KURUDI KWA MOZA: 29 Doto alimuangalia Salome kwa hasira sana kwani alionekana ni msichana mdogo ila aliyekuwa na amri zaidi, ila bado alikuwa hajielewi elewi hata alivyorudishwa nyumbani na kumuuliza swali Salome bado hakuelewa kabisa, akataka kutoka tena nje ila kabla hajatoka akamuona mama yake akiwa na Ana wakija kwa kasi sana na wameshika sufuria la maji ya moto na kummwagia Salome, ila muda huo huo alishangaa kuona kuwa yale maji kumbe alikuwa anamwagiwa yeye na sio Salome, alijikuta akipiga kelele za maumivu. Rose na Ana walistaajabu pia kwani hakuna aliyedhania kuwa yale maji yangemmwagikia Doto, kitendo cha Doto kupiga kelele kiliwafanya watupe sufuria na kwenda kumshikilia hata Sara na ndugu yake Kulwa walikuja kwa kasi ya ajabu kwani kelele za Doto ziliwashtua hadi mlinzi getini aliingia ndani kuona kuna nini tena maana zile kelele hazikuwa za kawaida. Sara alimkuta mama yake amemshikilia Doto huku nae analia pia, Sara akauliza “Kuna nini?” “Nenda kachukue funguo ya gari tumpeleke Doto hospitali” Sara akaenda chumbani kwa mama yake kuchukua funguo kisha kurudi nazo, ambapo mama yake aliwaomba wasaidiane kumkokota Doto mpaka kwenye gari ili wampeleke hospitali. Wakati huo Salome alikuwa pembeni tu kanakwamba haoni tukio linalotokea ila alikuwepo na alikuwa akiwaangalia tu, walimpakiza Doto kwenye gari kisha nyumba nzima wakaenda kumpeleka hospitali kasoro Salome na mlinzi ambaye anabaki kulinda nyumba. Walipoondoka, huyu mlinzi alimshangaa sana Salome na kumfata kumuuliza, “Mbona unaonekana hujali kabisa! Utafikiri kitu hakijatokea ndani, yani kama mtu ambaye hujui kinachoendelea” “Ulitaka nifanyeje” “Yani huonyeshi kujali kabisa, wenzio wote wameenda hospitali kasoro wewe” “Mbona na wewe hujaenda?” “Mimi ni mlinzi” “Ila unajua kwamba mimi naweza kufika hospitali kabla yao? Ila wale hawaendi hospitali kwasasa” “Wanaenda wapi?” “Wakirudi watakwambia walipoenda” “Unajua wewe sikuelewi toka siku umefika hapa” “Na kamwe hutokaa unielewe” Kisha mlinzi akaamua kwenda kuendelea na kazi yake kwani kiukweli hakumuelewa kabisa Salome na muda wote alimuona kama mtu wa ajabu. Wakiwa ndani ya gari kwenda hospitali, walienda mwendo mrefu sana na kuona hospitali kisha wakashuka ila wakashangaa tena hapakuwa hospitali ila ni kwa mganga. Rose alikumbuka kuwa huyo ndiye mganga aliyekuwa akizungumza na Ana kuwa ataenda kwa huyo, watoto wake walimuuliza kwa mshangao, “Mama vipi tena, mbona hapa sio hospitali? Panaonyesha ni kwa mganga” “Hata mimi mwenyewe sielewi tumefikaje hapa, ila nadhani ni Mungu katuleta kwani mganga huyu nilikuwa namuhitaji sana bora tuingie tu” Ana alimuangalia mama yake na kumtahadhalisha, “Mama tulisema tunampeleka kaka hospitali, ila hatukukubaliana kumleta kwa mganga. Sidhani kama tupo sehemu sahihi” “Mwanangu Ana, usiwe na mashaka. Acheni mimi niingie kwa mganga maana huu ni uchawi aliofanyiwa Doto” “Ila mama kumbuka kuwa yale maji tuliyopanga kuyamwaga hayakuwa ya kichawi, tunamuumiza Doto ujue, bora tumpeleke hospitali” Hapa ndio wengine wote wakaelewa kuwa mama yao na Ana wanafanyaga uchawi ndiomana wamesema maji waliyoyamwaga hayakuwa ya uchawi. Rose alikuwa mbishi sana, kwavile tayari alishafika kwa mganga kwahiyo aliona ni vyema kuingia kwa mganga na kuzungumza nae. Rose alivyoingia kwa mganga, Ana akawapa ushauri ndugu zake kuwa wampeleke Doto hospitali kwakweli hata wao walishangaa sana kuwa moyo wa Ana umebadilika kiasi kile, Kulwa aliingia kwenye gari kisha wote kupanda kwenye gari na kuanza kuulizia kwa watu waliowaona pale njia ya kuelekea barabara kuu na kuulizia hospitali. Rose hakujua kama amebaki mwenyewe kwa Yule mganga, kisha akaanza kumueleza matatizo yake, “Yani hapa nilipo, mwanangu kaungua na maji mwili mzima. Naomba unisaidie, ni