KURUDI KWA MOZA: 27 Wakawa wanacheka pale, mama yao nae alitoka sebleni wakamsalimia akaitikia na kutaka kwenda nje. Ila Salome alimuuliza, “Mama, unataka kwenda wapi?” “Safari zangu hazikuhusu” Rose akataka kufungua mlango, ila kabla hajafungua Salome alimwambia, “Usihangaike, mgeni wako nimekuletea” Kisha Salome ndio akaenda kufungua mlango na mara akaingia Yule mganga. Kwakweli Rose alishangaa sana alijikuta akikaa chini kabisa kwani hakuelewa kabisa kinachoendelea na aliona kiini macho kikifanya kazi vilivyo, ila Salome akamwambia Rose, “Sasa umeshtuka nini? Unakosa raha kwanini? Si nio ulikuwa ukimuhitaji huyu! Ulitaka hadi kwenda kutuma dereva wa kumfata, mimi nimekuletea eti unaishiwa nguvu kabisa” Rose hakujibu chochote ila Yule mganga aliingia na kukaa pia, halafu akamuangalia Rose na kumsalimia, “Habari za tangu jana” Rose akajibu, “Mbaya” Salome aliwaambia watoto wengine wa Rose wamuache mama yao aongee na mgeni, “Kwetu nilifundishwa kuwa mama anapopata mgeni natakiwa kuondoka na kumuacha mama anazungumza na mgeni, kwahiyo kitendo cha kukaa hapa wakati mama kapata mgeni sio picha nzuri” Basi nao wakasikiliza ushauri wa Salome kisha kila mmoja kuinuka na kwenda zake chumbani ila Salome alienda kwenye sebule ambayo wale mapacha walipenda kuitumia kwa sana. Rose alibaki sebleni na Yule mganga, kisha akamuangalia kwa makini kwani alihisi kama ni kiini macho, akamuuliza “Hivi ni wewe au ni nini?” “Ni mimi ndio” “Umefikaje hapa?” “Niliona yaliyokutokea usiku wa jana, kwahiyo leo mapema nikaanza safari ya kuja huku. Ni sababu tulishakuja mwanzo kwahiyo nilishika njia” “Ulishika njia vile tumekuja na kurudishwa kimaajabu?” “Ndio nilishika njia, kwahiyo huniamini kuwa ni mimi!” “Nakuamini ila mambo yamenichanganya sana, unajua umekuja kiajabu ajabu mpaka nimeshangaa. Kwahiyo tutafanya dawa siku ya leo?” “Ndio tutafanya dawa, ila kwanza ukanionyeshe kila kitu ambacho huwa unatumia kwenye mambo yako” Rose akafikilia kidogo kisha akakubali kwenda kumuonyesha kwahiyo yeye na Yule mganga wakahamia ndani na baada ya muda walitoka na kuondoka kabisa pale nyumbani, na Rose alimuaga mwanae Ana tu kuhusu anapoenda na Yule mganga. Baada ya muda watoto wa Rose walirudi sebleni na siku hii Salome aliwaandalia chakula cha kuwafurahisha sana, hadi wakawa wanamsifia haswa wale mapacha, “Yani wewe Salome ni binti mdogo ila unajua kupika kila chakula jamani halafu unapika vizuri balaa” Kisha Doto akamuangalia dada yake Sara na kumwambia, “Dada na wewe ujifunze kupika jamani, kwa staili yako utaolewa kweli wewe!” “Aliyekwambia anataka kuolewa nani, hebu nitoleeni balaa” “Basi dada usichukie kiasi hiko jamani, leo wifi yako anakuja. Nishampigia simu kumuelekeza kwahiyo akafika tu nitaenda kumchukua nje na utamuona na hakika utamfurahia” “Bora uongelee mada za hivyo sio kuniletea mada za upishi upishi kama sijui kupika ni mimi msinilazimishe” Sara alionekana kuchukizwa kabisa na swala la kuambiwa kuwa atakosa mume sababu hajui kupika, na kujikuta akimkumbuka Ommy ambaye alijua wazi kuwa Sara hajui kupika ila alionyesha kumpenda hivyo hivyo, ila akakumbuka kuwa Ommy kafichwa na uchawi wa mama yake na kujikuta akikumbuka kuwa Ommy alimsaliti na mtu mwingine, kila alipokumbuka Ommy ni msaliti basi