MOYO USINIDANGANYE NO .05 Siku iliyofuata nilishinda hivyo hivyo, sikumtafuta Ninah siku nzima, naye hakupiga hivyo ikapita siku nzima bila kuwasiliana. Niliporudi nyumbani, baada ya kuoga na kupumzika, uzalendo ulinishinda. Nilimtumia ujumbe mfupi wa simu, NAKUPENDA SANA NINAH. Hiyo ilipata mida ya saa nne usiku. Sikutegemea anijibu, lakini kwa jinsi nilivyokuwa nahisi, niliona bora tuu niandike. Sikujali kama pengine mida hiyo angekuwa na yule jamaa aliyenipiga mkwara juzi au la. Dakika kama tano baada ya kutuma ule ujumbe alipiga simu. Upande mmoja niliogopa kuipokea, nikihisi ataanza kunionya nisiendelee kumfanya kama mpenzi wangu, lakini kwa upande mwingine nilitamani kusikia sauti yake. Nilipopokea simu, sauti ikiwa ya chini na ya upole sana, nilimsalimu na kumwambia kuwa nimefurahi kupokea simu yake. Alinijulia hali kisha akaniuliza kama tunaweza kuonana. Moyo ulistuka sana, nikamuuliza tuu, unahitaji kuniona lini? “Hata kesho”, alijibu kwa ufupi. "Ngoja nitafute kama nitapata ndege ya kesho sasaivi halafu nitakujulisha," nilimuitikia. Kwa penzi nililokuwa nalo juu ya Ninah, gharama ya ndege za dharura sikuona kuwa ni kitu. Umbali wa Dar es Salaam na Mwanza kwangu ulionekana kama ni wa kutupa jiwe. Niliingia mtandaoni usiku huo na kutafuta ndege, kwa bahati haukuwa msimu wa wateja wengi hivyo nilipata ndege ya kesho yake saa 12 asubuhi, ingawa bei ilikuwa juu. Nilimpigia kijana wangu, kumuomba afike nyumbani saa kumi alfajiri, akanisindikiza uwanja wa ndege, nikampa na maelekezo muhimu ya biashara, nikaondoka. Niliwaza ni nini hasa binti huyu anataka kuniambia, kwa dharura ya namna hiyo. Nilijipa moyo kwamba hawezi kunisumbua, kunitoa Mwanza kama hana jambo la msingi la kuniambia, lakini sikutaka kuweka matumaini kwamba atakuwa ananikubali. Ni siku chache tuu, nilipata simu kunithibitishia kuwa yuko kwenye mahusiano, na haingekuwa rahisi hata kidogo kunipa nafasi mimi pia. Hata hivyo, wito wake ulikuwa muhimu mno kwangu. Jioni ilifika, nikamfata kazini mapema kidogo, kwani alitaka nimfate saa tisa. Tulipoonana, nilishuka kwenye gari kumpokea, nikamshika mkono, nikajikuta nimemvuta kumkumbatia. Nadhani nilichohitaji ni kumkumbatia, nijifariji kwa uwepo wake karibu yangu. Sielewi ujasiri huo niliupata wapi, lakini nashukuru hakukataa kumbato langu, japo hakuniruhusu kuendelea kwa muda mrefu. Tuliingia kwenye gari, na siku hiyo sote hatukuwa wachangamfu kama awali. Tulizungumza tuu mambo ya msingi, hakukuwa na utani wowote kati yetu. Nilimuuliza kama alikuja na gari, akasema alikuja nalo lakini amemuachia rafiki yake funguo hivyo tunaweza kuondoka pamoja. Akili yangu wakati huo iliwaza, kama Ninah angeniambia huu ndio mwisho wetu, sijui ningefanyaje. Nilihisi kumpenda kuliko nilivyowahi kupenda kabla. Tulienda hoteli fulani kubwa, iliyo kando mwa bahari, tukakaa sehemu ya wazi jirani na maji. Tukiwa tumeagiza vinywaji, ghafla mvua ilianza kunyesha, hizi mvua za Dar zinazokuja bila taarifa. Tulipokaa hapakuwa na mwanvuli juu, palikuwa wazi tuu, mbali kidogo na majengo ya hoteli. Tuliinuka sote kwa haraka, nikamshika mkono ili tukimbie kujikinga na mvua, lakini badala ya kukimbia, tulijikuta tumesimama pale kwa muda kiasi tukitazamana, huku mvua kubwa ikinyesha. Nilimtazama machoni, nikiashiria nataka anitazame pia, zikapita