KURUDI KWA MOZA: 44
Wakati Yule daktari akianza tu zoezi lake, Mishi alishangaa kumuona daktari akianguka chini huku akitapatapa na povu kumtoka mdomoni, wakati anamshangaa vile mara Yule daktari akawa kimya kabisa kama mtu aliyekufa.
Mishi akaanza kuogopa na kushuka kitandani, halafu akamkimbilia daktari pale chini akimshika shika huku akimuita,
“Daktari, daktari”
Ila daktari Yule alikuwa kimya kabisa, Mishi hakujielewa, alitoka kwenye kile chumba na kwenda kuita madaktari wengine ambapo walipoingia walishangaa pia, wakamchukua mwenzao kwenda kumpima ila wakati huo huo waliomba askari wa pale hospitali wamshikilie Mishi maana ilikuwa bado haijajulikana kuwa ni kitu gani kimempata mwenzao.
Mishi alikuwa kashikiliwa huku ana wasiwasi bila kiasi, alikuwa na hofu kubwa sana moyoni mwake, mara akamuona kuna daktari ambaye huwa anamfahamu akifika kama anataka kuzungumza nae ila Yule daktari alivyofika pale akamnasa kibao Mishi na kumfanya ashangae,
“Mbona umenipiga?”
“Muuaji mkubwa wewe”
“Sijaua jamani sijaua mimi”
“Mpelekeni kituoni huyu msichana ni muuaji, kamuua daktari”
Wale askari waliokuwa wamemshikilia Mishi waliita defenda kisha Mishi akapakiwa humo na kupelekwa kituoni, alijikuta akilia sana ila tu hakujua kuwa imekuwaje kuwaje maana ni kitu ambacho hakukielewa kabisa.
Ana alikuwa sehemu ya tofauti kabisa na nyumbani kwao, na sehemu aliyojikuta yupo ni nyumbani kwa mama Jack ambapo hakujua hata imekuwajekuwaje hadi kufika pale, hakuwahi kupajua kwa mama Jack ila alitambua ni nyumbani kwa mama Jack baada ya kukuta watu kwenye nyumba hiyo wakiongelea kuhusu kifo cha mama Jack, Ana alimsogelea kijana aliyeonekana akimuhadisia mdada kuhusu kifo cha mama Jack, Ana alipowatingisha walishtuka sana na kumuuliza kuwa ameingiaje,
“Umepitia wapi wewe?”
“Sijui”
“Wewe ni mwizi?”
“Hapana, mimi si mwizi ila hata mimi sijui nimeingilia wapi. Nilikuwa kwetu ila cha kushangaza nipo huku, sipajui, sijawahi kufika ila mtu mnayemuongelea namjua tena alifia nyumbani kwetu”
Hapo Yule kijana aliacha kuwa na maswali zaidi kwani alitaka kusikia kuwa mama yao alikufaje kufaje,
“Alikufa nyumbani kwenu? Ilikuwaje?”
“Mama yenu na mama yangu ni wachawi yani hilo halipingiki ila utofauti wa uchawi wao ni kuwa, mama yenu alikuwa anafanya wa jumuiya ila mama yangu ni wa peke yake, huwa anafanya uchawi kwaajili ya mambo yake tu. Mama alipelekwa kwa mganga na mama yenu, na Yule mganga alimwambia mama kuwa atoe kafara watoto wake. Kwenye familia yetu kuna mtu wa ajabu sana ameibuka na mtu huyu ana mazuri na mabaya yake, nay eye ndiye kawaponya ndugu zangu ila akasababisha mama yenu akafa”
“Kivipi, hebu tueleweshe vizuri”
Ana aliwaambia kutokana na uelewa wake, maana kidogo yeye aliweza kuelewa kuwa kifo cha mama Jack kilikuwaje, ni baada ya mama yao kuacha kutaja majina aliyoambiwa ya kutoa kafara na kuanza kutaja jina la mama Jack sababu alimkuta ndani kwake kwa mshangao.
“Mmmh na huyo mtu anayefanya vitu hivyo hatuwezi kupambana nae?”
“Kupambana na mtu huyo ni kujiingiza matatizoni, yani mnaweza mkaingia kwenye matatizo makubwa zaidi ya haya. Mama mwenyewe kajaribu mara kadhaa kupambana nae ila mwisho wa siku ni matatizo tu na anazidi kuivuruga familia sababu ya kupambana na huyo mtu”
“Ndugu zetu wameenda tena kwa mganga, na lengo ni moja tu kupambana na huyo kiumbe na kumrudisha mama yetu kama ikiwezekana”
“Hawezi kurudishwa, kwanza kazikwa kwenye kaburi lenye maji”
“Kuna uhusiano gani wa kaburi lenye maji na kurudishwa?”
“Sijui, ila ninachojua ni hawezi kurudishwa. Waaambieni hao ndugu zenu waache tu. Mimi mwenyewe hapa sijui nitarudije nyumbani, kilichoniponza ni kutaka kumsaidia mama”
Yani Yule kijana kuna baadhi ya maneno alikuwa anamuelewa Ana ila kuna baadhi ya mambo alikuwa hamuelewi kabisa, ila kwavile Ana alifika kimaajabu Yule kaka alimwambia kuwa siku hiyo alale hapo halafu kesho yake atamsindikiza kwao.
Mume wa Mishi alishangaa kupigiwa simu kuwa mkewe yupo kituo cha polisi, ikabidi afanye hima aende maana hakuelewa ni jambo gani limempata mkewe, na kweli alimkuta kituo cha polisi na alipewa muda kidogo tu wa kuzungumza nae,
“Imekuwaje Mishi tena jamani!”
Ikabidi Mishi asifiche maana tayari alifikwa na majanga,
“Nilikuwa na lengo la kutoa hii mimba, na daktari tulielewana vizuri kabisa, kilichotokea wakati anataka kunitoa ndio sikielewi hadi muda huu maana Yule daktari alianguka chini”
Mume wa Mishi alishangaa sana na kumtaka Mishi amuelezee zaidi, ambapo Mishi alimueleza ilivyokuwa hadi yeye kufikishwa hapo kituoni,
“Inasemekana Yule daktari amekufa, lakini mimi sijamuua daktari. Kwanza nimuue kwa lipi jamani, kweli mimi naweza kuua mtu jamani! Yani nimechanganyikiwa kabisa”
“Ila na wewe mke wangu ni nani alikutuma kwenda kutoa hiyo mimba?”
“Jamani sidhani kama ni wakati muafaka wa kubishana huu, fanya hima nitoke humu Napata shida ujue, nateseka mimi. Sijamuua daktari”
“Najua kama hujamuua, na ninajua kama kuua huwezi ila sijui uliingiwa na nini mke wangu hadi kwenda kutoa mimba. Kwahiyo alikutoa?”
“Hivi jamani na wewe hunielewi au ni nini? Nimekwambia wakati anataka kunitoa akaanguka, kwahiyo hakunitoa, yani hata sielewi kuwa nijielezaje. Kwa maelezo yangu pia nitafungwa maana sharia za nchi haziruhusu kutoa mimba, yani nimechanganyikiwa hapa. Naomba ufanye kitu nitoke”
Basi mume wa Mishi akaongea pale na mke wake na kumuahidi kumtafutia dhamana ili aweze kutoka halafu wafatilie kesi, ila alipoenda kwaajili ya dhamani ilikataliwa kabisa, na kushindwa kumsaidia Mishi kwa siku hiyo, na kuamua kwenda kujipanga kwa namna nyingine.
Wakati mume wa Mishi anaondoka njiani alikutana na Salome aliyekuwa akitabasamu, kisha akamsalimia mume wa Mishi,
“Habari yako?”
“Hivi tunajuana mimi na wewe?”
“Ndio tunajuana, au umechanganyikiwa sababu ya mkeo kuwa rumande!”
“Umejuaje”
“Najua”
Yani akili ya mume wa Mishi kwa wakati huo hata haikuwa ya kawaida kabisa kwani iligubikwa na mawazo mengi sana ya jinsi gani atamsaidia mkewe, kwahiyo hata hakuwa na kumbukumbu kuwa Salome ndiye aliyemwambia ukweli kuhusu mke wake kule kwa mganga,
“Nimechanganyikiwa kweli, mke wangu hata sijui nitamsaidiaje”
“Utamsaidia vipi muuwaji!”
“Sio muuwaji mke wangu, daktari alianguka mwenyewe”
“Mkeo sio muuwaji, na kile kiumbe alichotaka kukitoa sio uuwaji ule? Au kwavile unadhani mkeo ni mimba yake ya kwanza ile? Unajua ni ngapi ametoa? Mkeo ni muuwaji na kumsaidia itakuwa ni ngumu sana”
“Sikuelewi, inamaana wewe unajua kilichotokea?”
“Najua ndio”
“Basi usitangaze hivyo kuwa mke wangu alitaka kutoa mimba”
“Sasa nimetangaza au nimekwambia wewe muhusika, unaona sababu viumbe vya tumboni haviwezi kulilia haki zao, haviwezi kushtaki kuwa vimeuliwa kwa makusudi kabisa, mkeo ni muuwaji. Yule daktari nae anahaki ya kufa maana kashaua watoto wengi wasio na hatia kwa tamaaa ya pesa. Hata ufanyaje mkeo kwasasa hatotoka mule ndani mpaka ajifunze adabu na aelewe anapoambiwa kitu, maana kichwa chake ni kigumu kuelewa. Nishamwambia mara nyingi asiitoe ile mimba, najua ni mchezo wake ndiomana nikamuonya sana kuwa asiitoe ile mimba, halafu wewe unakazana kuugua moyo sababu ya Yule muuwaji! Ukitaka msaada wangu zaidi utanitafuta”
Kisha Salome akaondoka, mume wa Mishi alimuangalia Salome hadi alipoishia ndio akakumbuka kuwa ni huyu binti aliyemwambia tabia za mkewe ndipo alipokumbuka maneno ya mkewe kuwa huyo binti hakuwa mtu wa kawaida, ikabidi aendelee kwenda nyumbani ila alijipanga kwenda tena polisi ili akamuulize vizuri Mishi anapoishi Yule binti na aweze kwenda tena kuongea nae.
Nyumbani kwa Rose, walikaa watoto wake sebleni na muda kidogo alikuja Salome na kuwafanya wote washtuke maana wakikumbuka yale maneno kuwa Salome ndiye Moza walipatwa na mashaka ila Salome akawauliza,
“Mbona mnaonekana kuniogopa?”
Walikaa kimya hakuna aliyeweza kumjibu, na kufanya Salome aendelee kuongea
“Najua mama yenu atakapotoka kwenye adhabu ambayo amejipa kutokana na matendo yake yasiyoeleweka, ataenda kuwafungulia wale watu aliowafungia kwa miaka mingi”
Walikuwa kimya tu wakimsikiliza, hakuna aliyeongea chochote kwani ilionyesha wazi wanamuogopa Salome kutokana na hoja kwamba ndiye Moza, baada ya kimya kidogo Kulwa aliuliza kwa mashaka,
“Wewe ni Moza?”
Sauti yake ilikuwa ya kutetemeka sana,
“Kwa mfano mimi nikiwa ndiye Moza mtafanyaje?”
Wakawa kimya tu, na kufanya Salome aendelee kuongea
“Mimi nikiwa ndiye Moza, inamaana kuwa Moza mwenyewe yuko wapi, na Salome mwenyewe yuko wapi? Je Moza alikuwa ni jinni kiasi kwamba aweze kuingia kwenye mwili wa mtu mwingine na kufanya mambo yake? Msiniogope, mimi sipo kwaajili ya kuwatisha ila nipo kwaajili ya kuwasaidia, na kikubwa kinachonisumbua ni kuhusu hao watu ambao mama yenu kawatunza ndani, sishindwi kuwatoa ila nikiwatoa mimi nitasababisha madhara makubwa sana ndiomana nataka awatoe yeye mwenyewe”
Kidogo Salome alivyosema hivi walipata hata kauli za kuongea nae kwani uoga uliwaondoka kwa kiasi Fulani tofauti na mwanzo walivyokuwa wamejawa na uoga usio kifani, kisha akawaambia kuwa ni yeye ndiye aliyewaandalia chakula cha asubuhi, wakatamani kumuuliza kuwa mbona chapatti zilinoga kama zimepikwa na Moza, ila hakuna aliyeweza kuuliza hilo swali ingawa kwa wakati huu uoga ulikuwa umepungua.
Salome aliwaambia kuwa kwa siku hiyo wote walale hapo sebleni, yani hapakuwa na cha mlinzi wala nani kwani hakutoka tena kwenda getini, ni toka siku ile ya majanga ya kumuokota Rose, alikuwa akiishi tu mule ndani.
Kulipokucha mume wa Mishi alienda tena kituoni na kuongea na mkewe ambapo mkewe alimpa maelekezo ya anapopatikana Salome, kisha mume wa Mishi alimuahidi kufanya hivyo kwa muda huo maana hakuwa na namna nyingine yoyote, kesi ya Mishi ilikuwa ni kubwa sana na kama ikisomwa yani Mishi ana kifungo cha maisha pale, kwakweli mume wa Mishi alikuwa akihofia sana swala la mkewe kufungwa maisha ukizingatia ni siku chache tu tangu aoane na huyo mwanamke.
Aliondoka pale na kufata maelekezo hadi nyumbani kwa Rose, ila kabla hajagonga geti Salome alikuwa ameshamfungulia,
“Nilijua tu utakuja, na kwa hakika unajutia makosa ya mke wako nay eye anajutia makosa yake”
“Ni kweli anajutia sana mke wangu, mimi nipo tayari kuilea ile mimba na kulea mtoto na tena nitampenda kama mwanangu ila sasa mke wangu anawakati mgumu sana hata sijui nitafanyaje kumsaidia”
“Sasa umenifata mimi ndiyo hakimu wa kesi ya mkeo kusema nitaamuru asifungwe?”
“Najua kuwa wewe sio hakimu, ila wewe ulimpa laana mke wangu na laana hiyo ikampata. Ulimkataza mke wangu kufanya jambo lolote kinyume, na amefanya amepatwa na mabalaa makubwa sana, najua unauwezo wa kufanya mke wangu asikutwe na hatia”
“Lakini mkeo katoa mimba nyingi sana, hata akikutwa na hatia ni halali yake”
“Hawezi kurudia tena, ni ujana ndio ulikuwa unamsumbua. Naomba umsamehe mke wangu”
Mume wa Mishi alipiga magoti kwa Salome huku akionyesha simanzi ya hali ya juu,
“Nihurumie mimi, nampenda sana Mishi. Yeye ni mwanamke nimpendaye, ndoa yetu ni changa kabisa, hata miezi miwili haina ila majanga kama haya. Nakuomba nihurumie tafadhali”
Salome alicheka sana na kumwambia mume wa Mishi ainuke kisha akamwambia,
“Nenda nyumbani kwako”
“Halafu badae niende polisi!”
“Sijakwambia uende polisi, nenda nyumbani kwako kunguni wewe.”
Mume wa Mishi hakubisha na moja kwa moja alifanya safari ya kwenda nyumbani kwake, alipofika alifungua mlango na kushangaa mkewe kasharudishwa nyumbani.
Neema alikuwa nyumbani kwake na siku hiyo aliamua kuanza kufunga kama ambavyo alikuwa ameshauriwa na mama Pendo, alijitahidi afunge ingawa ilikuwa vigumu sana kwake kupambana na njaa yake, kwenye mida ya saa kumi jioni alishikwa na usingizi na kuamua kujilaza ila alijiwa na ndoto ambapo kwenye ndoto hiyo alimuona binti yake Salome amelala tena amelala kwenye kilekile chumba chake ila amelala usingizi mzito sana kiasi kwamba hashtuki kabisa, halafu akamuona Moza ambaye alionekana akibadilika kwa pembeni na wakati mwingine kuwa na mwili wa Salome na wakati mwingine kuwa na mwili wake, Neema alishtuka sana kutoka usingizini, na moja kwa moja akachukua simu yake na kumpigia mama Pendo huku akimueleza vile ambavyo ameota kwenye ndoto,
“Usihofu ndugu yangu, tunatakiwa kuingia kwenye maombi”
“Lakini naogopa”
“Usiogope, muombe Mungu akupe ujasiri na utaweza kupambana na hali yoyote. Kesho tutakuja huko”
Basi Neema alikuwa na mashaka ya hali ya juu, akaamua kwenda tena chumbani kule alipokuwa analala Salome, huku akitembea na tahadhari kubwa sana, akafungua chumba na kumfanya ashtuke vilivyo maana alimuona kweli Salome amelala hoi kitandani.
Itaendelea kesho usiku……!!!!!!
By, Atuganile Mwakalile.
KURUDI KWA MOZA: 45
Basi Neema alikuwa na mashaka ya hali ya juu, akaamua kwenda tena chumbani kule alipokuwa analala Salome, huku akitembea na tahadhari kubwa sana, akafungua chumba na kumfanya ashtuke vilivyo maana alimuona kweli Salome amelala hoi kitandani.
Neema hakuweza kuvumilia, alikimbia hadi nje huku akihema juu juu, akaunganisha matukio ya jinsi Salome wake alivyoanguka na kukauka kwenye kaburi la Moza, na jinsi alivyoota kuhusu Salome kulala chumbani kwake halafu Moza kuonekana akiingia kwenye mwili wa Salome na vile alivyoenda chumbani kwa Salome na kumkuta kuwa ni kweli amelala chumbani kwake, Neema alikuwa na hofu kubwa moyoni huku akijikuta akiogopa kuingia ndani kwake, akaita mmoja wapo wa wanae mapacha kuwa aende ndani akamletee simu kwa madai kuwa yeye alikuwa na kazi nje kumbe kiukweli alikuwa anaogopa ndani, Yule mtoto aliingia ndani ila ilichukua muda mrefu sana na hakurudi pale nje, ikabidi amuite pacha mwingine na amuagize ila naye ikawa hivyo hivyo na kufanya hofu kubwa itande kwenye moyo wa Neema, alikuwa na uoga wa hali ya juu. Badae akajiuliza kuwa yawezekana alichokiona ni maruweruwe ya usingizi kutokana na ile ndoto aliyoota,
“Ila wanangu niliowatuma ndani mbona hawajarudi?”