huruma yake kwa Ommy ilipotea muda huo huo. Alikuwa kimya kwa muda hadi Salome akamshtua, “Unawaza nini dada Sara?” “Niache tu” “Pole sana, mapenzi yanaumiza eeh! Ila bado, utaona yanavyoumiza zaidi” “Kivipi Salome mbona sikuelewi” “Utanielewa tu, mapenzi yanaumiza sana ila kuna jambo linaweza kutokea ukajihisi labda utapata unafuu wa moyo ila ukashangaa unafuu hupati zaiddi ya maumivu” Wale mapacha nao wakaingilia hizo stori, “Jamani achene hizo habari za kuumizwa na mapenzi, wengine hatutaki kusikia kabisa. Ziacheni bhana, kila mtu ashughulike na penzi lake” Salome alitabasamu tu kisha akaenda tena kwenye ile sebule ambayo mapacha wa Rose huwa wanapenda kukaa. Kwa upande wa Ana alikuwa chumbani kwake tu toka mama yake katoka na Yule mganga kwani yeye alijikuta akiwaza kuwa ni mtego tu mama yake kawekewa maana hakuwa na wazo kuwa Yule ni mganga waliyoendaga kabisa, “Na kama ni yeye amewezaje kuja mapema hivi ukizingatia kule anakotoka ni ndani ndani sana? Nina mashaka” Akajaribu nae kukaa akifanya fanya dawa zake huku akiwa amejifungia kabisa kwenye chumba chake, hakutaka kabisa kuongea na mtu yeyote kwa muda huo. Wakiwa pale sebleni Sara na kaka zake, basi kaka yake akasema kuwa mchumba wake amefika kwahiyo akaenda kumpokea kwahiyo Sara na kaka yake mwingine wakabaki wenyewe wanamsubiri huyo wifi kwa Sara na shemeji kwa Kulwa. Ila Sara alimuuliza kaka yake, “Vipi unamjua huyo mchumba wa Doto?” “Hata simjui kabisa, Doto msiri sana hajawahi kunionyesha hata mara moja huyo msichana wake” “Wewe je umeshawahi kumuonyesha wa kwako?” “Hapana, mimi mwenyewe sijawahi kumuonyesha hata mara moja ila nimepanga siku nimtambulishe hapa nyumbani. Hata leo nilitamani aje pia ila kaniambia amepata udhuru” “Sawa” “Na wewe wako? Najua ni Ommy ila sijamuona siku zote hizi” “Achana na huyo mtu, kwanza ananiumiza kichwa tu. Yani mapenzi yameniumiza kweli mimi, kumbe Ommy alikuwa ananisaliti, kunionyesha kote upendo kule kumbe amepata kasichana kengine ananisaliti nako. Siku niliyogundua niliumia sana” “Kwahiyo Ommy yuko wapi?” “Achana nae bhana, atajijua mwenyewe alipo” “Mmh dada jamani, unajua mtu akikusaliti unatakiwa kuwa mpole kwanza, ujue ni kwanini amekusaliti sio kuweka hasira mbele” Sara alianza kukohoa na kumuomba kaka yake huyu akamchukulie maji ya kunywa, “Mmmh maneno yangu yamekufanya upaliwe, basi pole. Ngoja nikakuchukulie hayo maji” Basi Kulwa akainuka na kwenda kumchukulia maji ya kunywa Sara, ila muda huu huu Doto nae alikuja na kuingia ndani kisha akamwambia dadake asimame kumkaribisha mgeni maana ameshafika, “Mmmh kama tunamkaribisha raisi jamani! Kumbe utamu wa mtu” “Acha maneno yako Sara bhana” Basi akamkaribisha Yule msichana ndani, ila Sara alipoangusha macho yake kwa Yule msichana alishtuka sana kwani alikuwa ni Mishi, alijikuta akimuuliza kaka yake kwa umakini huku akifikicha fikicha macho, “Kaka, mwanamke mwenyewe ndio huyo?” “Ndio, kwani vipi mzuri eeh!” Sara alifikicha tena macho yake, ila kabla hajasema chochote Kulwa nae alikuwa ametoka jikoni akiwa na glasi ya maji ila alipomuona shemeji yake huyo, alihamaki na kumuita kwa mshangao, “Mishi!!!” Mishi aliangalia kwa aibu sana, na hakuongea lolote zaidi ya kufungua mlango wan je na kuondoka kuelekea getini, alifika