sekunde kadhaa, nikamwambia,’nakupenda sana Ninah, nakupenda’. Mvua ikiendelea kunyesha, alinivuta kunionesha tunatakiwa kuondoka eneo hilo, tukaelekea sehemu ambapo mvua haifiki, lakini sote wawili tukiwa tumelowa kiasi. Nilimuhurumia kuwa angesikia baridi, hivyo haingekuwa sawa kukaa na nguo mbichi. Nilimuomba tuondoke hapo hotelini, tukaondoka, nikampitisha kwenye duka moja la nguo, nikamnunulia gauni simpo, nikamuomba twende hoteli niliyofikia. Nilimpa funguo ya chumba changu, akaingia kubadili nguo huku nikimsubiri kwa nje, halafu nami nikaingia kubadili alipotoka, nikavaa kinyumbani zaidi yaani pensi na tisheti na viatu vya wazi. Tulipanda juu kwenye mgahawa, tukaagiza kahawa na kuanza kunywa. Nilitamani Ninah aanze kuzungumza, lakini niliogopa kumuharikisha kwani sikuwa najua nini hasa angetaka kuniambia. Muda si mrefu, alianza kuongea. “Uliniuliza kuhusu mahusiano yangu, sikutaka kuzungumzia. Lakini mara ya pili tunaonana nilikuwa na mpenzi wangu, hilo unajua. Yule mwanaume nilimpenda sana, na nilitegemea tungeoana. Wakati ule alikuwa ametoka masomoni, ni mwanajeshi, hivyo alipokuwa masomoni kwa muda mawasiliano hayakuwepo kabisa, muda wa kama mwaka mzima, lakini alipokuja tuliendelea na sikuwahi kuwa na mwanaume mwingine kwa kipindi kile chote. Tulikaa huku nikitegemea tuanze taratibu za kuoana kwani uhusiano wetu tayari ulifikisha miaka mitatu wakati huo, lakini yeye alikuwa mzito kidogo. Baada ya kuvutana kiasi, alinivisha pete kwa mshtukizo yaani sapraizi, kabla hata hajatoa barua ya posa. Sikufurahia sana kile kitendo, japo yeye alidai kuwa ni hatua kubwa sana katika kuoana. Tulikaa kama miezi sita bila kuendelea na hatua yoyote. Sasa wiki kadhaa zilizopita nimepata habari kuwa ana mtoto aliyemzaa na mwanajeshi kipindi yuko masomoni, na mama yake amekuja hapa mjini kumtafuta. Nimefatilia nikajua ukweli, japo mwanzo nilimuuliza akakataa kabisa, lakini baada ya kubaini ukweli amekubali na kuanza kuniomba msamaha. Mbaya zaidi huyo mwanamke nahisi bado wanaendelea na mahusiano. Juzi kati, tukiwa kwenye huu mgogoro, alipiga akidai kuwa sitaki kumsamehe kwakuwa nimepata mwanaume mwingine. Kuna kitu aliwahi kufanya kipindi cha nyuma tukagombana sana, alifuatilia simu yangu mitandaoni, kuangalia nani nawasiliana naye sana. Hakukuta siri yoyote, akajikuta ameniambia, tukagombana sana, nikamuonya kuwa hiyo ni kuonesha kiasi gani haniamini. Hivi karibuni amerudia tena kufanya hivyo japo aliniahidi hangefanya tena. Mimi ni muaminifu kwake, na anaruhusiwa kuchukua simu yangu kuiangalia, lakini si kwenda nyuma ya pazia. Alivyokuta jumbe zako, ambazo kwenye simu yangu sikuwa nazihifadhi, alihamaki sana na kushindwa kujizuia kuniambia. Wakati huo tulikuwa kama tumeachana kwajili ya hayo mambo niliyogundua, kwani sikuwa tayari kuwa naye akiwa na mwanamke mwingine. Sasa baada ya kuona jumbe zako, juzi, alinipigia simu akigomba sana na kuniambia kuwa amekupigia uachane na mke wake. Anadai wewe ndiye unanipa jeuri ya kumuacha japo bado sijakukubali.” Maelezo ya Ninah yalinifanya nimuhurumie kwakweli. Jinsi alivyo mrembo na laini niliona hakustahili kuumizwa hata kidogo. Nilijikuta nimeropoka,”Watu wanachezea bahati!”, akatabasamu tuu. Nilitamani ningeipata hiyo nafasi mimi, nikajiahidi nafsini mwangu, kwamwe singeipoteza. Sikuongea sana, nikamuacha aendelee na maelezo yake. “Unisamehe nimekusumbua kukutoa Mwanza, lakini nilihisi nahitaji kuongea nawewe. Sasa hivi sijui tena nini hasa cha kukwambia, ila kiukweli nilihitaji kukuona Maxwel”. Hapo akili za kuambiwa, nilichanganya na za kwangu, nikaelewa binti ananihitaji. Nilisogelea kiti cha karibu naye, nikahama nilichokuwa nimekaa kilichotazamana naye. Niliweka mkono wangu begani kwake, nikamtazama usoni, naye akaniangalia, nikamwambia,”Najua unachotaka kuniambia, naweza kusoma mawazo yako, hivyo usihangaike kusema. Humuhitaji tena huyo mwanaume, lakini unajihisi mpweke kiasi. Niko hapa Ninah, kukufanya ujisikie salama na usiwe mpweke tena. Nakupenda sana, kuliko unavyodhani.” Nilizungumza nikiwa nimemkumbatia kwa mkono mmoja, nikimaanisha kuifariji nafsi yake. Nilijua najiweka hatiani kutaka penzi kwa binti ambaye pengine moyo wake bado umebeba mtu mwingine, nilifikiri endapo mpenzi wake wa awali akimbembeleza wakarudiana nitakuwa kwenye hali gani. Lakini kwangu faraja ya Ninah ilikuwa muhimu. Sikutaka awe na huzuni japo pia nilitumia fursa hiyo kujiweka karibu. Labda bahati ingeniangukia, akanipenda mimi moja kwa moja. Usiku ule ulikuwa wa kipekee sana kwangu, nilimrudisha Ninah saa nne na nusu usiku, alipotaka yeye, kwani angeniruhusu tungekaa mpaka asubuhi. Wakati tunaarudi alikuwa amerejea katika hali ya uchangamfu hivyo nikajipongeza kuwa kazi nimeifanya vizuri. Tulifika kwake, nikashuka na kuja upande wake. Si kuwa nina tabia za kizungu sana, kumfungulia mwanamke mlango wa gari, au nataka kujionesha hivyo kwa Ninah, ila niliona hiyo ndiyo njia rahisi ya kupata kumbato lake kwa mara nyingine tukiwa tumesimama. Alishuka kwenye gari, nikashika mikono yake miwili, nikamvuta karibu na kumkumbatia kwa nguvu sana. Mara hii hakunizuilia mapema, basi nikakaa pale kama dakika nzima au zaidi. Nadhani unaelewa hisia zilizoendelea ndani yangu wakati huo, yani nilitamani kuendelea kumuweka kifuani kwangu hata kwa saa nzima, lakini hilo lisingewezekana. Tuliagana, akaondoka. Niliporudi hotelini, baada ya kuoga na kuingia kitandani, nilimpigia simu kumuuliza kama amelala tayari. Sikuwa na cha kumwambia hasa, lakini nafsi yangu ilifurahi kumsikia kwa simu. Usiku kucha nilimuwaza Ninah, nikiwaza tulivyokumbatiana na nilivyojihisi, niliwaza huzuni aliyokuwa nayo na nilivyotumia fursa ile kujiweka karibu, niliwaza alivyotabasamu, niliwaza alivyolitamka jina langu, yani kila kitu mpaka alivyokosa cha kuniambia. Nilijifariji kuwa ameanza kunipenda na ndio sababu amenitoa Mwanza ili nikae naye tuu wakati anapitia ugumu kwenye mahusiano yake. Nilitamani kesho yake ifike haraka nimtafute tena, nimuombe kuonana. Wiki hiyo nzima Ninah alinipa nafasi ya kuonana naye kila siku, tukiwa na wakati mzuri wa pamoja jioni, tukitembelea maeneo tofauti tofauti, lakini hata siku moja hakunitamkia neno lolote kunionesha kwamba naweza kuwa nimeanza kuchukua nafasi moyoni mwake. Niliridhika kuwa rafiki wa karibu, nilifarijika kukaa naye, kula naye, kucheka na kuzungumza na huyu mwanamke niliyempenda sana. INAENDELEA...

at 8:35 PM

Bagikan ke

0 comments:

Copyright © Braytonofficiallove
Designed by Siyamdezign | Edited By braytonofficiallove
braytonofficiallove | braytonofficiallove | braytonofficiallove
Powered By Blogger
Back to Top