KURUDI KWA MOZA: 38
Akafanya tena dawa zake kama kwa nusu saa hivi, na mwili ukatoweka kweli. Sasa muda huu alitaka kujua kuwa ulipo mwili ni kitu gani kinatokea, akachukua kioo chake na kuangalia alishangaa sana kuwa muda huo mwili wa mama Jack ulionekana nyumbani kwa mama Jack na watu kwenye nyumba hiyo walikuwa wakishangaa tu.
Mganga alishtuka sana na kumuangalia msaidizi wake,
“Sijui ni wapi nimekosea yani sijui, badala mwili uende nyumbani kwa Rose eti umerudi kwa familia yake”
“Sasa tutafanyeje?”
“Sijui ila kuurudisha huku siwezi, hata mwanzo nimeshangaa ulirudi huku sasa sijui ndio ulienda nyumbani kwa Rose au ni kitu gani halafu saivi umeenda nyumbani kwa mama jack. Sina jinsi itabidi tu nikubali kuwa anaenda kuzikwa nyumbani kwake ingawa ni mbaya sana ila sina cha kufanya”
Msaidizi wa mganga alikuwa kimya tu huku akishangaa matukio ya siku hiyo.
Nyumbani kwa mama Jack, walishtushwa sana na kitendo cha kukuta mwili wa mama yao upo ndani tena inaonyesha alikufa siku mbili au tatu zilizopita, kwakweli walilia sana na kufanya wakose hata la kufanya na mwili huo, wengine wakawaambia wakazike tu maana utakuwa na harufu, ila walikataa kuwa haiwezekani kuzikwa bila ya kuchunguzwa kwanza, kwahiyo wakakubaliana kuwa mwili ule ukafanyiwe uchunguzi maana hata ulivyofika pale nyumbani ilikuwa ni kiajabu ajabu kwahiyo wakaita watu na kusaidiana kupakia kwenye gari ili kuupeleka hospitali kwaajili ya uchunguzi, kila mmoja alikuwa haelewi na watoto wa mama Jack walilia tu kuwa mama yao umekuja mwili amekufa wakati walijipa moyo kuwa yupo, na kama mama yao kauwawa hao waliomuuwa walikuwa na lengo gani maana gari halikuibiwa lilikutwa tu nyumbani ila mwili wa mama yao umekutwa ndani, hakuna aliyeelewa moja kwa moja kuwa yale ni mambo ya kishirikina.
Basi walipanda kwenye gari na ule mwili wa mama yao ila wakati wanakaribia hospitali ule mwili ulitoweka kwahiyo walifika hospitali bila ya ule mwili kuwepo kwenye gari, kila mmoja alimtazama mwenzie na kufanya waanze kuogopa sasa, huku wakirudi na gari upesi upesi nyumbani n hakuna aliyeweza kubaki nyumbani hapo kwani wote walikuwa na mashaka muda wote, ndipo kuna ndugu yao mmoja aliyetoa wazo kuwa waende kwa mganga wa kienyeji ili wakaangalie maana yake hayakuwa mambo ya kawaida.
Upande wa Yule mganga, walitulia kwa muda na kuhisi kuwa ule mwili wa mama jack utakuwa tayari umeshazikwa kwake ila walishangaa gafla mwili ukirudi kwenye kibanda chao, kwakweli mganga hakutaka tena kushindana na zile nguvu zaidi ya kumuomba kijana wake watafute vijana wawasaidie kuchimba kaburi kisha auzike huo mwili,
“Nitamkomesha huyu mwanamke aitwaye Rose, anadhani ni rahisi rahisi hivi kunitesa mimi! Nitamkomesha”
Yule msaidizi akaenda kutafuta vijana nao wakachimba kisha kwenda kwaajili ya kuzika ila kaburi lilijaa maji, mganga hakutaka kujisumbua zaidi kuwa wachimbe kaburi lingine badala yake aliwaambia wazike hivyo hivyo kaburi likiwa na maji, nao wakafanya hivyo ili wakimbizane na muda kwani giza lilikuwa linaanza kuingia, na walipomaliza waliondoka zao.
Rose alifika nyumbani kwake na kukutana na watoto wake getini wanataka kuondoka, ikabidi awaulize kulikoni,
“Mama kuna vioja huko ndani, unajua tulikuwa tumekaa pale sebleni mara ikaletwa maiti ya Yule rafiki yako na kuwekwa pale kati kati yetu yani kila mmoja hapa alichanganyikiwa na gafla ikapotea tena”
“Mmmh jamani, sio mawazo yenu tu!”
“Mawazo yetu! Mawazo wapi? Kila mmoja ameona kwakweli ni mambo ya ajabu, hakuna anayeweza kuishi tena humo ndani”
“Kwahiyo na Ana yuko wapi?”
“Yupo chumbani kwake, yeye hajatoka kabisa tangia muda ule”
“Wanangu tafadhari msiondoke, maana hata mkiondoka hamtatui tatizo kabisa, hili ni tatizo ila halimalizwi kwa kuondoka”
“Mama tunaondoka”
Mlinzi akawaambia,
“Hata msijisumbue kuondoka, mtashtukia mmerudishwa hapa hapa”
Ndipo wakakumbuka na maneno ya Moza kuwa wasikimbie nyumba hiyo kwani hata wakikimbia watarudi, pia wakakumbuka siku ambayo walikimbia na kwenda kulala hotelini ila wote walirudishwa nyumbani kwenye vyumba vyao, mwisho wa siku wakaona hata kukimbia ni kazi bure na kuamua kurudi na mama yao ndani, ila walipoingia tu ndani wakamwambia mama yao,
“Mama tafadhali toa ile misukule yako kwenye kile chumba cha siri maana ndio vitu vinavyotumika kututesa sisi”
Rose aliwashangaa wanae kuwa wamejuaje kuhusu kile chumba chake cha siri, ila Kulwa aliendelea kujua,
“Usishangae tu kuwa tumejuaje kuhusu kile chumba cha siri ila ujue kwamba tumejua kuwa ulitaka kututoa kafara watoto wako. Mama umeugua sana na kifo cha Ashura, hivi watoto wako sisi sio zaidi ya huyo Ashura? Sisi si ndio uliotutolea uchungu mama, ila ukataka kututoa kafara mama ili upate faida gani? Na kama kupata mali, utumie na nani wakati watoto wako umetutoa kafara”
Rose alikaa chini kwanza kwani hakufikiria kuwa watoto wake wamejua habari zake za kutaka kuwatoa kafara pia, yani habari za chumba hazijaisha zimekuja habari zingine za kutaka kuwatoa kafara. Akajikuta tu akiongea kwa unyonge,
“Nani amewaambia habari hizo wangu?”
Kulwa ndiye aliyemjibu mama yao maana leo alijitoa muhanga haswaa kwa hakika alichoshwa na kilichokuwa kinaendelea kwenye nyumba yao.
“Mama sekeseke lilianzia kwenye chumba chako cha siri ambako mtoto wako nilipigwa na shoti, sijui umeweka nini kwenye kile chumba. Nilizimia ila nililetwa ulipo kwa mganga na alikupa machaguo mawili kuwa umzike rafiki yako au uwatoe kafara watoto wako”
“Lakini sikuchagua kuwatoa kafara wanangu”
“Mama hukuchagua ndio ila kumbuka kuwa ulishataka kuwatoa kafara Doto na Sara, hivi wewe ni mama wa aina gani ambaye huna upendo na watoto wako? Siku zote umekuwa ukihangaika kwaajili ya maisha yetu, kuhangaika kwako huku ili tule vizuri na tulale vizuri, leo hii uliowahangaikia uwatoe kafara kweli?”
“Nisameheni wanangu”
Rose alijikuta akitoa machozi tu, muda ule ule Ana nae alitoka chumbani na kusema,
“Tena nisingekuwahi mama, ungeenda tu kumzika Yule rafiki yako basi ungetutoa kafara na sisi maana uliambiwa utaje majina wakati unamzika, yani ungemtaja mwanao mmoja mmoja na huku ingekuwa kwaheri”
“Umejuaje Ana?”
“Mama, tambua kuwa mimi nina utambuzi mkubwa sana. Nashukuru lile jiwe la dhahabu nililoliokota maana lilikuwa na nguvu za ajabu, mwanzoni tulipotoweka nilijilaumu kuliokota lile jiwe ila baada ya kujua ukweli nashukuru kwa kuliokota lile jiwe. Mama hata mimi uchawi umenichosha sasa, jamani ndugu zangu msiniogope ila nisaidieni natamani kuacha uchawi”
Wote walimshangaa Ana kuwa amebadilika hivyo kwa muda mfupi tu, na amekubali kuacha uchawi, Sara alijikuta akimsogelea mdogo wake ingawa kwa uoga uoga ila alimkumbatia na kumpongeza kutaka kuachana na uchawi, ila alikuwa anampongeza huku ana mashaka bado, sema Kulwa hakuacha hoja yake kumwambia mama yao kuwa atoe misukule aliyoiweka kwenye chumba chake cha siri, mama yao akawaomba kuwa wampe muda kidogo ajifikirie kwanza, akainuka na kwenda chumbani kwake.
Ana alibaki na wale ndugu zake huku akiwauliza kuwa atawezaje kuacha uchawi,
“Si unaacha tu”
“Haiwezekani kuacha uchawi kirahisi rahisi hivyo jamani”
Wakaangaliana kwa muda kisha kuulizana kuwa uchawi unaachwa vipi kirahisi, hakuna aliyekuwa na jibu,
“Ni vigumu sana kuacha uchawi kirahisi rahisi hivyo, itanigharimu maisha yangu yote. Natamani kuacha uchawi ila ni vigumu kwangu kuacha uchawi kirahisi rahisi”
“Mfano mama akiacha uchawi, na wewe si utaacha?”
“Mama hataki hata kusikia habari za kuacha uchawi ingawa unamtesa sana sasa hivi, ila mkiweza kumshawishi aache basi mtakuwa mmefanya vyema”
Ana aliondoka na kuelekea chumbani kwake, ila bado ndugu zake walijiuliza kama kweli Ana ana lengo la kuacha uchawi huku Sara akikumbuka alivyopofushwa na ndugu yake kichawi pia akawasimulia ndugu zake jinsi Ommy alivyopotea kwenye nyumba yao na kuwaambia kuwa nae ni mmoja wapo wa misukule wa mama yao, walikuwa wakishangaa tu uchawi wa mama yao jinsi ulivyo na bila wao kujua kama mama yao ni mchawi tena wa kudumu kiasi kile.
Waliongea sana ila badae walipoona muda umeenda sana wakakubaliana kuwa waende wakalale ila Sara akatoa tena ushauri,
“Jamani na leo kwanini tusilale wote sebleni?”
“Bado unaogopa tu kulala mwenyewe?”
“Ndio naogopa”
“Basi kalale na Ana”
“Weeee hapana jamani, siwezi kulala na Ana jamani”
“Kwanini lakini wakati kasema anaacha uchawi”
“Hata kama siwezi kulala na Ana kwakweli, bora nikalale ndani kwangu peke yangu”
Sara akainuka na kwenda ndani kwake kisha wale mapacha nao waliamua kuondoka na kwenda chumbani kwao kwahiyo pale sebleni kwao palibaki hapana mtu.
Baada ya muda kupita kidogo na kimya kutanda ndipo Rose alipoamua kwenda kufanya mambo yake sebleni sasa na kwavile aliona hakuna mtu hata mmoja akahisi ni vyema kufanyia vitu vyake hapo kwani yeye alikuwa anapenda zaidi kufanyia mambo yake sebleni kisha yanatawala nyumba nzima ila siku za hivi karibuni hakufanya sababu ya kutingwa na mambo mengi sana, taratibu alianza kufanya mambo yake pale kwa kuwasha dawa zake za kujifukiza na kuanza kujifukiza sasa.
Sara hakupata usingizi kabisa kwa usikiu huo kwani yeye alihisi kutokewa na vitu vya ajabu ajabu tu na kufanya ashindwe kulala, mara akasikia harufu kuwa kama kuna kitu kimewashwa hivi, uoga ukamshika kwani alihisi kuwa ndio huenda ni yale mambo ya ajabu yameanza tena, akatamani kujificha ila hakuwa na pakujificha ila akajivika ujasiri na kusema kuwa atatoka ili aende kuona kinbachoendelea.
Akanyanyuka taratibu huku akiwaza kuwa kama ataona vitu visivyoeleweka basi atapiga kelele ili kaka zake nao waamke na wamsaidie.
Taratibu akatoka chumbani kwake na kugundua kuwa ule moshi unatoka sebleni, kwahiyo akanyata hadi sebleni akashangaa kumuona mama yao akiwa mtupu kabisa akijifukiza na dawa zilizokuwa zikifuka moshi, akasema kwa hamaki,
“Mama!”
Mama yake aligeuka na kumtazama ila sura yake ilikuwa tofauti na alivyoizoea, ilikuwa ni sura ya kutisha sana, Sara akajishangaa kuwa anaanza kukimbia na badala ya kukimbilia chumbani alikuwa akikimbilia mlango wa kutoka nje ilia toke nje na kukimbia ila kabla hajafika mlangoni alijikwaa na kuanguka halafu mguu wake ukaanza kutoka damu, alimuona tu mama yake akiweka mikono kichwani na kusema,
“Masikini mwanangu jamani! Na yeye ndio anapotea hivyo!”
Mara gafla akatoweka, hakuwepo tena pale sebleni wala uwepo wake haukuonekana kama hata amechungulia mahali hapo, Rose aliacha kuendelea na zile dawa zake, alibeba vitu vyake na kwenda chumbani, alijibadilisha na kuwa kawaida kisha akaanza kulia huku akiumia sana moyoni,
“Sara mwanangu jamani kwanini lakini! Kwanini unataka kunifedhehesha mama yako? Kwanini unataka nikose raha mama yako, unajua ulipoenda ni pagumu sana, unaweka maisha yangu klwenye ugumu wa hali ya juu”
Rose alilia sana na kumfanya ashindwe kabisa kulala wala kuendelea na jambo lolote kwa usiku huo hadi panakucha.
Ndugu wa mama Jack walienda kwa mganga ila Yule mganga aliwatahadhalis
ha sana,
“Ndugu yenu aliingia kwenye mtego mbaya sana, na hata hivi ninavyoongea ameshazikwa”
“Amezikwa?”
“Ndio kazikwa, na sehemu aliyozikwa ni kaburi lenye maji kiasi kwamba siwezi hata kufanya dawa yoyote kwaajili yake, hata hivyo alikaa muda mrefu sana kabla ya nyie kugundua kifo chake.”
“Sasa tutafanyaje?”
“Sijui cha kufanya ila hata huyu mganga aliyechukua jukumu la kumzika mama yenu kwenye kaburi lililojaa maji ana jambo gumu sana na kubwa linaenda kumpata”
“Sasa ndugu yetu tutamkoa vipi?”
“Jamani ngojeni pakuche, usiku mzima nitafanya dawa zangu ila huyu aliyemfanyia mama yenu hivi lazima aumbuke kabla hapajakucha. Ngojeni nifanye dawa zangu, leo msiondoke hadi kesho tutakuwa tumepata majibu ya kueleweka”
Ndugu wa mama Jack waliamua siku hiyo kulala nyumbani kwa mganga ili kujua hatma ya ndugu yao maana kifo chake kilikuwa na utata sana.
Kulipokucha, Neema alienda kumuamsha Salome na kumkumbusha kuhusu lile swala la kwenda nae kwenye maombi, ni kweli Salome hakubisha kabisa halafu wakaanza kujiandaa walipomaliza safari yao ikaanza huku Neema akimsisitiza mwanae kuwa wakifika huko aeleze kila jambo linalomsibu ili iwe rahisi kuombewa, Salome alimuitikia mama yake na alikubaliana nae kwa kila kitu.
Walifika kituoni na kushuka kisha safari ya kuelekea kwenye maombi ikaanza sehemu yenyewe haikuwa mbali na kituo cha basi, wakati wanakaribia kufika Salome alimuomba mama yake kuwa aende dukani kununua maji mara moja kwani alikuwa na kiu sana, Neema alikubali kisha Salome akaanza kwenda dukani ambako napo hapakuwa mbali sana, ni nyuma kidogo tu na walipokuwa.
Neema akaona kama mwanae anakawia dukani na kuamua kumfata, ile anafika dukani tu alishtukia akiwa nyumbani kwake tena bado yupo chumbani kitandani yani ndio anaamka.
Itaendelea
No comments:
Post a Comment