Home → ushauri
→ CHOMBEZO: NILAMBE HUMO HUMO
SEHEMU YA TANO
Wengine ndugu zao wa kiume walikuwa wamewadhulumu mali za urithi walioachiwa na wazazi wao, wengine walikuwa yatima walioondokewa na wazazi wao na kukosa mtu wa kuwaangalia! Wengine walikuwa wametupwa na wazazi wao baada ya kuzaliwa wengine… wengine!
Basi ilimradi kulikuwa na mlolongo wa matatizo ambayo kwa hakika yalichusha na kuudhi.
Hofu ya ukimwi je?
Walikuwa nayo lakini wangefanyaje? Waliona bora waishi kwa furaha leo kwa kuwa hata kesho wasipokufa kwa ukimwi kama watajitunza, basi watakufa kwa njaa, umasikini na adha zingine kadha wa kadha.
Ugunduzi huu ukanifanya nisiwatizame kwa jicho baya tena, bali nikawaona kama wahanga fulani hivi!
Nikajitengenezea utaratibu mzuri wa kwenda pale na kuhudumiwa mara nne kwa wiki! ulikuwa utaratibu nilioupenda na kuufuatisha kama ibada, utaratibu mtamu kweli, mtamu haswaa.
* * *
Asubuhi kulipokucha, Akimu allikuja kunigongea, nikainuka na kufungua mlango.
‘’Mambo?’’ Akanisalimu akiingia ndani.
“Poa!’’
‘’Vipi mbona hivi, leo huendi?”
‘’Wapi?” Nikamuuliza kwa wasi wasi kidogo.
‘’Mara hii umesahau kuwa juzi tulikubaliana kwamba leo tutakuwa na round discussion kuhusu Utambuzi wa Short na mitihani ya mwisho inayokuja?
“My God!’’ Nikaguta. Nilishasahau kabisa, ukweli leo sikujisikia kujadili chochote mwenyewe nilikuwa nataka masaa yaende mbio jioni niende zangu uwanja wa miutamu.
‘’Sorry Akimu!’’ Nikamwambia Akimu “Sitaweza kuja katika discussion leo nataka nifue then nipumzike kabla sijajisomea kisha nitakwenda mahala!’’
‘’Lakini tulikubaliana utakuja!’’
“Ndio hivyo tena!’’
‘’Basi itakubidi umueleze Shamsa kabisa maana binti yule asipokuona hasomi sawa sawa!’’ Nikatabasamu “Nitamwambia!’’ nikajibu.
Wakati anataka kujibu akakiona kitabu cha gwiji wa riwaya nchini marehemu Eddie Ganzel ’Kijasho chembamba’, vile anavyopenda riwaya za Ganzel akainuka na kukitwaa.
Alipokiinua tu kadi za mapenzi, zenye picha nzuri na maua ya kuvutia pamoja na barua za mapenzi zikaonekana chini yake, akaniuliza maswali machache kuhusu nilikokipata kitabu kile, halafu akauliza
‘’Hivi haya maua na hizi kadi bado tu hujazipeleka kwa Shamsa?’’
“Bado!’’
Akimu akanitumbulia macho kwa mshangao!
Alikuwa na haki ya kushangaa, alikuwa nayo. Mosi ni
yeye aliyekuwa mwandani wangu, alifahamu vingi na mengi kunihusu, pili alikuwa shuhuda wa macho wa namna nilivyoathirika kwa kumpenda binti yule.
Na ni yeye aliyetoa ushauri wa kumpelekea zana hizo na kama vile haitoshi alikuwa amenisindikiza kuzinunua, kubuni maneno mazuri yaletayo faraja na kuyaandika juu ya kadi hizo, tena alikuwa amenitaka kumpelekea haraka iwezekanavyo ili kama kuna lolote tulijadili kwa pamoja.
Na sasa ulikuwa umepita mwezi na kidogo toka tulipoziandaa
“Kwanini hujazipeleka? Ibra usiniambie ulikosa ujasiri, maana nilikwambia wewe ukishindwa kumkabidhi nipe mimi nitamkabidhi!’’ Akatua kwa kila hali alikuwa na hasira, mimi nikatabasamu na kumjibu.
‘’Nimeona haina haja Akimu!’’
‘’Eti?!’’
‘’Enh! Hanisumbui tena nimesha muweka chini ya himaya yangu!’’ ikawa zamu yake kunitazama kwa mshangao, nusu akitabasamu nusu akitaka kushangilia.
‘’ Ina maana umeisha… umeisha….! Mungu wangu, mbona siamini!’’
‘’Sijafanya nae mapenzi wala hajanikubali niwe mpenzi wake! Ila nimemdhibiti, hanisumbui tena! Maelezo yangu yakazidi kumchanganya Akimu. Akanisaili tena.
‘’Unamaana gani Ibra?’’
‘’Nina maana kuwa kuna mahala ninapoupoza moyo wangu kwa maji baridi, maji ya ya mapenzi, maji ya uzima!’’
“Inamaana umepata mpenzi mpya unayempenda kuliko Shamsa?”
“Sijasema simpendi Shamsa!’’ Nikasema kwa karaha “Nikingali nampenda na nitaendelea kumpenda maisha yangu yote!”
‘’Basi nyoosha Kiswahili Ibra, hata hao wahenga misemo na mithali zao zilieleweka kwa urahisi!’’
“Nitakwambia!” Nikamwambia huku tabasamu likiwa limeupamba mdomo wangu “Nitakwambia rafiki yangu, tena nitakwambia ukweli mtupu naomba tu uniwie radhi kwa kukuficha!”
Nikakaa vizuri na kumueleza ugunduzi wangu wa kule Fisi. Nilimueleza kwa tuo pasipo kuacha hata tukio moja. Nilipo maliza Akimu alikuwa ameshika kichwa kama aliyepoteza kitu cha thamani sana!
‘’Ni kweli unielezayo Ibra?” Sasa machozi yalikuwa yakimlenga
‘’Ni kweli kabisa!’’
‘’Umepotea rafiki yangu, tena umepotea vibaya sana. Sio watu wale ni balaa!’’
‘’Tatizo lao liko wapi Akimu? Kama nilivyo kwambia nimewastadi vya kutosha kabla ya kuamua kuwa nao chanda na pete.
‘’Hawako salama wale! Kila mwaka wanakufa! Na wanakufa na idadi kubwa sana ya watu! Hii ni kwa vile wanafanya mapenzi na watu wengi sana, wengine hutembea mpaka na wanaume elfu sita na mia sita kwa mwaka hadi elfu saba na mia mbili.
Ni washenzi wa tabia wasio na utu walioamua pesa iwe yao kwa kila hali, ukiwa na pesa unaweza kumwambia akuuzie hata utumbo wake na akakuuzia! Zaidi na zaidi ni wabaya wazee na wasiovutia kwa chochote! Ndio maana nasema umepotea!”
Akiwa na jazba Akimu alitumia zaidi ya robo saa kuwaponda makwini wa fisi. Alipomaliza ndipo nami nilipoanza kum’bishia. Tulibishana sana na mwisho wa siku ikawa imeamuliwa mimi na yeye twende uwanja wa fisi wote akajionee, nae akasisitiza mimi nikajionee, tukaondoka mchana huo huo!
Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuingia uwanja wa fisi mchana. Eh! zaidi ya maajabu yalikuwa yakinisubiri
Wanawake karibuni wote waliokuwa wakiuza miili yao walikuwa watu wazima hasa, wazima kweli, umri umekwenda mno. Sura zao zilikuwa tisho jingine. Mbali ya kuwa zimekomaa kwa namna ya kuchusha, huo mkorogo waliojimwagia sikuwahi hata kuufikiria. Mkorogo hadi mapajani! Mkorogo hadi miguuni, hadi katika matiti!
‘’Niliwezaje kufanya mapenzi na watu hawa?” nikajiuliza nikitikisa kichwa kwa masikitiko. Nikajuta. Akimu akanikokota tukarudi chuoni nikiwa nimenyongea.
‘’Kwanini uliamua kuja huku Ibra?” Akanisaili kwa upole baadae.
‘’Msongo rafiki yangu! Mhemko! Nilihemkwa na kutamani ngono kupita kitu chochote! Nikaona huku ndio pa’ kuponea! Laiti ningelijua…,” Nikalia kimya kimya. Akimu akinifariji.
Kwa shinikizo lake niliweza kushiriki katika Round discussion ingawa nilipooza Kama ugali uliokosa moto wa kuuivisha sawa sawa. Shamsa alikuwepo na alifurahi kuniona, nikamtaka radhi kuwa sikuwa nikijisikia vizuri.
Mpaka tunamaliza majadiliano yetu sikuwa nimechangia lolote!
* * *
‘’Kanini umenileta huku Akimu? Nikamuuliza tukitembea kutoka sokoni, tulikuwa Songambele, kijiji kimoja kilichoko mkoani pwani ndani kabisa wenyewe walikuwa wamekibatiza jina la Gobba , ingawa jina lake la asili lilikuwa Songambele Sotele.