Akajaribu kuwaita lakini hawakumuitikia, alikaa nje mpaka mida ya saa moja jioni badae akajisemea,
“Natakiwa niwe jasiri,hivi mama gani mimi naogopa ndani na kuwatuma watoto! Haya sasa watoto hawajarudi halafu mimi bado naogopa na cha kushangaza kabisa huko ndani kwangu eti namuogopa mtoto wangu mwenyewe Salome, itabidi tu nijiweke ujasiri”
Akajitia ujasiri na kuingia ndani kwake, kisha akawasha taa za nyumba nzima na kuanza kuwaita wale wanae mapacha ambao aliwakuta chumbani kwao wamelala hoi, akawaamsha wakaamka huku wakidai kuwa na usingizi sana,
“Amkeni mle kwanza ndio mtalala”
Akatoka nao hadi sebleni, kisha akamuagiza mmoja wao,
“Nenda chumbani kwa dadako kamuamshe nae aje kula”
Basi yeye alikuwa na hofu sana pale wakati mwanae mwingine ameenda kumuita Salome, baada ya muda kidogo mwanae alirudi na kumwambia,
“Mama, mbona dada hayupo chumbani kwake? Una uhakika alikuwa amelala?”
“Mmmh labda ametoka”
Kisha Neema akaenda jikoni kuandaa chakula cha usiku huo kwani hata kufuturu hakufuturu kutokana na uoga wake, akijipa matumaini kuwa huenda ni mawazo yake tu kuwa alimuona Salome.
Muda huu Salome aliingia ndani na moja kwa moja alienda chumbani kwake, ila Kulwa alimfatilia Salome kwa nyuma na alipofika kwenye mlango wa chumba cha Salome alichungulia kwa kutumia kitasa cha mlango, akamuona mama yao akiwa anafanya shughuli zisizoonekana ila alikuwa amechoka sana, halafu akamuona Salome akimfata mama yao, na walisikika wakiongea ambapo Salome alimuuliza Rose,
“Umechoka?”
“Nimechoka ndio”
“Upo tayari kuwaachilia wale uliowafungia?”
“Naogopa maisha yangu”
“Kwahiyo maisha yako ni bora kuliko maisha ya wale uliowafungia?”
“Naogopa tu”
“Rose, jua naweza kufanya kwa lazima ila itakugharimu maisha yako kupita vile unavyofikiria, hebu waza jinsi nitakavyowatoa wale watu kinguvu nini kitatokea kwako”
“Najua nitakufa”
“Sasa kufa na kufilisika kipi bora”
Rose alionekana kukaa kimya na kufanya Salome aendelee kuongea,
“Mali nyingi umezipata kwa njia isiyo ya halali, umetesa watu. Umefanya wengine kuwa mandondocha yako sababu tu upate mali unayoitaka. Haya sasa kuna hasara gani ya hizi mali zikipotea?”
“Mali zangu zikipotea nitaweka wapi sura yangu, siku zote nimekuwa nikihangaika sababu ya hizi mali. Nihurumie Moza”
Hapa Kulwa alishtuka sana ila kwavile aliyemuona yeye kupitia kile kitasa cha mlango alikuwa ni Salome, aliendelea kujipa moyo kuwa huenda mama yao amechanganyikiwa tu kumuita Salome kuwa Moza. Ila huyu Salome aliendelea kuongea na Rose,
“Nakupa leo tu, ukishindwa basi mimi kesho nitafanya ninavyojua mimi. Nimekuvumilia sana Rose, unatesa watu, unawaumiza watu wasio na hatia ili wewe ufurahie maisha yako, waachie watoto wa watu, wanahitajika pia kwenye familia zao. Yani watu hawajulikani walipo kwao, familia hizo zimelia hadi basi kumbe wapo kwako huku umewafungia. Waachie watoto wa watu Rose”
“Basi nitafanya hivyo leo usiku”
“Mimi nakwambia kweli usipofanya hivyo unajitafutia mabalaa, kesho nitafanya mwenyewe na utaogopa sana”
Rose alionekana kutetemeka kiasi, Kulwa nae aliondoka pale kwenye kitasa cha mlango na kwenda kuwapa taarifa wenzie kuhusu kile alichokiona na kukisikia.
Neema akiwa bado na mashaka ya maisha ingawa muda tayari ulikuwa umeenda, akataka tena kwenda kuangalia kwenye chumba cha Salome kwani muda wote alisikia kama aende kuangalia ilia one kuwa atakutana na maajabu gani, ila kabla hajaenda popote uliingia ujumbe mfupi kwenye simu yake, alipoangalia ulikuwa unatoka kwa Salome,
“Mama nimeshakwambia, achana na maswala ya kufatilia chumbani kwangu. Hakuna chochote utakachokipata zaidi zaidi kujiweka kwenye mawazo tu”
Neema aliogopa sana huku mapigo yake ya moyo yakienda kwa kasi ya ajabu, akaamua kuchukua simu na kumpigia mama Pendo ila hakumpata hewani kwa wakati huo, basi ndio moyo wake uligubikwa na uoga mwanzo mwisho. Akajikuta akiogopa kwenda kulala mwenyewe kwenye chumba chake hivyo alienda kulala na watoto wake mapacha.
Mume wa Mishi alistaajabu sana kwa uwepo wa mke wake nyumbani, akamuuliza kwa mshangao kuwa amefanikiwa vipi kupata dhamani,
“Sio kupata dhamana tu mume wangu bali sina kesi tena”
“Kivipi?”
“Unajua alikuja Yule binti niliyekwambia, ndio kanitoa polisi hata sijui kaongea nao nini ila ndio kanitoa polisi na hakuna tena kesi wala kuripoti siendi kuripoti, kwa kifupi nimefutiwa kesi”
Mume wa Mishi alishangaa sana, ikabidi amueleze Mishi kuwa alienda kupatafuta hapo anapoishi huyo binti ili kumuomba amsaidie mke wake, kwahiyo swala la kusema kuwa Yule binti alishaenda polisi na kumsaidia lilimshangaza sana, akamuuliza tena mke wake kuwa hilo swala lilitokea muda gani,
“Kwanza asante sana mume wangu maana sikujua kama ni wewe ulienda kuzungumza nae, ila nilimuona polisi pale askari waliponifungulia na kumkabidhi kuwa niondoke nae. Nilipotoka nae alinipa onyo moja kuwa nisijaribu kuitoa hii mimba tena na nisijaribu kutoka nje ya ndoa yangu. Ila aliposema hapo tu kama kawaida kimaajabu nimejikuta nipo hapa ndani, mume wangu Yule binti sio mtu wa kawaida kabisa. Mume wangu, nakuhakikishia kuanzia muda huu, mimi ni Mishi mpya tena mpya kabisa, sitashawishika tena na chochote. Hii mimba nitalea na mtoto nitampenda kupita maelezo ya kawaida, sirudii kutoa mimba, sirudii tena kuhangaika hangaika na wanaume”
“Kwahiyo Yule daktari amekufa kweli”
“Ndio Yule daktari kafa kweli, tena nasikia leo ndio ilikuwa mazishi yake. Ni amekufa, ila inasemekana Yule daktari kashiriki sana kutoa wanawake mimba, yani Yule daktari nimemjua kupitia rafiki zangu, ni wengi sana kawatoa”
“Hapo sasa unatimia ule msemo usemao, mshahara wa dhambi ni mauti. Mke wangu tabia ya kutoa mimba uache, tutaliliwa siku ya mwisho na watoto mbalimbali tuliokatisha maisha yao”
Mishi alimuahidi mumewe kubadilika kabisa kwani kwa muda aliokaa kule rumande hakutamani kurudi tena kwani aliona kama dunia ikimuelemea ukizingatia yeye alikuwa anajiona kuwa hana hatia.
Siku hiyo waliwahi sana kulala ili kupata muda wa kupumzika kutokana na ile misukosuko ya siku hiyo na zile siku za nyuma.
Kulwa alipowaeleza wenzie kwahiyo wakawa tayari kwa kuona maajabu kwa usiku huo huku uoga ukiwa wa hali ya juu, wakakubaliana kulala sebleni tena ila usiku huo Salome hakulala nao sebleni maana hakutoka kabisa chumbani kwake, kwahiyo walibaki wenyewe ila walijawa na hofu ya hali ya juu kiasi kwamba hata wakisikia mjusi anapita wanatamani wakimbie, yani siku hiyo hakuna aliyelala kabisa hadi kuna muda walisikia mlango unabamizwa walijikuta wakikimbia wote na kukimbilia mlango wa kutokea nje ila walishangaa mlango haukufunguka yani hofu ikawajaa huku wakiwaza kuwa wataona vitu vya ajabu ila muda kidogo wote watatu wakasikwa na usingizi mzito sana.
Kesho yake walishtuka kila mtu akiwa amelala sehemu yak echini pale sebleni ila hakuna cha tofauti ambacho walikiona kwenye nyumba yao kwahiyo walijiona kuwa ni uoga tu ndio uliowasumbua ndiomana walikuwa na hali ile usiku.
Ilikuwa ni siku nyingine tena ambapo Ana alimuomba Yule mkaka amsindikize sasa nyumbani kwao, ila ndugu mmoja wa Yule kaka akajaribu kumkumbusha kuwa hata mama yao kilichomponza ni kumsindikiza Yule binti,
“Ila mimi sio mchawi”
“Sasa unauhakika gani kuwa mama yetu alikuwa mchawi?”
“Mifupa tuliyoikuta chumbani kwake, na huyu dada aliyetolewa msukule”
“Wewe ndugu yangu wewe, hakuna mwenye uhakika kuwa mama alikuwa mchawi, amesingiziwa tu na Yule binti ila mimi cha kukushauri usiende peke yako huko. Nenda na mtu mwingine”
Yule kijana alikubaliana na wazo la ndugu yake huyo, ila Ana aliuliza jambo moja kwao,
“Mama yenu alizoeleka kwa jina la mama Jack, huyo Jack ndio yupi kati yenu?”
“Jack ni mtoto wa mama aliyezoeleka sana, alikuwa na mapenzi na watu wengi ndiomana mama hakuitwa majina yetu yote ila aliitwa mama Jack, tena alikuwa ni mtoto wa mwisho kwa mama yani ndio mdogo wetu. Ila cha kushangaza, mdogo wetu huyo alipoteaga na hadi leo hatujui alipo”
“Kheee kumbe! Au nae katolewa kafara?”
“Hata hatujui kwakweli, dada yetu huyu tulijua amekufa kumbe yupo katolewa kafara, ila kuhusu Jack hakuna anayejua alipo Jack, alipotea kwenye mazingira ya kutatanisha na hadi leo hajawahi kuonekana”
“Mama yenu alichukua hatua gani kuhusu kupotea kwa huyo Jack?”
“Hatujawahi kumuelewa zaidi ya kusema ataenda kuagua kwa mganga ili ajue mwanae Jack yuko wapi, ila kila siku alisema bado haijajulikana alipo”
Ana aliwaelewa kisha akaondoka nao na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwakina Ana.
Leo mapema kabisa Neema alimpigia simu mama Pendo kisha akamuelezea kuhusu ndoto ambayo aliota jana yake na jinsi alivyoenda chumbani kwa Salome na kukuta amelala, akamuelezea jinsi alivyowatuma wanae na kugundua kuwa ni maruweruwe,
“Hapana Neema, hapo lazima kuna kitu wala sio maruweruwe”
“Mmmh unanitisha sasa, si mtakuja leo?”
“Kuna udhuru kidogo imetokea, tutakuja kesho”
“Sasa mimi nifanyeje, jamani naogopa mwenzenu”
“Cha kukusaidia ni kuwa uendelee na mfungo leo”
“Mmmh jamani nifunge tena?”
“Ndio funga tena, halafu hujui tu unafikiri hiyo ndoto umeota burebure, ni faida ya kufunga hiyo. Kufunga kuna faida”
“Mmmh haya”
“Funga bhana, usikate tama kuna faida ya kufunga. Kuna faida ya kufanya maombi, yani wewe usijali kuwa sisi hatujaja nyumbani kwako, unaweza kuomba mwenyewe na Mungu akakusikia, cha msingi kuwa na imani tu”
Neema alimkubalia mama Pendo na kukubali kuwa siku hiyo ataingia kwenye mfungo tena ingawa mwanzoni alikuwa anaona kuwa mfungo ni swala gumu sana kwake kwani aliona njaa ndio kitu cha kusumbua zaidi akili yake.
Wakati amekaa kwenye mida ya mchana mchana alisikia hodi, na alipofungua alikuwa ni Patrick amerudi, kwa upande mwingine Neema alifurahi sana kwani aliona sasa ataishi bila uoga sababu kuna mtu mkubwa ndani ya nyumba yake, ila kwa upande mwingine aliona ni mtihani kwake kwani atatkiwa kumpikia Patrick chakula wakati yeye amefunga, kwahiyo anaweza akajikuta anaonja na kufungulia.
Alimkaribisha vizuri sana, ambapo alipoingia tu cha kwanza alidai kuwa ana njaa sana, kwahiyo ikabidi Neema aende kumuandalia chakula,
“Mmmh huu ni mtihani sasa, nitaweza kuandaa chakula kweli bila kuonja? Huu ni mtihani kwangu”
Neema alijiona akianza kushindwa kufunga kwa siku hiyo mapema sana kabla hata siku haijaenda ukingoni.
Nyumbani kwa Rose, leo aliingia jikoni Salome na wote walikuwa sebleni kwa wakati huo kasoro Ana ambaye hakuwepo nyumbani, kwahiyo pale sebleni alikuwepo mlinzi, Kulwa na Doto.
Leo Salome alipika chakula na kila mmoja alisikia harufu ya kuungua kwa kile chakula,
“Jamani kama chakula kinaungua?”
“Ni kinaungua kweli”
“Ila si Salome yupo jikoni”
Ikabidi mmoja aende akamuangalie Salome jikoni, akashangaa sana kwani hakuwa Salome tena bali alikuwa ni Moza.
Itaendelea kesho usiku……!!!!!
By, Atuganile Mwakalile
.KURUDI KWA MOZA: 46
Ikabidi mmoja aende akamuangalie Salome jikoni, akashangaa sana kwani hakuwa Salome tena bali alikuwa ni Moza.
Uoga ulimshika na akarudi haraka haraka huku akiwapa wenzie ishara kuwa wakajishuhudie wenyewe kwa macho yao halafu yeye alikimbilia mlangoni kwa lengo la kutoka nje, nao waliinuka na kwenda jikoni, ila walipomuona Moza walipatwa na uoga wa hali ya juu, wakarudi haraka haraka na kuanza kugombeana mlango wa nje ambapo Kulwa nae alikuwa akihangaika nao ila haukufunguka ilikuwa kamavile vile usiku kuwa umejikaza na kufanya uoga uwazidi hata wasiweze kusogea kwenda mahali popote.
Wakiwa pale sebleni wakamuona Moza akitoka jikoni na kwenda pale walipo, kwa uoga waliokuwa nao hakuna aliyeweza kumtazama Moza, ila Moza aliwaambia
“Leo lazima nimalize kazi yangu, sitaweza tena kukaa, kwani Salome anatakiwa kurudi kwao”
Wote hawakuweza kumjibu kitu chochote na uoga waliokuwa nao ulikuwa ni maradufu, huku wakijiuliza kuwa Salome ni nani na Moza ni nani, iweje Salome ageuke na kuwa Moza na iweje Moza aseme kuwa Salome anatakiwa arudi kwao, hawakuweza kuuliza ila walibaki wakitetemeka kwa uoga.
Neema akiwa nyumbani kwake, gafla alijihisi kutetemeka mwili mzima halafu akawa na shauku ya kwenda tena kuchungulia chumbani kwa Salome, akainuka na kwenda kuchungulia akamuona Salome amelala, alipiga kelele za uoga ambapo Patrick nae alimfata ili kujua tatizo ni nini,
“Ni Salome”
“Kafanyaje?”
“Salome sio Salome wa kawaida”
“Kivipi sio wa kawaida?”
“Muone”
Neema alionyesha kidole alipo Salome pale kitandani, Patrick aliangalia kisha akamwambia Neema,
“Mbona mtoto amelala kawaida tu”
“Sio wa kawaida Patrick”
Patrick hakumuelewa kabisa Neema, ikabidi asogee kwenye kitanda cha Salome kisha alijaribu kumuamsha bila ya kuamka na alionekana amelala usingizi mzito sana, ndipo Neema akatoa tena wazo la kumpigia mama pendo ili awaite tena wale waombaji wamsaidie binti yake.
“Kuna tatizo huku naomba msaada wenu”
“Lakini ni mpaka kesho”
“Haiwezekani kuvumilia, Salome kalala haamki, tunamuita haitiki, sio kwamba amekufa ila kalala haamki”
Mama Pendo alishangaa sana kwa jinsi alivyoelezewa na Neema hivyo kumuahidi kuwa wanaenda na wale waombaji.
Ana alikuwa ameongozana na wale vijana hadi nyumbani kwao, alipofika mlangoni alishangaa harufu ya kuungua kwa chakula ambapo harufu hiyo ilikuwa ni kali kiasi kwamba ilimchanganya na yeye kwani anajua fika masharti ya nyumba yao kutokuunguza chakula cha aina yoyote halafu siku hiyo chakula kilikuwa kinaunguzwa kwa hali ile, akafungua mlango ila ulikuwa mgumu kwahiyo ikabidi agonge, alifunguliwa na kushangaa sana,
“Moza!!”
“Ndio ni mimi, nimekuja kumaliza kazi yangu”
Ana alitaka kukimbia ila miguu yake iligoma kwenda popote na kujikuta akiingizwa ndani pamoja na wale vijana, wakiwa wanashangaa shangaa kwa uoga pale sebleni mara walianza kuona watu wa ajabu wakitokea kwenye korido ya nyumba yao kama wakitokea vyumbani, wale watu walikuwa wakitoka mmoja mmoja na walipofika pale sebleni walikaa chini, ni hapo ndipo walipomuona Ommy na Sara wakiwa wameambatana na wale watu wengine, kiukweli kila mtu alishangaa, ila cha kushangaza zaidi ni kwa wale vijana kumuona mdogo wao jack akiwa ameambatana na wale watu,
“Mungu wangu, jamani si Jack huyu”
Walikuwa wakishangaa sana ila wale watu walitoka wote na kukaa chini pale sebleni ilionyesha kama akili zao bado haziko sawa kwani hakuna kati ya waliotoka aliyekuwa akishangaa kuwa yupo wapi na anafanya nini.
Moza aliingia jikoni na kutoka na sufuria ambayo mboga ilikuwa inaungua kisha akaweka maji halafu akaanza kummwagia mmoja mmoja kwa wale waliokaa chini ambao wametoka vyumbani, yani kitendo cha kumwagiwa kila mmoja alijikuta akili zake zikirudi timamu na kujishangaa zaidi kuhusu mahali alipo na jinsi alivyo, walikuwa jumla watu kumi na tano.
Wale vijana walimsogelea ndugu yao Jack, wakati huo Kulwa na Doto walimsogelea dada yao Sara huku wengine wakibaki wanajishangaa na kuona kuwa wamepata uhuru wa gafla bila ya kutegemea.
Moza alikuwa akitabasamu tu, na kupiga mluzi mkali ambapo Rose alitokea chumbani baada ya mluzi huo, ila alipowaona watu hao alishtuka sana na kupiga magoti kwa Moza,
“Umenimaliza Moza, umenimaliza Moza”
“Angalia ulivyowatesa watu hawa, wengine wana miaka mitano kwenye chumba chako kile kidogo umewafungia kimazingara. Unajiona bado una faida?”
“Umenimaliza Moza”
Rose alikuwa na kauli moja tu kuwa Moza umenimaliza yani alionekana kuteseka sana na kile kitu alichokifanya Moza.
Ila Moza alionekana kumpulizia kitu machoni ambapo Rose alianguka chini na kuonekana kama amezimia, watoto wake wakataka kwenda kwa mama yao ila Moza akawaambia kwa ukali,
“Asimsogelee mtu yeyote, hakuna kumsogelea Rose ni hatari kwa maisha yenu kwasasa. Haya wote tokeni nje ya nyumba hii, na mkae mbali kabisa”
Ana alijaribu kumtetea mama yake,
“Msamehe mama”
“Nyamaza na wewe, tena wewe kila kitu chako kinaenda kuteketea pamoja na uchawi wa mama yako. Hivi unadhani kuwatesa watu hawa kwa miaka yote ni vizuri? Mama yenu amekuwa mtu war oho mbaya sana kwa muda mrefu, aliweka zindiko baya kwenye nyumba yake hii, mtu usijikwae kwenye nyumba hii unapotea ili yeye azidi kufurahia maisha ya kutesa viumbe visivyokuwa na hatia. Nasema hivi ondokeni wote, tokeni nje, hapa mtuache sisi wenyewe. Nyie kakaeni mbali kabisa”
Macho ya Moza yalikuwa yanawaka kama moto hivyo kufanya wote washikwe na uoga, hakuna aliyeweza kubaki mule ndani ukizingatia Moza alikuwa anaongea kwa ukali sana halafu alikuwa anatisha, wote wakatoka nje ya nyumba yao na kukaa mbali kabisa, mara gafla wakiwa nje walishangaa kuona nyumba yao ikilipuka na moto mkubwa ukiwaka, moto ambapo uliwaka kwa muda mchache tu lakini kila kitu cha kwenye nyumba ile kiliteketea, yani kilibaki kiwanja na majivu, ilikuwa ni kitendo cha kufumba na kufumbua kila kitu hakikuwepo tena.
Wana maombi na mama Pendo walifika nyumbani kwa Neema na kwenda chumbani kwa Salome, ambapo walimkuta vile vile amelala wakambeba na kwenda nae sebleni halafu wakaanza maombi huku wakimuita Salome kuwa arudi kwani ilionyesha wazi kuwa Salome pale yupo kimwili tu.
Baada ya maombi ya muda kidogo, Salome alionekana kuamka na kukaa huku akishangaa kila alichokiona mbele yake, mama yake alikuwa bado na uoga ila alimfata na kumkumbatia.
Salome alimuangalia mama yake na kumuuliza,
“Mama niko wapi na kuna nini”
“Salome mwanangu, ulikuwa umelala ndio nimewaita waombeaji waje wakuombee”
“Nililala? Muda gani? Na kwanini niombewe?”
“Ulibeba vitu vyako vyote ukaondoka mwanangu ukaniachia ujumbe tu, ila nikakukuta umelala chumbani kwako”
“Sikuelewi”
Neema akaamua kumshika mwanae mkono ili ampeleke chumbani kwake huenda labda akamuelewa, ila alipofika kwenye chumba cha Salome alishangaa kuona kuwa nguo za Salome na vitu vya Salome vyote vilikuwepo mule ndani yani hakuna kitu ambacho kilihamishwa kama yeye alivyofikiria mwanzo, Neema alipiga kelele na kuwaita wale wanamaombi chumbani kwa binti yake, ila walimtaka awe mpole kwanza na akae chini atafakari huku akifanya mambo taratibu taratibu,
“Ukifanya kwa papara hutaelewa chochote kile, unatakiwa kuwa mpole na utafakari. Mungu ni mwema, na mwanao ni mzima kwahiyo swala la kuanza kumkandika maswali utashindwa kuelewa kipi ni kipi”
Ikabidi Neema akubaliane na ushauri wa mama Pendo ingawa kiuhalisia hali ya mwanae ilimchanganya sana kwani mwanae hakuwa na kumbukumbu yoyote ile.
Basi wale wanamaombi na mama Pendo wakaaga huku wakimsisitiza Neema ampelekage mwanae kwenye maombi hadi atakuwa sawa kabisa.
Neema alibaki ndani, yeye, mwanae na Patrick ila aliendelea kumuhoji Salome ambaye alionyesha kila kitu hakijui hata uwepo wa Patrick hakuuelewa kabisa, kwani kila kitu kilikuwa kigeni machoni mwake. Alianza kumuhoji mama yake kuhusu Patrick,
“Mama, huyu ni nani?”
“Ni baba yako huyu”
“Baba yangu! Mama si ulisemaga kuwa sina baba!”
Neema akawa kimya kwa muda kisha akamuangalia mwanae na kumwambia,
“Si wewe Salome uliyeamua kwenda kumtafuta baba yako hadi kuamua kuhamia nyumbani kwake. Huyu ni baba yako uliyemtafuta kwa kipindi chote, na ni wewe ndiye uliyemleta hapa nyumbani”
“Sikuelewi mama”
Neema alijaribu kumuelewesha vilivyo ila Salome hakumuelewa kitu chochote, halafu akauliza tena maswali yaliyomchanganya kabisa Neema,
“Vipi kule nyumbani kwetu? Mbona tuko huku, ni kwa nani huku? Yuko wapi mamdogo Ashura?”
“Mmmh hata sijui nikujibu vipi Salome yani vitu vingine unauliza wakati ulifanya mwenyewe, wewe si ulisema Ashura alitaka kukuua ukamuwahi na kummaliza”
“Kummaliza! Kivipi sikuelewi mama”
“Ashura alikufa”
Salome alianza kulia baada ya kusikia kuwa Ashura alikufa, kwakweli Neema alimshangaa sana mtoto wake na kuhisi kama kuna mchezo mbaya kachezewa mwanae,
“Mmmh wale wa maombi nao au wamefanya kitu kibaya kwa mwanangu”
Patrick aliamua kumkanusha Neema,
“Usiwaseme vibaya watu wamekuja kutusaidia, wameshasema kuwa kuna kitu hakipo sawa kuhusu mtoto wetu huyu sasa maneno ya nini. Mimi naona cha msingi labda tumpeleke Salome kule nilipokuwa naishi mimi labda ataweza kuweka kumbukumbu zake sawa na kuelewa kila kitu”
Neema aliona hilo ni wazo jema sana kwa wakati huo, kwahiyo akaenda kujiandaa kisha kuondoka kwenye gari na Salome ili wakamuonyeshe walipokuwa wanaishi.
Walifika na kushangaa watu wamejaa halafu eneo limekuwa majivu tupu, halafu Kulwa na Doto pamoja na Ana walipomuona Salome walimkimbilia na kupiga magoti mbele yake,
“Tafadhali msamehe mama yetu, najua hatorudia tena. Tunajua una uwezo wa kubadilisha huu moto na kurudisha nyumba yetu. Sisi hatuna haja na nyumba ila tunahaja na mama yetu, tusaidie Moza”
Neema na Patrick waliwashangaa sana huku wakiuliza kuwa ni kitu gani kimetokea, ila Ana alimwambia Patrick kuwa amuulize Yule binti yake anajua kila kitu,
“Huyu tumekuja nae hapa sababu tupo nyumbani haelewi chochote kile, ndiomana tumemleta hapa labda awe na kumbukumbu. Kwani kumefanyaje tena mbona nyumba imeteketea?”
Salome nae akaongea,
“Mbona umeniita Moza, Moza si alishakufa na mlivyo na roho mbaya mlinikataza hata kumuaga Moza mara ya mwisho”
Wakamshangaa, na Neema alikuwa wa kwanza kumshangaa binti yake kuwa anakumbuka vyema kitendo cha yeye kutaka kumuaga Moza na mwisho wa siku kuingia kwenye kaburi la Moza, ila hilo tukio la kuingia kaburini hakujua kama analikumbuka, ikabidi amuulize
“Walivyokukatalia kumuaga Moza ilikuwaje?”
“Sijui ila nakumbuka tulirudi nyumbani nikalala”
“Mmmh ukalala!”
“Ndio nikalala, si ni jana tu ndiyo Moza amekufa!”
Walikuwa wakimshangaa hata wale vijana waliomleta Ana na kumkuta ndugu yao Jack kwenye nyumba hiyo walishindwa kumuhoji maswali yoyote Salome kwani alionekana akiongea kama mtu asiye na mwelekeo.
Patrick alihoji kwa makini maana ile ilikuwa ni nyumba yake pia, ikabidi mlinzi wao ajaribu kumuelekeza kwa kifupi jinsi ilivyokuwa mpaka kushtukia nyumba ikiungua,
“Kwahiyo Rose ameungulia humo”
“Sijui, itakuwa hivyo maana sisi tuliamriwa tutoke nje na tulipotoka tu nyuma yake kukatokea mlipuko wa hali ya juu na gafla kila kitu kilikuwa kimeteketea kama ilivyoonekana yani hakuna tulichookoa”
“Kwahiyo huyo Moza mlimuona kabisa”
“Ndio, na mwanzoni alikuwa ni huyo Salome halafu badae ndio akageuka na kuwa Moza”
Patrick aliona kuwa hapo kutakuwa na tatizo, hivyo akamuomba Neema waondoke pamoja na Salome kurudi nyumbani maana walikuwa wakimsonga songa kumuuliza maswali Salome ambapo hakuwa na jibu ya swali hata moja.
Walimchukua Salome na kuondoka nae, huku wakiacha pale watu wakiendelea kufurika na kushangaa yale majanga ya moto, wakati wanaondoka Kulwa aliwashtua ndugu zake kuwa wawafate hao watu maana hawakuwa na pakukaa kwa kipindi hicho na wala hawakujua kuwa ni wapi waelekee.
Walipofika nyumbani, wakina Kulwa nao walikuwa wamegika,
“Tafadhalini tupokeeni, hatuna pa kwenda sisi”
Patrick aliwatazama, na kwavile hali nzima ya kilichotokea hakuielewa aliwahurumia na kuwakaribisha pale nyumbani huku akisema kuwa atatafuta utaratibu wa wao kupata sehemu ya kuishi.
Ila kwa upande wa Neema bado alikuwa na maswali kwa binti yake tu,
“Eti wewe ndio ulikuwa Moza!”
“Sikuelewi mama”
“Eti ulikuwa ukitoweka toweka?”
“Mama sikuelewi yani maswali yote unayoniuliza ni yananichanganya tu”
“Mwanangu, mimi ndio sielewi kabisa. Ulikuwa wapi kipindi chote hiki kama huna kumbukumbu ya chochote kilichotokea, inamaana kipindi chote hiki nilikuwa naishi na Moza!”
Alisisimka mwili kwa uoga, ila bado hakuelewa chochote.
Siku zilipita ila hakuonekana Rose wala Moza tena na akili ya Salome ilikuwa ikirudi kwa taratibu kwani kila kitu kilikuwa ni kipya machoni mwake kwa kipindi hiko.
MWISHO
TOA MAONI YAKO KWA SIMULIZI HII.
*_USIKOSE HADITHI MPYA LEO JION YA BEST YANGU*_
No comments:
Post a Comment