KURUDI KWA MOZA: 30 Mishi akainuka pale ila cha kushangaza alitokea kwenye sebule ya kina Doto, na pale sebleni alikuwepo Kulwa, Sara na Ana wakinywa chai kwahiyo nao wakapatwa na mshtuko kumuona ndani kwao. Wakainuka wote kwa mshangao na kutaka kumfata ila Mishi akaanza kutafuta sehemu ya kutokea na bahati akauona mlango wa kutoka nje na kufungua akakimbia, wakataka wamfate maana hakuna aliyekuwa anaelewa kuwa imekuwaje vile yani kila mmoja alishikwa na uoga wa hali ya juu huku akishangaa mara gafla kabla hawajatoka nje akatokea Salome huku akicheka sana, wakajikuta wakisema kwa pamoja tena kwa mshangao, “Salome!!” “Ndio ni mimi, mnadhani mnaota?” “Umekujaje kimiujiza?” “Mbona huyo aliyeondoka hamkumuuliza kuwa amekujaje?” Wakamuangalia Salome, kisha wakamuacha na kwenda getini ambako walimkuta Mishi ndio akiishia getini kutoka, Ana alimfata mlinzi na kumuuliza, “Mbona umemuachia atoke?” “Sikumuelewa na yeye pia anaonyesha hajielewi, sijamuona kuingia ila nimemuona kutoka kwakweli sikumuelewa” “Na Salome yupo ndani” Mlinzi alishtuka sana kusikia kuwa na Salome yupo ndani wakati hakumuona akiingia, “Mbona sijamuona akiingia?” “Ndio ushangao hapo, Yule msichana ni mchawi hata naogopa kulala ndani ya nyumba” Muda kidogo Kulwa na Sara nao walitoka wakidai kuwa hawawezi kulala ndani ya nyumba yao maana Salome hakuwa mtu wa kawaida, basi wakakubaliana kuwa watoke nje hata waende wakakodi hoteli ya karibu na kulala huko, mlinzi alitamani pia kuondoka ila alihofia kazi yake huku akiwa na mashaka sana, aliwashuhudia tu wakipanda kwenye gari na kutoa gari nje kisha kuondoka zao. Mlinzi alikuwa na mashaka sana ila Salome alimfata Yule mlinzi pale getini na kumwambia, “Umefanya jambo jema sana kutokufatana nao” “Ila naogopa pia, hivi wewe Salome ni mtu wa kawaida kweli?” “Kwanini mimi nisiwe mtu wa kawaida?” “Sijakuona ukiingia ila gafla nakuona ukitokea ndani” “Yani hiyo tu ndio inafanya mimi nisionekane mtu wa kawaida? Mbona Yule msichana pia hukumuona akiingia na umemuona akitoka, je nae ni mchawi? Ila usiogope sana, hata mimi natoka siwezi kuendelea kulala humu ndani peke yangu” “Unaogopa?” “Ndio naogopa pia, mimi ni mtu wa kawaida kwahiyo kitu cha ajabu kama hivi kikitokea lazima niogope” Salome alitoka na kumuacha Yule mlinzi pale getini, kwakweli aliogopa sana huku akiangalia ile nyumba kwa uoga ila alijipa moyo sababu yuko nje kwahiyo alihisi lolote baya likitokea basi atakimbia. Mishi alikuwa na uoga wa hali ya juu maana hakudhania kama ingetokea muda angerudishwa kimaajabu kwakina Doto, kwakweli alichanganyikiwa sana. Njiani aliona vijana watatu alianza kukimbia huku akipiga kelele kwani alijua ni lazima angebakwa tu, ila wakati anakaribia nyumbani kwao walitokea vijana wengine na kumpiga teke kisha kuanza kumbaka, Mishi alipiga kelele sana na watu walijitokeza kumsaidia kisha wale vijana wakakimbia, wale waliomsaidia Mishi walikuwa ni ndugu zake, na walimrudisha nyumbani huku wakimpa pole na kumuonea huruma sana, mama yake alikaa karibu na binti yake chumbani kumpa moyo, “Yani mwanangu tulikumbwa na uoga wa hali ya juu ndiomana wote tulikuwa macho tukikutafuta, maana mwenzio alivyosema umetoweka kila mmoja alishikwa na mashaka hapa. Ilikuwaje mwanangu?” “Hata sielewi mama” “Ulitowekaje?” “Hata sielewi mama” “Haya ni maajabu sana mwanangu, sijui hata tufanye nini yani hadi naogopa. Hapa naogopa hata kulala” “Sio wewe tu mama, hata mimi mwenyewe naogopa hata kulala” “Ndugu zako wote hapo nje wapo kwaajili wamepata habari ya kutoweka kwako, wale mafirauni waliokuwa wanakufanyia kitendo cha kikatili hatujawapata mwanangu, yani tutawatafuta popote pale” “Mnadhani mtawapata mama? Hata msijisumbnue, kesho nitakupeleka mahali nilipopewa hii laana” “Laana! Umepewa laana kivipio mwanangu?” “Mama, ni aibu hata kusema ila nimepewa laana na binti mdogo kabisa yani nadhani yote haya yanatokea kwa laana yake. Mama nipo tayari kuolewa na mzee Juma” “Kheeee upo tayari kuolewa tena?” “Ndio, bora niwe mke wa mtu labda itapotea hii laana. Naomba niolewe mama” “Sasa mwanangu mbona gafla sana, na kwa huyo mtu tutaenda saa ngapi?” “Tutaenda kesho, lakini baada ya mimi kuolewa. Naomba ukaongee na mzee Juma kesho asubuhi mwambie nipo tayari kuolewa nae, iwe kesho, tufunge ndoa hata ya fasta ila niolewe tu mama” Mamake Mishi alimshangaa sana binti yake kwa maamuzi hayo ila kwavile hakujua ni kitu gani kilimsumbua binti yake huyo, ikabidi tu akubaliane nae kwani hata yeye tukio la binti yake kutoweka lilimshtua sana. Sara, Kulwa na Ana walifika kwenye hoteli moja ndogo kisha kulipia vyumba vitatu vya kulala kwani Ana na Sara bado ilikuwa haiivi kulala kwenye chumba kimoja, kwahiyo kila mmoja aliingia kwenye chumba chake kisha wakakubaliana kuwa asubuhi waamshane mapema ili wawahi kurudi nyumbani na waandae chakula cha kumpelekea mgonjwa. Cha kushangaza walipoamka kila mmoja alijikuta kwenye chumba chake nyumbani kwao, kwahiyo kila mmoja alikuwa na mshangao peke yake kuwa imekuwaje tena. Sara aliinuka na kuangalia vizuri, alikumbuka fika kuwa mara ya mwisho alilala kwenye chumba cah hoteli sasa imekuwaje kujikuta wamelala ndani kwao? Alikuwa na mashaka sana, akaamua kutoka nje na kwenda sebleni, ni kweli ilikuwa ni ndani kwao, muda kidogo alimuona Kulwa akitoka na Ana akitoka na wote wakiwa na mshangao huku wakiulizana, “Jamani imekuwaje?” “Labda tukuulize Ana imekuwaje!” Sara alisema hivyo ila hiyo kauli ilimkera Ana kwani ilionyesha wazi kuwa yeye ana nguvu za ajabu na ndio amefanya hivyo kwao, ila Ana aliwajibu kawaida tu “Jamani, mimi na nyie tulikuwa eneo moja kwahiyo swala la kuniuliza kuwa imekuwaje hata mimi sijui. Cha muhimu tumesharudi nyumbani basi tukamuandalie chakula kaka na tumpelekee hospitali” Ikabidi wakubaliane kufanya hivyo ingawa hawakujua kuwa ni chakula gani wataenda kumpelekea hospitali kwa wakati huo, na wakaona kuandaa itawachukua muda mrefu kwahiyo wakajadiliana kuwa waende tu hospiatali kisha wataenda kumnunulia chakula huko huko. Ikabidi waende kujiandaa tu muda huo, kila mtu alijiandaa upesi upesi kwani kila mtu alikuwa na mashaka kupita maelezo ya kawaida, na walipomaliza walitoka nje, walipofika getini mlinzi alishtuka sana na kuwauliza “Mmeingiaje humu ndani?” Hawakumjibu kitu kwani hata cha kumjibu kingekuwa ni kitu gani, ila