Home → simulizi
→ MUME WANGU SHUJAA WANGU -1
Kaka admin, baada ya kusoma taarifa na mafunzo mbalimbali katika ukurasa wako huu wa Ndoa Maridhawa, imenipa ujasiri wa kuwashirikisha simulizi yangu mwenyewe.
Baba yangu alifariki dunia nilipokuwa darasa la 3. Ni siku ambayo ilibadilisha maisha yetu kutoka kwenye hali nzuri kwenda kwenye hali mbaya. Mama yangu alikuwa mama wa nyumbani na alitegemea moja kwa moja kipato cha baba yetu. Kuanzia hapo, mama yangu akachukua jukumu la matunzo yangu na kaka yangu mkubwa George. Ndugu wa baba yangu walichukua mali zetu zote ikiwemo nyumba tuliyokuwa tukiishi. Baada ya miaka miwili ya tabu na mateso, hatimaye mama yangu alipata kazi kama mfanya usafi kwenye eneo ambalo baba yangu alikuwa akifanya kazi.
Nilipofika darasa la 7 na kaka yangu akawa amefika chuo, mama yetu kipenzi alifariki dunia. Hakuna aliyekuwa tayari kutuchukua mimi na mtoto wa kaka yangu, Belinda aliyekuwa na umri wa miaka 4. George alipata mtoto nje ya ndoa alipokuwa kidato cha 3, mwaka mmoja baada ya kifo cha baba yangu. Mama ndiye aliyekuwa akimhudumia mtoto huyo tangu alipozaliwa.
Mungu ni mkubwa, rafiki mkubwa wa mama yangu kutoka kanisani, Jessica alituchukua. Alikuwa mjane mwenye mtoto mmoja tu. Binti yake, Hamasa na mimi tulikuwa kama mtu na dada yake, hivyo tulipendana sana. Shangazi Jessica alikuwa mtu mzuri na mwema, alituhudumia kama watoto zake halisi. Kaka yangu alikuwa akija siku za likizo mpaka alipohitimu masomo yake.
Nilichagua kusomea uuguzi baada ya kuhitimu masomo yangu ya kidato cha sita kwa sababu nilitaka kuchukua kozi ambayo itakuwa rahisi kupata kazi.
Nikiwa mwaka wa mwisho chuoni, nilikutana na mume wangu Moses na tulifunga ndoa baada ya mwaka mmoja na nusu wa mahusiano yetu…
Baada ya kujifungua mtoto wangu wa pili, kaka yangu George alifariki dunia katika ajali ya gari. Hakika nilichanganyikiwa sana. Mimi na kaka yangu tulipendana sana na tulielewana mno. Aliacha mke na watoto wanne. Belinda hakuweza kuwa na maelewano mazuri na mama yake wa kambo, hivyo nilimchukua. Sikutaka apate usumbufu kwenye masomo yake. Wakati huo alikuwa kidato cha 3 na niliamini kuwa atafaulu vizuri sana.
Mwaka mmoja na nusu tulikuwa katika maelewano mazuri, lakini baada ya kujifungua mtoto wa 3, Belinda alianza kubadilika. Ushauri wangu kwake haukuwa na maana yoyote, alimsikiliza Moses tu. Alikuwa akinitazama na kusema kuwa mimi ni mnene sana na kwamba wanaume wanapenda wanawake wembamba kama yeye.
Mwanzoni ilionekana kama utani tu lakini baadaye ikawa kama mazoea. Nilikuwa nikimwambia kuwa wanaume wanatofautiana katika uchaguzi wao na pia mimi sikuwa mnene sana kama alivyokuwa akiongeza chumvi.
Siku moja tulikuwa tukitazama mashindano fulani kwenye televisheni, akaanza kucheka kwa sauti kubwa huku akinyoosha kidole kwa mmoja wa washiriki wa mashindano na kusema: “Shangazi Faith, usipoangalia uzito wako utaishia kuwa kama yule”. Mwanamke aliyemuelezea alikuwa na kilo 442, nami nilikuwa na kilo 60. Hapo mume wangu akaonekana kusononeka na kumwambia kuwa nilikuwa na uzito sahihi na mzuri hata kama nina watoto 3 na akamuonya asirudie kuzungumza nami kwa namna ile… Ukweli mimi sikuchukulia kuwa ni tusi kwa sababu alikuwa mtu wa karibu mno kwangu, lakini mume wangu aliposema vile, akawa kama amenifungua macho!
ITAENDELEA…
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: