na hatia ulikumbuka maandiko? Ulipomtumia Ashura ajifanye anaundugu na Neema ili tu azidi kumkandamiza ulitumia maandiko? Wakati Salome anateseka na maisha wakati baba yake anakula raha ulitumia maandiko? Na zaidi ya yote, uliowafuga ndani kwenye chumba chako cha siri unatumia maandiko?” Patrick akashtuka sana kusikia kuwa mkewe kuna watu anawafuga pia kwenye chumba cha siri, “Kheee wewe mwanamke kweli ni shetani yani wewe una matendo hata shetani anayaogopa. Kwahiyo kuna watu umewafuga ndani kwako?” “Salome jamani usizidi kunikandamiza jamani, nisameheni” “Nani akusamehe mwanamke shetani kama wewe? Yani umefanya maovu mengi napo umeona hayatoshi ila ukaongezea na kuwafungia watu kwenye chumba cha siri!” “Anafuga watu ndio huyu, hujui tu baba ila ndio hivyo anafuga watu huyu. Siku ukinijua vizuri utaelewa nimejuaje siri zako na njia zako, sipendi unavyowatesa wale watu, waachie waendelee na maisha yao mengine” Kisha Salome akamgeukia Patrick na kumwambia, “Wasichana wa kazi wote wanaopotea kwenye nyumba yako halafu anasema kawafukuza ni muongo, anawafungia kwenye chumba cha siri, ikitokea mtu kaumia kwenye nyumba hii damu ikamtoka basi asitoke mlangoni maana akitoka tu anajikuta kwenye chumba cha siri, huyu mama ni mpumbavu sana, anafanya mambo ya kijinga. Watu wa watu wamekonda sababu ya kufungiwa, ni bora ujue ndugu yako amekufa kuliko kujua ni msukule, huyu mama ni mbaya sana” Sara na Kulwa walikuwepo mlangoni na walisikia yote ambayo mama yao alikuwa akishutumiwa, muda huu Ana alikuwa getini na mlinzi ila wao wakati Salome ameenda ndani walienda kukaa mlangoni, kwahiyo kila kitu kilikuwa wazi kwenye masikio yao na kuelewa kirahisi kuwa wote wanaohisi wamepotea kumbe mama yao amewafungia kwenye chumba cha siri, ndipo Sara nae alipojiwa na swala la Ommy, akaweza kufikiria ni jinsi gani Ommy alikuwa akiteseka kwenye hiko chumba cha siri, alijikuta akiingia ndani na kumwambia mama yake, “Mama tafadhali mfungulie Ommy wangu” Sara machozi yalimlengalenga kwani leo alielewa mchezo vizuri kabisa kuwa mama yao ni mchawi tena mchawi haswaa wala sio wa kusingiziwa kama wengine. Rose hakuweza kuvumilia hizi shutuma akaamua kukimbilia chumbani, kwahiyo sebleni alibaki Salome, Patrick na Sara. Hizi habari za mkewe kuwa na chumba cha siri zilimshtua sana Patrick kwani aliweza kupata kumbukumbu kuwa kuna rafiki yake aliwahi kupotea kwenye nyumba yake hiyo na hakujulikana alipoenda hadi leo hajui ila hapo kapata jibu kuwa huenda nay eye amefungiwa kwenye chumba cha siri, akamuangalia mwanae Salome na kumuuliza, “Wewe umejuaje hizi habari za huyu mwanamke kufungia watu kwenye chumba cha siri” “Nilijua toka siku ya kwanza nilipokuja kufanya kazi humu” Sara na Patrick walishangaa na kujikuta wakimuuliza kwa pamoja, “Ulipokuja kufanya kazi humu!!” “Ndio, ila msinihoji zaidi yani nyie mjue tu kwamba nilijua.” “Sasa tutafanyaje ili awatoe” “Najua cha kufanya ila njia yangu ni hatari sana, hatari kwake na kwa familia yake ndiomana nataka awatoe mwenyewe kwa hiyari yake” Wakajikuta wakimuangalia Salome na ilionyesha wazi hawamuelewi elewi maana vitu vingine aliongea kamavile ni mtu wa aina nyingine na sio wa kawaida, Kulwa nae aliingia ndani na kuwaambia kuwa kasikia kila kitu na anashangazwa na habari hizo za mama yake kuwa kuna watu amewaeka msukule, basi akawa anajadiliana pale na dada yeka kisha Salome aliomba kutoka na baba yake ambapo alikubali na kuondoka na Salome halafu wakawaaga pale. Neema alikuwa bado yupo chumbani kwake tangu muda ule walipotoka hospitali hadi anaiona jioni ikikaribia, akapigiwa simu na rafiki yake mama Pendo na kuanza kuzungumza nae ambapo mama Pendo alimkumbusha Neema swala la kumpeleka mwanae salome kwenye maombi, “Usipuuzie Neema, mwanao anatakiwa aombewe” “Sijapuuzia, nilisafiri ndiomana uliona kimya” “Sasa lini utakuwa tayari ili nimwambie mchungaji wetu” “Nitakwambia tu, siwezi kusema siku wakati Salome mwenyewe sijaongea nae chochote. Nikiongea nae nitakwambia ni lini” Basi akakubaliana nae hivyo na kukata simu, kisha akatoka na kuanza kumuita Salome ila akaona kimya na kugundua kuwa Salome ameondoka, aliwakuta tu wanae wale mapacha wakiandika andika, “Nyie dada yenu kaenda wapi?” “Sijui ila ametoka” “Yani huyu mtoto ameanza tabia ya kutoka bila kuniaga! Kweli wa kufanyiwa maombi huyu” Ikabidi Neema aanze kufanya kazi zake za hapa na pale, ila hadi anamaliza kupika kisha watoto wake wale mapacha kwenda kulala ila Salome alikuwa hajarudi na kushangaa kuwa Salome kama alikuwa anaenda kulala huko huko si angalau angemuga basi, wakati analalamika hivyo akasikia hodi, alipoenda kufungua alikuwa ni Salome na Patrick ambapo aliwakaribisha vizuri tu kisha Salome akawaambia, “Mi naenda chumbani kwangu, kwahiyo nyie endeleeni na mazungumzo tu” Salome aliondoka, ila Patrick na Neema waliganda tu wakiangaliana na hakuna aliyemsemesha mwenzie kwani kwa muda huo kila mmoja alijiuliza kuwa nani anastahili kuanza kuongea kati yao. Muda nao ulizidi kwenda ikabidi Neema ajitoe muhanga, “Nakusikiliza Patrick” Wazo la haraka haraka la Neema alihisi kuwa Patrick ameenda kudai zile pesa zake alizomleteaga ndiomana alishindwa kuanza kuongea nae, ila Patrick leo alikuwa kama mtu aliyeshikwa na ganzi, “Sijui hata nisemaje, ila nisamehe Neema” “Mi nishakusamehe siku nyingi mbona” “Nifanye nini unisamehe?” “Wewe mbona mimi nishakusamehe jamani!” Patrick alikuwa kimya tena kwani kadri alivyomuangalia Neema aliona anazidi kuwa mzuri, alimuona Neema akiwa mrembo zaidi kupita Yule Neema aliyemuoa akiwa na miaka kumi na sita, alijikuta akitamani kumuuliza kuwa mbona urembo ulizidi ila mdomo ulikuwa mzito, Neema nae alimuona Patrick akiwa zaidi ya vile alivyomuoa kipindi cha nyuma, alimuona Patrick amekuwa na sura ya kuvutia hatari, akajikuta anamwambia, “Naenda kulala bhana” Neema hakutaka tena kumuangalia Patrick kwani alihisi kumtamani ila ile alivyoinuka baada ya kumwambia naenda kulala, Patrick nae aliinuka na kufatana na Neema hadi chumbani, kwahakika Neema hakuweza kumfukuza Patrick ukizingatia alishakuwaga mume wake. Kulipokucha, Patrick alikuwa amelala pembezoni mwa Neema na alijisikia vizuri sana, walijiona kamavile mapenzi yao ndio wametoka kutongozana. Waliamka wakitabasamu, na walipotoka chumbani walikuta Salome ameshawaandalia kifungua kinywa, kisha akawakaribisha mezani na kusema, “Baba, kuanzia leo naomba uhamie hapa” Patrick alicheka tu ila kicheko cha furaha kwani alijihisi kama amekuwa mtu mpya kabisa kwa siku hii na alikubaliana na kila jambo aliloambiwa na Salome. Rose aliamshwa na sauti ya mlinzi wake aliyemuomba kwaajili ya maongezi, alipotoka alimsalimia kisha Yule mlinzi akamwambia hoja yay eye kutaka kuondoka kwenye nyumba hiyo. “Jamani kwanini unataka kufanya hivyo?” “Mama siwezi, sijawahi kukukosea heshima hata mara moja mama yangu ila kwa hili naomba tu nirudi nyumbani, siwezi kuendelea kuishi humu ndani” “Jamani nimekuzoea ujue Lazaro, sipendi unavyosema unaondoka. Nitakuongezea mshahara ila usiondoke hapa nyumbani kwangu” “Mama, hapana acha tu nirudi kwetu” “Tumetoka mbali Lazaro, kumbuka wewe ni mtu pekee unayefahamu vitu vingi kuhusu mimi, nakuomba Lazaro usiondoke. Kumbuka umeanza kukaa kwangu ukiwa kijana mdogo sana, tafadhali Lazaro usiondoke jamani” “Basi, naomba niruhusu niende nikasalimie tu halafu baada ya wiki nitarudi” Kuhusu hilo ikabidi Rose akubali ila wazo la Yule mlinzi ilikuwa akiondoka tu basi harudi tena, basi Rose akampa mlinzi wake hela baadhi na kuagana nae. Mlinzi alibeba kila kilicho chake kwani lengo lake lilikuwa ni kuondoka na kutokurudi tena kwenye nyumba hiyo, na kweli aliondoka eneo hilo na kwenda kupanda basi la kwenda kwao, ila alipofika tu stendi ya kwao na kushuka kwenye lile basi alijikuta yupo ndani kwenye nyumba ya Rose huku mizigo yake ikiwa pembeni. Itaendelea kesho usiku…..!!!!! By, Atuganile Mwakalile.

at 4:49 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top