getini na kutoka ila alivyotoka tu alijishangaa akijikuta tena yupo pale pale sebleni halafu mara Salome nae alitoka kwenye ile sebule nyingine akicheka, na kuwakuta pale sebleni huku Mishi akiwa anashangaa shangaa, kisha Salome akasema, “Sasa Mishi unashangaa shangaa nini? Unaona kama maajabu eeh! Wakati unatenda vitu vya namna hii hukujua kama ni maajabu ya namna hii yangetokea mbele yako? Unataka kukimbia uende wapi na ukimbie kwasababu ya nini? Kaa hapo ujieleze, ni kwanini umechanganya ndugu hawa” Doto alikuwa na hamaki tu na kujikuta akimuuliza Kulwa, “Kwani huyu msichana unamfahamu?” “Nio huyu nilisemaga mchumba wangu mwenyewe, leo nilitaka anitembelee pia akasema ana kazi kumbe ananichanganya na pacha mwenzangu!” Sara nae akadakia na kutoa dukuduku lake la moyoni, “Yote tisa, kumi ni kuwa huyu dada ndio kidudu mtu aliyekuwa anatembea na Ommy hadi moyo umeniuma sababu yake” Wote wakashangaa kuwa Mishi amewachanganya kiasi kile, Doto akajikuta akimwambia, “Yani kukuhudumia kote kule Mishi bado ulikuwa unanichanganya na ndugu yangu!” Mishi alikuwa kimya kabisa kwani aibu aliyoipata leo hakuitegemea kabisa, Salome nae akaongea, “Yani sio kwamba wewe Doto ulikuwa ukimuhudumia peke yako, ni hivi huyu binti wote mmeshiriki kumuhudumia. Kulwa pia umemuhudumia sana huyu binti, halafu hata Sara umemuhudia sana maana hela zote ulizokuwa unampa Ommy alikuwa anapeleka kwa huyu binti. Haya sasa nirudi kwako wewe fundi wa kuumiza mioyo ya watu, hivi hukuwahi kuwaza kuwa mambo unayoyafanya ipo siku utaumbuka? Hivi ni bahati za watu wangapi umezifunika wewe mmoja? Yani wewe utembee na Kulwa, wewe utembee na Doto na wewe utembee na mwanaume wa dada yao, kwahiyo umechanganya familia vilivyo” “Nisameheni sikujua kama ni ndugu” MIshi alipiga magoti, na kumfanya Salome acheke sana na kusema, “Kwahiyo kama si ndugu ni sawa kuwafanyia hivyo? Mwanzoni nilijua ni Ommy anakudanganya kumbe ni wewe unaewadanganya wenzio, hivi ungefanyiwa wewe hivi ungejisikiaje?” “Nisamehe jamani, nisameheni” Sara alikuwa na hasira sana na huyu Mishi, hata wale mapacha nao walikuwa na hasira nao vilivyo wakatamani wote wamvamie na wampige ila Salome aliwakataza na kwenda kumkinga Mishi ili wasimpige. “Tafadhalini jamani msimpige wala msimuumize, mwacheni jamani nataka huyu atembee na laana yangu” Doto alikuwa na hasira sana, ila Salome alimzuia kabisa kumpiga mishi yani alijikuta akiganda tu bila kumpiga. Salome alifungua mlango na kumruhusu Mishi aondoke ila akamwambia, “Kumbuka utatembea na laana yangu siku zote, leo utafurahi sana kuwa umewachanganya ndugu lakini hujafanywa lolote ila utatembea na laana yangu siku zote. Laiti kama ningekuwa wewe nisingeondoka leo ila ningekesha nikiomba msamaha” Mishi hakutaka kusikiliza sana kwani alitoka muda huo huo na hakutaka tena kubakia kwenye nyumba hiyo kwani alijiona kama anamkosi kwa siku hiyo. Kwakweli si Sara wala wale mapacha waliofurahishwa na kitendo kile kwani kila mmoja alienda njia yake mule ndani akiwa na mawazo yake, haswa Doto alihisi kudhalilishwa sana na Yule mwanamke, kwahiyo sebleni alibaki Salome peke yake. Mishi alitumia muda mrefu sana kufika kwao, hata akashangaa kuwa imekuwaje tena wakati ametoka kule muda mrefu. Wakati akitembea aliona usiku umeingia, mara alikatisha kwenye njia hiyo na kujiona yupo mwenyewe hadi akaogopa na kujiuliza, “Hii njia leo vipi jamani? Imekuwaje yani sioni watu!” Mara akashikwa bega, kugeuka ni chizi alikuwa amemshika bega, alishtuka sana na kuanza kukimbia ila Yule chizi alimzidi nguvu na kuanguka chini halafu akapiga kelele lakini hakuna mtu yeyote aliyeonekana kumsaidia hadi Yule chizi akambaka halafu akamwambia, “Asante sana kwa penzi lako” Yule chizi akaondoka zake na kumuacha Mishi akilia sana, muda kidogo walitokea vijana wawili ambapo Mishi alipowaona aliwaita na kuwaomba msaada kwahiyo wakamuinua Mishi pale chini huku wakimpa pole “Pole sana dada, ila saizi saa saba usiku mtoto wa kike unatafuta nini njiani?” Mishi alishangaa sana kuwa ni usiku wa saa saba wakati aliondoka mapema sana kwakina Doto, “Jamani nisaidieni jamani, sikujua kama ni usiku sana saa hizi” Wale vijana waliondoka na Mishi ila njiani nao wakamgeuka na kumbaka, kwakweli siku ya leo ilimfanya Mishi achanganyikiwe kabisa kwani walimbaka kwa nguvu hadi akazimia pale pale. Rose alirudi nyumbani kwake usiku, na kwenda chumbani kwa Ana moja kwa moja ili ampe habari ya kitu alichofanya na Yule mganga. Ila cha kushangaza kabla hajamueleza chochote, Ana alianza kusema, “Mama ila sina imani na Yule mganga uliyeondoka nae. Naogopa hata usiniambie ambacho umefanya na Yule mganga maana sina imani nae kabisa. Simuamini Yule mganga mama” “Usiseme hivyo mwanangu, nimefanya nae vitu vingi sana” “Ndio mama ila sina imani nae, kwanza ujio wake wa kiajabu ajabu sina imani nae kabisa” “Mwanangu lakini kanirekebishia vitu vingi sana, utaona mabadiliko kuanzia kesho” “Kabla ya hayo mabadiliko, naomba kesho asubuhi twende kwa huyo mganga tujue mbivu na mbichi mama manake sina imani kabisa hapa” “Kwahiyo hutaki nikueleze chochote ambacho kimetendeka leo” “Hata usinieleze na wala usiniambie ulipokuwa siku ya leo, sina furaha kabisa na sidhani kama ulipokuwa palikuwa ni pema” Ikabidi Rose akubaliane na mwanae kuwa ataenda nae kesho yake kwa Yule mganga, ingawa yeye binafsi alikuwa ameridhika kwa huduma ambazo alifanyiwa siku hiyo na Yule mganga, kwahiyo akaenda chumbani kwake baada ya kumaliza maongezi na Ana. Ila siku hiyo Ana hakuweza kulala kabisa kwani alikuwa na mauzauza yaliyopitiliza, hakuweza kufanya chochote na wala hakuweza kulala alitamani tu pakuche ili aende na mama yake kwa huyo mganga, alihisi kwa siku hiyo mamake badala ya kuyajenga yani ndio kayabomoa kabisa. Basi kulivyokucha tu ni yeye ndiye alienda kumuamsha mama yake ambaye alimkuta amelala hoi kabisa, yani siku hiyo Rose alilala hadi alijisahau basi mwanae alivyomkurupua ndio akaenda kujiandaa kisha wakatoka na mwanae na kuanza safari ya kwenda nyumbani kwa mganga. Walivyofika walishangaa kuona watu wengi sana wamejaa kwa mganga Yule na walipoulizia kwa umakini zaidi, walipewa taarafa ya kuwashangaza sana, “Eti kuna nini?” “Kwani huna taarifa?” “Taarifa gani?” “Mganga amekufa” “Kheee amekufa? Lini tena jamani wakati jana nilikuwa nae” “Ulikuwa nae wapi na muda gani wakati kafa usiku wa kuamkia jana!” Rose alimuangalia mwanae Ana akiwa anashangaa sana. Itaendelea kesho usiku…….!!!!!! By, Atuganile Mwakalile.

at 4:46 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top