NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 21
Wakati mama mkwe wangu anaondoka kituoni hapo akiwa ameinamisha kichwa chini kwa aibu, nikatafakari alichosema huyu afande, nikagundua aliniita mchawi kwa sababu ya ile michoro ya pentagram na maandishi mekundu ya namba za Kiarabu, na kingine pengine ni ile harufu isiyokuwa na chanzo ndani kwangu.
Lakini niligundua pia kuwa kumbe walimtisha bosi wangu na shehe walipotaka kunitolea dhamana eti kisa watawafunga nao ili kupeleleza kama wamesaidiana na mimi kwenye mauaji, kama walivyomtishia mkwe wangu.
Baada ya hayo, nikaanza kuyatafakari maneno ya mama mkwe kuwa Rabia amechanganyikiwa hadi kiasi cha kutaka kujiua, nilijua kwa vyovyote kuna kitu ambacho Jay Love alikiacha kwa Rabia ambacho kinamfanya aendelee kuweweseka na penzi lake.
“ Hivi kwa akili ya kawaida kama mzimu unajua kwamba ukisahauliwa unakosa nguvu na kurudi ahera je, kweli na wenyewe utakuwa umekaa tu bila kufanya jitihada za kukumbukwa? Jibu likawa hapana.
Sikutaka kumuona mke wangu akijiua, Nilitakiwa nifanye jambo kwa kuwa ilikuwa wazi kuwa Jay Love amefanya jambo kwa Rabia. Nikasimama na kushika vyuma vya selo na kuchungulia koridoni, nikamuona afande mmoja anapita nikamwomba anisikilize, kweli akasogea hadi pale.
Nikamtajia namba ya Shehe kwa kichwa, kisha nikamwomba aipige lakini nikashindwa kumwambia amuelezee kuwa mzimu wa Jay Love unamsumbua mke wangu, nilihofia atajua nini kinachoendelea na mwishowe nikaonekana mshirikina bure; hivyo nikamwambia amtumie meseji maneno yakiwa: MKE WANGU, KUMBUKUMBU, JAY LOVE, TAFUTA”
Yule afande akasema; “nipe hela!” nikamwambia amwambie yule Shehe kuwa mimi nimesema amtumie elfu tano, akaondoka pembeni na sikujua kama alimpigia simu au lah lakini baada ya dakika kumi baadaye nilimuona akija na tabasamu akanioneshea ishara ya dole gumba maana yake poa.
Kidogo moyo ukatulia. Ikawa usiku ukawa mchana, hatimaye wiki ikapita na ikabaki siku moja tu. Kwa mujibu wa Jay Love kuwa nitakufa!
Je, Denis atakufa! Usikose Kesho.
No comments:
Post a Comment