kweli maji nimemmwagia mwenyewe ila lengo langu ilikuwa ni kummwagia mtu mwingine ila eti akamwagikiwa yeye, si nifanyiwa mambo yasiyofaa hayo babu” “Sikia Rose, unajua kwamba wewe ndio chanzo cha wale waganga wawili waliokufa, yani wote walitaka kukusaidia wewe wakafa. Sasa umekuja na kwangu unataka kunimaliza na mimi!” “Hapana, ila nahitaji maisha yangu yarudi kama zamani. Nahitaji kufurahia tena maisha, ona mume wangu hataki hata kuniona na hata sijui akija siku na hasira zake atanifanya nini, dawa zangu hazifanyiki. Nyumba yangu ila siwezi kufanya chochote utafikiri sio nyumba yangu” “Kwanza niambie umefikaje leo hapa” Rose akamuelezea kwa kifupi kuwa walikuwa wakimpeleka mwanae hospitali ila wakashangaa wamefika hapo, “Hata hukugundua kuwa umebadilishiwa njia, badala ya kwenda hospitali ukaja huku! Na kama ameweza kukubadilishia njia huyo mtu basi ujue kuwa anauwezo wa kuzunguka na wewe kila mahali, kwahiyo tunaweza tukapanga dawa mimi na wewe ila akawa ameshatusikiliza yote. Huyo mtu lazima anajua kuwa unapenda sana waganga ndiomana amekuleta kwangu kwa makusudi kabisa” “Babu, nahitaji kujua ni mtu gani huyo anayenifanyia vitu hivi?” “Mfano ukishamjua, utafanyaje?” “Tumshughulikie” Basi Yule babu akaanza kupiga ramli zake kwa muda kidogo kisha akatulia na kumwambia, “Siwezi kukwambia nimekatazwa” “Jamani babu, umekatazwa na nani?” “Sikia Rose nikwambie kwa usalama wako, rudi nyumbani kwako na ukiona kuna mtu nyumbani kwako anakuelekeza sana basi fatilia anachokiataka mtu huyo” “Mtu anayependa kunifatilia nyumbani siku hizi ni mmoja tu, na tangu amefika nyumbani kwangu ndio mambo yamebadilika simpendi hata kidogo ila sidhani kama ana nguvu za kichawi kiasi kwamba aniumize mimi” “Kwanza unajua kama muda umeenda sana, na usiku umeingia. Huwa sifanyi kazi usiku ila alfajiri ndio muda mzuri kwangu” “Kwahiyo unanishauri nije kesho” “Ndio njoo kesho” “Bora nilale hapa hapa na wanagu ili niwahi kesho” Rose hakuwa na wazo la haraka haraka kuwa Doto anahitajika hospitali kwani alichowaza yeye ni kutibiwa na mganga tu. Basi akatoka nje ili akawaambie watoto wake ujumbe wa mganga ila hakuwakuta, alishtuka sana kwani hata gari hakuikuta na vitu vyake vyote aliviacha kwenye gari. Akarudi tena kwa mganga, ila mganga alimshauri alale hapo hadi asubuhi ili waangalie watoto wako wapi, Rose hakuwa na namna zaidi ya kukubali tu. Neema nae alifika usiku na familia yake yani wale watoto wake mapacha, akiwa amechoka sana ila alikuta ndani kwake kama kuna mtu na kuhisi ni Salome, kisha akagonga mlango na kweli Salome alienda kuwafungulia na kuwapokea huku akionyesha tabasamu zito sana. Neema alikaa na kuzungumza na mwanae, “Hukuondoka kabisa nini toka siku ile?” “Niliondoka mama” “Sasa umejuaje kama leo ndio narudi?” “Sikujua ila huwa narudi kila jioni, halafu nikahisi kama mnarudi vile ndiomana nikapika kabisa” Neema alitulia tu ila huyu Salome wake wa kipindi hiki alikuwa akimshangaza sana, kwanza Salome wake ni muoga ila kaweza kulala hapo nyumbani kwa siku zote alizokuwa safarini, halafu Salome wake alikuwa mvivu ila huyu kazi zote anafanya, kama hapo kawapikia kabisa kwahiyo walienda kujimwagia maji tu na kula huku akimpa salamu Salome za kutoka kwa bibi zake na ndugu zake wengine, “Ila wamekukumbuka, haswaaa bibi yako anaomba uende ukamsalimie” “Nitaenda tu hata wasijali” “Ila mwanangu umebadilika sana” “Kwanini mama?” “Ulikuwa mvivu sana zamani, yani kama leo ningekuta hujafanya chochote. Halafu ulikuwa muoga sana yani ningekuta umeenda kuishi kwa marafiki huko” “Nimekuwa mama” “Amakweli umekuwa sasa” Aliongea ongea nae kisha akamuaga na kwenda kupumzika huku wadogo zake Salome wakiwa wamelala muda tu walipomaliza kula kutokana na uchovu wa siku hiyo. Basi Salome nae akaenda chumbani kwake, kwahiyo ilijulikana kuwa nae amelala. Kwenye mida ya saa tano usiku ndio Sara, Ana na Kulwa walirudi nyumbani na kumuacha Doto akiwa amelazwa hospitali, kwahiyo walifika wakiwa wamechoka sana. Mlinzi aliwauliza kuwa imekuwaje huko hospitali, “Amelazwa, ni ameumia sana” “Eti Salome alisema hamuendi hospitali” Ana akauliza, “Yeye Salome yuko wapi yani huyo msichana ni nuksi tena nuksi kabisa. Ni kweli hospitali tumeenda badae maana mwanzoni tulijikuta kwa mganga. Hivi wewe unamuonaje huyu Salome, kwanza yupo?” “Hayupo, ametoka” “Basi nitakuja tuongee vizuri” Mlinzi alishangaa sana kwa Ana kuongea vizuri vile na yeye kitendo hicho kilimshangaza sana ingawa mambo ya Salome ndio yalikuwa yanamshangaza zaidi. Waliingia ndani huku wakiamini kwa vyovyote vile mama yao amebaki kwa Yule mganga, walitamani kumuuliza Ana ila walimuogopa maana ana muda wake wa kubadilikia watu. Ana aliwaacha ndugu zake ndani na kutoka tena kwenda kuongea na mlinzi wao. “Hebu niambie, kwanza wewe unamuonaje huyu Salome!” “Kwakweli sijui nisemaje ila simuelewi yani huwa simuelewi kabisa kabisa” “Unahisi anaweza akawa ni mchawi?” “Inawezekana maana haeleweki kabisa. Na mama mmemuacha wapi?” “Yani habari ya mama sijui tukuelezeje ila kwa kifupi amebaki kwa mganga. Hivi mtu akitaka kuacha uchawi anafanyaje? Anaenda kwa mganga kutolewa au anafanyaje?” “Kwa mganga ni kuuzidisha uchawi sijui sasa mtu anawezaje kuacha uchawi, unataka kumpeleka Salome?” “Hapana, kuna jambo nataka kulifanya. Utalijua tu” Kisha Ana akarudi tena ndani na kuwaona dada yake na kaka yake pale wakijadiliana na kukubaliana kesho wawahi hospitali kisha waende kumchukua mama yao maana hakuna aliyejua kuwa mama yao atarudije ila kitu pekee walichojua ni kuwa yupo kwa mganga wa kienyeji. “Sasa basi tuchemshe chai tunywe tu na ile mikate tuliyonunua” “Ndio tufanye hivyo hakuna namna” Kwahiyo Sara akaenda kuandaa chai ili waweze kunywa. Mishi akiwa ndani kwao, mara alijiwa na rafiki yake ule usiku, ikabidi atoke kumsikiliza, “Mmmh mbona usiku sana, saa sita kasoro hii!” “Ni usiku kweli ila sijaweza kulala na habari hii” “Habari gani?” “Leo nilikuwa hospitali kumuona ndugu yangu, gafla nikaona kuna mgonjwa analetwa na ameungua vibaya vibaya ndio wametoka kumfunga funga mabandeji na kumpaka dawa, kila mtu kashikwa na huruma pale, ikabidi nimsogelee kumpa pole. Jamani ni Doto Yule mpenzi wako” Mishi akashangaa sana na kumuuliza rafiki yake, “Una uhakika ni Doto?” “Ndio ni Doto maana nilisikia ndugu zake wakimuita Doto” Mishi alikaa kimya kwa muda kwanza kwani tukio la Doto lilimshangaza toka muda alikuja kuongea nae, akakumbuka kuwa alienda pale kuongea nae ila alitaka kumpiga kibao na mara hakumuona huyo Doto mwenyewe halafu muda huu anapata habari kuwa Doto ameungua na maji ya moto haikumuingia akilini kabisa. “Au Doto amekufa, aliyekuja kwangu huku ni mzimu!” “Hapana hajafa bhana, ni mzima ila ameungua sana” “Unajua watu kufa huwa wanachelewa chelewa kidogo, usikute amekufa anangoja tu muda wa kufa kabisa hapo” “Kwanini unasema atakuwa amekufa?” “Sababu Doto alikuja kuongea na mimi jioni jioni hivi na akataka kunipiga mara gafla akatoweka hata nikaogopa” “Alitoweka?” “Ndio alitoweka” “Alitowekaje?” “Hata sijui nikuelezee kwa namna gani ila alitoweka” “Inawezekanaje mtu atoweke jamani? Mbona haiwezekani au ulikuwa unaota Mishi! Na kwanini alitaka kukupiga?” “Hakuna kitu bhana, ila endelea kushangaa kutoweka kwake” Mishi akainuka pale ila cha kushangaza alitokea kwenye sebule ya kina Doto, na pale sebleni alikuwepo Kulwa, Sara na Ana wakinywa chai kwahiyo nao wakapatwa na mshtuko kumuona ndani kwao. Itaendelea kesho usiku……!!!!! By, Atuganile Mwakalile.

at 4:48 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top