Home → simulizi
→ NILIVYOFANYA INTERVIEW NA LUSIFA 14
Jambo la kwanza kulifanya ilikuwa ni kuwasiliana haraka na yule shehe, nilitaka anielekeze jinsi ya kukimaliza kabisa kile kiumbe, maana nilijua hakitachukua muda mrefu kabla ya kuamka na kuendelea na mapambano yake dhidi yangu, tena kitarudi kikiwa na hasira kwa jinsi nilivyokifanya.
“Umefanya nini, Denis?” aliuliza shehe akiwa haamini baada ya kumtaarifu nilivyoweza kuutuliza mzimu wa Jay Love.
“Hauwezi ukawa sahihi hakuna binadamu wa karne hii aliyewahi kufanya hivyo. Kama ndivyo basi haraka chora pentagram kuuzunguka huo mzuka kisha weka tembe za vitunguu saumu kwenye hizo pembe tano haraka! “Kwa dakika tano nitakuwa tayari ndani kwako lakini usishtuke njia nitakayokuja nayo,” alisema haraka huyo shehe kiasi kwamba nilikuwa bado sijaelewa nini maana ya ‘pentagram’aliyoniambia niichore ardhini na ‘baada ya dakika tano atakuwa kwangu!’ alimaanisha nini.
Asante kwa google, nikasachi na kuona kuwa kumbe pentagram ni mchoro wa nyota (nimeuambatanisha hapo juu) nikauchora haraka kwa kutumia unga wa ngano na kuweka tembe za vitunguu saumu huku nikizingatia mchoro wangu kuuzunguka sawia mzimu wa Jay Love.
Wakati nikiwa nimemaliza zoezi hilo ambalo nikiri kuwa nililifanya kwa uoga ili Jay Love asije akaamka na kuniangamiza, ghafla nilishuhudia pembe ya ukuta wa chumba changu ikifunguka kisha nikamuona Shehe akiingia ndani baadaye ukajifunga tena.
Kwa usiku huo isingekuwa kawaida mtu kutoka Magomeni hadi Salasala kwa dakika tano, lakini Shehe kwa nguvu zake, majini wake na elimu aliyoipata aliweza kufanya hivyo na nilimuona kwa macho yangu.
Nilijisikia ahueni kidogo kwa uwepo wake, lakini nilishangaa kumuona akiwa mwanafunzi zaidi yangu, akawa ananiuliza maswali mengi ambayo sikuyaelewa hata kidogo, akaanza kuniuliza kama nilikuwa nina nguvu za ziada za kupambana na nguvu za kishirikina, nikamjibu sijui chochote kuhusiana na jambo hilo. Alikaa kimya japo hakuonekana kuridhika kabisa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: