Home → simulizi
→ WHATSAPP CHATTING
WHATSAPP CHATTING.
Nilikuwa ninaendesha gari kwa mwendo wa kawaida sana kuelekea Mlimani City kwa ajili ya kufanya shopping moja ya kawaida sana, kununua baadhi ya vitu kama juisi na vitu vingine ambavyo vilikuwa vimepungua katika jokofu langu. Sikuwa nimeoa, nilikuwa nikiishi peke yangu ndani ya chumba cha kupanga, chumba ambacho kama kijana wa kisasa, kilionekana kukamilika kila idara.
Ndani ya chumba changu, ukuta ulikuwa na rangi ya pinki, rangi ambayo nilikuwa ninaipenda kupita kawaida. Hapo ukutani, nilikuwa nimeweka picha zangu mbili, picha ambazo nilinekana kuwa smati sana, picha ambazo kama kulikuwa na msichana yeyote ambaye angeziona, lazima angevutiwa na mimi tu.
Kitanda kilikuwa kikubwa, kitanda cha chuma ambacho nacho nilikipaka rangi ya pinki. Kitandani kulikuwa na godoro kubwa lililokuwa linapendeshwa na mashuka kadhaa kila siku, mashuka yaliyokuwa na rangi mbalimbali za kuvutia. Kitandani hapo, kulikuwa na mito ile laini ambayo nilikuwa nikipenda kuinunua Mlimani City kwa Sh. Elfu thelathini na tano kila mmoja, kulikuwa na mito zaidi ya saba. Ukiachana na hivyo, kitandani hapo kulikuwa na midoli minne, midoli ambayo nilikuwa napenda sana kuiweka katika kila pande kitandani hapo.
Ukiachana na hapo, chumba kilikuwa na marumaru, dirisha lilikuwa moja ambalo kwa gharama yangu nikaamua kuweka dirisha la kioo. Chumbani hapo kulikuwa na kabati kubwa la nguo ambalo lilikuwa na mashati zaidi ya ishirini, fulana zaidi ya kumi na nane, suruali zaidi ya kumi na mbili pamoja na pensi zaidi ya saba. Ndani ya kabati hilo, nilitenga sehemu maalumu ya saa zilizokuwa na rangi mbalimbali. Nilipokuwa nikitaka kuvaa shati au fulana ya bluu, nilikuwa nikivaa saa ya bluu au kama nguo nyekundu, nilikuwa nikivaa saa nyekundu. Ndani ya kabati hilo kulikuwa na saa zaidi ya nane.
Kuhusu manukato, nilikuwa nimenunua ya kutosha sana tena yaliyokuwa na harufu mbalimbali za kunukia. Ukitoka kabatini, chumbani humo, pembeni kulikuwa na stendi ya viatu ambayo ilikuwa na pea za raba zaidi ya nane, sendozi pea tatu na kandambili za kuendea bafuni.
Sikuwa nikirudia nguo mara mbili, nilizitenga nguo zangu kwa siku, leo nilikuwa nikivaa hii, kesho hii na hata siku nyingine kubadilisha mara mbili kwa siku. Ndani ya chumba hicho ukutani nilikuwa nimeweka tv moja iliyokuwa na nchi arobaini na tisa ambayo niliunganisha na king’amuzi cha DSTV ambacho nilikuwa nikikilipia kwa mwaka. Ukiachana na vitu hivyo vyote, pia kulikuwa na taa ndogo zile zenye umbo la uyoga, taa mbili ambazo nilikuwa nikiziwasha kila nilipokuwa nikihitaji mwanga hafifu nyakati za usiku.
Huwa sipendi jokofu niliache tupu, mara nyingi nilikuwa nahakikisha kila aina ya vinywaji vinapatikana isipokuwa pombe. Nilikuwa nikiweka maziwa ya kutosha, juisi, soda, maji pamoja na vitu vingine mbalimbali. Kuhusu maisha, kwa kiasi fulani nilionekana kujipanga sana japokuwa nilikuwa nikijiona bado kabisa.
Muda mwingi nilikuwa nikionekana nadhifu, mtaani kwetu nilionekana kuwa kivutio cha warembo, kila msichana alikuwa akitaka sana kuwa katika mahusiano na mimi lakini sikuonekana kujali. Nilikuwa nikinukia sana kila nilipopita mbele yao. Sikuwa na nyodo, nilipenda kuwapa salamu na hata pale ambapo walionekana kutokuwa na fedha, niliwasaidia.
Latifa ndiye msichana pekee ambaye aliwahi kuingia chumbani kwangu. Kwa muonekano, alionekana kuwa radhi kwa kila kitu lakini kwa sababu sikuwa katika hali ya kufanya chochote kile, nikaachana nae. Yeye ndiye akawa redio, akawaelezea wasichana wenzake vile alivyoviona chumbani jambo ambalo kila mmoja akatamani kuja chumbani kwangu.
MIMI: Latifa, mbona umewaambia marafiki zako mengi kuhusu chumba changu?
LATIFA: Hapana, sikuwaambia.
MIMI: Sasa nani kawaambia?
LATIFA: Sijui.
MIMI: Okey! Hakuna tatizo (Nikaanza kuondoka mahali hapo)
LATIFA: Nyemo (Nikageuka na kuanza kumwangalia) Nije kwako leo?
MIMI: Hapana, nitakuwa bize kidogo, kuna hadithi nitatakiwa kuandika kwani zinahitajika gazetini.
LATIFA: (Huku akionekana kuwa mnyonge) Sawa.
Kiukweli Latifa alikuwa amenikasirisha sana, sikupenda kitendo alichokifanya cha kuwaambia marafiki zake kuhusiana na muonekano wa chumba changu. Sikutaka kujali sana, niliendelea kufanya mambo yangu kama kawaida.
Katika siku hii ndiyo nilikuwa naingia Mlimani City huku nikiwa kwenye gari yangu ya kawaida sana, Vitz. Nilipofika ndani ya eneo lile, nikaelekea sehemu na kisha kulipaki. Kwanza sikuteremka kutoka garini, nikabaki nikiwakodolea macho warembo ambao walikuwa wakipita kuingia na kutoka ndani ya jengo lililokuwepo mahali hapo. Niliporidhika, nami nikateremka.
Moja kwa moja nikaanza kuelekea ndani ya jengo hilo, macho yangu hayakutulia hata mara moja, nilikuwa naangalia huku na kule, nami nikaingia. Kwanza kwa mbaliiiii nikamuona msichana mmoja aliyekuwa amevaa suruali ya jinzi, alionekana mrefu kidogo japo si kama mimi, nywele zake zilikuwa ndefu na mwendo wake ulikuwa wa madaha, alikuwa akiingia katika duka la nguo lililokuwa karibu na sehemu walipokuwa wakikatia tiketi za kuingia Cinema.
Japokuwa sikuwa na lengo la kuingia ndani ya duka lile la nguo, nikaona haiwezekani, nikaanza kupiga hatua kuelekea katika duka lile. Nilipomuona anaacha mkoba wake kwa wahusika wa duka lile, mimi nikajifanya nazugazuga kuangalia nguo huku taiming yangu nikiwa nimemuwekea yeye tu.
Alipomkabidhi mhusika mkoba wake, akaanza kupiga hatua kuelekea katika sehemu zilizokuwa na nguo mbalimbali za kike, nami nikamfuata huku nikiendelea kuangalia huku na kule kana kwamba nami nilitaka kununua nguo. Kiukweli, msichana huyu alionekana mzuri sana tofauti na jinsi nilivyomuona kwa mbali. Kwa karibu, uzuri wake ulikuwa umeongezeka zaidi, alionekana kuwa mtoto wa mama, mtoto ambaye hata nguo hakuonekana kuwahi kufua kwa mikono yake.
MIMI: Hiyo inakufaa (Nilimwambia mara baada ya kumuona akiwa kaishika blauzi moja nyekundu. Akayageuza macho yake kwangu, kwa mbali akatoa tabasamu na kunipotezea)
Mtu mzima nikaona nimegonga mwamba, ilitakiwa nifanye kitu kingine cha ziada kabisa, kitu ambacho kingenifanya kuweka mazoea na yeye. Nikasahau kile nilichokuwa nikienda kukifanya katika jengo lile kubwa, akili yangu ikaamua kutulia na msichana yule.
MIMI: Na hiyo nayo nzuri (Nilimwambia huku nikitoa tabasamu baada ya kuitoa blauzi nyingine na kujifanya kuijaribisha kwa juu juu)
MSICHANA: (Kimyaaa)
Sikuchoka, bado nilikuwa nikiendelea kuleta shobo lakini msichana yule alionekana kuwa mgumu sana kunipa kampani katika kila neno ambalo nilikuwa nikiliongea. Sikutaka kukata tamaa kwani niliamini kwa siku ya kwanza msichana kama msichana huwa mzito kuzoeana na mtu asiyemfahamu.
MIMI: Na hiyo nayo nzuri (Nilimwambia maneno ambayo yalimfanya kuniangalia tena)
MSICHANA: Wewe ni mhudumu wa duka hili?
MIMI: Hapana. Kwa nini umeuliza? (Nikaona kashakwisha, unaanzisha mazungumzo na mimi, utake usitake lazima utaingia tu, maneno yangu matamu ya ushawishi niliyokuwa nayo yalinifanya kujiamini popote pale)
MSICHANA: Naona kila nguo unaniambia inanifaa, au unataka ninunue mpate faida?
MIMI: Hahaha! (Nikaanza kumsogelea kwani niliona mbali mbali ilikuwa hailipi) Umbo lako, rangi yako, tabasamu lako na hizo blauzi, zinakutoa sana. Nimependa rangi zake.
MSICHANA: Hahaha! Najua, napenda rangi hizi. Tatizo bei zao kubwa sana.
MIMI: Kwani hizo kiasi gani?
MSICHANA: Elfu sitini kila moja.
MIMI: Mmmh! Kweli kubwa lakini kwa nyie wasichana, nadhani inastihili, tena kama mimi ningekuwa mpangaji wa bei halafu nikakuona unakuja, ningeongeza na kuweka laki moja na nusu.
MSICHANA: (Huku akinitolea tabasamu) Kwa nini?
MIMI: U mzuri, umbo lako halitakiwi kuvarishwa na nguo za elfu sitini. Yaani kwa uzuri na umbo lako, unatakiwa kuvarishwa na nguo za laki moja mpaka milioni moja (nilipomwambia hilo, nikatoa tabasamu)
MSICHANA: Hahaha! Asante. Mungu alipenda niwe hivi.
MIMI: Usijali. Ila umezipenda?
MSICHANA: Yeah!
MIMI: Hakuna noma. Ngoja nikubebee (Nikaanza kuzichukua zile blauzi)
MSICHANA: Wewe kaka, unazipeleka wapi?
MIMI: Si umesema unazipenda na ndiyo maana nakubebea.
MSICHANA: Nimekwambia bei kubwa.
MIMI: Usijali. Kama umezipenda, haina budi kukubebea (Nilimwambia)
Nafanya kazi, sina msichana, ninaingiza kiasi cha shilingi milioni moja kwa wiki kutokana na biashara zangu, naishi peke yangu, fedha hazina matumizi, hivi kweli lingekuwa suala la kujiuliza sana kuamua kutumia kiasi fulani cha vocha katika kumnunulia nguo msichana huyu? Hapana, sikuona kama ulikuwa uamuzi mbaya.
Nilikuwa nimekwishampenda msichana huyu ambaye alijitambulisha kwa jina la Lisa, tukaanza kupiga stori na kumlipia zile nguo alizozitaka. Tukatoka katika duka lile na kisha kuingia Game ambapo huko nikanunua laptop moja aina ya Apple pamoja na mito mingine kadhaa na kisha kutoka. Katika kipindi chote hicho Lisa alikuwa pembeni yangu, tukatoka hapo na kisha kwenda katika duka la vyakula na kisha kununua nilivyovitaka. Kwa muonekano fulani Lisa alionekana kunishangaa, hakunielewa, nilikwishajua kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi juu yangu, alikuwa akijiuliza mimi ni mtu wa aina gani, sikuonekana kujali sana, niliendelea na mambo yangu kama kawaida.
Baada ya kumaliza, tukatoka na kwenda ATM, si kwamba sikuwa na fedha mfukoni, kila kitu nilichokuwa nakifanya kilikuwa kama mtego kwa Lisa, nilitaka ajue kwamba mtu aliyekutana nae alikuwa tofauti sana. Nilipomaliza kila kitu, nikaondoka nae na kuelekea Samaki Samaki.
MIMI: Unataka nini?
LISA: Chochote tu.
MIMI: Acha hizo Lisa, sema unataka nini jamani.
LISA: Chochote tu. (Alinijibu huku akionekana kuwa na aibu. Nikamuita mhudumu ambaye akafika mahali pale tulipokuwa tumekaa)
MIMI: Samahani. Una miguu ya kuku?
MHUDUMU: Miguu ya kuku?
MIMI: Yeah!
MHUDUMU: (Huku akianza kucheka) Hakuna.
MIMI: (Nikamwangalia Lisa) Hawana miguu ya kuku. Hebu chagua mwenyewe.
LISA: (Akatoa tabasamu pana na kutoa kicheko cha chini chini) Naomba juisi.
MHUDUMU: Ya nini?
LISA: Matunda.
MHUDUMU: Na hapo kaka
MIMI: Naomba maziwa.
Mhudumu akaondoka zake na mimi kubakia na Lisa. Tukaanza kupiga stori. Unajua hata kama unakutana na msichana kwa mara ya kwanza na kufanya kila kitu kwa mpangilio basi kamwe huwezi kufeli katika mishemishe zako. Sikuwa nikipenda kwenda Mlimani City huku nikiwa sina fedha, kwenda kule nilikuwa najipanga, kujipanga huko leo hii kukawa kumeniletea mtoto Lisa. Baada ya kuletewa vinywaji, tukanywa na kisha kuanza kuondoka.
MIMI: Unaishi wapi?
LISA: Upanga.
MIMI: Okey!
LISA: Wewe unaishi wapi?
MIMI: Naishi Tandale.
LISA: Tandale? (Akaonekana kushtuka kupita kawaida)
MIMI: Yeah! Mbona umeshtuka sana?
LISA: Hakuna kitu. Ila najua umenidanganya tu.
MIMI: Hahaha! Kwa nini?
LISA: Basi tu. Nahisi umenidanganya. Kwa hiyo hapa unakwenda kupanda daladala au unachukua bajaji?
MIMI: No! Nitakwenda na usafiri wangu (Wakati namwambia hivyo tukawa tumekwishafika kwenye gari langu na kisha kumfungulia mlango. Bado Lisa akaonekana kunishangaa sana. Kichwa chake kilionekana kuhisi kwamba nilikuwa nikimdanganya kwa sababu mtaa wa Tandale ulijulikana kwamba ni uswahilini sana, hakujua kwamba Tandale ya zamani ni tofauti sana na Tandale ya sasa.
MIMI: Ngoja nikupeleke Upanga kisha mimi nitarudi Tandale.
LISA: Mmmh! Siwezi kukuamini Nyemo.
MIMI: Kwa nini?
LISA: Basi tu.
MIMI: Hahaha! Niamini bwana. Hebu andika namba yako hapa (Nilimwambia huku nikimpa simu yangu, ilikuwa iPhone 5.
LISA: Hapana Nyemo, unanidanganya.
MIMI: Usibabaike na muonekano Lisa, mimi ni mtoto wa uswahilini tu ila fahamu kwamba Tandale unayoijua wewe imebadilika sana. Nadhani kuna siku utakuja, utajionea kwa macho yako.
LISA: Sawa.
MIMI: Upo whatsapp?
LISA: Yeah!
MIMI: Nilijua tu, msichana mrembo kama wewe usiwepo huko.
LISA: Hahaha! Acha zako Nyemo.
MIMI: Kweli tena.
Muda wote tulikuwa tukiongea tu, tayari Lisa akaonekana kuvutiwa na mimi lakini bado kichwa chake kilijua kwamba nilikuwa nikimdanganya. Muonekano wangu ulimfanya kutokuamini kwamba nilikuwa nikiishi Tandale, sikutaka kujali sana. Tulitumia zaidi ya dakika kumi na tano, tukafika mitaa ya kwao. Sikutaka kumuacha hivi hivi, nikambusu shavuni, akateremka na kuondoka huku akiwa amechukua vitu vyake.
Kuna nini tena? Mtoto kashaingia ndani ya kumi na nane, mtoto mzuri hata zaidi ya malaika akawa amefagilia mziki, sikutaka kuwa na pupa, nilitaka kwenda mdogo mdogo mpaka kinaeleweka na mwisho wa siku kuwa wangu. Kama ni usajili wa mchezaji, wakati huo alikuwa akielekea kupimwa vipimo vya afya, akifuzu, anakuwa mchezaji wa timu, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Lisa, alikuwa kwenye vipimo.
Nikapiga gia, nikasepa mahali hapo huku nikiwa na furaha sana.
Je, nini kitaendelea?
Huu ni mwanzo tu wa hadithi hii ya kizushi na ya kusogeza siku.
Tukutane Alhamisi mahali hapa ujue ilikuwaje kwa Lisa na yule LAtifa wa kitaa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: