MAPENZI YA FACEBOOK-05 Nilizidi kushangazwa na kile nilichokuwa nikikiona katika akaunti ya mke wangu, kuna muda sikutaka kuamini kabisa lakini kila nilivyokuwa najitahidi kujidanganya ndivyo moyo wangu ulikuwa unaumia. Nilikuwa naumia sana maumivu ambayo naweza kusema Facebook ndiyo chanzo. Laiti kama nisingekubali mke wangu ajiunge na mtandao huu na amini leo hii nisingekuwa katika haya maumivu yanayoendelea kunitafuna mwilini. Nilichoamua kukifanya ni kuanza kupitia komenti moja baada ya nyingine, kwa kweli ilikuwa ni vigumu sana hasa kwa kuzipitia zote kwani komenti zilikuwa ni nyingi mno ambazo zilikuwa zikiniumiza sana, nilijikaza kiume na kuamua kuyavumilia yote. Komenti ninayoikumbuka mpaka leo hii ninapokusimulia haya ni ya mzungu mmoja ambaye alijulikana kwa jina la Stewart. Aliandika “My Wife.” Kwa kweli nilijisikia vibaya sana, sikutaka kuamini kama mbali na ndoa yetu kuwa mke wangu alianzisha mahusiano mengine Facebook kiasi kwamba wakafikia kuitana mke na mume. Hili lilizidi kuniuma sana. Asikuambie mtu mapenzi yanauma sana, mapenzi yanakosesha amani, mapenzi yanaweza yakakufanya ukaamua maamuzi ambayo haukuwahi kuwaza kuamua hapo kabla. Wivu niliyokuwa nao kwa mke wangu sikutaka uendelee kubaki katika kilindi cha moyo wangu, kwa niliyobahatika kuyaona yaliniridhisha tosha. Sikutaka kuendelea kujiumiza tena japo machozi ya maumivu ya moyo wangu yalinidondoka lakini nilivumilia. Nilikuwa naililia ndoa yangu, mke wangu, mwanamke ambaye nilikuwa nikimpenda sana. Niliamua kumsimulia rafiki yangu Juma yale yote yaliyokuwa yametokea. “Aisee pole sana ndugu yangu, mimi bado niponipo sana sioi leo wala mwakani,” aliniambia Juma maneno yaliyozidi kuniumiza sana, inamaana nimeikurupukia ndoa? Nilijiuliza swali lililoniacha katika wakati wa maumivu. “Sasa unanishauri nini?” nilimuuliza, wakati huo tulikuwa katika bar moja, nilikuwa nikinywa pombe kwa ajili ya kupunguza mawazo yaliyokuwa yakinisibu. “Kuna kitu huwa unakosea sana,” aliniambia Juma ambaye alikuwa akinywa maji kwa wakati huo. “Kitu gani?” “Binadamu anaishi kwa mazoea.” “Mazoea, mbona sikuelewi?” “Najua nivigumu mno kunielewa kwasababu na wewe ni miongoni mwa wakoseaji.” “Juma nipo hapa kwa ajili ya ushauri wako yani kiukweli akili yangu imechanganyikiwa sana, sitaki hata kumuona Ester.” “Nikuulize kitu.” “Ndiyo niulize.” “Unahisi pombe ndiyo suluhisho la mawazo?” “Sasa unataka nifanye nini?” “Mwanaume anasifika kwa kuwa na maamuzi thabiti wala hatishiki na lolote lile linalomsibu. Usiwe mtu wa kupelekeshwa na hisia bali wewe ndiyo unatakiwa uzipelekeshe hisia.” “Una maanisha nini?” “Yani na hapo pia bado hujanielewa?” “Juma nimechanganyikiwa kiukweli.” “Najua hata nikisema umuache mkeo kisa Facebook kwakweli wapo ambao watanishangaa kwa ushauri wangu ila labda nikuulize kitu hivi bado unampenda mkeo?” “Ndiyo nampenda sana lakini kwa anayonifanyia kwa kweli yananiumiza sana.” “Msamehe mkeo.” “Nimsamehe?” “Ndiyo sasa ulitaka nikwambie muache, ok basi muache mkeo,” aliniambia Juma katika namna ya utani, sikuwa katika utani hivyo aliamua kuniambia nifanye uchunguzi ndipo niweze kufanya maamuzi. Nakumbuka alichoniambia suluhisho la matatizo ya ndoa yangu bado yalikuwa katika himaya ya mikono yangu. “Phidelis suluhisho la matatizo yako unayo mikononi mwako, kuwa na maamuzi pia usikurupuke kufanya maamuzi kwani yatakugharimu,” aliniambia Juma maneno yaliyoniingia vyema. **** Nilirudi nyumbani majira ya usiku, nakumbuka ilikuwa ni majira ya saa tano za usiku. Nilimkuta mke wangu akiwa amekasirika sana, nililigundua hilo baada kumsalimia, hakuitikia salamu yangu jambo ambalo lilizidi kuniumiza. Ina maana hakuisikia salamu yangu? Nilijiuliza kisha nikamsalimia tena. “Mke wangu umeshidaje?” nilimsalimia. “Unatoka wapi usiku huu?” “Mke wangu foleni.” “Foleni, na mbona usinipigie simu.” “Nilijua kuwa nitawahi hata hivyo nikaona nisikusumbue.” “Hee! Yani wewe mwanaume umenishinda na mbona unanukia pombe siku hizi unakunywa?” “Pombe?” “Ndiyo.” “Mimi?” “Kwani naongea na nani hapa?” aliniuliza huku mikono yake ikiwa kiunoni. “Mke wangu,” nilimuita kwa sauti ya utulivu sana. “Sema,” alinijibu huku akiwa ameubetua mdomo wake. “Wewe ndiyo sababu ya mimi kuwa hivi, mimi sio mlevi lakini nimejikuta nakuwa miongoni mwa walevi, mapenzi niliyonayo kwako sijui kwanini unashindwa kuyaheshimu,” nilimwambia kwa kukurupuka maneno ambayo yalituingiza katika ugomvi mkubwa sana, Ester alizidi kugombana na mimi huku akiwa hajui sababu ya mimi kuyasema yale. “Kwahiyo mimi sasa hivi ndiyo nakufundisha ulevi?” aliniuliza kwa sauti ya ukali. “Hapana simaanishi hivyo.” “Ila?” aliniuliza. Kuna muda nilitaka kumwambia yale niliyoyaona Facebook lakini niliyakumbuka maneno ya Juma, sikutakiwa kukurupuka katika hilo niliamua kuwa mweye subira. Niliamua kuomba msamaha kwa yale yaliyokuwa yametokea kisha amani ikarejea katika ndoa yetu. Niliishi kwa maumivu makali mno. Kila nilivyokuwa nikimtazama Ester pamoja na upole aliyokuwa nao kwa kweli sikutaka kuamini kama ni yule ambaye alikuwa akibinua makalio yake Facebook. Nilizidi kuumia mno, mapenzi yalikuwa yakinitesa Phidelis mimi ambaye sikuwa mzungumzaji sana. Je, nini kitaendelea? Usikose sehemu ijayo.....

at 7:26 PM

Bagikan ke

Lintaskan

0 comments:

Copyright © 2025 Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top