MUME WANGU SHUJAA WANGU – 2
Siku zilivyozidi kusonga mbele, nilibaini kuwa Belinda ni binti mtata na ni ngumu kumridhisha. Alitaka vitu vingi, sikushangaa kwamba ilikuwa vigumu kwake kuishi na mama yake wa kambo, ambaye alikuwa mwanamke mzuri na mwema.
Jioni moja ya Jumapili kabla sijaanza zamu ya usiku kazini kwangu, alianza kuniambia kuwa mimi ni mwanamke mzuri na kwamba nina bahati sana kuolewa na mwanaume kama Moses. Alinieleza waziwazi kwamba angependa kupata mume kama yeye. Jioni ile nilishawishika kuamini kwamba alikuwa akimtaka mume wangu lakini nilimwambia kuwa anatakiwa kuweka macho yake kwenye masomo, Mungu atampa anayoyatamani!
Nilishindwa kukaa nalo, nilimpigia simu Hamasa na kumwambia kuhusu jambo hilo. Alinishauri niwe makini sana na Belinda.
Siku mbili baada ya kuanza zamu ya usiku kazini, nilihisi kukosa utulivu na nilikuwa nikimpigia simu mume wangu mara kwa mara na kumuuliza kama yuko salama. Mume wangu aliniambia kuwa kila kitu kipo shwari na yeye yuko salama, hivyo sikuwa na wasiwasi kuhusu chochote. Saa moja baadaye usiku wa manane, nilipata ujumbe wa simu kutoka kwa mume wangu akiniambia: "Belinda alikuja chumbani kwetu akiwa mtupu na kutaka nifanye nae mapenzi”.
Nilihisi kama nataka kuanguka, nikawa na maswali mengi kichwani, itakuwaje kama kweli alifanya, na sasa anataka kujisafisha na kujionesha kuwa ni mwanaume mwema? Ni wanaume wachache sana wanaoweza kukataa ofa yenye majaribu kutoka kwa msichana mzuri na mrembo.
Baada tu ya kumaliza kusoma ujumbe wa mume wangu, nilipokea ujumbe mwingine kutoka kwa Belinda akisema kuwa kuna kitu muhimu anataka kuniambia. Usiku ule ulikuwa mrefu kwangu, sikuweza kuweka nguvu kwenye mambo mengine.
Ilipofika saa 10 alfajiri, niliomba ruhusa na nilidanganya kuwa mwanangu anaumwa, hivyo nilihitaji kuondoka mapema. Nilipewa ruhusa nilipofika nyumbani Belinda alianza kulia akisema kuwa hajui kilichomtokea na kwamba ana hofu sana.
Aliponieleza, ndipo nilipoamini kuwa mume wangu alikuwa akisema ukweli. Nilipoingia chumbani kwetu mume wangu alinyanyua na tukakumbatiana kwa dakika kadhaa. Nilijivunia sana kuwa nae na kuona kuwa mimi ni mwanamke mwenye bahati, ilikuwa ajabu sana.
Nilichanganyikiwa mno kwa sababu Belinda ni mpwa wangu ambaye nilimpenda sana. Ni binti wa marehemu kaka yangu na niliahidi kumlea mpaka atakapoweza kujitegemea, sasa nilifanya kosa gani kumchukua? Nikimfukuza nyumbani, ataenda wapi? Sijui mama yake mzazi alipo, nitafanyaje sasa?
ITAENDELEA…
No comments:
Post a Comment