NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 20
Niliamka asubuhi nikiwa ndani ya selo na watu wakizidi kuongezwa kila saa, kitu kizuri nilichokifanya ni kuwahi sehemu ya ukutani ambapo niliweza kuegemea na kulala vizuri.
Ukuta ulikuwa kama dhahabu ndani ya selo na kama ukikosa ukuta, basi utajikuta ukiumia siku nzima kwa kulala katikati ambapo hauwezi kuegemea popote.
Kadri watu walivyozidi kuingia ndivyo, msongamano, harufu kali na joto lilivyozidi humo ndani. Haikuwa mara yangu ya kwanza kuwekwa ndani lakini tofauti na selo za vituo vidogo, hii ya hapa tuliwekwa watu wengi kwa pamoja na niliambiwa kuwa hiyo inatokana na watuhumiwa kutoka vituo vidogo vyote vya kanda ya Kipolisi kuanzia Mbezi hadi Bunju kuletwa hapa.
Namshukuru Mungu, ilipofika majira ya saa nne asubuhi mama mkwe wangu alifika pale kituoni na kuniletea chai na mikate ambayo iligombewa vilivyo na wafungwa wenzangu na mimi nikiambulia kidogo tu.
Kwa muda huo mdogo mkwe wangu akaniambia: “Tulivyofikiria sivyo! Rabia anaonekana kuchanganyikiwa kabisa juu ya Jay Love hataki kula wala kulala tena hali zaidi ya mwanzoni na mbaya zaidi amejaribu kujiua kama mara nne kuanzia jana usiku.”
Kabla hajaendelea, askari wa pale kituoni alirudi na kumtaka mama mkwe wangu aondoke haraka pale selo tena akamsindikiza na matusi: “Mama toka haraka hapo, kazi yako si umemaliza? Au na wewe ndiyo mlishirikiana na huyu mchawi kwenye mauaji? Tutakuweka ndani na wewe!”
No comments:
Post a Comment