Kilikuwa kijiji ambacho Akimu alisomea elimu yake ya sekondari kabla hajafaulu vizuri, akakataa kuendelea na masomo ya juu na kuja kusomea umeme pale VETA. Hili lilijiri kwa kuwa Baba yake alikuwa fundi umeme aliyefanikiwa sana kimaisha kupitia kazi hiyo.
“Nimegundua rafiki yangu u’mhanga wa starehe! Starehe ya mapenzi. Huku utaburudika utastahali na kuneemeka vya kutosha. Na uzuri wanawake wa huku hawatokitoki hovyo nje ya vijiji vyao kwahiyo ni salama kwa kiasi kikubwa!”
Akanijibu. Angejua nilivyojiapiza kutofanya tena mapenzi tangu ulipojiri ule ugunduzi wa yaliyopo Uwanja wa fisi, wala asingejisumbua! Moyoni mwangu alibakia Shamsa pekee na vile tulibakiza miezi sita tuhitimu, nilijua nitamtamkia wakati huo na kitakachofuatia ni ndoa mara moja.
Nikiendelea kutembea, niliendelea kukiperuzi kijiji hiki cha Gobbah kuona kama kingeweza kunifariji. Hakikuwa na chochote cha kujivunia! Mifugo michache yenye siha na afya ya wastani, wakazi ambao mwonekano wao uliashiria umasikini uliotukuka na ardhi kubwa yenye rutuba ambayo haikuwa imelimwa, vilikuwa baadhi ya vitu vilivyoipamba Songambele Sotele a.k.a Gobbah.
Jioni tulikuwa baharini, tuliogelea na kufurahi pamoja na wenyeji wa eneo hilo ambao walikuwa na ukarimu unaovutia. Halafu tukaelekea mpirani. Usiku tulikuwa kwenye vijiwe vya kahawa ambapo tulipiga soga mpaka usiku ulipokomaa, tukaenda kulala.
Siku mbili zilizofuatia tuliishi katika mtindo huu.
Wakati nimeanza kuchoshwa na maisha haya katika siku ya tatu na nikiwa tayari kumwambia Akimu turudi Dar es salaam; ndipo lilipotokea lile ambalo ni miongoni mwa mambo matatu muhimu yalinifanya nishike peni na karatasi na kuandika mkasa wangu huu ambao Uncle Wamaywa ameamua kuuita chombezo.
‘’Jiandae Ibra,’’ Akimu Aliniambia kwa bashasha. ‘’Leo kuna ngoma! Watoto aina kwa aina wanakusanyika toka kata nzima. Hii hakuna kulala ni kutimbwirika hadi majogoo!”
Nikamtazama nisimuelewe! Ngoma ni miongoni mwa vitu ambavyo sikuwa na hobi navyo, Nikamuuliza taratibu hali nikiwa nimemkazia macho. ‘’Najua unajua kwamba mimi sipendi ngoma!”
‘’Najua sana, lakini hii tunaita ngoma kimazoea! Jina lake hasa ni mnanda!”
“Mnanda?!”
‘’Ndiyo!”
‘’Mnanda ni nini na Ngoma ni nini?!”
‘’Yanini tuandikie mate il-hali wino upo? mnanda unaanza saa kumi na mbili jioni na sasa ni saa kumi jioni subiria masaa mawili tu utapata majibu timilifu, majibu ya vitendo! Jiandae tu!”
Maswali yalikuwa mengi kichwani, lakini kila nilipomuuliza Akimu jibu lake lilikuwa moja tu. ‘’Jiandae, jiandae!’’
Nikajiandaa.
Kweli, jioni tukakusanyika mnandani watu aina na aina wakijisogeza na kumsherehekea binti huyu anayeolewa. Wasichana na niseme wanawake walikuwa wamejikwatua vilivyo na walikuwa wakijituma hasa pale dimbani.
Nikashangaa kwa kuwa sikuwa nimewaona kabla. Akimu akinijulisha kuwa nisingeweza kuwaona kwa kuwa ule ni mkusanyiko wa watu kutoka kata nzima na pengine tarafa.
‘’Mambo zaidi utayaona usiku!’’ akahitimisha wakati nikianza kusisimkwa! Ule uchezaji wao ulivutia kwa hakika, ulikuwa uchezaji ambao ungekulazimisha kuangalia huku mwili ukipatwa na joto ghafla.
****Nini kitajiri USIKU huu unaosemwa……IBRA tayari amesisimka….
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: