MAPENZI YA FACEBOOK-07 Nilikuwa katika maumivu makali sana moyoni mwangu, kila nilivyokuwa nikimuangalia Ester na kwa jinsi alivyokuwa akilia, nilihisi kumchukia sana. Moyo wangu ulikuwa umeshachoka kwa vile vituko alivyokuwa akivifanya. “Nisamehe mume wangu,” aliniambia huku akilia machozi, machozi ambayo kiukweli niliyafananisha na yale machozi ya waigizaji wa bongo muvi. “Nikusamehe?” nilijikuta nikimuuliza swali ambalo liliniropoka, sikuwa sawa kabisa. “Mume wangu naomba unisamehe,” alizidi kuniomba msamaha. “Nimekuuliza huyu Osmon ni nani?” nilimuuliza huku nikiendelea kuyatazama yale machozi yake, sikutaka moyo wangu ulainike kirahisi kwa kuyaonea huruma machozi yale. “Ni…ni…ni,’ alisema kwa kigugumizi kilichozidi kuniweka katika hasira kubwa sana. “Ni nani?” “Ni rafiki yangu wa facebook.” “Rafiki?” “Ndiyo mume wangu.” “Rafiki ndiyo muitane baby.” “Hapana mume wangu.” “Halafu unakataa?” “Ni rafiki yangu ila….” “Ila nini, halafu mimi ni baba yako?” “Hapana wewe ni mume wangu,” alinijibu huku akiwa amepiga magoti, alizidi kunisihi nimsamehe kwa kile kilichokuwa kimetokea. Nilizidi kujisikia vibaya sana, nilikumbuka jinsi alivyokuwa akichat na yule mwanaume. Roho yangu ilizidi kuniuma sio siri. Maumivu niliyokuwa nikiyapata kiukweli siwezi kuyafananisha na kidonda nilichowahi kukipata katika mwili wangu. Niliyakumbuka maneno ya wahenga waliyosema kuhusu ndoa pamoja uvumilivu wake. Kwa kweli akili yangu haikutaka kuyakubali kabisa maneno yao. Nilihisi walikuwa wakidanganya, yani Phidelis mimi ninayeumizwa na ndoa yangu, mke wangu halafu eti! Niendelee kuvumilia? Hapana haiwezekani! Asikuambie mtu ndugu yangu, mke anauma, ndoa inauma. Mapenzi ni mazuri endapo utapata ambaye anakupenda kwa dhati lakini mapenzi ni mabaya endapo utampata mtu ambaye hakupendi kwa dhati, anaishi kwa kukudhihaki. Hilo ndilo lililonitokea katika maisha yangu, maisha ya ndoa yangu. Sikutaka kuamini kabisa kwa kile kilichokuwa kimetokea, niliyakumbuka maneno ya Juma aliyoniambia kuwa suluhisho la matatizo yanaiyokuwa yakiikabili ndoa yangu yalikuwa mikononi mwangu. Nilizidi kupagawa sio siri na ni hapa ambapo nikajikuta natokwa na maneno ambayo siyo siri yalikwenda kuugharimu moyo wangu, moyo wa mapenzi uliyokuwa umemuhifadhi Ester mwanamke niliyeamini aliumbwa maalumu kwa ajili ya maisha yangu. Sikutakiwa kuwa mpole katika hili, niliamua kusema kile nilichoamini kiliuridhisha moyo wangu. “Kwanini lakini niendelee kuteseka kiasi hiki, kwanini uendelee kuwa msumari unayeupigilia moyo wangu bila kujali maumivu yangu unanidhihaki. Nakupenda sana lakini wakati mwingine inanibidi niamini kuwa hakuna mapenzi yasiyokuwa na maumivu. Umekuwa sababu ya maumivu ninayoyapata katika moyo wangu. Najitahidi kuvumilia lakini imefikia kikomo, nakiona kifo changu katika macho yangu na chanzo ni wewe, unashiriki katika kuuvunja moyo wangu lakini ni kwanini unayafanya haya? Unasahau kuwa mimi ni mume wako, unasahau kuwa mimi ndiye mwanaume wako, unasahau kuwa mimi ndiye kila kitu kwako, sasa kwanini unasahau yote hayo lakini? Facebook amekuwa adui anayekufanya uniumize kila siku. Nakupa kila kitu lakini huridhiki. Mwanzo nilipoziona komenti za wanaume waliyokuwa wakikomenti katika picha zako nilihisi wenda hakukuwa na chochote kilichokuwa kikiendelea, nilijipa moyo na kuamini kuwa labda walikuwa ni marafiki tu ambao hata ulikuwa hauwafahamu lakini kumbe nilikuwa najidanganya. Umeona urafiki haautoshi sasa umeamua kujenga uhusiano nao, umekubali kuwa katika mapenzi na mwanaume wa facebook halafu bado unasahau kuwa wewe ni mke wa mtu, Kwanini Ester kwanini lakini unanifanyia haya?” nilimuuliza swali lililosindikizwa na maneno yaliyotoka katika kitako cha moyo wangu, nilikuwa katika maumivu makali sana. Nilijitahidi kuvumilia machozi yasinidondoke lakini nilishindwa kabisa mwisho machozi yalichukua hatamu yake, yalinitiririka mashavuni mwangu. Je, nini kitaendelea? Usikose sehemu ijayo…

at 12:44 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top