mlinzi aliendelea kusema “Kwa stahili hii sidhani kama kuna umuhimu wa mimi kuendelea kulinda hapa, ikiwa watu wanavyoingia ndani siwaoni ila nawaona wakati wa kutoka tu” Wakina Sara hawakumjibu zaidi ya kumsalimia tu, kisha wakatoa gari na kuondoka zao. Walivyofika hospitali walimkuta ndugu yao akiwa anaendelea afadhali kidogo kisha wakamuuliza chakula cha kumletea, “Hapana msihangaike, Salome alikuja hapa saa kumi na mbili na kaniletea mtori. Kaninywesha hadi nimeshiba kabisa, Yule binti ana moyo wa huruma sana” Ana akadakia, “Ana moyo wa huruma wakati ndio chanzo cha kuungua kwako” “Ana nyamaza usitake niongee sana, yeye ni chanzo wakati chanzo ni wewe na mama, si wewe na mama ndio mmenimwagia maji ya moto! Unafikiri sikumbuki eeh! Nakumbuka vizuri, ni nyie ndio mmefanya niteseke hivi” “Mmmh basi yaishe, cha muhimu upone tu na uendelee salama” Wakaongea ongea nae pale na kumuaga kuwa wataenda tena mchana kumuona, naye aliwaitikia kisha wakaondoka na kuanza safari ya kumfata mama yao ambaye walimuacha kule kwa mganga. Nyumbani kwa Neema, siku hiyo alishangaa asubuhi asubuhi binti yake amepika na kuondoka halafu muda kidogo akarudi, “Kheee ulienda wapi Salome?” “Kaka yangu amelazwa” “Kaka yako!” “Ndio, mtoto wa Yule mama wa kule mke wa baba” “Kheee anaumwa nini tena” “Eti aliungua na maji ya moto” “Basin a mimi tutaenda wote kumuona mchana” Salome alimkubalia mama yake kuwa mchana wa siku hiyo ataenda nae kumuona hospitali, huku akionekana kushughulikia chakula cha mgonjwa. Yani Salome alikuwa akifanya vitu ambavyo alijua badae vitaleta majibu gani. Wakina Sara walienda hadi kwa Yule mganga ambaye walimuacha mama yao na walikuta bado mama yao akiwa ndani ya kile kibanda cha mganga kumbe kulipokucha bado mganga aligoma kumuhudumia kwahiyo alikuwa akimbembeleza, ilibidi watoto wake wamsubiri tu. Rose aliendelea kumuomba Yule mganga amsaidie, “Sasa wewe mganga unavyokataa hivyo, mimi atanisaidia nani? Maji yamenifika shingoni sasa” “Sijui nani atakusaidia kwakweli ila mimi siwezi, maisha yangu nayapenda sana. Watoto wangu bado wadogo, wengine wananitegemea kwakila kitu, sipo tayari kuwaacha. Nilikuwa nakupa moyo tu jana ila kukusaidia siwezi” “Inamaana na wewe unamuogopa huyo anayetutisha kwenye nyumba yetu!” “Wewe Rose una dawa nyingi sana, fanya dawa zako na wewe kuweza kutokomeza hali hiyo” “Ni kweli nina dawa nyingi lakini sijui jinsi ya kuzitumia” “Na mimi siwezi kukwambia namna ya kufanya na siwezi kukusaidia kwakweli, labda uende kwa waganga wengine” Rose alitumia muda mrefu sana kumshawishi huyu mganga ila jitihada zake ziligonga mwamba, ikabidi aanze kumfikiria mganga mwingine wakati akili yake imepata jibu juu ya mganga mwingine wa kwenda akaamua kufanya hivyo, ndipo alipotaka kutoka kwa mganga Yule ila alishangaa Yule mganga akimzuia na kumwambia kuwa atamsaidia, Rose alifurahi na kukaa chini ili kusikiliza Yule mganga atamsaidiaje, kisha Yule mganga akaanza kupiga tunguli zake, na alipomaliza akaanza kuongea nae, “Kwanza kabisa, Yule mtoto wako ambaye kaungua na maji ya moto hamtakiwi kumpeleka hospitali” “Mmmh mganga sijui kama watoto wangu watarudi tena hapa, kumbuka usiku sikuwaona au bado wapo nje?” “Sijui ila hutakiwi kumpeleka hospitali” “Basi ngoja nijaribu tena kuwatafuta” Rose alitoka mule kwa mganga huku akiwa na mawazo sana kuwa watoto wake walielekea wapi ila alishangaa kufika nje, kuona gari yake na watoto wake ndani ya gari na ilionyesha wazi walikuja kumfata mama yao. Alijiuliza kuwa mbona usiku wa jana hakuwaona, kwamaana hiyo waliondoka au imekuwaje hapo, hakupata jibu kabisa. Aliwafata na kuwauliza kulikoni mbona usiku wa jana hakuwaona alipotoka kwa mganga, Sara alikuwa wa kwanza kumjibu mama yao, “Mama tumekuja kukufata wewe, Doto kalazwa hospitali twende ukamuone” “Kwahiyo Doto mmempeleka hospiatali?” “Ndio mama” “Nyie watoto jamani mbona mnanitafutia ubaya!” “Ubaya upi mama? Doto yupo hospitali na tungemchelewesha tu tungemkosa, naomba twende mama” Rose alikuwa ameduwaa tu nje huku akiwa hajielewi kuwa afanye kitu gani, Kulwa alishuka kwenye gari na kumpakia mama yao kinguvu kisha akapanda kwenye gari na kuondoa gari hiyo. Rose alikuwa kimya tu kwani bado alikuwa akitafakari bila ya jibu, mganga kamwambia kuwa mtoto wake asipelekwe hospitali na huku washampeleka hospitali kwahiyo hata akienda kumbembeleza tena mganga ni kazi bure kwa wakati huo. Ikabidi atulie tu kwenye lile gari, na alijiuliza tena kuwa mganga alikuwa na maana gani kuwa mtoto wake asipelekwe hospitali! Bado hakuwa na jibu, hadi wanafika hospitali ilikuwa ni mchana tayari, ila walipofika walizuiliwa na kuambiwa kuwa muda wa kuona wagonjwa umeisha, ikabidi Sara aulize “Jamani mbona asubuhi mlituruhusu wakati muda ulikuwa umeisha?” “Asubuhi aliyewaruhusu aliwaruhusu kimakosa, njooni jioni ndio muda uko wazi” “Sasa mgonjwa wetu hajala” “Ameshakula, kuna ndugu yenu kashampa chakula. Atatoka muda sio mrefu” Yule nesi alisogea kidogo, na muda sio mrefu wakamuona Salome akiwa ameongozana na mwanamke mmoja, Rose alipomuangalia vizuri Yule mwanamke aligundua ni Neema ambaye ni mama yake na Salome. Salome na mama yake hata hawakuangalia upande, walikuwa wanaondoka tu ila Rose alimuita Neema, “Neema” Neema akageuka na kumuona kuwa ni Rose, uoga ukamshika kwani bado alikuwa anamuogopa Rose vilivyo, ila Rose alimsogelea Neema na leo kwa mara ya kwanza alimsalimia vizuri kabisa, “Hujambo Neema” “Sijambo shikamoo” “Mbona unaniogopa hivyo!” Salome akadakia, “Anakuogopa sababu umezoea kumtishia” Neema alimkatisha mwanae kuwa asiendelee kuongea maneno hayo, Rose alimwambia Neema “Sina ugomvi na wewe na nimefurahi kukuona. Natumai umetoka kumuona mwanangu, mwanao pia nimempokea vizuri kwenye nyumba yangu ila mwanao ni mshirikina” Neema akashtuka “Mshirikina!” Salome akacheka sana, kisha akamshika mama yake mkono na kumlazimisha kuwa waondoke eneo hilo, ila Neema alikuwa mbishi kufanya hivyo. Salome alimwambia mama yake, “Mama, sijakuleta hapa kuja kubishana na huyu mtu. Halafu nina mambo mengi ya kufanya siku ya leo, tafadhali tuondoke nyumbani” Neema alikuwa mbishi mbishi kwani bado alitaka kusikia kuwa kwanini mwanae kaitwa mshirikina ila ikabidi akubaliane tu na mwanae kuwa waondoke, ambapo salome alikodi bajaji iwapeleke nyumbani kwao ila kitendo cha Salome na mama yake kuondoka na ile bajaji, Rose alienda kuwaomba watoto zake kuwa waifate hiyo bajaji hadi wajue wanapoishi Salome na mama yake, kwahiyo walifanya hivyo na kuanza kuifatilia ile bajaji. Nyumbani kwakina Mishi mamake alipoenda tu kumwambia mzee Juma kuhusu maamuzi ya Mishi wala hakubisha Yule mzee kwani siku zote alitamani Mishi akubali amuoe ukizingatia kashakula hela zake nyingi sana, kwahiyo hakutaka hata kupoteza muda ni siku hiyo hiyo akaita watu na kumuoa msichana huyo, ilifungwa tu ndoa ya kawaida yani haikuwa na shamra shamra zozote kwani ni ndoa ya haraka halafu haikupangwa ila Mishi alifurahi kuolewa na mzee huyu na hakumwambia kama alibakwa au alikutwa na matukio yaliyomfanya akubali kuolewa nae, ingawa alikuwa akijiuliza sana kuwa inakuwaje kuwaje mambo hayaeleweki kabisa. Alipomaliza kufunga ndoa, akatembelewa na mgeni na kuambiwa kuwa kuna mgeni wake, alitoka kwa mashaka sana kwani bado hakuwa na imani na jambo lolote na uoga ulikuwa umemtawala. Alipoenda kuzungumza nae alishangaa kuwa ni Salome, akataka hata kurudi kwa ndugu zake ila alishangaa miguu yake ikigoma kufanya hivyo, kisha Salome akaanza kuongea nae, “Usiniogope mimi sio mla watu, wala sio mchanganya wanaume kama wewe” Mishi alikuwa kimya tu akimsikiliza, “Umefanya uamuzi wa haraka sana kuolewa, hivi unajijua kama hapo ulipo una mimba? Au unataka hiyo mimba umsingizia Yule mzee wa watu?” “Nina mimba ya nani?” “Mi nitajuaje na umebakwa na watu wengi. Unajua wakati wa kubakwa ni vigumu kujizuia tofauti na ukitaka mwenyewe, sasa vipi unataka kumsingizia mzee wa watu!” “Hapana sikuwa na nia hiyo ila nimeamua tu kutoka moyoni kuolewa” “Kama umeamua kutoka moyoni mwambie ukweli, Yule mzee anakupenda na atakuelewa tu. Halafu kama umeamua kweli kwa moyo wako, tulia na mumeo. Ni mwanaume gani anaweza kukubali kufunga ndoa ya haraka haraka kiasi hiko? Anakupenda mwenzio, ni wa kawaida tu Yule hata sio mtu mzima kihivyo, mpende sababu umeamua mwenyewe uache tabia ya kuumiza moyo wake” “Nimekuelewa na ninakuahidi nitampenda sana na nitamwambia ukweli wa kila kitu” “Usiniogope, mimi ni binadamu wa kawaida tu kama wewe. Kwavile umesema utatulia kwa mumeo, naifuta laana yangu kwako” Salome aliondoka, na Mishi alikuwa anamuangalia hadi alipoishia, hata alipoulizwa na mama yake kuwa mtu huyo alikuwa anaongea nae nini bado hakuweza kumjibu kwani kwake bado lilikuwa ni swala la aibu. Wakiwa ndani ya bajaji, Neema alimshangaa mwanae amelala mpaka wanafika nyumbani ndio anamshtua kuwa washuke na waingie ndani, walipoingia ndani mara na wao wakina Rose walikuwa wamefika ila Salome alifanya jambo na kumfanya mama yake kuingia chumbani ili wakigonga mlango wa sebleni wasimkute mama yake na wamkute yeye. Basi kweli wakagonga mlango wa sebleni na kusikia sauti ya Salome ikiwakaribisha, “Fungua mlango ingia” Basi wakafungua na kuingia, Rose alikuwa wa kwanza kuingia mule ndani ila alishtuka sana kwani alijiona yupo nyumbani kwake na aliyewakaribisha alikuwa ni Patrick na sio Salome. Itaenmdelea kesho usiku……!!!!! By, Atuganile Mwakalile.

at 4:48 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top